Usiogope
“[Yehova] ndiye anisaidiaye, Sitaogopa; mwanadamu atanitenda nini?”—Ebr. 13:6.
1. (a) Kwa karne nyingi, ni nini kimetawala maisha za watu wengi? (b) Kujiacha kwa Wakristo wa kweli wapatwe na woga huo kwaweza kuwa na matokeo gani juu yao?
KWA KARNE nyingi maisha za watu wengi zimetawalwa na woga wa kudhani watashindwa kujiruzuku wao wenyewe na jamaa zao. Kwa kuwa woga huu unaweza kuleta uharibifu wa kiroho, unapaswa kuzuiwa na watumishi wa Yehova Mungu. Walakini, sikuzote si vyepesi kufanya hivyo. Zaidi ya kupatwa na matatizo yale yale yanayopata watu wengine kujiruzuku, huenda Wakristo wa kweli wakapatwa na mikazo zaidi ya ulimwengu kwa sababu wanashikamana na Neno la Mungu kwa uaminifu.
2. Madai ya tajiri wa kazi yawezaje kuletea Mkristo matatizo?
2 Mtumishi wa Yehova ajua kwamba Biblia yakataza kusema uongo na huamuru tujitenge na ulimwengu na njia zake. (Kol. 3:9; Yak. 4:4) Lakini huenda tajiri wake akataka amsemee uongo, apotoe mambo, atie watu moyo wafuate roho ya kilimwengu ya kuadhimisha sikukuu, aingie katika siasa, au mambo kama hayo. Huenda mtu huyo akatishwa kwamba atapoteza kazi yake asipofanya aombwavyo na tajiri wake.
3. Huenda Mkristo anayeendesha biashara akakabiliwa na vishawishi gani?
3 Huenda Mkristo akawa anaendesha biashara na kuona inaendelea kuwa vigumu zaidi kujiruzuku. Huenda akashawishwa aingie katika mazoea ya kichinichini ya biashara au aseme uongo juu ya mapato yake ili asitozwe kodi. Ingawa huenda wengine wakawa wanafanya mambo hayo, mtu anayetaka kumpendeza Yehova ajua kwamba kujiachilia ashawishwe ni kosa. Biblia yasema: “Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani . . . Mizani ya haki, vipimo vya haki . . . ndivyo mtakavyokuwa navyo.” (Law. 19:35, 36) “Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru.”—Rum. 13:7.
4. Huenda mtu akajuaje juu ya kazi yake baada ya kujifunza Biblia kwa muda?
4 Kwa kujifunza Biblia na mmoja wa mashahidi wa Yehova wa Kikristo, huenda mtu akajua kwamba analofanya ajipatie riziki lavunja kanuni za Maandiko. Hiyo inatokeza tatizo halisi. Huenda ikawa vigumu kwake kupata kazi nyingine. Kuacha kazi yake na kuanza nyingine huenda kukafanya apate mshahara wa chini zaidi na kupoteza faida za bima, afya na malipo ya uzeeni.
5. Hatua zinazochukuliwa na serikali zaweza kuelekeaje kuharibu uchumi wa mtu?
5 Kwa sababu ya marufuku zinazopigwa na serikali, huenda nyakati nyingine Wakristo wa kweli wakaelekea kulazimishwa waache kazi. Huenda serikali ikadai watii na kuunga mkono isivyofaa chama cha kisiasa kinachotawala. Kwa njia hiyo, huenda serikali ikadai iabudiwe. Ufunuo 13:16, 17 waonyesha kwamba ingekuwa hivyo ulimwenguni, na hapo twasoma juu ya “mnyama,” au taratibu ya kisiasa ya ulimwengu, na twasoma kwamba watu wote wangelazimishwa, “wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.”
JINSI YA KUZUIA MKAZO
6. Ni maoni gani juu ya vitu vya kimwili yatakayotusaidia tuzuie kishawishi cha kukubaliana na wapinzani kwa tumaini la kuhifadhi riziki yetu?
6 Njia moja ya kusaidia mtu azuie mkazo wa kuacha yaliyo haki kwa tumaini la kuhifadhi riziki yake ni kukadiri vitu vya kimwili ifaavyo. Katika Waebrania 13:5, kitiamoyo hiki chatolewa: “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo.” Mtu akiridhika na “nguo na chakula” hatahangaikia hasara atakazopata ikiwa lazima atafute kazi nyingine. (1 Tim. 6:8) Pia, kuridhika na mambo ya lazima kutampa kazi za namna nyingi ambazo kwazo aweza kuchagua atakayo. Hata ikiwa anayoweza kupata ni kazi ya mshahara mdogo tu, hapaswi kuikataa ati kwa sababu anaona hailingani na cheo chake. Apaswa kuwa na nia ya kujaribu hata kazi za kujiandika mwenyewe zinazoelekea kuwa ovyo sana machoni pa wengine.
7. Msaada ulio mkubwa zaidi ni nini katika kuepuka kuacha yaliyo haki mtu anapopatwa na mkazo wa uchumi?
7 Walakini, msaada ulio bora zaidi katika kuzuia kishawishi cha kuacha yaliyo haki unapopatwa na mkazo wa uchumi ni kuwa na imani isiyotikisika kwamba Yehova aweza kuruzuku wale wanaompenda. Baada ya kukazia nia inayofaa kuwa nayo juu ya vitu vya kimwili, Waebrania 13:5, 6 yaendelea kusema hivi: “[Mungu] amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, [Yehova] ndiye anisaidiaye, sitaogopa; mwanadamu atanitenda nini?”
8. Kwa sababu gani mtu asione amepoteza riziki akipoteza kazi kwa ajili ya Ufalme?
8 Ingawa wanadamu wanafanya mtu apoteze kazi, hawawezi kuzuia Yehova Mungu asijibu ombi hili, “Utupe leo riziki yetu.” (Mt. 6:11) Kupoteza faida fulani za kimwili hakumaanishi bila shaka mtu atapoteza riziki yake. Kwa kweli, Yesu Kristo alimpasisha Baba yake kuangalia wale wanaotanguliza faida za kiroho na kushikamana kwa uaminifu na kanuni ya Mungu ya yaliyo haki. Alisema: “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? au Tunywe nini? au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho.”—Mt. 6:31-34.
9. Kwa sababu gani si jambo la akili mtu kuwa na wasiwasi isivyofaa juu ya kesho?
9 Kupatana na maneno ya Yesu, yatupasa tukumbuke kwamba kila siku ina matatizo yake yenyewe. Kwa hiyo mtu hapaswi kuongeza matatizo hayo kwa kuwa na wasiwasi usiofaa juu ya kesho. Hata mtu hawezi kuwa na hakika kabisa kwamba atakuwa hai kesho! Hakuna kitu katika mazingira ya sasa ya kibinadamu kinachodumu sana. Ugonjwa, tukio lisilotazamiwa na kifo yanaweza kuleta upesi mabadiliko yanayoweza kubadili kawaida yote ya maisha. Ulimwengu wa wanadamu unafanana sana na jukwaa, ambapo tamasha za maonyesho hubadilikabadilika haraka. Ni kama vile mtume Paulo alivyowaandikia Wakorintho: “Tamasha ya ulimwengu huu inabadilika.” (1 Kor. 7:31, NW) Bila shaka, sana sana mtu atakuwa hai kesho. Hata hivyo, kuwa kwake na wasiwasi bila sababu juu ya mambo yatakayotukia kesho hakutafanya mambo yawe afadhali. Ikiwa yeye ni mtumishi wa Yehova, anaweza kuwa na hakika kwamba Mungu wake atamwezesha kutatua matatizo ya maisha.
10. Yatupasa tufikirie nini uhai wetu ukielekea kumalizwa?
10 Lakini namna gani mikazo ikiwa mingi sana hata ielekee kumaliza uhai wa mtu wenyewe? Ikiwa hivyo, onyo la upole la Yesu Kristo, linalopatikana katika Mathayo 10:28 litatumika: “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na [nafsi]; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na [nafsi] pia katika jehanum.” Marufuku au mateso yakitia riziki ya Mkristo hatarini, akiacha yaliyo haki bado atapoteza uzima. Huenda akapata faraja ya muda katika hali yenye magumu sana. Lakini aweza kupoteza haki yake ya kuishi kisha aingie katika uharibifu wa milele. Akitoweka wakati hukumu ya kimungu ifikilizwapo au akifa kabla ya wakati huo akiwa katika hali ya kutoshikamana na Mungu na Kristo, atapoteza tumaini la kufufuliwa kwa wafu, asitazamie uzima wa milele. Kwa upande mwingine, mtu afaye akiwa ameendelea kuwa mkamilifu anahakikishiwa kwamba atafufuliwa kwa wafu. Hakuna mwanadamu anayeweza kuzuia Mungu asifufue mtu huyo. Hata mambo yaelekee kuwa magumu namna gani, mkono wa Yehova haukatwi ukafupika. Matendo yake ya zamani akiwa Mpaji wa watu wake yahakikisha hilo kabisa.
MATENDO YA ZAMANI YA MUNGU KAMA MPAJI
11. Daudi alikabiliwa na hali gani alipochukiwa na Mfalme Sauli?
11 Chukua mfano wa mtumishi mwaminifu wa Yehova, Daudi. Mfalme Sauli aliona wivu mwingi sana akapanga kumwua Daudi kwa sababu alipendwa na kujulikana na watu wengi. Ingawa majaribio ya Sauli ya kuua Daudi yalikosa kufanikiwa mara nyingi, Daudi alilazimika kukimbia akaokoe uhai wake, na baadaye watu mia nne wakajiunga naye. (1 Sam. 22:1, 2) Mwisraeli ye yote aliposaidia Daudi na watu wake alichukiwa na Mfalme Sauli, kwa maana Daudi na watu wake walikuwa kama maharamia. Inaweza kuonekana vile Sauli alivyoona watu wo wote wenye kuunga Daudi mkono kutokana na yaliyompata Kuhani Mkuu Ahimeleki na jamaa yake. Ahimeleki alimpa Daudi mkate na upanga akidhani alikuwa katika utumishi wa Mfalme Sauli. Sauli aliamuru Ahimeleki na jamaa yake wauawe kwa sababu ya kufanya hivyo. Mwana mmoja tu, Abiathari, ndiye aliyeokoka.—1 Sam. 22:9-20.
12. Je! nia ya Mfalme Sauli ilizuia Yehova asitumie Waisraeli mmoja mmoja wasaidie Daudi na watu wake?
12 Walakini, uchungu wa Sauli na Waisraeli wengine haukuzuia Yehova asitumie watu mmoja mmoja wasaidie watu wake. Hii inaonyeshwa vizuri katika kisa kinachohusu tajiri Nabali na mkewe Abigaili. Daudi na watu wake walikuwa wamelinda kundi la Nabali na wachungaji wake hata hawakupata hasara. Daudi na washirika wake walikuwa na haki ya kufanyiwa ukarimu kwa sababu ya utumishi huo. Lakini, wakati Daudi alipotuma wajumbe kwa Nabali, akiomba misaada yo yote ambayo Nabali angekuwa na nia ya kumpa, Nabali alimtolea makelele akimkemea. Lakini Abigaili alimpelekea Daudi msaada kwa ushujaa, akitambua kwamba ndiye aliyekuwa amechaguliwa na Mungu awe mfalme. Alifanya haraka akamkusanyia yeye na watu wake misaada mingi. Hivyo, kwa kumtumia Abigaili, Yehova aliwapa vitu walivyohitaji.—1 Sam. 25:9-19, 23-31.
13. Daudi alisaidiwaje na Yehova katika eneo la Wafilisti?
13 Wenye kushangaza zaidi ni uhakika wa kwamba adui wakubwa sana wa Waisraeli walisaidia Daudi na watu wake. Daudi alikuwa amekuwa shujaa wa kutokeza kulipokuwa na mapigano na Wafilisti. Walipowalaki washindi wenye kurudi, wanawake Waisraeli waliimba wakisema: “Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu yake.” (1 Sam. 18:7) Kwa hiyo, huenda mtu akadhani kwamba Daudi na watu wake wasingetaka kamwe kufikiria kukimbilia eneo la Wafilisti wakapate usalama. Hata hivyo walikimbilia huko. Mfalme Mfilisti Akishi alivutwa sana na Daudi na watu wake, akawapa mji wa Zilagi uwe makao yao. Hakuweza kamwe kujua kwamba Daudi na watu wake waliendelea bado kuwa Waisraeli thabiti. (1 Sam. 27:1-6) Akishi hata aliwatetea mbele ya mabwana na wakuu wenzake Wafilisti. Baadaye alimwambia Daudi hivi: “Aishivyo [Yehova], wewe umekuwa mwenye adili, tena kutoka kwako na kuingia kwako pamoja nami katika jeshi ni kwema machoni pangu.” (1 Sam. 29:2-6) Kwa hiyo, Akishi alitumikia kama chombo cha Yehova kusaidia Daudi, bila ya yeye mwenyewe kujua.
14. Kutokana na mambo yaliyompata, Daudi alimwonaje Yehova kama msaidiaji?
14 Nyakati nyingine nyingi Yehova Mungu alimtafutia Daudi njia ya kutokea, akampa vitu alivyovihitaji. Kwa kuwa Yehova alikuwa amemsaidia ajabu, Daudi alikuwa na hakika kwamba asingeachwa kamwe. Daudi alisema, “Baba yangu na mama yangu [wakiniacha], . . . [Yehova] atanikaribisha kwake.”—Zab. 27:10.
15. Ni katika maana gani Daudi hakuogopa alipozungukwa na adui?
15 Hiyo haimaanishi kwamba Daudi hakuogopa wakati wo wote. Bila shaka aliogopa. Lakini hakuogopa kamwe kwamba Yehova angemwacha kabisa. Kwa kuongozwa na Mungu, Daudi aliandika hivi: “Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi. Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe; kwa msaada wa [Yehova] nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; mwenye mwili atanitenda nini?”—Zab. 56:2-4.
16. Yehova hakuacha nini kimpate Yeremia wakati wa mazingiwa ya Yerusalemu?
16 Huenda hali zikaonekana bila tumaini kabisa. Lakini hazitamzuia Yehova Mungu asihakikishe kwamba watumishi wake wanapokea vitu ambavyo yeye aona wanahitaji. Mfano mmoja ni nabii Yeremia. Wakati wa mazingiwa mabaya sana ya Yerusalemu, aliwekwa kizuizini kama mfungwa. Hakuwa na chakula kingi. Hali ilipata kuwa mbaya sana hata baadaye wanawake fulani wakala nyama za watoto wao wenyewe. (Omb. 2:20) Lakini je! Yehova Mungu aliruhusu nabii wake afe njaa? Sivyo. Biblia yasema hivi: “Wakampa kila siku mkate mmoja uliotoka katika njia ya waokaji, hata mkate wote wa mji ulipokwisha. Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.”—Yer. 37:21.
17. Ebedmeleki alitumikiaje kama chombo cha Yehova kumsaidia Yeremia?
17 Kisha ulikuwako wakati ambao ilielekea kuwa hakika kwamba Yeremia ataangamia. Wakuu wa Uyahudi walimshtaki kwa uongo kwamba alifitini serikali. Sedekia alikubali walivyosema akamtia nabii mikononi mwao. Wakamtupa Yeremia katika tangi lenye matope, afe kwa kukosa chakula. (Yer. 38:4-6) Towashi mmoja Methiopia, aitwaye Ebedmeleki, alijihatirisha kwa kumwendea Mfalme Sedekia hadharani akamsihi kwa ajili ya nabii wa Yehova, Yeremia, mwenye kuchukiwa sana. Ebedmeleki alisikilizwa vizuri. Baada ya hapo Ebedmeleki aliokoa nabii akisaidiwa na watu 30. Kwa kutumikia faida za Yehova hivyo, Ebedmeleki alihakikishiwa hivi: “Wala hutatiwa katika mikono ya watu wale unaowaogopa. Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga, lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema [Yehova].”—Yer 39:17, 18.
18. Mashahidi wengi Rhodesia walipataje kuangaliwa na Yehova kwa upendo?
18 Vilevile, leo watu wanaomtumaini Yehova wanaangaliwa naye kwa upendo. Mamia ya mashahidi wa Yehova wa Kikristo Rhodesia waliona kwamba wanaangaliwa hivyo. Mashahidi hao waliacha kazi zao walipofahamu kwamba kuhusika katika utengenezaji wa tumbako kulivunja kanuni za Kikristo. Haikuwa rahisi kufanya hivyo, kwa maana hiyo ilimaanisha hawangekuwa wakitibiwa hospitalini bila malipo, hawangepewa mashamba na vitu vingine vya kuwalinda. Lakini walikuwa na nia ya kujinyima na wamebarikiwa sana kwa kufanya hivyo. Walipata kazi mpya, na wengi wao waliandikwa na waamini wenzao. Wengi walihamia maeneo ambako ujumbe wa ufalme wa Mungu haukuwa umehubiriwa zamani. Kwa njia hiyo hawakujifaidi wenyewe tu kiroho bali pia waliletea watu wengine wengi tumaini katika Rhodesia. Mashahidi hao waliangaliwa kweli kweli na Yehova kwa njia ya kipekee sana.
ENDELEA KUTUMAINI UWEZO WA YEHOVA WA KURUZUKU
19. Yehova hatasahau nini kamwe, na hiyo itutieje moyo tunapopatwa na mkazo wa uchumi?
19 Bila ya kujali ni mkazo wa uchumi wa namna gani utakaokupata, kumbuka kwamba Yehova ataruzuku na kuthawabisha watumishi wake leo kama alivyofanya zamani. Yeye hakusahau ukarimu ambao Wakristo Waebrania walitendea waamini wenzao. Mtume Paulo aliwakumbusha hivi: “Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia.” (Ebr. 6:10) Wayahudi waliofanywa Wakristo, waliokuwa wakiishi Yerusalemu hasa na sehemu nyingine zote za Uyahudi, waliangaliwa na Mungu kwa upendo walipopatwa na shida. Waamini wenzao, kutia na watu wengi wasio Wayahudi, waliongozwa na roho ya Mungu wasaidie kutayarisha misaada ya kuwapelekea. (Matendo 11:28, 29; Rum. 15:25-27; 1 Kor. 16:1-3; 2 Kor. 9:5, 7) Hakuna shaka kwamba Waebrania hao walikuwa na sababu za kuwa na tumaini hakika kwamba Yehova asingewasahau. Wala hatatusahau sisi.
20. Tufanyeje tupatwapo na matatizo mazito?
20 Wawezaje kushindwa Yehova akiwa msaidiaji wako? Kwa hiyo, kaza nia ulinde uhusiano wako naye maana ndiyo mali yako yenye thamani zaidi. Jitahidi kuendelea kuwa na nia iliyotajwa katika maneno yanayofuata ya mtunga zaburi aliyeongozwa na Mungu: “Ni nani niliye naye mbinguni, wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe. Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu na sehemu yangu milele.” (Zab. 73:25, 26) Unapopatwa na matatizo, mtegemee Yehova akutie nguvu, ukiwa na tumaini hakika kwamba atakusaidia uendelee kuwa mtumishi wake anayemkubali.—1 Pet. 5:7.