UPARA
Kutokuwa na nywele kichwani, ingawa si lazima iwe kupoteza nywele zote kichwani. Kwa kawaida upara hutokea kwenye maeneo fulani ingawa katika sehemu nyingine za kichwa nywele hukua kama kawaida. Asilimia 90 ya watu wenye upara wana aina hiyo ya upotevu wa nywele. Biblia inataja kuhusu “upara” (Kiebr., qor·chahʹ), na “upara sehemu ya mbele ya kichwa” (Kiebr., gib·beʹach na gab·baʹchath). (Law 13:41-44; 21:5) Haijulikani ni nini hasa kinachosababisha upara. Sababu ya msingi inayoonekana kuchangia mtu kupata upara ni kupitia urithi, hata hivyo, huenda sababu nyingine zikawa kuambukizwa, hitilafu za homoni, uzee, magonjwa ya neva, baadhi ya matibabu, na ugonjwa wa kaswende.
Upara ni kasoro inayoathiri mwonekano wa mtu na hivyo watu wa nyakati za zamani, waliuhusianisha na aibu, maombolezo, au huzuni. (Isa 3:24; 15:2; Yer 47:5; Eze 27:31; Amo 8:10; Mik 1:16) Hata hivyo, chini ya sheria ya Musa upara haukumfanya mtu kuwa asiye safi. (Law 13:40) Sheria iliyotolewa kupitia Musa haitaji upara katika orodha ya kasoro ambazo zingemzuia mtu kutumikia kama kuhani. Katika maono ya nabii Ezekieli amri ilitolewa kwamba makuhani hawakupaswa kunyoa vichwa vyao wala kuacha nywele za vichwa vyao ziwe ndefu, bali walipaswa kuzipunguza.—Eze 44:20.
Elisha, nabii wa Yehova alikuwa na upara. Baada ya kurithi cheo cha Eliya, alikuwa akipanda kutoka Yeriko kuelekea Betheli alipodhihakiwa na umati wa watoto ambao walipaaza sauti hivi: “Panda juu, wewe mwenye upara! Panda juu, wewe mwenye upara!” Inaonekana sababu kuu iliyowafanya wapaaze sauti haikuwa kwamba Elisha alikuwa na upara bali walimwona mwanamume mwenye upara akiwa amevaa vazi rasmi la Eliya. Hawakutaka mtu yeyote arithi cheo cha Eliya. Alipaswa ama asonge mbele kuelekea Betheli au apae mbinguni kwenye dhoruba ya upepo kama mmiliki wa vazi hilo rasmi alivyopaa. (2Fa 2:11) Ili kuonyesha kwamba alikuwa mrithi wa Eliya na ili kuwafundisha vijana hao na wazazi wao kumheshimu nabii wa Yehova, Elisha aliulaani umati huo uliokuwa ukipaaza sauti katika jina la Mungu wa Eliya. Alijaribiwa ikiwa kweli yeye ni nabii. Yehova alithibitisha kwamba Elisha ana kibali chake kwa kufanya dubu jike wawili watoke kwenye msitu uliokuwa karibu na kuwararua vipandevipande watoto 42 kati yao.—2Fa 2:23, 24.
Baadhi ya watu walizoea kujiwekea upara wa bandia kwa kunyoa nywele zote walipoomboleza kifo cha mtu wa ukoo au kwa sababu za kidini, lakini Waisraeli walikatazwa kufanya hivyo. (Kum 14:1) Makuhani waliamriwa moja kwa moja kwamba wasinyoe upara au kukata ncha za ndevu zao kwa sababu ya wafu. (Law 21:5) Waisraeli waliamriwa wasinyoe masharafa yao wala kingo za ndevu zao.—Law 19:27; Yer 9:26; ona NDEVU.
Kwa ujumla, wanaume wa Misri walinyoa vichwa vyao, na waliona ndevu kuwa ishara ya maombolezo au uchafu. Kwa sababu hiyo, Yosefu alipotolewa gerezani alinyoa nywele kabla ya kupelekwa mbele ya Farao. (Mwa 41:14) Hata hivyo, Wamisri walifunika upara wao kwa nywele bandia, na wengi walionyoa vichwa vyao na ndevu zao walivaa nywele na ndevu za bandia. Kwenye funjo la Ebers, maandishi ya matibabu ya Kimisri kuanzia mwaka 2000 K.W.K., kuna maagizo 11 ya daktari ya kuzuia upara.
Katika Sheria, mtu mwenye ukoma kichwani alipaswa anyoe kichwa chake mwanzoni mwa kipindi cha kutengwa kwake, kwenye siku ya utakaso, na tena katika siku ya saba. (Law 13:33; 14:8, 9) Ikiwa Mnadhiri angechafuliwa, basi wakati wa kuthibitisha utakaso wake angenyoa kichwa chake. (Hes 6:9) Mwanamke mateka ambaye mwanajeshi Mwisraeli alitaka kumchukua awe mke wake alipaswa kunyoa kichwa chake.—Kum 21:12.
Wanajeshi wa Nebukadneza walipata upara kwa muda fulani wakati wa kazi ngumu ya kuzingira jiji la Tiro. Yehova alimwambia Ezekieli kwamba “kila kichwa kilitiwa upara, na kila bega lilisuguliwa na kuchubuka ngozi” wakati Nebukadneza alipofanya “kazi kubwa” ya kutekeleza hukumu dhidi ya Tiro. Vichwa vyao vilipata upara kutokana na kusuguliwa sana na kofia za chuma na mabega yao yalichubuliwa na vifaa walivyobeba (ili kujenga minara na ngome).—Eze 26:7-12; 29:17, 18.
Katika baadhi ya maeneo katika siku za mitume, kama vile jiji la Korintho lililojaa ukosefu wa maadili, wanawake waliokamatwa wakifanya uzinzi au uasherati waliadhibiwa kwa kukatwa nywele zao. Watumwa wa kike walikuwa na nywele fupi. Inaelekea Paulo alikuwa akirejelea hali hiyo kama mfano akionyesha kwamba katika kutaniko la Kikristo mwanamke ambaye atasali au kutoa unabii bila kufunika kichwa chake, ni kana kwamba amejifunua na kuonyesha aibu yake kwa kudharau kanuni ya Mungu ya ukichwa sawa na kunyoa nywele zake zote.—1Ko 11:3-10.