Mfano wa Unabii Uliofananisha Wokovu
1. Kwa sababu gani dunia ilikuwa imekuwa mahali pa hatari kuishi katika mwaka wa elfu mbili wa kuwako kwa mwanadamu?
HUKO nyuma, zamani za kale, katika mwaka wa elfu mbili wa kuwako kwa mwanadamu, dunia ilikuwa imekuwa mahali pa hatari kuishi. Ndiyo, kama ilivyo kwetu leo, ilikuwa kwa sababu jeuri ilikuwa ikiijaza dunia. Hiyo ilikuwa hivyo, ingawa watu huko nyuma hawakuwa na bastola na mizinga na silaha za atomiki. Mungu alikuwa ametangulia kujua mambo yatakavyokuwa wakati wa kipindi hicho cha kale, na hivyo ndivyo yeye alivyoieleza hali ya ulimwengu. Zaidi ya karne moja kabla ya hali iliyo mbaya zaidi katika mambo ya kibinadamu kufikiwa, aliamua kuchukua hatua ifaayo naye akaweka wakati barabara wa kuichukua.
2. Mungu alikiwekea kizazi hicho kilichokuwa kimeishi muda mrefu ukomo gani wa wakati, kipatwe na kifo cha namna gani?
2 Katika maneno yaliyosemwa kwa mwanadamu, Mungu alisema hivi: “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.” (Mwa. 6:3) Yeye asingetenda kwa uvumilivu kuelekea kizazi hicho kilichoendelea kuishi muda mrefu kwa wakati usiojulikana, bali sasa aliweka ukomo wa kizazi hicho kiingie katika udhilifu wake zaidi na zaidi, kiwe tofauti sana na mfano na sura ya Mungu ambayo kwayo alikuwa amemwumba mwanadamu wa kwanza mwenye nyama na damu. Makumi kumi na mawili ya miaka yangeruhusiwa kabla hakujawa na “tendo la Mungu” la ulimwenguni pote. Kizazi hicho kisingekufa kifo cha asili!
3. Mungu alisema nini juu ya ubaya wa wanadamu wakati huo, nasi twauliza ulizo gani juu ya kizazi chetu kikilinganishwa na cha wakati huo?
3 Ebu na tukilinganishe kizazi cha sasa cha kibinadamu kwa habari ya adili yake na hicho cha wakati huo, tunaposoma sasa namna Mungu alivyoiona hali ya wanadamu, ambao yeye ndiye aliyewaumba: “[Yehova] akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. [Yehova] akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. [Yehova] akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. . . . Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.” (Mwa. 6:5-7, 13) Je! twaweza kusema kwamba kizazi cha wanadamu cha sasa ni bora kuliko kile cha kale kinachosimuliwa hivyo, au kuna sababu yo yote kuamini kwamba ni kibaya hata zaidi?
4. Imetupasa tujiulize ulizo gani mmoja mmoja, nasi tusitazamie kuokoka tendo la Mungu la ulimwenguni pote tukifanya nini?
4 Si kwamba tunataka kulaani wengine kwa kujitakia haki wenyewe na kujisahau sisi wenyewe. Tuna wajibu wa kujiuliza wenyewe hivi: Je! mimi mwenyewe ni mpotovu kwa kadiri ya kizazi hicho cha kale? Imetupasa tujiulize wenyewe ulizo hilo mmoja mmoja, kwa maana tumo katika ulimwengu huu na twaishi na hiki kizazi cha sasa. Namna gani tukijikuta tu sehemu ya jamii hii ya ulimwengu na twapenda kuwa sehemu yake ijapokuwa kumbukumbu lake la kihistoria mpaka sasa? Basi, ikiwa kushikamana kwa Mungu na kanuni na mwendo ule ule sikuzote sasa kunamlazimisha achukue hatua kwa sababu ya kulingana kwa kizazi hiki na kile cha kale, hatuwezi kutazamia kuokoka wakati Muumba atakapofanya “tendo la Mungu” tena la ulimwenguni pote. Tusingeweza kutazamia wokovu. Tungetiwa katika jamii moja na wengine.
5. Ni jamaa gani iliyokuwa tofauti na jamii hiyo ya ulimwengu, nayo masimulizi ya Biblia yasema nini juu ya jamaa hiyo?
5 Bila shaka, si kila mtu nyuma huko aliyekuwa wa jamii hiyo potovu ya ulimwengu; ama sivyo, taifa la wanadamu lisingekuwapo leo. Ilikuwako jamaa iliyokuwa tofauti, naye Mungu aliijua. Jamaa iliyokuwa tofauti ilikuwa ile ya Nuhu, mwana wa Lameki, mwana wa Methusela. (Mwa. 5:25-32) Ebu na tuangalie tofauti kati ya Nuhu na jamii ya ulimwengu ya siku zake, kulingana na masimulizi haya ya Biblia: “Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu. Nuhu akazaa wana watatu wa kiume, Shemu na Hamu, na Yafethi. Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma. Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.” “[Yehova] akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.”—Mwa. 6:9-12; 7:1.
6. Nuhu hakutaka atiwe katika kikundi cha watu gani waliotajwa kwa unabii na Henoko, naye alitembeaje pamoja na Mungu wa kweli?
6 Nuhu alikumbuka yale ambayo babu yake Henoko alikuwa ametabiri chini ya uongozi wa roho: “Angalia, [Yehova] alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.” (Yuda 14, 15; Mwa. 5:18-24) Nuhu hakutaka apangwe katika kikundi hicho kisichomcha Mungu wa kweli, Yehova, kwa kuendelea kupatana naye. Alikuwa mwenye furaha kupatanisha mwendo wake wa maisha na kusudi la Mungu kwa kujithibitisha kuwa yeye ambaye kupitia kwake taifa la wanadamu la wazao wa Adamu na Hawa limepaswa lihifadhiwe kupita wakati ambapo “tendo la Mungu” la ulimwenguni pote lingefanywa. Kwa sababu ya Nuhu kupatanisha mwendo wake wa maisha na kusudi la Mungu, twajikuta tupo leo baada ya zaidi ya miaka elfu nne na mia tatu. Sisi leo tuna nafasi mbele yetu kama ile ya Nuhu.
7. Nuhu na nyumba yake waliokoka nini, kwa kupatanisha mwendo wake wa maisha na kusudi la Mungu kwa njia gani?
7 Je! twatambua Nuhu na jamaa yake, wote pamoja wakiwa nafsi nane za kibinadamu, waliokoka nini huko nyuma? Ulikuwa mwisho wa ulimwengu! Bila shaka gharika ya dunia nzima ya maji yaliyowafutilia mbali wapotovu wote, kizazi cha wanadamu wasiomcha Mungu watoke usoni pa dunia, haikuiharibu dunia yetu. Ingali hapa chini ya nyayo zetu. Ili kuishi kupita gharika hiyo ilimpasa Nuhu apatanishe mwendo wake wa tendo na kusudi la Mungu lisilobadilishwa kwa kuijenga safina ya ajabu kulingana na maagizo ya Mungu, nyumba yake ipate kuhifadhiwa na aina za msingi za wanyama wa nchi kavu na ndege wa angani. (Mwa. 6:14 mpaka 8:22) Uhakika wa kwamba Nuhu na jamaa yake waliokoka uharibifu wa ulimwengu unatajwa waziwazi chini ya uongozi wa kimungu katika maandiko yafuatayo yenye masimulizi:
8. Petro ashuhudiaje kwamba Nuhu na jamaa yake waliokoka uharibifu wa ulimwengu?
8 “Kwa maana ikiwa Mungu . . . hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu; . . . [Yehova] ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; . . . Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu; kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.”—2 Pet. 2:4-9; 3:5, 6.
WOKOVU WA UHARIBIFU WA ULIMWENGU
9. Ni kwa njia gani wokovu wa Nuhu na jamaa yake haukuwa mfano tu wa kuokoka uharibifu wa ulimwengu, na wokovu ambao watu walio wengi leo wanafikiria?
9 Yawezekana! Wokovu wa uharibifu wa ulimwengu wawezekana duniani! Wokovu wa Nuhu na jamaa yake kupita gharika ya dunia nzima ya miaka ya 2370-2369 B.C.E. ni mfano wa hili. Lakini, ni zaidi ya hilo! Ni unabii unaofananisha wokovu wa wengine hapa duniani wa uharibifu wa ulimwengu unaokaribia kasi, mwisho wa ulimwengu wa leo wa watu wasiomcha Mungu. Yamaanisha kuokoka kwao mwisho kamili wa taratibu hii mbovu ya mambo iliyochafuliwa. Watu walio wengi leo duniani wanaridhishwa na kuziokoka nyakati za sasa zenye magumu na kuishi kupita hatari moja ya ulimwengu baada ya nyingine na mwishowe wafe baada ya kutumainia nyakati bora, ambazo hawazioni kamwe. Huo ndio wokovu wa pekee wanaoujua au kuufikiria, wanapojaribu kutegemea uzima wa kibinadamu maadamu wanaweza. Hii hailingani na wokovu uliofananishwa na kupita kwa Nuhu akiwa salama katika gharika.
10. Wokovu ambao Mungu anatolea viumbe vya kibinadamu sana wamaanisha nini, nao utapatikana kwa njia gani, kama vile katika habari ya Nuhu?
10 Wokovu ambao sasa Mungu anavitolea viumbe vyake vya kibinadamu duniani ni wokovu wa mwisho wa taratibu hii mbovu ya mambo pamoja na nafasi ya waokokaji kuishi milele duniani chini ya taratibu Yake mpya ya mambo. Je! hilo si jambo linalostahili kuokokea? Lakini wokovu huu mzuri sana hautakuwa kwa kutumia njia zo zote za kujiokoa za kutungwa na wanadamu, wala hautakuwa wokovu wa walio katika hali nzuri zaidi ya kujikinga wenye maoni ya mageuzi. Tena, utakuwa kwa kupatanisha mwendo wa tendo wa mtu na kusudi la Mungu. Katika habari ya Nuhu, ilimpasa aonyeshe imani kuu katika onyo la Mungu kuhusu uharibifu wa “ulimwengu wa kale” (NW) na kufanya yale ambayo Mungu alimwambia ayafanye apate kujihifadhi mwenyewe na jamaa yake. Alipewa onyo wakati mwingi ukiwa umebaki. Katika karne ya sita ya maisha yake alipokuwa baba ya wana watatu waliooa ndipo alipoambiwa ajenge safina yenye nafasi tele, yenye kufaa kwa hali ya hewa wakati huo na ya mbao ambamo angejificha na maji ya gharika ya dunia nzima. Alitii.
11, 12. Kwa sababu gani safina ya mbao zisizopenywa na maji isingefaa kuokokea ‘dhiki kubwa’ inayokuja, kama ionyeshwavyo na maneno gani ya Petro?
11 Safina ya mbao isiyopenywa na maji ilifaa kuokokea mwisho wa “dunia ile ya wakati ule.” Safina hiyo isingefaa kwa “dhiki kubwa” itakayokomesha “ulimwengu” (NW) wa sasa au jamii ya kibinadamu. Si jamaa moja tu inayohusika. Wale wanaotumainia na kujitayarisha kuokoka wako katika sehemu zote za dunia yetu. Zaidi ya hayo, uharibifu kamili wa taratibu hii ya mambo hautakuwa kwa maji. Ndivyo Mungu alivyosema baada ya Gharika. (Mwa. 9:8-16; Isa. 54:9) Karne 24 baada ya uhakikisho huo kutoka kwa Mungu mtume Petro aliyeongozwa kwa roho aliandika barua yake ya mwisho na kusema hivi:
12 “Dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia. Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo [la Mungu], zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. . . . Siku ya [Yehova] itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.”—2 Pet. 3:6, 7, 10.
13. Gharika ya dunia nzima iliifanyia dunia nini, nao “moto” wa siku inayokuja ya hukumu utaifanyia nini?
13 Je! ingepatana na kusudi la kwanza la Mungu juu ya mwanadamu na makao yake ya kidunia kwa Mungu kuiteketeza dunia hii kwa moto halisi na kuifanya kaa lililochomwa lisilo na wakaaji? Hiyo ingemaanisha kwa Mungu kukubali kushindwa kwa kusudi lake na Adui wake Mkuu, Shetani Ibilisi. Hili halitatukia kamwe, kwa maana Mungu Mwenye Nguvu Zote aweza kutimiza kusudi lake likafanikiwe kwa njia ya utukufu. Gharika ya maji ya siku za Nuhu haikuiharibu dunia, bali ilifutilia mbali “ulimwengu wa watu wasiomcha Mungu” (NW) watoke usoni pa dunia na kuisafisha, ikaipa mwosho mzuri. Vivyo hivyo, moto wa siku ya Yehova, kuja kwa hukumu, hautaiharibu dunia, wala viumbe vyote vilivyomo, bali utaiharibu itoke usoni pa dunia jamii ya watu wasiomcha Mungu na pia matendo yao yasiyopatana na kusudi la Mungu. Sayari yetu ya kidunia na jua letu pia na mabilioni ya majua mengine katika kundi la nyota ndogo ndogo, ambayo tayari ni matufe ya moto, itaiokoka siku hiyo ya hukumu.
14. Ni moto wa namna gani utakaoweza kuziharibu “mbingu” na “nchi,” na kwa matokeo gani?
14 Moto wa halisi ulio wa kawaida kwa dunia yetu na jua letu na sayari nyingine usingeweza kamwe kumteketeza Shetani asiyeonekana na mashetani zake wa kiroho au kuwaharibu wasiwe mbingu zisizoonekana za kiroho ambazo zimetawala wanadamu tangu kufukuzwa kwa Adamu na Hawa kutoka Edeni mpaka sasa. Wingi wa maandiko ya Biblia waonyesha kwamba “moto” wa siku inayokuja ya hukumu ya ulimwengu ni wa mfano, lakini ni wenye kuharibu kama moto; na namna ambavyo moto wa halisi wa vitu kama vile umeme unavyoweza kutumiwa hasa siku hiyo na Yehova Mungu, hatujui sasa. Uwezo wa Yehova wa kufisha utamwondoa Shetani na mashetani zake kutoka cheo chao cha kimbinguni cha kusimamia wanadamu nao utaiharibu jamii ya kidunia (au, “ulimwengu,” NW) ya watu wasiomcha Mungu. Hivyo, tena dunia ya halisi itasafishwa kama vile dhahabu na fedha zinavyosafishwa na moto. Dunia ndipo itakapokuwa makao mazuri kwa waokokaji.
15. Mtume Petro atuhakikishiaje kwamba kutakuwa na jambo linalostahili kuokokewa?
15 Kwamba kutakuwa na kitu bora cha kuokokea, mtume Petro anatuhakikishia anapoendelea kusema hivi: ‘Mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka. Lakini, kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.’—2 Pet. 3:12, 13.
16. Katika mfano unaotimizwa sasa hivi, Nuhu, mke wake na wana wake watatu na wake zao walifananisha nani?
16 Sasa ulizo ni juu ya namna ya kuokoka na kuingia katika hiyo “nchi mpya” chini ya “mbingu mpya” za ufalme wa Kristo. Ili kuishi kupita uharibifu wa huo “ulimwengu wa kale” (NW), Nuhu aliijenga safina kama alivyoambiwa na Yehova Mungu. Kwa kupatanisha mwendo wake wa tendo na kusudi la Mungu la kuhifadhi taifa la kibinadamu, Nuhu na jamaa yake walikuwa mfano wa unabii wenye utimizo katika kizazi chetu. Kwa hiyo, Nuhu alimfananisha Yesu Kristo, na mkewe alimfananisha “Bibi arusi” wa Kristo, au, zaidi hasa, mabaki ya “Bibi arusi” mzima ambao wangali duniani. Wana watatu wa Nuhu na wake zao wanafananisha wale waabudu waliobatizwa wa Yehova Mungu ambao sasa wanashirikiana na mabaki ya jamii ya “Bibi arusi” na wanaotazamia kuwa watoto wa kidunia wa Baba wa Milele, Yesu Kristo, chini ya ufalme wake wa miaka elfu. (Isa. 9:6, 7) Katika mfano huu wa unabii kama unavyotimizwa kati ka siku ii hii yetu, je! safina ya Nuhu ya fananisha nini?
17. Safina ya Nuhu ilijengwa wakati gani, na kwa hiyo ifananisha nini leo?
17 Basi, Nuhu aliijenga safina kwa msaada wa wana wake waliooa, kwa muda unaopungua karne moja kabla gharika haijatokea. Kwa hiyo ujenzi wa safina ulitokea “wakati wa mwisho” wa huo “ulimwengu wa kale.” Kwa hiyo lazima tutazamie kitu cha pekee huu “wakati wa mwisho,” kitu ambacho kutokana nacho kizazi kilichopo cha wanadamu chaweza kufaidi wakati wa haraka ya nyakati. Kwa Andiko na utimizo wa unabii wa Biblia imethibitishwa vizuri kwamba “wakati wa mwisho” wa “ulimwengu” huu uliopo ulianza katika vuli ya mwaka wa 1914, wakati Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilipokuwa ikiendelea kwa nguvu. Safina ya Nuhu basi ingefananisha mpango wa wokovu ambao Mungu afanya kwa waabudu wake waaminifu kupitia kwa Kristo wakati mwisho wa taratibu hii ya mambo unapokaribia. Mpango huo wa kimungu ndiyo paradiso ya kiroho ambamo Mungu amewaingiza waabudu wake waaminifu tangu mwaka wa 1919 C.E., ambamo wanaishi kama watu wake waliorudishwa kwenye kibali yake na chini ya ulinzi wake.
18. Mabaki yenye kutubu wa jamii ya “Bibi-arusi” waliingizwa katika paradiso hii ya kiroho wakati gani, na kwa njia gani?
18 Paradiso hii ya kiroho ya amani na usalama bila shaka imekuzwa duniani tangu mwaka uliofuata vita wa 1919. Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza na nyakati zake zenye magumu na mateso kwa mashahidi wa Kikristo wa Yehova, wao walichochea hasira nyingi ya kimungu kwa sababu ya mwendo wao wa kuridhiana na makosa mengine kama Wakristo. Yehova Mungu aliwaacha waingizwe katika utumwa wa Babeli Mkuu wa kidini na hawara zake wa kisiasa, wa kijeshi na wa mahakma. Lakini katika mwaka uliofuata vita wa 1919 mabaki yenye kutubu waliamua kupatanisha mwendo wao wa tendo ulioungana na kusudi la Mungu lililofunuliwa kulingana na maarifa ya Biblia aliyoanza kuwafunulia. Kwa hiyo kwa neema Mungu alimtumia Mwanawe Yesu Kristo kama Koreshi wa kisasa awakomboe watu wake wenye kutubu kutoka uhamishoni chini ya Babeli Mkuu. (Isa. 44:28 mpaka 45:6) Baada ya kurudishwa kwao kwenye uhusiano wenye amani na Yehova Mungu katika mwaka wa 1919, kama ilivyokuwa kwa makao yao ya kiroho waliyopewa na Mungu, paradiso ya kiroho ilikuzwa, makundi mengi ya mashahidi wa Yehova wa Kikristo yakianzishwa katika dunia yote.—Isa. 35:1-10; Eze. 36:35.
19. Ni uzuri wa namna gani uliomo katika paradiso hii ya kiroho kwa wingi, nayo ni kama mji gani wa Israeli ya kale kwa wakaaji wake?
19 Humu katika paradiso hii ya kiroho, katikati ya “ulimwengu” huu uliohukumiwa na wenye kuchafuliwa, ndimo ulimo uzuri wa kweli wa kiroho, ambamo tunda la roho ya Mungu linakomaa. Ndimo amani na udugu wa kweli wa Kikristo ulimo, na kila mtu anajaribu kujenga wengine kiroho na kuwatayarisha kukutana na siku ya Yehova inayokaribia. (2 Pet. 3:14-18) Kwa hiyo, twaweza kusema, huu ndio ‘mji wa makimbilio,’ ambamo wamo salama kutoka kwa “mwenye kutwaa kisasi” Aliye Mkuu atakayefikiliza kisasi cha Yehova juu ya “ulimwengu” wote wenye hatia ya damu katika ‘siku ya hukumu ijayo, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.’—2 Pet. 3:7; Hes. 35:12, 19-27.
20. Ni nani wanaofananishwa na wana watatu wa Nuhu na wake zao, nao wokovu wao ulisemwaje kwa unabii katika Ufunuo?
20 Si mabaki ya “Bibi arusi” wa Kristo peke yao, waliofananishwa na mke wa Nuhu, wanaoikaa paradiso hii ya kiroho sasa, mahali hapa pa uhusiano uliorudishwa wenye amani na Mungu. Tangu mwaka wa 1935 wale ambao walifananishwa na wana wa Nuhu na wake za wana hawa wameingia katika paradiso hii ya kiroho. Hawa ndio wanaotazamia kuwa watoto wa kidunia wa Baba wa Milele, Yesu Kristo, Nuhu Mkuu. Wamewekewa nafasi ya kuiokoka ‘dhiki kubwa’ ya ulimwengu, inayokaribia sana, na kwa hiyo mfano wa unabii unaotolewa katika Ufunuo 7:9-17 unatumika kwao. Watatumiwa kuufanyiza “mkutano mkubwa,” ambao juu yake humo inasemwa hivi: “Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.” (Ufu. 7:14) Sasa wanajiunga na mabaki ya “Bibi arusi” wa Kristo kuabudu penye hekalu la kiroho la Mungu.
21. (a) Ili wale waliomo katika paradiso ya kiroho waiokoke ‘dhiki kubwa,’ lazima wafanye nini? (b) Ni viumbe vya namna gani vitakavyookoka pamoja nao?
21 Ili kuiokoka ‘dhiki kubwa’ wote wale ambao sasa wamo katika paradiso ya kiroho lazima wabaki humo, kama vile Nuhu na jamaa yake katika safina, ambayo mlango wake Mungu aliufunga kabla ya gharika kuuzukia ulimwengu. (Mwa. 7:1) Ni kwa kubaki tu katika mahali pa Mungu palipowekwa pa kibali, upendeleo na ulinzi wanavyoweza kutumainia kuuokoka uharibifu wenye moto wa taratibu ya mambo ya kilimwengu. Zitakuwako pia chini ya ulinzi wa Mungu pamoja nao namna za ndege, viumbe vyenye kuruka angani, wanyama wa nchi kavu na samaki na viumbe vingine vya baharini, kwa maana waokokaji wa kidunia wa ‘dhiki kubwa’ watalitimiza agizo la kimungu kutiisha namna hizi za chini za viumbe ili viumbe hivyo ya Mungu vilivyo hai vipate kuhifadhiwa.
22. (a) Katika gharika ya siku za Nuhu, ni nini kilichoipata Bustani ya Edeni? (b) Katika ‘dhiki kubwa’ inayokuja, ni nini kitakachoipata paradiso ya kiroho, na kwa sababu gani?
22 ‘Dhiki kubwa’ inayokuja itafikia upeo katika “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” yenye moto penye Har–Magedoni. (Mt. 24:21, 22; Ufu. 16:14-16) Ili waabudu wa Yehova, mashahidi wake wa Kikristo, wapite dhiki hiyo kwa usalama, safina yao ya mfano, paradiso ya kiroho, lazima iendelee kuwapo, nao wakae ndani. Katika gharika ya siku za Nuhu Bustani ya Edeni au Paradiso ya Furaha, ambayo kutoka kwayo Adamu na Hawa walikuwa wamekwisha fukuzwa, iliharibiwa. Lakini namna gani juu ya paradiso ya kiroho ya mabaki na “mkutano mkubwa”? Kama vile safina ya Nuhu, itaiokoka “siku ya hukumu” yenye moto. ‘Dhiki kubwa’ inayokaribia kutoka kwa Yehova Mungu haikusudiwa iiharibu paradiso ya kiroho ya waabudu Wake, ambao wamejitahidi kuhifadhi hali yao ya kiroho na ukamilifu wa Kikristo. Imekusudiwa iiharibu taratibu ya mambo isiyo mfano wa paradiso. Baada ya paradiso ya kiroho kuiokoka ‘dhiki kubwa,’ waabudu wenye kuokoka wa Yehova, Mungu wa Nuhu, watatia jitihada zao wairudishe paradiso ya halisi kwenye dunia itakayosafishwa chini ya “mbingu mpya” za ufalme wa Mungu wa Kimasihi.
23. Ni nini kionyeshacho kwamba Adamu na Hawa hawakuelekezwa kwenye maisha ya kujikalia tu, na kwa hiyo namna gani wale ambao sasa wamo katika paradiso ya kiroho?
23 Uzima katika paradiso ya kiroho huu “wakati wa mwisho” si uzima wa kujikalia tu bila jambo la kufanya kwa wale wenye kufurahia upendeleo wa Mungu na ulinzi humo. Kuishi humo kuna kusudi kulingana na mapenzi ya Mungu. Mwanzoni mwa kuwako kwa mwanadamu, Mungu alimweka Adamu katika iliyokuwa paradiso ya kidunia hapo kwanza au “bustani ya Edeni,” si ajikaliekalie na kupoteza wakati wake kivivu, bali ‘ailime na kuitunza.’ Mungu alitia kusudi katika maisha za Adamu na Hawa kwa kuwapa agizo la kukuza jamaa ambayo kwa muda wa miaka elfu saba ingeijaza dunia yote na kuifanya dunia yote kuwa bustani ya Paradiso na kutiisha namna zote za chini za viumbe kwa njia yenye manufaa. (Mwa. 2:15; 1:26-28) Kwa hiyo, pia, katika paradiso ya kiroho tangu mwaka wa 1919 C.E. kuna kazi ya kufanya ya ulimwenguni pote, kabla ya ‘dhiki kubwa.’ Wale wanaokaa humo lazima wapatanishe mwendo wao na kusudi la Mungu.
24. (a) Wale waliomo katika paradiso ya kiroho sasa wanajaribu kufanya nini? (b) Kupatana na kusudi hilo, lazima sasa washiriki katika kazi gani?
24 Wale ambao sasa Mungu anawakubali waingie katika paradiso hii ya duniani hawatafuti mahali pa salama tu na wokovu wakati wa ‘dhiki kubwa’ inayokuja. Wanajaribu kuwa wenye kustahili na kujitayarisha kwa uzima wa milele katika kipindi chenye haki cha Mungu cha “mbingu mpya na nchi mpya.” (2 Pet. 3:13) Wanajua sana kwamba ni kusudi la Mungu kuleta kipindi hiki chenye amani na chenye haki cha ufalme wake wa Kimasihi ulio mikononi mwa Mwanawe aliyetawazwa, Yesu Kristo. Kupatana na kusudi hilo la Mungu, lazima washiriki katika utimizo wa unabii wa Yesu juu ya “mwisho wa taratibu ya mambo,” yaani, “Habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.” Pia, lazima watii amri ya moja kwa moja ya Kristo kwao, ‘kufanya wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote, kuwabatiza.’ (Mt. 24:14; 28:19, 20, NW) Kwa njia hiyo watafutaji wengi wa Mungu wanaingizwa ndani ya paradiso yake ya kiroho iliyo salama wapate wokovu na uzima katika kipindi Chake kipya chenye haki.
25. Ikiwa twataka kuokoka na kuishi katika taratibu mpya ya Mungu, lazima tufanye nini sasa?
25 Je! twataka tuiokoke ‘dhiki kubwa’ na kuishi milele tukiwa chini ya ulinzi wa “mbingu mpya na nchi mpya” za Mungu zilizoahidiwa? Ili kufanya hivyo, lazima tujipatanishe sasa na kusudi la Mungu.
—Kutoka The Watchtower, Nov. 1, 1974.
[Picha katika ukurasa wa 208]
Safina yafananisha paradiso ya kiroho ambamo Mungu ameleta waabudu wake leo
Nuhu amfananisha Yesu Kristo
Mke wa Nuhu afananisha “Bibi-arusi” wa Kristo
Wana wa Nuhu na wake zao wafananisha waabudu wa Yehova leo wenye tumaini la kupata uzima wa milele duniani