Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w78 9/15 kur. 16-20
  • Mwamuzi Mnyenyekevu Aliyetaka kuwa na Hakika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwamuzi Mnyenyekevu Aliyetaka kuwa na Hakika
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • YEHOVA ACHAGUA ‘ALIYE MDOGO’
  • MATAYARISHO YA VITA YASIYO YA KAWAIDA
  • MASOMO YA MAANA KWA NYAKATI HIZI
  • “Upanga wa Yehova na wa Gideoni!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Gideoni na Wanaume Wake 300
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Wazee—Jifunzeni Kutokana na Mfano wa Gideoni
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2023
  • Gideoni Aliwashinda Wamidiani
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
w78 9/15 kur. 16-20

Mwamuzi Mnyenyekevu Aliyetaka kuwa na Hakika

LILITUKIA katika karne ya 13 K.W.K., kama miaka 200 baada ya kifo cha Yoshua aliyechukua uongozi wa Musa. Mahali pa tukio hilo palikuwa bonde la Yezreeli katika sehemu ya kaskazini ya nchi ambayo Mungu alikuwa amewaahidi Israeli.

Ni tukio gani lililotukia huko nyuma ambalo linatupendeza sisi leo? Mmoja wa waamuzi wa Israeli alifukuza jeshi la adui lililopata kuwa watu 135,000 akiwa na jeshi la watu 300 tu.

Jambo kama hilo lingetukiaje? Jambo la maana lilikuwa kutaka sana kwa mwamuzi huyu kuwa na hakika kwamba Yehova alikuwa akiwaunga mkono.

Habari ya Biblia ya tukio hili la ajabu inapatikana katika kitabu cha Waamuzi, sura za 6 hadi 8, ambayo inaanza hivi: “Kisha wana wa Israeli walifanya yalio maovu mbele za macho ya [Yehova]; [Yehova] akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba. Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli.” (Amu. 6:1, 2) Ikiwa Israeli wangepanda mbegu, Wamidiani pamoja na wanyang’anyi wengine wangepanga “marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng’ombe, wala punda.”​—Amu. 6:4.

YEHOVA ACHAGUA ‘ALIYE MDOGO’

Kwa kukata tamaa sana, Israeli ‘wakamlilia [Yehova] kwa sababu ya Midiani.’ (Amu. 6:7) Kwa hiyo, Mungu alimwinua kama mwamuzi mwanamume wa jamaa ya Abiezeri (sehemu ndogo ya kabila la Manase), Gideoni mwana wa Yoashi. Gideoni alipokuwa akipepeta nafaka ndani ya shinikizo, ili asionekane na adui, malaika alimtokea, akasema: “[Yehova] yu pamoja nawe, Ee shujaa.” Kwa kushangaa, aliuliza ingekuwaje kwamba Mungu yu pamoja na Israeli, kwa kuwa walikuwa katika taabu kubwa. “[Yehova kwa malaika wake] akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huo, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! si mimi ninayekutuma?”​—Amu. 6:11-14.

Namna Gideoni alivyoitikia agizo hili kutoka kwa Mungu alionyesha alikuwa na nia ya unyenyekevu. Alijibu hivi: “Ee [Yehova], nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.” Hata hivyo, Mungu alimhakikishia hivi: “Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.”​—Amu. 6:15. 16.

Hata hivyo, Gideoni alijua shida iliyokuwako katika kupigana vita na Wamidiani pamoja na taifa jingine lo lote ambalo huenda lingejiunga nao. Kwa hiyo aliomba “ishara” ili awe na hakika kwamba agizo hili lilikuwa limetoka kwa Mungu kweli kweli. Alileta zawadi ya nyama na mkate usiotiwa chachu na mchuzi, akaweka vitu hivyo juu ya mwamba mkubwa akazimwagilia huo mchuzi. Malaika akaguza nyama na mkate kwa fimbo yake. Moto ukaanza kutokea katika ule mwamba ukateketeza hilo toleo, naye malaika akatoweka. “Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa [Yehova].”​—Amu 6:17-22.

Usiku huo Yehova alimjaribu huyo mwamuzi wake aliyemchagua. Mungu alimwamuru aiangushe madhabahu ya baba yake ya mungu wa Baali, na kuikata ashera iliyokuwa karibu nayo, na pahali pake amjengee Yehova madhabahu na kumtoa ng’ombe wa miaka saba (bila shaka ng’ombe aliyekuwa wakf kwa Baali) wa baba yake Yoashi juu ya madhabahu hiyo. Ashera hiyo ingetumika kama kuni. Kwa ujasiri, Gideoni alikubali mgawo huo. Lakini ili kuwa mwangalifu, aliufanya usiku.​—Amu. 6:25-27.

Watu wa mji walipoamka asubuhi yake na kuona hivyo, walitaka kumwua Gideoni. Walakini, baba yake, Yoashi, alimsaidia akawaambia kwamba ikiwa kweli Baali alikuwa mungu anapaswa kujitetea mwenyewe.​—Amu. 6:28-32.

MATAYARISHO YA VITA YASIYO YA KAWAIDA

Baada ya hapo habari ya Biblia inaeleza kwamba “Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli.” Ndipo roho ya Yehova ikaja juu yake Gideoni. Akawakusanya Waabiezeri kwa vita, na vilevile akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote na kwa Asheri, Zebuloni na Naftali, wakiwahimiza watu wajiunge pamoja naye. (Amu. 6:33-35) Wale waliojiunga naye walikuwa watu 32,000. Walakini, adui zao walikuwa watu 135,000, wakiwazidi Israeli mara 4.

Wakati huu Gideoni alimwuliza Mungu afanye miujiza miwili, ili tena awe na hakika kwamba Mungu angewaunga mkono wanapopigana na Wamidiani. Aliomba kwamba ngozi ya kondoo iliyoachwa nje usiku katika kiwanja cha kupuria iwe na umande nayo nchi yote inayoizunguka iwe kavu, na usiku unaofuata ngozi ya kondoo iwe kavu, nchi ikiwa na umande. Mungu akamtimizia maombi yote mawili.​—Amu. 6:36-40.

Gideoni na jeshi lake walipopiga kambi wakitayarisha kukutana na adui, Yehova alitoa amri isiyotazamiwa: “Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. Basi sasa, enda tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke.” Kwa kutii, Gideoni akawajaribu. Matokeo? “Ndipo watu ishirini na mbili [22,000] elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi [10,000].” (Amu. 7:2, 3) Mara hiyo adui wakawa wanazidi Israeli mara 13.

Baada ya hapo, Yehova alimwagiza Gideoni awaongoze watu waliobaki 10,000 kwenye maji ili wajaribiwe tena. Idadi kubwa yao walijiachilia, wakapiga magoti kunywa maji kwa pupa. Lakini, watu 300 waliendelea kuwa macho, wakiinama kidogo tu ili wachote maji ya kunywa kwa mikono yao. Kisha Mungu akasema: “Kwa watu hawa mia tatu . . . nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako.” (Amu. 7:4-7) Hii iliwafanya adui wazidi Israeli mara 450.

Mungu akamwambia Gideoni kwamba, ikiwa anaogopa, yeye pamoja na mtumishi wake wanapaswa wapeleleze kambi ya adui usiku. Alifanya hivyo, akasikia mtu mmoja akisimulia mwenzake ndoto. Mtu huyo alikuwa ameota juu ya mkate wa shayiri ulioanguka katika kambi ya Wamidiani, ukaipiga hema moja ikaanguka hata ikalala chini. Mwenzake akapaza sauti hivi: “Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake.”​—Amu. 7:9-14.

Akiwa ametiwa nguvu, Gideoni alirudi katika kambi ya Israeli akafanya mpango wa kuvamia adui. Lakini kikundi cha watu mia 300 kingewezaje kushinda watu kama 135,000?

Mwamuzi huyu mwenye busara alipanga jeshi lake katika vikosi vitatu kila kimoja watu mia moja. Hii iliwawezesha wakaribie adui kutoka pande tatu. Alimpa kila mtu tarumbeta (baragumu), na mtungi wa udongo na mwenge ndani ya mtungi, akiwaeleza: “Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa [Yehova], na kwa Gideoni.” (Amu. 7:16-18) Mpango huu ulikuwa na matokeo gani? Habari ya Maandiko inaendelea kueleza hivi:

“Basi Gideoni, na wale watu mia waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa [Yehova] na wa Gideoni. Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele wakawakimbiza. Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye [Yehova] akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi.”​—Amu. 7:19-22.

Mpango huo ulikuwa na matokeo yenye kuangamiza kweli kweli! Kule kupiga tarumbeta, kuvunja-vunja mitungi, kuinua mianga na kupiga kelele bila shaka kuliwafanya Wamidiani wasadiki kwamba walikuwa wamezungukwa na jeshi kubwa. Huenda walidhani kwamba kila mwenge uliwakilisha si mtu mmoja bali kikosi kizima cha askari. Kwa kushikwa na woga, walikimbia, hata wakaufanya “upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe” kati yao wenyewe.

Akiazimia kuwafukuza adui kabisa, sasa Gideoni aliomba msaada kutoka kwa kabila la Manase, Asheri, Naftali na Efraimu. Hawa waliwavamia Wamidiani waliokuwa wakikimbia, wakifunga njia zao za kukimbilia. Wanaume wa Efraimu wakawakamata na kuwaua wakuu wawili wa Midiani Orebu na Zeebu.

Kisha jambo moja likafanyika ambalo lilionyesha tena maoni mazuri ya Gideoni; tunasoma hivi: “Watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini wewe kututendea sisi kama haya? hata usituite, hapo ulipokwenda kupigana na Midiani? Nao wakateta naye sana.” Walakini, mwamuzi huyu shujaa, aliitikia kwa unyenyekevu wenye kusifika: “Je! mimi nimefanya nini sasa kama mlivyofanya ninyi? . . . Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi.” Jibu hili la upole lilituliza hasira zao.​—Amu. 8:1-3; Mit. 15:1.

Ingawa alikuwa amechoka, mwamuzi huyu shujaa, pamoja na watu wake mia tatu, walivuka Yordani wakiwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani. Wakiwa njiani, Gideoni aliwaomba watu wa Sukothi chakula, lakini wakuu wa Sukothi walikataa, wakisema: “Je! mikono ya Zeba na Salmuna i mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate?” Jambo ilo hilo likatokea katika mji wa Penieli.​—Amu. 8:4-9.

Ijapokuwa shida zao, Gideoni na watu wake waliendelea kuwafuatia. Mwishowe, waliwapata Zeba na Salmuna, pamoja na wanaume waliobaki wapata 15,000 hesabu yao. Kwa mara nyingine tena, mwamuzi huyu aliyechaguliwa na Mungu alionyesha uangalifu, kwa kuwa “alianza kupiga kambi hiyo wakati kambi hiyo ilikuwa haijilindi.” (Amu. 8:10, 11, NW) Zeba na Salmuna walikimbia, lakini walikamatwa wakauawa na Gideoni.​—Amu. 8:12, 18-21.

Watu wa Israeli walifurahia sana ushindi kamili wa Gideoni hivi kwamba walimwomba yeye na nyumba yake watawale juu yao. Lakini yeye hakutaka fahari na kuabudiwa kunakotokana na utawala wa kibinadamu. “Mimi sitatawala juu yenu, yeye [Yehova] atatawala juu yenu.”​—Amu. 8:22, 23.

Kisha Gideoni akaomba michango ya pete za dhahabu zilizokuwa zimetekwa. Kutokana navyo akafanya naivera, au vazi la kuhani, lenye bei kubwa sana, labda likipambwa kwa mawe ya bei kubwa. Huenda alikuwa na kusudi jema akifanya hivyo, labda akiona vazi hilo kama kumbukumbu la ushindi juu ya Midiani. Walakini, ilionekana kuwa kikwazo, kwa kuwa “Israeli wote wakaenda na kuiandama [hiyo naivera] kwa ukahaba huko; nayo ikawa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake.” (Amu. 8:27) Ni wazi kwamba Waisraeli walilitumia hilo vazi la bei kubwa katika namna fulani ya ibada ya uongo.

MASOMO YA MAANA KWA NYAKATI HIZI

Habari ya Biblia kuhusu Gideoni ina masomo ya maana sana kwa watu wanaoishi leo. Kwa mfano, ebu angalia uangalifu wake. Je! uliona namna mwamuzi huyu alivyotafuta mara kwa mara ushuhuda wa miujiza wa kwamba Mungu alikuwa akimsaidia? Huu haukuwa wonyesho wa kukosa imani. Imani ilihitajiwa ili kuwa na nia ya kukubali kupiga vita na adui waliowazidi mara 4, bila kutaja namna walivyoendelea kuwazidi mara 13, na mwishowe, mara 450. Na hata ingawa alikuwa na imani kubwa, Gideoni alitaka kuwa na hakika kwamba Mungu alikuwa akimsaidia katika kazi hii isiyowezekana kwa mwanadamu. Hata baada ya kupata uhakikisho huu, Gideoni alisonga mbele kwa uangalifu, akiwavamia adui wakati hawakuwa na ulinzi.

Vivyo hivyo leo, Wakristo wanaona wakizidiwa sana na ulimwengu ulio na uadui na waabudu wa kweli wa Yehova. (Yohana 15:18, 19) Wale wanaoweza kumpendeza Mungu katika wakati huu lazima waendelee kuchunguza Biblia ili wawe na hakika kwamba utumishi wao mtakatifu unapatana nayo na kwamba unaungwa mkono na Mungu. (2 Kor. 13:5) Kama vile kwa uangalifu Gideoni aliangusha madhabahu ya Baali usiku, ni lazima Wakristo wawe “na busara kama nyoka” wanapofanya kazi yao ya kutoa ushuhuda na kufanya wanafunzi, ambayo inaangusha mafundisho ya uongo ya kidini. (Mt. 10:16; 24: 14; 28:19, 20) Wao wanatafuta nyakati na njia zinazofaa ambazo zitawezesha ujumbe wa Kikristo uwe na matokeo yanayowafaidi wenye mioyo minyofu.

Mfano mwingine mwema unaotolewa na Gideoni ni ule wa unyenyekevu. Maandiko yanawashauri Wakristo kusitawisha nia iyo hiyo, “msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu.”​—Flp. 2:3.

Kuongezea hayo, habari hii ya Biblia ni mfano wa unabii. Mwamuzi Gideoni anafananisha Kristo Yesu, ambaye kwake Mungu “amempa . . . hukumu yote.” (Yohana 5:22) Maandiko yanatoa unabii kwamba karibuni Yesu, pamoja na majeshi ya kimalaika, atapigana vita na “wafalme wa nchi, na majeshi yao.” (Ufu. 19:11, 14, 19) Matokeo yake yatakuwa kulingana na sala ya mtunga zaburi ya ukombozi ulioletwa na Gideoni: “Uwatende kama Midiani . . . Uwafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, na . . . kama Zeba na Zalmuna. Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.”​—Zab 83:9-18.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki