“Mwanamke Mwema” Aonyesha Upendo Mshikamanifu
“Mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema,”—Rut. 3:11.
1, 2. Ni kukutana gani kwa usiku kunavutia akili zetu, nako kunatokeza maulizo gani?
GIZA la usiku limeingia na Bethlehemu, Yuda na nchi inayoizunguka imekuwa kimya. Katika sakafu ya kupuria nafaka katika shamba moja mwanamume wa makamu analala. Lakini, tazama! Mwanamke kijana anakaribia polepole, amfunua kidogo na kulala. Mwanamume huyo anaamka, na kumwona mwanamke huyo amelala miguuni pake, na kumwuliza, “Ni nani wewe?” Jibu lake? “Ni mimi, Ruthu, mjakazi wako.” Amemjia akiwa na kusudi la pekee na lenye maana kubwa sana. Kwa kweli, akikiri wema wake wanapoendelea kuzungumza, anasema: “Mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema.”—Rut. 3:9-11.
2 Ni jambo gani limeongoza kwenye kukutana huku kwa usiku? Kwa kweli, mwanamke huyu ni nani? Naye mwanamume huyo wa makamu ni nani? Kwa sababu gani yeye anasema kwamba mwanamke huyu anajulikana kama “mwanamke mwema”? Ni sifa gani anazozionyesha? Maulizo haya na mengine yanajaa akilini mwetu tunapofikiria tamasha hii ya usiku isiyo ya kawaida.
3. (a) Sasa tunataka kuangalia kitabu gani? (b) Kitabu hiki kiliandikwa wakati gani na kiliandikwa na nani, na kinavuta fikira kwenye jambo gani?
3 Habari iliyoandikwa kwa uongozi wa Mungu ambayo tutafikiria, inaelekea iliandikwa katika siku za Daudi (kama mwaka 1090 K.W.K.) na nabii Mwebrania Samweli, ni ya pekee ikiwa mojawapo vitabu viwili peke yake vinavyoitwa kwa majina ya kike. (Kingine ni Esta.) Ingawa wengine wanaona kitabu cha Ruthu kama hadithi ya mapenzi yenye kupendeza, ni zaidi ya hiyo. Habari hiyo inavuta fikira kwenye kusudi la Yehova la kutokeza mrithi wa Ufalme, Masihi aliyekuwa amengojewa kwa muda mrefu. Zaidi ya hayo, kinatukuza fadhili za upendo za Mungu.—Mwa. 3:15; Rut. 2:20; 4:17-21.a
MSIBA WATOKEA!
4. Matukio yanayoelezwa katika kitabu cha Ruthu yalitukia kipindi gani cha wakati?
4 Matukio yanayoelezwa katika habari hii yalitokea “zamani za Waamuzi walipoamua” mambo katika Israeli. Wakati huu ni lazima uwe mapema wakati wa kipindi hicho, kwa kuwa mwanamume tuliyemwona na Ruthu sakafuni ya kupuria nafaka alikuwa Boazi, mwana wa Rahabu aliyeishi siku za Yoshua. (Rut. 1:1; Yos. 2:1, 2; Mt. 1:5.) Hadithi hii yenye kusisimua inapoendelea; itaendelea kwa muda wa miaka 11, labda karibu na mwaka 1300 K.W.K.
5. Elimeleki alihamisha jamaa yake kwenda Moabu kwa sababu ya hali gani na kwa sababu ya kujua jambo gani, na je! hili lina uhusiano (upatano) wote na madaraka ya Kikristo?
5 Njaa imetokea katika nchi ya Yuda na ikawa kubwa sana katika Bethlehemu (au Efrata). Sana sana msiba umeipata jamaa ya mwanamume fulani, Elimeleki. Akitambua haja ya kutoa mambo ya lazima ya maisha kwa wale wa nyumba yake mwenyewe, anachukua hatua. Upesi, Elimeleki, mkewe Naomi, na watoto wao wawili wa kiume Maloni na Kilioni wanaonekana wakivuka Mto Yordani. Waefrata hawa wanakuwa wahamiaji katika nchi ya Moabu, nchi iliyoinuka iliyoko mashariki mwa Ziwa la Chumvi na kusini mwa Mto Arnoni.—Rut. 1:1, 2; linganisha 1 Timotheo 5:8.
6. Eleza hali ambazo zinaongoza kwenye kufiwa na waume kwa Naomi.
6 Baada ya muda fulani Elimeleki akafa, akamwacha Naomi mjane anayeendelea kuzeeka. Baadaye, wanawe wawili wakaoa wanawake wa Moabu. Maloni akamwoa Ruthu, naye Kilioni akamchukua Orpa kama mkewe. (Rut. 1:4, 5; 4:10) Miaka 10 hivi ikapita, halafu msiba ukatokea tena. Wana wote wawili wa Naomi wakafa, bila mtoto. Sasa wanawake hao watatu wako peke yao, na kwa kweli kufiwa na mume na kuwa mjane ni jambo gumu kuvumilia.
7. Ni uwezekano gani unaonekana ukiwa mbali sana na Naomi mjane?
7 Na zaidi Naomi ndiye mwenye huzuni zaidi. Yeye ni Myahudi na anajua habari ya baraka ya pekee ambayo Yakobo alitoa kwa mwanawe Yuda alipokuwa kitandani mwake akiwa karibu kufa kwa maneno haya: “Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria katika miguu yake, hata atakapokuja Yeye [Shilo], mwenye milki, ambaye mataifa watamtii.” Huyo Shilo atakuwa na fimbo ya enzi—kwa kweli, yeye atakuwa ndiye Masihi, Uzao wa Ibrahimu ambaye katika yeye mataifa yote ya dunia yatajibarikia. Basi, inawezekana wanawake wa Yuda wakazaa watoto wa kiume ambao wangekuwa babu za huyo Mtiwa Mafuta! Lakini wana wa Naomi wamekufa bila watoto, naye amepita umri wa kuzaa watoto. Uwezekano wa kwamba Naomi na jamaa yake wanaweza kushiriki katika nasaba ya Kimasihi ni mdogo sana.—Rut. 1:3-5; Mwa. 22:17, 18; 49:10, 33.
8. Ni mambo gani yanayomsukuma Naomi arudi Uyahudi ingawa kunaweza kuwa na hatari njiani?
8 Hata hivyo, kuna tumaini dogo sana kwamba jambo zuri linatokea. Naomi amesikia, labda kutoka kwa wanabiashara Waebrania wenye kusafiri, kwamba Yehova “amewajilia watu wake na kuwapa chakula.” Ndiyo, njaa imekwisha, na kwa baraka ya kimungu, kuna chakula tena katika Yuda, chakula kifaacho katika Bethlehemu, “nyumba ya mkate.” Haukupita muda mrefu kabla ya wanawake hao watatu waliofiwa na waume zao kuonekana wakiondoka “wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda.” Hii haikuwa safari rahisi, kwa kuwa ilikuwa lazima wapitie sehemu zilizokuwa zimejaa wevi na wanaume hatari. Walakini kujitoa kwa Naomi kwa Yehova Mungu pamoja na tamaa yake kubwa ya kutaka kuwa na watu wake ilimsukuma aendelee ijapokuwa kuwe na hatari zo zote njiani.—Rut. 1:6, 7.
WAKATI WA KUAMUA
9. Kwa sababu gani Ruthu na Orpa wanaambiwa warudi “kila mmoja nyumbani kwa mamaye.”?
9 Je! wajane hawa vijana watamtendea kwa hesima mkwe wao mzee kwa kuambatana naye mpaka mpakani wa Moabu na Israeli tu? Au wataendelea zaidi? Tutaona. Njiani wanapoendelea, Naomi asema: “Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye.” (Rut. 1:8) Kwa sababu gani “mamaye,” wakati babaye Ruthu angali anaishi? (Rut. 2:11) Basi, huu ni usemi wa kawaida wa mwanamke mzee kwa mwanamke kijana, na mama zao walikuwa na nyumba zilizoimarishwa, kinyume cha alivyokuwa mkwe wao maskini. Kwa vyo vyote, upendo wa mama ungemfariji zaidi binti mwenye huzuni.
10. Naomi ana nia ya kuwaachilia wakweze wawili akiwa na tumaini gani?
10 Sikiliza anapoendelea Naomi: “[Yehova] na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. [Yehova] na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe.” (Rut. 1:8, 9) Wanawake hao wawili wa Maobu wameonyesha fadhili za upendo, au upendo mshikamanifu kwa Naomi na waume zao waliofariki. Wao hakuwa kama wake Wahiti wa Esau ambao ‘walijaza roho za Isaka na Rebeka uchungu.’ (Mwa. 26:34, 35) Sasa kwa kuwa Naomi hakuwa na mali, angemtazamia Yehova tu awape hao wakweze zawadi. Na anataka kuwaruhusu waende akitumaini kwamba Yehova atampa kila mmoja wa hawa wanawake vijana raha na faraja inayotokana na kuwa na mume na nyumba, kwa njia hiyo waondolewe ujane na huzuni yake.
11. (a) Kwa wazi, ni kwa sababu gani kuachana na Naomi kunaweza kuhuzunisha Ruthu na Orpa, na Je! hili linaonyesha jambo lo lote kwa habari ya uhusiana (ushirikiano) wa jamaa kati ya Wakristo leo? (b) Je! kuna nafasi nzuri za Ruthu na Orpa kuolewa tena wakiambatana na Naomi? Kwa sababu gani?
11 Lakini Ruthu na Orpa hawamwachi. Naomi anapowabusu, wanaanza kupaza sauti zao na kulia. Kwa wazi, yeye ni mkwe mwenye fadhili na upendo ambaye kumwacha kunaweza kutokeza huzuni. (Rut. 1:8-10; linganisha Matendo 20:36-38) Walakini Naomi anaendelea, akiwatolea sababu: “Je! mimi ninao watoto wa kiume tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? mngejizuia msiwe na waume?” Ndiyo, hata kama Naomi angepata watoto wapya wa kiume badala ya wale waliokufa, na wakakua wakawa watu wazima, je! hawa wanawake vijana wangejizuia wasiolewe na mtu mwingine? Lingekuwa jambo lisilo la akili kufikiri hivyo. Tena, wakiwa wanawake wa Moabu, nafasi yao ya kuolewa na waume katika nchi ya Yuda na kuwa na jamaa ingekuwa ndogo sana.—Rut. 1:11-13.
12, 13. Ruthu na Orpa wanajaribiwaje, naye Orpa anafanya uamuzi gani?
12 “La, sivyo, wanangu;” Naomi aendelea kusema, “maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa [Yehova] umetoka juu yangu.” (Rut. 1:13) Naomi hamshtaki Mungu kwa kufanya makosa; lo lote afanyalo au kuruhusu ni lazima liwe haki. (Mit. 19:3) Lakini anahuzunika kwa ajili ya wakweze. Na kwa upande wao huu umekuwa wakati wa kufanya uamuzi. Je! wataenda na Naomi bila choyo? Makusudi na ushikamanifu wao unajaribiwa.
13 Orpa afanya uamuzi wake. Ambusu mkwewe kwa machozi na kumwacha. “Tazama,” Naomi amwambia Ruthu. “Shemeji yako [mjane] amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako [mjane].” (Rut. 1:14, 15) Ndiyo, Orpa alikuwa akirudia watu wake na “mungu wake.” Wao wawili yeye na Ruthu walilelewa miongoni mwa “watu wa Kemoshi” na huenda akawa hata alikuwa ameshuhudia kutolewa kwa watoto kama dhabihu katika ibada ya mungu huyo wa uongo wa Wamoabu. Orpa alikuwa akiyarudia hayo yote!—Hes. 21:29; 2 Fal. 3:26, 27.
14. Ruthu anajielezaje kwa Naomi na kwa hivyo ni uamuzi gani umefanywa na mwanamke huyu Mmoabi?
14 Lakini hivyo sivyo ilivyo kwa Ruthu. “Usinisihi nikuache, nirejee nisifuatane nawe,” asema, “maana wewe uendako nitakwenda, na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapokufa nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa.” Kwa haya yote Mmoabi huyu anaongeza kiapo mbele za Mungu, akasema: “[Yehova] anitende hivyo na kuzidi, ila kufa tu kutatutenga wewe nami.” Lo! ni wonyesho wa upendo mshikamanifu namna gani? Kwa kweli, ni zaidi ya hayo. Ruthu amechagua maisha ya kumtumikia Yehova, na watu wa Naomi—wale walioko katika uhusiano (urafiki) wa agano na Mungu wa kweli—ndio watakaokuwa watu wake. Mmoabi huyu ameazimia kumtumikia Yehova kwa uaminifu. Kwa hivyo, Naomi aacha kufanya jitihada zo zote za kumrejeza kwao.—Rut. 1:16-18.
15. (a) Kufikia hapo, Ruthu ameonyeshaje upendo mshikamanifu? (b) Tunaweza kufaidikaje kutokana na maamuzi yaliyofanywa na Ruthu na Orpa?
15 Myahudi huyu mzee na mwanamke kijana Mmoabi wanapoendelea na safari yao ngumu wakiambatana pamoja, tunakuwa na nafasi ya kufikiria tamasha zenye kuhuzunisha ambazo tumeshuhudia. Orpa amechukua mwendo wa kujipendeza mwenyewe. Maendeleo yo yote aliyokuwa amefanya katika kujifunza juu ya Yehova hayakutosha kumzuia asiwarudie watu wake na “mungu wake.” Kama Ruthu angependezwa sana na nchi ya kwao, yeye, pia, angeirudia. (Linganisha Waebrania 11:15.) Lakini mwanamke huyu kijana Mmoabi ameonyesha upendo mshikamanifu, si kwa Naomi mzee peke yake, bali sana sana kwa Yehova. Ameonyesha roho ya kujinyima na azimio la kumtumikia Mungu wa kweli kwa imani. Tunapoona maamuzi haya yenye kutofautiana, sisi pia tunatiwa moyo ‘tusisite na kupotea,’ bali tuwe “na imani ya kutuokoa [nafsi] zetu.” —Ebr. 10:38, 39.
BETHLEHEMU WAAMKA
16. Kwa sababu gani wanawake wa Bethlehemu wanaendelea kuuliza. “Je! huyu ni Naomi?”
16 Mwishowe, wale wanawake wawili wafika waendako, Bethlehemu. Kuwapo kwao kwaamsha mji wote. “Je! huyu ni Naomi?” ndivyo wanawake wanaendelea kuuliza. Amezeeka baada ya miaka kupita. Bila shaka, wanawake wanaona jinsi huzuni na msiba zimemfanya mwanamke huyu ambaye hapo zamani alikuwa mchangamfu. Kwani, hata kuitikia kwake kwaonyesha maumivu ya moyoni!
17. Usemi wa Naomi, ‘Msiniite Naomi, lakini niiteni Mara,’ una maana gani?
17 “Msiniite Naomi [maana yake, kupendeza],” asema. “Niiteni Mara [maana yake, uchungu]; kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana. Mimi nalitoka hali nimejaa [akiwa na mume na watoto wawili wa kiume], naye [Yehova] amenirudisha sina kitu; kwani kuniita Naomi, ikiwa [Yehova] ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa?” (Rut. 1:19-21) Ndiyo! Naomi anakubali yale anayoyaruhusu Mungu, hata hivyo bila shaka anaona kwamba Yehova anampinga. (Rut. 1:13; linganisha 1 Sam. 3:18.) Bila shaka, wakati tumbo la uzazi lenye kuzaa linaonwa kuwa baraka kutoka kwa Mungu na utasa kama laana, ni aibu mwanamke kutokuwa na watoto wanaoishi. Naomi anaweza kuwa na tumaini gani la kushiriki katika nasaba yenye kutokeza Masihi?
MWOKOTAJI MNYENYEKEVU WA MAVUNO APATA KIBALI
18. Katika kuokota mavuno, Ruthu atakuwa akifanya nini na “kwa majaliwa” yeye anakwenda katika shamba la nani?
18 Naomi na Ruthu wamefika Bethlehemu ‘mwanzoni mwa mavuno ya shayiri,’ mwanzoni mwa wakati wa masika. (Rut. 1:22) Akiwa mwenye bidii na mwenye upendo wa kutumikia, Ruthu, akiruhusiwa na Naomi, anaondoka na kuanza kuokota mavuno nyuma ya wavunaji katika ‘mashamba ya nafaka. Yeye anajua kwamba kuokota mavuno ni mpango wa upendo wa Yehova kwa ajili ya watu maskini na walio na taabu, wageni, na yatima na wajane. Katika Israeli hawa wanaruhusiwa wakusanye au waokote sehemu yo yote ya mavuno yanayoachwa nyuma na wavunaji kwa kujua au kwa kutokujua. (Law. 19:9 10; Kum. 24:19-21) Ingawa Ruthu ana haki ya kuokota, kwa unyenyekevu yeye anaomba ruhusa na anakubaliwa aokote katika shamba fulani. Walakini bila shaka mkono wa Yehova uko katika jambo hili kwa maana “kwa majaliwa” ameingia “katika eneo la shamba lililokuwa la Boazi.”—Rut. 2:3, NW.
19, 20. (a) Boazi ni nani? (b) Kwa sababu gani inaweza kusemwa kwamba Ruthu si mwanamke aliyeendekezwa?
19 Tazama! Boazi anakaribia. Yeye ni “mtu mkuu mwenye mali,” na ni mwana wa Salmoni na Rahabu. Ndiyo, Boazi ni Myahudi. Si kwamba Boazi ni bwana mwenye kuwafikiria watu wengine anayeheshimiwa sana na wafanya kazi wake tu, bali pia yeye ni mwabudu wa Mungu wa kweli aliyejitoa sana, kwa kuwa anawasalimu wavunaji kwa maneno haya, “[Yehova] akae nanyi,” nao wanajibu, “[Yehova] na akubariki.”—Rut. 2:1-4.
20 Kutoka kwa mwanamume kijana anayeangalia wavunaji, Boazi anajifunza kwamba Ruthu ndiye mwanamke Mmoabi aliyekuja Bethlehemu pamoja na Naomi hivi karibuni. Baada ya kupewa ruhusa, alikuwa amekuwa akiokota mavuno wakati wa asubuhi usio na jua kali mpaka kupanda kwa jua, akivumilia jua kali bila manung’uniko. Ila sasa tu alikuwa akikaa kwa muda kidogo tu ndani ya nyumba, ambayo kwa wazi ilikuwa ni kibanda tu cha wavunaji. Bila shaka Ruthu si mwanamke aliyeendekezwa!—Rut. 2:5-7.
21. Ni jambo gani aliionalo Ruthu ambalo linamvutia Boazi, na je! wanawake Wakristo wanaweza kuamua jambo lo lote kutokana na jambo hili?
21 Baadaye Boazi amhimiza Ruthu asiokote mavuno katika shamba jingine, bali afuatane na wasichana wake, ambao labda walifuata wavunaji wake wakifunga mavuno pamoja. Boazi amewaamuru vijana wasimguse, na anaruhusa ya kunywa maji kutoka katika vyombo ambavyo wamejaza. Kwa kuthamini sana, Ruthu kwa unyenyekevu anasujudu na kuinama mpaka chini, akauliza: “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni?” Basi, Boazi hajaribu kujifanya apendwe kwa kuwa yeye ni mwanamume mzee. Bali, yeye amesikia jinsi Mwanamke huyu Mmoabi alivyowaacha baba, mama na nchi yake, akashikamana na mkwewe mzee. Kwa wazi kwa kuvutwa na upendo mshikamanifu na unyenyekevu wa Ruthu, anasukumwa aseme: “[Yehova] na akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na [Yehova], Mungu, wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya [ulinzi wa] mabawa yake.” Kwa kweli, kama anavyokubali Ruthu, Boazi amemfariji na kumtia moyo kwa maneno yake.—Rut. 2:8-13; Zab. 9:1, 2, 4.
22, 23. (a) Boazi anamtendeaje Ruthu kwa ukarimu? (b) Ni kwa njia gani Ruthu anaonyesha bidii yake na kutokuwa na choyo kwake?
22 Wakati wa wavunaji kula chakula, Boazi amwambia Ruthu: “Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki [“divai iliyochacha”].” Lo! ni kitu cha kuburudisha namna gani wakati wa joto la mchana! Boazi amtolea Ruthu nafaka zilizookwa, akala akashiba, na zikabaki.—Rut. 2:14; linganisha The New English Bible.
23 Ukawa wakati wa kurudi kazini. Katika roho ya ukarimu, Boazi awaambia vijana wake wamwache Ruthu aokote “hata katika miganda” hata awaagiza “mtoleeni kidogo katika matita,” na kukiacha akiokote. Jioni inafika, na bado Ruthu anaendelea na kazi ‘akipiga,’ au kupura nafaka alizoziokota. Kwa kutumia fimbo katika kuzipiga nafaka kwa kutumia mkono sakafuni, mtu anaweza kutoa shayiri katika maganda yake. Basi, nafaka alizoziokota Ruthu kwa siku hiyo zikawa yapata efa moja ya shayiri! Akaichukua nyumbani Bethlehemu. Bila choyo, Ruthu pia atoa chakula kilichobaki wakati wa chakula cha mchana na kumpa mkwewe anayekihitaji.—Rut. 2:14-18.
24. (a) Kwa sababu gani si ajabu kwamba watu wanamwona Ruthu kuwa “mwanamke mwema”? (b) Kwa hiyo, kwa sababu gani Ruthu ni mfano mzuri kwa mwanamke ye yote anayemwogopa Mungu?
24 Ruthu anaonyesha Naomi upendo mshikamanifu mara nyingine. Ongeza kwa haya upendo wa mwanamke huyu kijana kwa Yehova, bidii na unyenyekevu wake, na si ajabu kwamba watu wanamwona kuwa “mwanamke mwema.” (Rut. 3:11) Bila shaka, Ruthu hali “chakula cha uvivu,” na kwa sababu ya kazi yake ngumu ana kitu cha kushiriki na mtu anayehitaji. (Mit. 31:27, 31; Efe. 4:28) Na kwa sababu ya kuchukua daraka juu ya mkwewe mjane mzee, mwanamke huyu Mmoabi anaona furaha inayotokana na kutoa. (Matendo 20:35; 1 Tim. 5:3-8) Kwa kweli, Ruthu ni mfano bora sana wa mwanamke ye yote anayemwogopa Mungu.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa mazungumzo juu ya maana ya unabii wa kitabu cha Ruthu, tafadhali tazama Mnara wa Mlinzi, Ago. 1, 1972, uku. 343-355, pia kitabu Preservation, uku.169-335, kilichochapwa mwaka 1932 na Watchtower Bible and Tract Society.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Ruthu amsihi Naomi: ‘Usinisihi nikuache wewe, kwa kuwa uendako na mimi nitakwenda’