Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w78 10/15 kur. 15-19
  • Mtume Petro—Kwa Sababu Gani Anapendwa Sana na Wengi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mtume Petro—Kwa Sababu Gani Anapendwa Sana na Wengi?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • PETRO MTUME MWEPESI WA KUSEMA NA KUTENDA
  • TENA MSEMA WAZI
  • MARA KWA MARA ANAONYESHWA MAKOSA
  • NGUVU IKIUNGANISHWA NA UDHAIFU
  • Alijifunza Kusamehe Kutoka kwa Bwana Wake
    Igeni Imani Yao
  • Alijifunza Kusamehe Kutoka kwa Bwana Wake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • Alikuwa Mshikamanifu Licha ya Majaribu
    Igeni Imani Yao
  • Alishinda Woga na Shaka
    Igeni Imani Yao
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
w78 10/15 kur. 15-19

Mtume Petro​—Kwa Sababu Gani Anapendwa Sana na Wengi?

“Alilokuwa akifikiri, alikuwa na uhuru wa kusema ambao pia unavuta wengi. Na ni lazima isemwe kwamba mara nyingi alisema jambo lenyewe.”

KATI ya watu waliopendelewa sana waliopata kutembea hapa duniani lazima watiwe ndani mitume kumi na mawili wa Yesu Kristo Mwana wa Mungu.

Lo! ni baraka za ajabu namna gani walizozifurahia wale kumi na wawili walipokuwa na Bwana yao! Walimsikia akieleza kanuni za Mungu zenye haki, kama vile katika Mahubiri ya Mlimani, walimsikiliza akieleza mithali zake wakamwona akiwakanusha viongozi wa dini akiwarudi kwa sababu ya unafiki wao wa kidini. Ndipo baadaye walipomwona Yesu akiponya vilema, akiwafanya vipofu kuanza kuona hata kufufua waliokufa​—pendeleo la ajabu sana walilokuwa nalo!

Maandiko yaliyoongozwa na Mungu juu ya Yesu na mitume wake hayaelezi habari za maisha yote ya kila mmoja wa mitume kumi na wawili. Iwapo tunajua jambo fulani juu yao ni mambo machache sana ama hali zao zilizowatofautisha mmoja na mwenzake. Kwa mfano, Nathanaeli alikuwa Mwisraeli ambaye “ndani yake hamna hila.” (Yohana 1:47) Mathayo naye hutambulikana kwa kuwa alikuwa mtoza ushuru. Tomaso alikuwa na tabia ambayo ilimfanya aitwe “Tomaso mwenye mashaka.” Na Yohana anajulikana kwa vile alikuwa mtume aliyependwa kipekee kabisa na Yesu. Lakini Petro ni tofauti. Mara nyingi sana maneno yake, matendo yake, na utu wake unavuta fikira zetu katika habari ya Injili.

Kwanza, Petro anatajwa kwa jina mara nyingi kuliko wengine wote wakiunganishwa pamoja, zaidi ya mara 180. Zaidi ya hayo wakati yeye na wengine wanapotajwa, jina lake linatangulia kutajwa nyakati zote; na inakuwa hivyo hata ikiwa wengine wote wanatajwa, au iwe ni watatu, wawili au mmoja wao. Bila shaka kunazo sababu nzuri. Habari ya Injili inaonyesha kwamba yeye alikuwa mwepesi wa kusema kuliko wengine wote na kwamba alikuwa kama mnenaji wa wenzake. Petro anatajwa katika maandiko kwa njia tano tofauti. Jina lake “Petro” (ambalo ni yeye peke yake aliyeitwa hivyo) alipewa na Bwana yake na maana yake ni “jiwe, kipande cha mwamba.” “Simeoni” (Kiebrania) Simon (Kigiriki), liko na maana ya “kusikia.” (Mwa. 29:33) Pia anaitwa “Kefa” jina ambalo lina maana moja na “Petro” katika lugha ya Kishemu, na mara nyingi mwungano wa jina hilo “Simon Petro” unaonekana mara nyingi.

Baba yake Petro alijulikana kama Yohana (Yona). Petro alitoka katika kijiji ama mji wenye wavuvi wa samaki wa Bethsaida, uliojengwa pwani ya Bahari ya Galilaya. Huko katika upande wa juu wa bonde la mto Yordani ndiko ndugu yake Andrea aliyekuwa mwanafunzi wa Yohana Mbatizaji, alikomjulisha Petro kwa Yesu aliyekuwa Masihi. Wakati huo ndio Yesu alipompa Simoni jina la Petro, na tangu siku hiyo na kuendelea Petro akawa mfuasi wa Yesu.​—Yohana 1:35-42.

Ni wazi kwamba miezi fulani baadaye, Yesu aliwaita Petro na ndugu yake wakati walipokuwa wakivua samaki, waache nyavu zao kisha wamfuate wawe ‘wavuvi wa watu.’ (Luka 5:1-11) Ndipo mwaka uliofuata na baada ya sala ya usiku kucha, Yesu alimchagua Petro na wengine kumi na mmoja wawe mitume wake.​—Luka 6:12-16.

PETRO MTUME MWEPESI WA KUSEMA NA KUTENDA

Ni kwa sababu gani wengi wetu sana sana tunampenda Petro? Ingeweza kusemwa kwamba ni kwa sababu Petro alikuwa “mtu mwema.” Linalotusaidia ni kwamba bila shaka tunajua mambo mengi juu ya Petro kuliko mwingineo ye yote. Linalotufanya tumpende ni hali yake changamfu na yenye shauku. Pamoja na hali yake changamfu alikuwa na wepesi wa kusema na kutenda, mara nyingine hata bidii. Alitenda kwa haraka kulingana na yaliyokuwa akilini mwake na moyoni mwake jambo ambalo hata sisi tunafanya mara nyingi.

Hivyo wakati Yesu alipowawezesha Petro na wenzake wapate samaki wengi baada ya kufanya kazi usiku kucha bila kupata kitu, Petro aliogopa akaanguka miguuni pa Yesu akasema: “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” (Luka 5:8) Petro alipomwona Yesu akitembea juu ya maji, alimwuliza Yesu amwezeshe naye kufanya lilo hilo, naye Petro aliweza kufanya hivyo alipoendelea kuwa na imani ya kutosha. (Mt. 14:25-32) Tena wakati kundi la watu wengi lilipokuja kumkamata Bwana yake, wengine wa mitume wake waliuliza, “Bwana tuwapige kwa upanga?” (Luka 22:49) Lakini sivyo Petro. Mara moja yeye alishambulia kwa upanga, lakini alilenga vibaya hivi kwamba alikata tu sikio la mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu.​—Yohana 18:10.

Pia kulikuwako wakati ambapo baada ya kufufuka Yesu aliwatokea wengine wa mitume wake akiwa kama mgeni, walipokuwa wakivua. Kwa mara nyingine tena aliwafanya wakamate samaki wengi. Kwa tendo hilo mtume wake Yohana alitambua akataja kwamba ni Bwana yao. Aliposikia hivyo, Petro hakungoja mashua yao iliyokuwa nzito kwa sababu ya kuwa na samaki wengi, ifike pwani. Mara moja alijitumbukiza ndani ya maji akaanza kuogelea kwenda pwani akawe na Bwana yake. (Yohana 21:1-8) Bila shaka wepesi huo wafanya wengi wanaopenda Biblia waitikie kwa huruma.

TENA MSEMA WAZI

Petro alisema kwa vyepesi kama vile alivyotenda kwa vyepesi. Alilokuwa akifikiri, alikuwa na uhuru wa kusema ambao pia unavuta wengi. Na ni lazima isemwe kwamba mara nyingi alisema jambo lenyewe. Labda Petro hakuwa na elimu nyingi lakini alikuwa mtu mwenye akili, aliyefikiri. Aliyefikiri? Ndiyo, kwa maana tunaona mara nyingi aliuliza maswali ya maana; lazima mtu afikiri ili afanye hivyo. Hivyo Yesu alipotumia mfano, Petro alimwuliza Yesu aeleze ule mfano kwao. (Mt. 15:15) Tena wakati mwingine, baada ya Yesu kutoa onyo juu ya kurudi kwake, Petro ndiye aliyeuliza “Bwana mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?” (Luka 12:41) Tena Petro ndiye aliyeuliza kwa niaba yake na ya wenzake hivi: “Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?” Yesu aliwahakikishia wote kwamba Yehova angewathawabisha (angewapa zawadi) wote wakati huo na wakati ujao.​—Mt. 19:27; Marko 10:29, 30.

Kwa kuwa msema wazi hivyo Petro alionyesha kwamba alimthamini sana Bwana yake. Baada ya Yesu kuulaani mtini fulani, Petro ndiye aliyevuta fikira kwenye matokeo ya laana ya Yesu: “Rabi, tazama mtini ulioulaani umenyauka.” (Marko 11:21) Yesu alipouliza mitume wake waliamini yeye alikuwa nani, tena Petro ndiye aliyekubali bila shaka lo lote: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Tena wakati Yesu alipowauliza mitume wake kama nao wangetaka kwenda kama wanafunzi wengine walivyofanya, Petro ndiye aliyesema: “Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele, nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” (Yohana 6:68, 69) Kwa kweli kuthamini huko kote kwa Petro na ushikamanifu wake ndiko kunakotufanya tumpende.

MARA KWA MARA ANAONYESHWA MAKOSA

Walakini, mara nyingine Petro alisema isivyofaa, Yesu akalazimika kumsahihisha, kumwonya. Petro hakugombana nyakati kama hizo mahali pake alikubali kwa unyenyekevu kusahihishwa huko, hilo nalo linatufanya tumwone kama ndugu yetu kweli kweli. Hivyo wakati Yesu alipowaambia mitume wake alilokuwa anaelekea kupatwa nalo, kwamba angepatwa na mateso mengi, auawe na katika siku ya tatu afufuliwe kutoka kwa wafu, Petro aliyekuwa na kusudi jema alimchukua faraghani akaanza kumkanya akamwambia “Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.” Ndiyo alikuwa na kusudi jema, lakini lo! jinsi alivyokosea! Alikuwa amekosea sana hivi kwamba Yesu alilazimika kumwambia: “Nenda nyuma yangu Shetani; u kikwazo kwangu, maana huyawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu.” (Mt. 16:21-23) Vivyo hivyo ni mara ngapi sisi tulitaka kufanya vizuri, lakini baadaye tukaona kwamba zilikuwa fadhili zisizofaa!

Wakati mwingine Petro alitaka kujua juu ya kusamehe ndugu yake mara nyingi hivyo. Je! ilikuwa lazima amsamehe “hata mara saba?” Yesu alimsahihisha: “Mimi nakuambia si, hata mara saba, bali hata mara sabini na saba.” Lo! Jinsi ilivyo vyepesi kwetu kuthamini namna alivyoona Petro, sana sana ikiwa mtu aliye karibu nasi anatukosea mara nyingi!​—Mt. 18:21, 22, NW.

Wakati fulani Yesu alisikia nguvu zikimtoka ambazo kwazo mwanamke mmoja aliponywa ugonjwa kwa sababu ya imani yake. Kwa hiyo Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Petro alimkaripia Yesu, akasema: “Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga.” Kwa njia nyingine ni kama kumwuliza ‘Yesu unauliza nini!’ Lakini Yesu alisahihisha Petro, akisema; ‘Najua ninalouliza!’ Ndipo yule mwanamke alipojitokeza wazi, basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya, enenda zako na amani.” Je! Petro hakuwa kama sisi nyakati nyingine, tukipinga jambo kwa sababu ya kutojua mambo yote ya hakika?​—Luka 8:43-48.

Mara nyingine tena Petro alisema isivyofaa wakati Yesu baada ya kuadhimisha sikukuu ya kupitwa pamoja na mitume wake, alipoanza kuwatawadha (kuwaosha) miguu. Petro alikuwa amemwona Yesu akiwaosha na kuwapangusa wengine wa wanafunzi wake. Kwa hivyo Petro akamwambia Yesu, “Wewe wanitawadha miguu mimi?” Kwa kweli Yesu alimwonya mara mbili pindi hilo. Petro alikuwa na makusudi mazuri, lakini alikuwa amekosea.​—Yohana 13:5-10.

Usiku uo huo Petro alisema isivyofaa mara nyingine. Yesu aliwaambia mitume wake kwamba wote wangekwazwa usiku huo. Lakini Petro alikuwa na hakika sana na ushikamanifu wake kwa Bwana yake kwamba hangevumilia wazo la kwamba yeye angemwacha Bwana yake. Labda wengine wangefanya hivyo, lakini sivyo yeye! Yesu alipoongeza kwamba Petro angemkana mara tatu, Petro alipinga vikali sana: “Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.”​—Mt. 26:31-35.

Hata hivyo Petro angejifunza juu ya udhaifu wake. Bila shaka kama angaliletwa mbele ya hakimu angalifanya mambo kwa njia nzuri sana. Lakini lililotukia halikutazamiwa hata kidogo. Mitume tisa walikuwa wametoroka. Yohana na Petro peke yao ndio tu waliokuwa wamemfuata Yesu mpaka kwenye ua wa kuhani mkuu, huko kijakazi mmoja akamwambia Petro, “Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya.” Kisha wengine wakaanza kumshtaki Petro. Hali zilizokuwako, wakati ulivyokuwa, aliyesema hayo, na zaidi namna yalivyosemwa, mambo hayo yote yakiunganishwa pamoja yalimfanya Petro kutenda bila kufikiri, yakimfanya amkane Bwana yake si mara tatu tu bali vilevile kuapa akisema “Simjui mtu huyu.” Upesi baada ya hapo jogoo akawika. Yote yalitukia kama alivyokuwa ametabiri Yesu. Wakati uo huo, Luka anatuambia, “Bwana akageuka akamtazama Petro.” Petro “akatoka nje akalia kwa majonzi.” Hakujaribu kutafuta sababu, wala udhuru, alitubu tu kwa moyo mkunjufu na mnyenyekevu. Bila shaka wote waliopata kulia kwa sababu ya kosa zito walilolifanya wanajisikia kama Petro na wanaweza kuthamini namna alivyojisikia wakati huo.​—Luka 22:61, 62; Mt. 26:69-75.

NGUVU IKIUNGANISHWA NA UDHAIFU

Maelezo ya Biblia juu ya Petro yanafanya mtu avutiwe sana anapoyasoma. Habari hiyo yake ni ufunuo wa ajabu sana wa asili ya kibinadamu na wa yale ambayo roho ya Mungu inaweza kufanyia wanadamu wenye makosa. Ingawa kosa la Petro lilikuwa zito sana, yeye hakuliruhusu liwe kikwazo kwake hata avunjike moyo na kuacha kumfuata Bwana yake. Yeye aliendeleza unyenyekevu wake pamoja na upendo wake kwa Bwana yake. Hili linaonyeshwa zaidi na jambo lililotukia baada ya Yesu kufufuka alipomtokea Petro na wengine pwani ya Bahari ya Galilaya. Kwa unyenyekevu Petro alikubali karipio la Yesu alipomwuliza mara tatu kama alimpenda na baadaye akamwagiza “lisha wana-kondoo wangu.”​—Yohana 21:15-17.

Mara nyingi Petro alikuwa akiongoza wale kumi na wawili; Hivyo baada ya Yesu kupaa mbinguni Petro ndiye aliyeanzisha tendo la kuweka Mathiya mahali pa Yuda. Katika siku ya Pentekoste Petro ndiye aliyekuwa mnenaji wa wale kumi na wawili, hivyo akatumia mojawapo wa “funguo za ufalme” alizokuwa ametangulia kupewa. Baadaye alitumia tena funguo hizo kwa kuwapelekea habari njema waongofu wa kwanza wa mataifa yasiyotahiriwa, Kornelio na watu wa nyumbani mwake.​—Matendo 1:15-26; 2:14-40; 10:1-48; Mt. 16:19.

Tunamwona Petro akisema kwa uhodari mwingi juu ya mwujiza ambao yeye na Yohana walifanya wa kuponya mtu aliyelemaa tangu kuzaliwa. (Matendo 3:12-26) Walipoletwa mbele ya watawala, Petro na Yohana walikuwa na uhodari sana wa kusema hivi kwamba watawala walishangaa. Ndipo walianza ‘kutambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.’ (Matendo 4:13) Na mara nyingi Petro na wenzake waliwakumbusha watawala hao kwamba utii wao wa kwanza ulikuwa kwa Mungu. Katika sura za kwanza kumi za kitabu cha matendo tunamwona Petro akitoa hotuba sita. Si ajabu kwamba Herode Agripa wa Kwanza alimfunga na alikusudia kumwua! Lakini Mungu alikuwa na mambo mengine ambayo angemtumia Petro ayafanye na kwa hiyo akamtuma malaika wake amwokoe.​—Matendo 12:3-17.

Vilevile Petro alishiriki sehemu ya maana sana katika mkutano wa baraza inayoongoza ya kundi la Kikristo walipofikiria ulizo la kutahiriwa kwa Mataifa. (Matendo 15:7-11) Walakini si muda mrefu baada ya hapo tunamwona akiacha kuogopa wanadamu, kuogopa Wayahudi Wakristo waliotoka Yerusalemu, kumfanye aache kufuata kanuni nzuri alizokuwa akifuata kwa kutoshirikiana na Wakristo wa mataifa. Udhaifu huu ulimfanya Paulo amkemee Petro kwa nguvu, jambo ambalo linaelekea lilifanywa mbele ya kundi lote. (Gal. 2:11-14) Hapa tena, tunaweza kuona “wema” wa Petro. Wote ambao mara nyingine wameogopa wanadamu wanaweza kuona alivyoona Petro wafaidike na kufarijiwa na mfano wake.

Katika kumalizia hatupaswi kusahau barua mbili alizoandika Petro, zina habari nyingi za kutia moyo sana sana kwa wale wanaoteswa kwa ajili ya haki. Barua hizi zinatufanya tumthamini Petro zaidi. Kwa kweli mtume Petro alikuwa mtu anayeweza kupendwa sana, alitumiwa sana na Mungu wake na Bwana wake pia, ijapokuwa udhaifu wake. Lo! maisha yake ni kitia-moyo namna gani kwa wale wote wanaojaribu kumfuata Bwana yao kama vile alivyofanya Petro!​—1 Petro 2:21.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki