Nyongeza ya B
Je, Uhai Ulitokana na RNA au Ulitoka Kwenye Anga la Nje?
Kwa sababu ya kushindwa kuelewa jinsi protini, DNA, na RNA, zilivyojitokeza zenyewe, baadhi ya watafiti wametokeza nadharia ya kwamba uhai ulitokana na RNA. Wanamaanisha nini? Badala ya kusisitiza kwamba DNA, RNA, na protini zilijitokeza zenyewe kwa wakati uleule mmoja na kutokeza uhai, wao wasema kwamba RNA ndiyo iliyokuwa kitu cha kwanza kuwa hai. Je, nadharia hii inapatana na akili?
Katika miaka ya 1980, watafiti waligundua katika maabara zao kwamba molekuli za RNA zingeweza kutenda pia kama vimeng’enya kwa kujigawanya mara mbili na tena kujishikanisha pamoja. Basi ilikisiwa kwamba huenda ikawa RNA ilikuwa ndiyo molekuli ya kwanza yenye kujigawanya. Inasemwa kwamba baada ya muda, molekuli hizi za RNA zilijifunza kufanyiza tando za chembe na kwamba hatimaye, zile RNA zilitokeza DNA. “Watetezi wa hiyo nadharia ya kwamba uhai ulitokana na RNA,” aandika Phil Cohen katika gazeti New Scientist, “huamini kwamba nadharia yao yapasa kuonwa kuwa kweli kabisa, na kama sivyo, basi ionwe kuwa angalau imekaribia kweli kabisa.”
Lakini, si wanasayansi wote wanakubali mambo hayo. Wenye kutilia shaka, asema Cohen, “walibisha wakisema kwamba hiyo ilikuwa hatua kubwa sana isiyowezekana ya kuonyesha kwamba molekuli mbili za RNA zilijikatakata katika maabara, hadi kudai kwamba RNA ina uwezo wa kufanyiza chembe ikiwa peke yake na kutokeza uhai Duniani.”
Vilevile kuna matatizo mengine. Mtaalamu wa biolojia Carl Woese asisitiza kwamba nadharia ya kwamba “uhai umetokana na RNA . . . ina kasoro kubwa sana kwa sababu haielezi mahali ambapo nishati ilitoka ili kuendesha utokezaji wa molekuli za kwanza za RNA.” Na watafiti hawajapata kugundua RNA ambayo inaweza kujigawanya yenyewe tu tokea kitu kisicho hai. Pia kuna suala la mahali ambapo RNA ilitoka. Ingawa nadharia ya kwamba “uhai umetokana na RNA” inaonekana katika vitabu vingi vya mafundisho, nyingi za nadharia hizo, asema mtafiti Gary Olsen, “ni madhanio tu.”
Nadharia nyingine ambayo wanasayansi wengine wametokeza ni kwamba dunia yetu ilipewa uhai kutoka kwenye anga la nje. Lakini nadharia hiyo haijibu lile swali, Uhai ulianzaje? Kusema kwamba uhai ulitoka kwenye anga la nje, asema mwandikaji wa sayansi Boyce Rensberger, “kunahamisha tu mahali pa lile fumbo.” Hakuelezi jinsi uhai ulivyoanza. Kunapuuza tu lile suala kwa kusema kwamba uhai ulianza katika mfumo mwingine wa jua au katika kundi jingine la nyota. Suala kuu bado lipo.