Je! Rehema ya Mungu Inafunika Dhambi Zako Zote?
“Yehova, Mungu mwenye rehema na fadhili, . . . mwenye kusamehe kosa na uasi na dhambi, lakini hatakosa kwa vyo vyote kutoa adhabu.”—Kut. 34:6, 7.
1. Watu wengine wanadai kwamba rehema ya Mungu inafika wapi?
JE! REHEMA ya Mungu ni isiyo na mipaka? Je! yeye amewakilishwa na wengi kwa njia ya kweli kama Mungu mwenye huruma sana na upendo unaowahusu wote hata anamkaribisha kila mtu, bila kujali mtu anaishi maisha ya namna gani? Kwa mfano, kama ilivyotajwa na mtaalamu wa kidini katika gazeti lililochapwa na jamii ya chuo cha uanadini: “Ikiwa Kanisa linatimiza mwito wake lazima litangaze kwa ujasiri kwamba wanaume wenye kulala wanaume wenzao na wanawake wenye kulala wanawake wenzao ni watu, waliofanywa kwa mfano wa Mungu, ambao Kristo aliwafia, na kwamba kwa neema ya Mungu wale wasiokuwa watu ni watu wa Mungu kwa maana wakati mmoja hawakuwa wamepokea rehema lakini sasa wamepokea rehema.” Je! rehema ya Mungu inamfunika mtu anayeendelea kuzoea mambo haya? Kiongozi mwingine wa kidini anadhani hivyo, kwa maana aliandika hivi juu ya habari ii hii katika gazeti la kanisa lililochapwa “kwa kibali ya kanisa”: “Ikiwa Mungu hamchukii sana, bali anampenda mwanamume mwenye kumlala mwanamume mwenzake au mwanamke mwenye kumlala mwanamke mwenzake akiwa na tabia aliyoumbwa nayo sisi hatuwezi kukosa kumpenda. Nayo hii yamaanisha kwamba lazima tumkubali huyo kama alivyo.” Je! Mungu anamkubali kama alivyo?
2. Ni mazoea gani ya Yesu yawezayo kufanya watu wengine waelewe vibaya nia ya Yesu juu ya watenda dhambi, lakini Yesu aliwajibuje wenye kumlaumu?
2 Kusoma Biblia bila uangalifu huenda kukafanya wengine wakubaliane na maoni yaliyotajwa na viongozi hawa wa kidini. Huenda wakawa wanawaza juu ya aliyoyafanya Yesu Kristo kama yale yaliyoandikwa katika Mathayo, sura ya tisa. “Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”—Mt.9:10-13.
REHEMA SI KUACHILIA DHAMBI
3. Maneno ya Yesu mwenyewe kwa kuwajibu wenye kumlaumu yaonyesha nini juu ya nia yake kuelekea watenda dhambi, nayo matendo yake yaliendeleaje kuonyesha hili?
3 Je! kwa kuyasoma haya vivi hivi tu isingeelekea kuonyesha kwamba Yesu aliwakubali wenye dhambi kwa sababu alikuwa na nia ya kushirikiana nao, akawalaumu Mafarisayo kwa kukataa kufanya hivyo? Walakini, angalia maneno ya Yesu ya utangulizi: “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.” Badala yake hii isingeonyesha kwamba sababu ya Yesu ya kushirikiana nao ilikuwa kuwapoza wala si kuwakubali tu wakiwa katika hali ya ugonjwa aliyowaona wakiwamo kama wenye dhambi? Yesu alionyesha rehema, sawa na alivyowaona wengine kwa upole katika Mahubiri yake juu ya Mlima, akisema, “Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema.” (Mt. 5:7) Walakini, kuonyesha rehema kwa Yesu juu ya wenye dhambi hakukuwa kuachilia dhambi zao. Bali, kulifanya kazi kwa njia ya huruma sawa na kulivyofanya kwa waliokuwa wagonjwa wa kimwili. Wakati mmoja mtu mwenye ukoma alimwona Yesu akaanguka kifudifudi na kumwomba, akisema hivi: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Kwa hiyo Yesu akanyosha mkono na kumgusa, akisema: “Nataka; takasika.” Mara hiyo ukoma wa mtu huyo ukamwacha. Nyakati nyingine alimwambia aliyekuwa mgonjwa ainue tu kitanda chake na kutembea. Lakini nyakati nyingine badala ya kusema hivyo alisema hivi: “Umesamehewa dhambi zako.”—Luka 5:12, 13, 20.
4. (a) Ni nini lililokuwa mojawapo la mambo ya maana zaidi ya huduma ya Yesu? (b) Katika barua yake ya kwanza kwa Wakorintho, mtume Paulo aliuonyeshaje uhusiano wa kweli wa watenda dhambi na rehema ya Mungu?
4 Hivyo ni wazi kwamba Yesu hakuwa akiwakubali watu wakiwa kama walivyokuwa katika dhambi zao. Bali, mojawapo la mambo ya maana zaidi ya huduma yake lilikuwa kupoza watu magonjwa yao ya kiroho, akiwawezesha wakubaliwe na Mungu kwa sababu ya njia yao ya maisha iliyobadilishwa. (1 Pet. 3:12; Mal. 3:18; Matendo 10:34, 35) Wanafunzi wa Yesu hawakuwa na maoni yaliyopotoshwa juu ya rehema ya Mungu. Kwa mfano, mtume Paulo aliandika hivi kwa Wakristo waliokubaliwa katika Korintho karibu miaka 22 baada ya Yesu kumaliza huduma yake ya kidunia kwa kufanikiwa: “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika [roho ya] Mungu wetu.”—1 Kor. 6:9-11.
5. Yohana alieleza dhambi na wanaoizoea kwa maneno gani, naye alionyesha mwisho wa hao utakuwa nini?
5 Yohana, mtume wa Yesu aliyependwa sana na Yesu, alieleza dhambi na wale wanaoizoea kwa maneno haya na kuonyesha mwisho wao utakuwa nini: “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye [Yesu] alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua. Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”—1 Yohana 3:4-8.
HAKUNA KUACHILIWA KWA WAZOEVU WA DHAMBI
6. Ni nini maoni ya Yehova ya wazi juu ya wale watendao dhambi?
6 Wale watakao kufurahia au kuendelea kufurahia kibali ya Mungu wamepaswa wayaangalie sana maneno ya Paulo kwa makundi ya Galatia: “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa [roho], katika [roho] atavuna uzima wa milele.” (Gal. 6:7, 8) Mungu husamehe dhambi na kuwarehemu na kuwahurumia watoto wa Adamu waliozaliwa dhambini. (Zab. 51:5) Walakini, Mungu wa kweli alijifunua kwa Musa kama “Yehova, Mungu mwenye rehema na fadhili, . . . mwenye kusamehe kosa na uasi na dhambi, lakini hatakosa kwa vyo vyote kutoa adhabu.” (Kut. 34:6, 7, NW). Hata kwa habari ya Mfalme Daudi, ambaye Yehova alifanya naye agano la ufalme, Mungu hakumtofautisha na watu wengine. Daudi aliadhibiwa kwa sababu ya dhambi zake, lakini kwa sababu alitubu alisamehewa pia kwa rehema. Walakini, msamaha wa Yehova hauwafikii wale wanaovunja kanuni zake za haki kwa makusudi ambazo kiti chake mwenyewe cha enzi kinazitegemea, wala wale wanaofanya kutenda dhambi njia ya maisha. (Linganisha Waebrania 1:8, 9.) Sivyo ilivyo. Cheo chake ni cha ukatili mwingi kwa hao na hawawezi kwa vyo vyote kuepuka hukumu aliyowawekea akibani.
7. Ni nia gani ifaayo ipaswayo kufuatwa juu ya rehema ya Yehova, lakini wengine wanaionaje?
7 Hii isitufanye tukate maneno kwamba Yehova si Mungu wa subira na uvumilivu. Kulingana na ushuhuda wake mwenyewe, katika kushughulika na taifa la Israeli nyakati zilizopita, asema hivi: “Sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi.” (Eze. 33:11) Na, ijapokuwa waovu wengine wanaitumia subira yake kwa upumbavu, hata kulidhihaki onyo la kwamba siku moja uvumilivu wake utafikia kikomo, yeye anaendelea kuvumilia hili ili wale walio na mioyo minyofu wapate kumwelekea yeye na kuokolewa.—2 Pet. 3:3, 4, 9, 15; Rum. 2:4.
8. Uvumilivu wa Yehova unafaidije wanadamu wote?
8 Wanadamu wote, hata waovu, wanafaidika kutokana na rehema ya Mungu. Yeye hawanyimi vitu vilivyo vya lazima kwa uhai. Yesu aliitaja sifa hii ya fadhili zisizostahili za Yehova kama mfano kwetu, akitukumbusha kwamba Baba yetu wa kimbinguni “huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” (Mt. 5:45) Na Adamu na Hawa walipoiasi sheria ya Mungu wakala katika mti wa maarifa ya mema na mabaya katika Bustani ya Edeni, rehema kwa wazao wao wasiozaliwa ilimfanya Yehova awaruhusu waishi mpaka watoto wao wamezaliwa.
9. Mamilioni yasiyohesabika ya watu wamekitumiaje kipindi cha uvumilivu wa Yehova, nao mwisho wao utakuwaje?
9 Wengi wamezikubali fadhili zisizostahili na uvumilivu wa Yehova unaoendelea kuwapo nao hawakukosa kusudi lake, lakini, kwa upande mwingine, mamilioni yasiyohesabika tangu siku za Adamu wamekitumia kipindi hiki cha katikati, kipindi cha uvumilivu wa Yehova, kama nafasi ya kuishi kumpinga Mungu na kuzoea namna zote za matendo maovu yasiyopatana na mapenzi ya Mungu yaliyotajwa kwa viumbe vyake. (2 Kor. 6:1; Rum. 1:28-32) Lakini Mungu hana lazima ya kuwavumilia kwa wakati usiojulikana kama asivyokuwa na lazima kwa Adamu na Hawa, walioshuka kuingia katika mauti ya milele katika wakati wake, sawa na Yehova alivyokuwa amewaagiza. (Mwa. 3:19; 5:5) Kipindi cha uvumilivu wa Yehova kinakaribia kikomo. Kitakapokwisha, majeshi ya kimalaika ya Yehova yataingia katika kazi yao waliyogawiwa ya kuua, nayo rehema ya Yehova haitawafunika wale watakaopatikana wakijitia bado katika matendo yao ya uasi, wasiogeuka na kupokea alama ya wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo. (Eze. 9:5, 6) Wakati huo utakapofika, je! rehema ya Mungu itafunika dhambi zote zako wewe?
KUKESHA KWENYE KUENDELEA KWAHITAJIWA
10. (a) Imewapasa wale walio wakf na waliobatizwa waioneje rehema ya Mungu inayoendelea kwa ajili yao? (b) Wanaweza kupata faraja gani katika maneno ya Yohana katika 1 Yohana 2:1-6?
10 Ikiwa wewe hujapata bado kuyajua na kuyakubali maagizo ya Yehova kama njia ya maisha, usipoteze wakati. Lazima utende kwa haraka ikiwa utasimama mbele ya majeshi ya Yehova ya kufisha ukiwa na alama ya kitambulisho cha kweli cha Kikristo. Hata hivyo, wako wengi wanaosoma kurasa hizi ambao wamekwisha tambua hali yao yenye dhambi mbele za Mungu na waliotubia njia mbaya hii na kugeuka, wakiukubali mpango wa Mungu wa upatanisho, zawadi ya Mungu kwa wanadamu isiyoelezeka, dhabihu ya Mwanawe mpendwa. Je! basi hii inawahakikishia kabisa kibali ya Mungu yenye kuendelea, rehema yake isiyobadilika kwa ajili yao? Wale waliojiweka wakf kwa Mungu wakaonyesha tendo hili kwa ubatizo wa maji wanajua kwamba kukesha kwenye kuendelea kwahitajiwa. (1 Kor. 10:12) Wakijua wao si wakamilifu, wanalitambua pigano lililomo ndani yao, hivi kwamba kwa mwili ni watumwa kwa sheria ya dhambi ingawa kwa akili wao ni watumwa kwa sheria ya Mungu. (Rum. 7:25) Wanajua kuna makosa ya uzito mbalimbali na kwamba dhambi zaweza kuwa za namna mbalimbali—dhambi juu ya wanadamu, dhambi juu ya Mungu na Kristo, dhambi juu ya mwili wa mtu mwenyewe, dhambi kwa kushiriki dhambi za wengine, na makosa mengine mengi ya namna hiyo. Walakini, wanafarijiwa na maneno haya ya Yohana: “Kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote. Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.”—1 Yohana 2:1-6.
11. Twawezaje kuonyesha kutokana na maneno ya Yesu kwamba kutumia vibaya utendaji wa kila siku kwaweza kutufanya tutoke katika njia ya uzima?
11 Wale waliomo katika njia ya uzima wanategemea rehema ya Mungu inayoonyeshwa kupitia kwa Yesu Kristo kwa matumaini nao watajitahidi kutembea katika njia ya Huyo. Lakini hata ingawa wanaziepuka dhambi nzito ambazo kwa wazi zingewatoa chini ya rehema ya Mungu, wanajua kwamba kuna matendo mengi ya kufanya au yasiyo ya kufanya yanayoweza kuhatirisha sana hali yao na Mungu. Kwa mfano, wanajua kwamba Yesu hakuwahesabia wanafunzi wake mabaya, lakini aliwaonya wawe waangalifu wasitumie vibaya utendaji fulani wa kila siku ambao ungeweza kuwafanya watoke katika njia ya uzima. Yesu alisema: “Jiangalieni ili mioyo yenu isije ikalemewa na kula kupita kiasi na kunywa kupita kiasi na masumbufu ya maisha, na kwa ghafula siku ile [ya kufikiliza kwa Mungu hukumu] iwazukie kama mtego.” (Luka 21:34, 35, NW) Kwa hiyo wale watakao kufuata hatua za Yesu karibu karibu wanajua kwamba hakuna jambo liwezalo kusahauliwa au kuonwa kama lisilo na maana sana kutoweza kukaziwa fikira zao zenye shauku na bidii.
12. Kwa sababu gani twapaswa tufikirie kwa uzito sisi twasamehe wengine kwa kadiri gani? Toa shauri la Maandiko.
12 Basi je!, tukiwa na onyo hili la Yesu lenye kuchochea mbele yetu, twaweza kuyapuza au kuyadharau maneno ambayo Yesu alitufundisha kusali: “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu”? Je! kwa unyofu na ufahamu unatoa ombi hili kwa Mungu? Haya si maneno ya kudharauliwa. Yesu aliongeza: “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.” (Mt. 6:12, 14, 15) Yesu aliendelea kuonya: “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”—Mt. 7:1-5.
SIFA IFAAYO YA REHEMA
13. Neno “rehema” lina maana gani mbalimbali kama lilivyotumiwa katika Maandiko?
13 Kuzoea rehema, kama vile neno hili linavyotumiwa katika Kiswahili, mara nyingi sana kunamaanisha kujizuia, kama vile katika kutoa adhabu, kujizuia huku kukivutwa na huruma na utu mwema. Nalo latumiwa kwa njia hii katika Biblia. Kuzoea rehema kwa Mungu sikuzote kunapatana na sifa zake nyingine na kanuni za haki, pamoja na uadilifu wake na ukweli. (Zab. 40:11; Hos. 2:19) Na kwa kuwa wanadamu wote ni wenye dhambi kwa urithi na wanapokea malipo ya dhambi mauti, ni wazi kwamba kusamehe makosa, au kupunguza hukumu au adhabu, mara kwa mara kunahusika katika kuzoea rehema kwa Mungu. Walakini, maneno ya Kiebrania na Kigiriki hayana maana ya kusamehe tu au kujizuia katika kutoa adhabu ya hukumu. Mara nyingi, rehema haimaanishi tendo lisilofaa, kuzuia (kama vile adhabu), bali tendo lifaalo, wonyesho wa huruma unaowaletea faraja wenye udhaifu na wanaohitaji rehema. Kwa hiyo, kama iwezavyo kutazamiwa, Maandiko yanaonyesha kwamba rehema ya Yehova Mungu si sifa inayotumika wakati tu watu ‘wanapohukumiwa’ mbele zake sababu wamefanya kosa fulani. Bali, ni sifa ya utu wa Mungu hasa, njia yake ya kawaida ya kuwaitikia walio na shida, sehemu ya upendo wake.—2 Kor. 1:3; 1 Yohana 4:8.
14. Matendo ya Yesu ya rehema yakaziaje maana ya neno hilo?
14 Ndivyo ilivyo na kwa Yesu. Yeye hakufanya matendo yake ya rehema kwa wale waliopinga au waliomkosea peke yao. Vipofu, wenye kupagawa na mashetani, wenye ukoma, na wale ambao watoto wao walikuwa wagonjwa walikuwamo kati ya wale walioonyeshwa naye rehema na huruma. (Mt. 9:27; 15:22; 17:15; Marko 5:18, 19; Luka 17:12, 13) Kwa kulijibu ombi, “Uturehemu,” Yesu alifanya miujiza akawakomboa hao. Alifanya hivyo, si kwa njia ya kawaida tu, njia ya ubaridi, bali kwa sababu ya ‘kuwahurumia.’—Mt. 20:33, 34.
15. Yohana analinganishaje upendo wa Mungu na ule wetu?
15 Je! hii haiyapi maneno ya ndugu wa mama-mzazi mmoja na Yesu Yakobo maana zaidi, aliyeonya hivi: “Kwa maana yeye asiyezoea rehema atapata hukumu yake bila rehema”? (Yak. 2:13, NW) Rehema ya Mungu kwetu sisi ni kubwa sana hata tunalazimika kuzoea rehema kwa wenzetu, hata tuwe tutaionyesha kwa njia ndogo namna gani ikilinganishwa na yake. Yohana alisema hivi: “Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.”—1 Yohana 4:7-11.
UMBALI AMBAO REHEMA YA MUNGU INAFIKA
16. Rehema ya Mungu kwetu yalinganaje na rehema tuwezayo kuonyesha, naye Yesu alionyeshaje hili katika Mathayo 18:23-35?
16 Huenda hii ikaonekana vigumu nyakati nyingine nayo makosa au yanayoelekea kuwa makosa ya ndugu zetu wa Kikristo huenda yakawa ya namna ambayo tunaelekea kuliachilia mbali takwa hili la kuonyesha upendo na kupanua rehema, kwa akili zetu wenyewe tukifikiri kwamba kwa kweli Yesu hakumaanisha imetupasa tusahau makosa “mabaya sana” ya wengine. Lakini Paulo anaukuza upendo wa Mungu juu ya wo wote tuwezao kuonyesha aliposema hivi: “Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Rum. 5:8) Dhambi ambazo Mungu ametusamehe sisi ni kubwa zaidi namna gani kuliko zo zote tuwezazo kutakiwa tuwasamehe ndugu zetu wa Kikristo! Nao uhitaji wetu wa rehema ya Mungu katika kutoa njia ya ukombozi hauwezi kulinganishwa na mahitaji ya ndugu zetu tuwezayo kutimiza. Je! ni ajabu kwamba rehema ya Mungu haiwezi kufikishwa kwa wale wasio na rehema?—Kol. 3:13; linganisha Mathayo 18:23-35.
17. Ingawa tuko wakf, twawezaje bado kuingia hukumuni, lakini Yakobo atoa uhakikisho gani?
17 Basi, tunalopaswa kuangalia kwa uzito sana ni ulizo hili: Je! rehema ya Mungu inafunika dhambi zangu zote? Ikiwa nimejiweka wakf kwa Yehova Mungu na kuuonyesha kwa ubatizo wa maji, nikifanya ombi kwa Mungu la dhamiri njema, ningali naweza kuja chini ya hukumu ya Mungu kwa kukosa kuzoea rehema, upendo kwa wengine? (1 Kor. 13:1-3) Yakobo alionya hivi, kama ilivyotajwa tayari: “Kwa maana yeye asiyezoea rehema atapata hukumu yake bila rehema.” Walakini, Yakobo aliongeza uhakikisho wenye kufariji kwa onyo hili: “Rehema yashangilia hukumu kwa ushindi.” (Yak. 2:13, NW) Kwa njia gani? Na ni kwa njia gani iwezayo kutuleta hukumuni tuwezavyo kushindwa kuzoea rehema hata sasa, kabla ya Siku ya Hukumu?
18. Ni mfano gani wa rehema uwezao kufikiriwa unafuata kielelezo gani cha rehema na katika mambo gani?
18 Mfano mmoja wa kutokeza wa rehema, iliyozoewa kabisa kama neno lenyewe linavyomaanisha, ni ule ulioonyeshwa na Yusufu, mwana mwenye kupendelewa wa Yakobo. Lakini Yusufu alikuwa akifuata kielelezo ambacho Yehova Mungu mwenyewe alikuwa akionyesha wakati ule ule, katika rehema aliyoionyesha. Kama Yusufu alijua mwanzoni kadiri yote ya rehema ya Mungu iliyoonyeshwa kwake na nyumba ya baba yake, masimulizi ya Biblia hayasemi. Lakini Yusufu alikuwa akiutegemea ukombozi wa Yehova kabisa naye hakuyumba-yumba hata kidogo katika uamuzi wake wa kufuata uongozi wa Yehova na kushikamana sana na matakwa yenye haki ya Yehova aliyokuwa amejifunza kwa baba yake Yakobo. Naye Yusufu alipokuwa na shida kubwa zaidi, rehema ambayo Yehova alimwonyesha sikuzote ilimsaidia na, katika wakati wake, ilimweka katika cheo cha pili kwa ukubwa katika ulimwengu wa siku zake, cheo cha uwezo mwingi sana hata angeweza kujilipiza kisasi bila kujiona mwenye hatia juu ya wote waliokuwa wamemtenda vibaya. Au, angeweza kutumia cheo chake awe baraka kuu kwao. Yusufu alizoea rehema, si kwa wale wenye hatia ya kosa tu, bali pia kwa huruma na kuwafikiria wenye shida, nayo hadithi hii ya maisha ya kweli iwezavyo kutuonyesha namna ‘rehema inavyoshangilia hukumu kwa ushindi,’ twaiachia makala ifuatayo ionyeshe. Kusoma kwa uangalifu Mwanzo, sura 37 mpaka 47, kabla ya kuziangalia kurasa hizi, kutapendeza na kufundisha sana.
[Picha katika ukurasa wa 76]
Kwa rehema, Yesu aliwaponya wagonjwa wa kimwili na wa kiroho pia, ijapokuwa hakuachilia dhambi