Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • it
  • Kuua

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuua
  • Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Habari Zinazolingana
  • Majiji ya Makimbilio—Uandalizi Wenye Rehema wa Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Vichwa vya Mazungumzo ya Biblia
    Vichwa vya Mazungumzo ya Biblia
  • Dhambi
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Sheria
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
Pata Habari Zaidi
Ufahamu wa Kina wa Maandiko
it

KUUA

Maneno tofauti-tofauti ya lugha ya awali yanayotafsiriwa “ua” na “chinja” yanarejelea kukatisha uhai wa mtu, huku muktadha au maandiko mengine yakiamua ikiwa uhai wa mtu huyo ulikatishwa kimakusudi na bila kuwa na ruhusa ya kufanya hivyo au kinyume cha sheria. Kwa mfano, katika amri hii: “Usiue” (Kut 20:13), ni wazi kwamba neno la Kiebrania linalotafsiriwa “kuua” (ra·tsachʹ) katika kisa hiki linarejelea kuua kimakusudi kinyume cha sheria. Lakini kwenye andiko la Hesabu 35:27 neno hilohilo linatumiwa kufafanua tendo ambalo mtu anayelipiza kisasi cha damu aliruhusiwa kutenda. Kwa hiyo, amri hii: “Usiue,” inapaswa kueleweka kwa kuzingatia Sheria yote ya Musa, ambayo iliruhusu kukatisha uhai wa mtu katika hali fulani hususa, kama vile kuwaangamiza wahalifu.

Historia ya Mwanzo. Mauaji yamekuwapo kuanzia mwanzoni kabisa mwa historia ya wanadamu. Kupitia kutotii kwake, Adamu alipitisha dhambi na kifo kwa wazao wake, na matokeo ni kwamba akawa muuaji. (Ro 5:12; 6:23) Ibilisi ndiye aliyechangia kimakusudi jambo hilo kwa kumshawishi Hawa, mke wa Adamu, atende dhambi, na hivyo yeye mwenyewe akawa muuaji, mwanzoni mwa njia zake akiwa mchongezi wa Mungu.​—Mwa 3:13; Yoh 8:44.

Miaka 130 hivi baadaye, mauaji ya kwanza ya kikatili, mauaji kati ya ndugu, yakatokea. Kaini, mwana wa kwanza wa Adamu, akichochewa na wivu wenye chuki, alimuua ndugu yake, Abeli. (Mwa 4:1-8, 25; 5:3) Kwa sababu hiyo, Kaini alilaaniwa na kufukuzwa na akawa mzururaji na mkimbizi duniani. (Mwa 4:11, 12) Baada ya gharika ya siku za Noa, Yehova aliwaruhusu wanadamu kutoa adhabu ya kifo.​—Mwa 9:6.

Chini ya Sheria. Karne nyingi baadaye Waisraeli walipewa Sheria ya Musa, na sheria hiyo ilikuwa na masharti thabiti kuhusiana na kuua. Ilitofautisha kati ya mauaji ambayo hayakukusudiwa na mauaji ya kukusudia. Mambo yaliyochunguzwa dhidi ya mtu anayedai kwamba aliua bila kukusudia yalitia ndani: Ikiwa mtu huyo (1) alikuwa akimchukia mtu aliyeuawa (Kum 19:11, 12; linganisha Yos 20:5), (2) alimvizia (Hes 35:20, 21), au (3) alitumia kitu au kifaa ambacho kilikuwa na uwezo wa kusababisha kifo (Hes 35:16-18). Hata watumwa, ikiwa wangepigwa na mabwana zao mpaka kifo kiwapate, kisasi kilipaswa kulipwa. (Kut 21:20) Kwa kuwa hukumu ya kifo ingetolewa kwa muuaji aliyekusudia na hakuna fidia ambayo ingekubaliwa katika visa hivyo, mtu aliyeua bila kukusudia angeokoa uhai wake ikiwa angeenda kwenye eneo salama katika majiji ya makimbilio.​—Kut 21:12, 13; Hes 35:30, 31; Yos 20:2, 3; ona MAJIJI YA MAKIMBILIO.

Baadhi ya matendo ambayo yalifanywa kwa kukusudia na yakasababisha au yangesababisha kifo cha mtu mwingine yalionwa kuwa ni sawa na mauaji ya kukusudia. Kwa mfano, mmiliki wa ng’ombe dume mwenye zoea la kuwapiga watu pembe, ambaye amepuuza maonyo aliyopewa mapema ya kufunga mnyama wake, anaweza kuuawa ikiwa ng’ombe huyo ameua mtu. Hata hivyo, katika baadhi ya visa, fidia ingeweza kukubaliwa kukomboa uhai wa mmiliki wa ng’ombe huyo. Bila shaka, waamuzi wangechunguza hali zilizohusika katika kisa kama hicho. (Kut 21:29, 30) Pia, mtu ambaye angepanga hila dhidi ya ndugu yake ili kufanya auawe, alipaswa kuuawa.​—Kum 19:18-21.

Sheria iliruhusu kujilinda, lakini ilidhibiti haki ya mtu ya kupigania mali zake. Licha ya mtu kumkamata mwizi akimwibia nyumbani mwake, angekuwa na hatia ya damu ikiwa angemuua mwizi huyo wakati wa mchana. Ilikuwa hivyo kwa sababu wizi haukuhukumiwa adhabu ya kifo na mwizi angeweza kutambulika na kuhukumiwa wakati wa mchana. Hata hivyo, wakati wa usiku ingekuwa vigumu kuona kile ambacho mvamizi anafanya na kujua nia yake. Kwa hiyo, mtu ambaye angemuua mvamizi wakati wa usiku alionwa kuwa hana hatia.​—Kut 22:2, 3.

Katika karne ya kwanza W.K. wale waliotafuta kumuua Yesu walitambuliwa kuwa ‘wana wa Ibilisi,’ muuaji wa kwanza. (Yoh 8:44) Waandishi na Mafarisayo waliyarembesha makaburi ya waadilifu wakidai kwamba hawangeshiriki kuwaua manabii hao. Hata hivyo, walidhihirisha roho ya uuaji sawa na hiyo kumwelekea Mwana wa Mungu.​—Mt 23:29-32 linganisha Mt 21:33-45; 22:2-7; Mdo 3:14, 15; 7:51, 52.

Chuki Ni Sawa na Kuua. Mauaji yanaanzia moyoni mwa mtu. (Mt 15:19; Mk 7:21; linganisha Ro 1:28-32.) Kwa hiyo, mtu yeyote anayemchukia ndugu yake ni muuaji. (1Yo 3:15) Pia Yesu Kristo alihusianisha mauaji na mtazamo usiofaa, kama pale ambapo mtu anaendelea kumkasirikia ndugu yake, akizungumza naye kwa ukali, au akimhukumu na kumshutumu isivyofaa kuwa ni ‘mpumbavu asiyefaa kitu.’ (Mt 5:21, 22) Chuki kama hiyo inaweza kupelekea kwenye kuua kihalisi. Inaonekana kwamba maneno haya ya Yakobo (5:6), “Mmemhukumu; mmemuua mwadilifu,” yanaweza kueleweka kulingana na muktadha huo. Watu waovu na matajiri waliowachukia wanafunzi wa Mwana wa Mungu na kuchukua hatua kali dhidi yao, waliwaua kihalisi Wakristo hao katika baadhi ya visa. Kwa kuwa Yesu anaona tendo lolote wanalotendewa ndugu zake kana kwamba anatendewa yeye mwenyewe, kwa njia ya mfano watu hao walimuua Yesu pia, na bila shaka Yakobo alikuwa na wazo hilo akilini.​—Linganisha Yak 2:1-11; Mt 25:40, 45; Mdo 3:14, 15.

Ingawa wafuasi wa Yesu wanaweza kuteswa na hata kuuawa kwa sababu ya uadilifu, lingekuwa jambo la aibu kwao kuteswa kwa sababu ya kuua au kufanya mambo mengine mabaya.​—Mt 10:16, 17, 28; 1Pe 4:12-16; Ufu 21:8; 22:15.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki