Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gt sura 124
  • Atiwa Mikononi na Kuchukuliwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Atiwa Mikononi na Kuchukuliwa
  • Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Habari Zinazolingana
  • Atiwa Mikononi na Kuelekezwa Kwingineko
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Yesu Akabidhiwa na Kupelekwa Akauawe
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Pontio Pilato Alikuwa Nani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Kutoka kwa Pilato Mpaka kwa Herode na Kurudi Tena
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
gt sura 124

Sura 124

Atiwa Mikononi na Kuchukuliwa

WAKATI Pilato, kwa kusukumwa na fahari tulivu ya Yesu aliyeteswa, ajaribupo tena kumfungua, makuhani wakuu wakasirika hata zaidi. Wamepiga moyo konde kutoacha chochote kivuruge kusudi lao bovu. Hivyo basi wao warudia tena kupaaza sauti hivi: “Msulibishe! Msulibishe [Mtundike, mtundike, NW]!”

“Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe,” Pilato ajibu. (Tofauti na madai yao ya mapema kidogo, Wayahudi waweza kuwa na mamlaka ya kufisha wahalifu kwa makosa ya kidini yaliyo na uzito wa kutosha.) Halafu, kwa mara kama ya tano, Pilato amtangaza Yesu kuwa hana hatia, akisema hivi: “Mimi sioni hatia kwake.”

Wayahudi, kwa kuona kwamba mashtaka yao ya kisiasa yameshindwa kuleta matokeo, warudia tena lile shtaka la kidini la kukufuru lililotumiwa mapema kidogo kwenye kesi ya Yesu mbele ya Sanhedrini. “Sisi tunayo sheria,” wao wasema, “na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”

Shtaka hilo ni jipya kwa Pilato, nalo lafanya awe na hofu zaidi. Kufikia sasa afahamu kwamba Yesu si mtu wa kawaida tu, kama vile ndoto ya mke wake na nguvu nyingi ajabu za utu wa Yesu vyaonyesha. Lakini eti “Mwana wa Mungu”? Pilato ajua kwamba Yesu ni wa kutoka Galilaya. Hata hivyo, je! angeweza kuwa aliishi kabla ya hapo? Akimrudisha tena ndani ya jumba la utawala, Pilato auliza: “Wewe umetokapi?”

Yesu akaa kimya. Mapema kidogo alikuwa amemwambia Pilato kwamba yeye ni mfalme, lakini kwamba Ufalme wake si sehemu ya ulimwengu huu. Sasa hakuna elezo lolote zaidi lingetimiza kusudi lenye mafaa. Hata hivyo, fahari ya Pilato yaumizwa na katao la kujibu, naye amwakia Yesu kwa maneno haya: “Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha [kukutundika, NW]?”

“Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu,” Yesu ajibu kwa staha. Amaanisha mamlaka ambayo Mungu amewapa watawala wa kibinadamu kusimamia mambo ya kidunia. Yesu aongezea hivi: “Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.” Kwa kweli, kuhani mkuu Kayafa na wenzi wake na Yuda Iskariote wote wana daraka zito kuliko Pilato kwa ajili ya kutendwa kwa Yesu isivyo haki.

Kwa kuvutiwa hata zaidi na Yesu na akiwa na hofu kwamba huenda ikawa Yesu ana asili ya kimungu, Pilato ajitahidi tena kumwachilia. Hata hivyo, Wayahudi wamjibu vikali Pilato. Wao warudia shtaka lao la kisiasa, wakitisha hivi kwa ujanja: “Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.”

Ijapokuwa hilo lamaanisha matokeo ya kuogopesha sana, Pilato amleta Yesu nje tena. “Tazama, Mfalme wenu!” bado awasihi tena.

“Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe [Mtundike, NW]!”

“Je! nimsulibishe [nimtundike, NW] mfalme wenu!” Pilato auliza kwa kukata tamaa.

Wayahudi wamekuwa wakiudhika chini ya utawala wa Waroma. Kwa kweli, wao wadharau kutawalwa na Roma! Na bado, kwa unafiki, makuhani wakuu wasema hivi: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”

Akihofia cheo na sifa yake ya kisiasa, Pilato mwishowe ashindwa na madai ya Wayahudi yasiyokoma. Amtia Yesu mikononi mwao. Askari wamvua Yesu joho la zambarau na kumvika mavazi yake ya nje. Yesu achukuliwapo kutundikwa, alazimishwa abebe mti wake mwenyewe wa mateso.

Kufikia sasa ni asubuhi katikati siku ya Ijumaa, Nisani 14; labda yakaribia kuwa mchana katikati. Yesu amekuwa macho tangu mapema asubuhi ya Alhamisi, naye amepatwa na mateso makali moja baada ya jingine. Basi inaeleweka kwa nini nguvu zinamwishia chini ya uzito wa ule mti. Hivyo basi mpitaji njia, Simoni fulani wa Kirene katika Afrika, alazimishwa katika utumishi ambebee mti huo. Wanaposonga mbele, watu wengi, kutia na wanawake, wafuata, wakijipiga-piga kwa huzuni kuu na kumwombolezea Yesu.

Akigeukia wanawake hao, Yesu asema: “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri [wenye furaha ni, NW] walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. . . . Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”

Yesu anarejezea mti wa taifa la Kiyahudi, ambao ungali una umajimaji fulani wa uhai ndani yao kwa sababu ya kuwapo kwa Yesu na kuwako kwa mabaki wanaomwamini. Lakini hao wakiisha kuondolewa katika taifa lile, ni mti mfu tu wa kiroho utabaki, ndiyo, tengenezo la kitaifa lililonyauka. Loo, kutakuwa na sababu iliyoje ya kulia machozi wakati majeshi ya Kiroma, yakitumiwa kuwa wafishaji wa Mungu, yatakapoliacha ukiwa taifa la Kiyahudi! Yohana 19:6-17; 18:31; Luka 23:24-31; Mathayo 27:31, 32; Marko 15:20, 21.

▪ Ni shtaka gani ambalo viongozi wa kidini wanafanya dhidi ya Yesu wakati mashtaka yao ya kisiasa yanaposhindwa kuleta matokeo?

▪ Kwa nini Pilato awa mwenye hofu zaidi?

▪ Ni nani wanaochukua dhambi iliyo kubwa zaidi kwa ajili ya yale yanayopata Yesu?

▪ Makuhani wanamfanyaje Pilato amtie Yesu mikononi ili auawe?

▪ Yesu awaambia nini wanawake wanaomlilia, naye amaanisha nini kwa kurejezea mti kuwa “mbichi” kisha “mkavu”?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki