Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w80 3/1 kur. 16-18
  • Mji Uliolindwa na Yehova

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mji Uliolindwa na Yehova
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • HALI YENYE HATARI YA YERUSALEMU
  • TISHO KWA UJENZI WA UKUTA
  • KURUDISHA TENA SHERIA ZA KIMUNGU
  • Kitabu Cha Biblia Namba 16—Nehemia
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Nehemia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
  • Kuta za Yerusalemu
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Mmetakaswa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
w80 3/1 kur. 16-18

Mji Uliolindwa na Yehova

IWAPO twatumikia Mungu kwa kuongozwa na dhamiri, na kushikamana na Neno lake, tutafaulu, hata ingawa huenda tukapatwa na mambo mengi yenye kuleta magumu, na yenye kujaribu imani. Na tukiendeleza imani na kumtumainia Mungu, twaweza kuitegemea ahadi hii: “Malaika wa [Yehova] hufanya kituo, akiwazunguka wamchao na kuwaokoa.”​—Zab. 3:7.

Kwa upande ule mwingine, hata tufanye kwa bidii namna gani, tunayofanya hayatafaulu iwapo tutategemea uweza wetu wenyewe, au wa wanadamu. Mfalme Sulemani alitaja kweli hii katika Zaburi: “[Yehova] asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure.” (Zab. 127:1) Kanuni hii ilionyeshwa katika ule uharibifu na baadaye kurudishwa tena kwa Yerusalemu wa kale.

Katika siku za Wafalme Daudi na Sulemani, Yerusalemu ulikuwa mji wenye kusitawi, mji mkuu wa taifa lenye nguvu. Walakini, kwa sababu ya kupuza sheria ya Mungu, na uonezi na upotovu uliofuata kama matokeo yake, mji huo ulipata kuwa mwovu sana. Mwishowe, Mungu aliondoa mkono wake wenye kuulinda. Ingawa ulikuwa na nguvu sana na kusimamishwa mahali pazuri pa kujikinga, Yerusalemu ulianguka mikononi mwa mfalme wa Babeli, ambaye aliufanya mji huo kuwa ukiwa kabisa.

Walakini Mungu alikuwa na mafikira mazuri kuelekea Yerusalemu ulioachwa mahame. Yeye alikuwa ameweka hekalu la ibada huko; jina lake lilishikamanishwa na mji huo. Yeye alikuwa na nia ya kutaka ujengwe upya. Je! ni wanadamu waliofikiria wazo hilo, au je! kurudishwa tena kwa mji huo kulifanywa kupitia kwa nguvu zao? Hasha. Kujengwa kwake upya kulikuwa mwujiza, hata machoni pa mataifa waliowazunguka.

Hekalu lilijengwa upya na hesabu ndogo ya Wayahudi ambao walifunga safari ya maili 500 (kilometres 805) yenye hatari kuvuka jangwa. (Ezra 6:15) Hata hivyo, kuonyesha kwamba kurudishwa tena kwa Yerusalemu hakukuachiwa wanadamu, na wanadamu wasingeweza kusifiwa kwa uwezo au kuazimia kwao, ulikuwa ukweli wa kwamba warejeaji hawa wa kwanza, kwa sababu ya upinzani kutoka kwa watu wenye kuwazunguka walidhoofika na mwishowe wakaanza kujishughulisha kabisa na mambo yao wenyewe. Waliharibika mpaka kwenye hali yenye kusikitisha sana, wakashutumiwa na adui zao, nayo mashutumu hayo yalielekea kwa Mungu waliyemwakilisha.

HALI YENYE HATARI YA YERUSALEMU

Yapata miaka 82 baada ya kurudi kwa warejeaji wa kwanza, Myahudi mmoja aliyeitwa Nehemia, aliyekuwa akitumikia kama mnyweshaji wa Mfalme Artashasta (Longimano) wa Uajemi, alipata habari kutoka kwa ndugu yake, Hanani, na watu wengine wa Yuda, juu ya hali yenye kusikitisha ya mji wa Yerusalemu. Waliripoti hivi: “Watu wa uhamisho, waliosalia huko . . . wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa [kulikuwa matundu makubwa ukutani], na malango yake yameteketezwa kwa moto [namna ambavyo mfalme wa Babeli alivyokuwa ameyaacha].”​—Neh. 1:1-3.

Jambo hili lilimfadhaisha Nehemia sana. Yeye alimwomba Mungu, hata alipokuwa akitoa ombi lake kwa Mfalme Artashasta, kwamba aruhusiwe kurudi apate kuwatia nguvu na kuwasaidia ndugu zake. Mungu alichochea moyo wa mfalme ampe Nehemia walinzi na watumishi, pamoja na mamlaka ya kupata vitu vya kujengea kutoka kwa maliwali wa sehemu hiyo.​—Neh. 2:3-9.

Kwa sababu ya uchungu wa moyoni wa adui waliokuwa kwenye ujirani, na hata wa Wayahudi fulani ambao waliendelea kupashana habari nao, hapo kwanza Nehemia hakumwambia mtu ye yote juu ya mpango wake. Yeye alipeleleza kadiri ya uharibifu na kukadiri yaliyopaswa kufanywa. Kisha akawakusanya makuhani, wa-kuu, watawala wasaidizi na wale ambao wangesimamia kazi ya kujenga upya na kuwagawia malango na sehemu fulani za ukuta. Mpango huo ulisonga mbele. Hata hivyo, tendo hili lilikabiliana na dhihaka kali kutoka kwa Sanbalati Mhoroni na Tobia Mwamoni, viongozi wa kabila jirani, ambao walifanya hila ya kuwaua wafanya kazi hao. Kwa sababu ya hili Wayahudi walisali kwa Mungu na kusimamisha mlinzi mchana na usiku.​—Neh. 4:1-9.

TISHO KWA UJENZI WA UKUTA

Mkazo wa kazi na mgawo wa ulinzi ulikuwa mwingi. Wafanya kazi wakavunjika moyo, walakini Nehemia alivuta fikira zao kwa Mlinzi wao wa kweli kwa maneno haya: “Mkumbukeni [Yehova], aliye mkuu mwenye kuogofya.” (Neh. 4:14) Nehemia aliwapa mgawo watumishi wake wa kipekee, nusu yao wafanye kazi na nusu nyingine wabebe silaha. Kila mbebaji wa mzigo (wa vitu vya kujengea na takataka) alifanya kazi kwa mkono mmoja, akishika silaha mkononi mwingine, huku kila mjenzi akiwa amefunga upanga kiunoni. Walipolala walibaki wamevalia mavazi yote, silaha zao zikiwa kwenye mkono wao wa kuume.

Wakiwa wanataka sana kuzuia kurudishwa upya kwa Yerusalemu, kwa hila adui hao walijaribu kumvuta Nehemia kwa mazungumzo (kwa kusingizia yalikuwa mazungumzo ya amani ya kusuluhisha tofauti zao), walakini kusudi hasa lilikuwa kumwua au kumteka nyara. Kwa kushindwa katika jambo hili, walitumia manabii wa uongo waliokuwa wakiishi katika Yerusalemu kusudi wajaribu kumwogopesha Nehemia. Walakini, akiwa anamtumaini Mungu, yeye hakukubali kuvutwa.​—Neh. 6:1-13.

Mwishowe, baada ya siku 52 (ambazo kwa kweli ndizo zilizokuwa kama kipimo ambacho wajenzi hao wangeendelea kufanya kazi chini ya hali hizo zenye kujaribu) ukuta ulimalizwa kujengwa. Kisha milango ya malango ikawekwa mahali pake na jeshi la walinzi likapewa mgawo. Walakini kazi nyingi ya kufanywa ya ndani ilibaki. Watu hao walihitaji maarifa yaliyo kamili zaidi ya sheria ya Mungu. Mambo fulani yasiyo ya kawaida na yasiyopatana na sheria yalihitaji kukaziwa fikira. Nehemia alikuwa anafahamu kwamba Mungu alikuwa amekuwa nao, na kwamba sheria Yake ilipaswa kutendeshwa kazi na kufuatwa tena katika Yerusalemu iwapo kibali Yake ingeendelea.​—Neh. 6:15; 7:4.

KURUDISHA TENA SHERIA ZA KIMUNGU

Hivyo, Nehemia aliadhimisha sikukuu ya mwezi mpya katika mwezi wa saba, na kufuatisha sikukuu ya vibanda, tangu siku ya 15 mpaka ya 22; kisha katika siku ya 24 Wayahudi hao walikutanika ili wafunge kula na kuungama dhambi zao. Katika pindi hizo zote kuhani Ezra alisoma kwa sauti kuu torati ya Musa mbele ya watu waliokusanyika.​—Neh. 8:l–9:3.

Hata wakati huo, Yerusalemu ulikuwa na idadi ndogo sana ya watu. Kwa hiyo wenye kujitolea walitafutwa, jamaa moja kati ya kila kumi yenye kukaa nje ya mji, ipewe mahali pa kuishi katika Yerusalemu kwa njia ya kura. Vilevile, Nehemia alipanga ushuru wa hekalu uanzwe tena, kulipa zaka na dhabihu za mazao ya kwanza, ili kwamba ibada ya kweli kwenye hekalu ipate kurudishwa tena kwa kupatana na Torati. Mambo hayo yalipowekwa kulingana na utaratibu, ukuta wa mji ulizinduliwa kwa shangwe kubwa. Lazima liwe lilikuwa jambo la kusisimua kuona maandamano yenye kuvutia ya vikundi viwili vikubwa vya waimbaji wenye kutoa shukrani vikiimba huku vikipiga hatua kuzunguka juu ya ukuta huo.​—Neh. 10:32–11:2; 12:27-39.

Hata hivyo mambo mengine yangali yalihitaji kukaziwa fikira. Upotovu na kupuza vilikuwako kuhusiana na ibada hekaluni. Wakati Nehemia alipoondoka kwa muda akamtumikie Artashasta, Eliashibu kuhani aliweka kando jumba la kulia kwa ajili ya Tobia Mwamoni. Huku kulikuwa kuvunja kubaya sana kwa sheria ya Mungu. Vilevile, Walawi walikuwa wamenyimwa posho lao lililoagizwa na sheria kwa ajili ya kujiruzuku na, kama matokeo yake, iliwalazimu kufanya kazi nyingine kusudi wajiruzuku. Aliporudi na kugundua matukio haya yenye kushtua, mara moja Nehemia alitupa nje vyombo vyote vya Tobia na kulirudisha jumba hilo kwenye kazi yake ifaayo kama ghala la hekalu. Kisha akafanya mipango ya kugawa nafaka, divai na mafuta yenye kuhitajiwa na Walawi.​—Neh. 13:4-14.

Nehemia alifahamu kwamba, iwapo sheria ya Mungu ilikuwa ikivunjwa, Yeye asingebariki mji huo, hata ingawa Alikuwa ameufanya utengezwe upya. Mapema zaidi, Nehemia alikuwa amekomesha zoea la kutoza riba na kuweka vizuizi kuzuia nyumba na mashamba kwa upande wa Wayahudi walio matajiri zaidi. Sasa alikataza kazi yote na mapatano ya kibiashara wakati wa Sabato. Isitoshe, aliwaamuru wafanya biashara wa kutoka nje wasiingie Yerusalemu wakati wa Sabato. Mwishowe, alirekebisha mapatano ya ndoa yasiyokuwa halali ambayo katika hayo Wayahudi walikuwa wakiwapa wanaume wageni binti zao na kupata wana wao wake wageni.​—Neh. 5:1-13; 13:2-27, 30.

Kazi ya Nehemia, ambayo ilifanywa kwa kushirikiana na kuhani Ezra, haikuwa bure. Yehova aliwatumia watu hawa waaminifu, walakini yeye mwenyewe hasa Ndiye aliyesitawisha na kulinda mji, hata kwamba, zijapokuwa jitihada zote za adui za kuuharibu, Yerusalemu ungali ulikuwako miaka 400 baadaye, wakati Masihi na mitume wake walipokuwa duniani, Hivyo, Yerusalemu ulikuwa mji ambamo katika huo nafasi yenye utukufu ya kuwa mrithi wa shirika pamoja na Kristo ilianza kutolewa ‘kwanza kwa Wayahudi na kwa Wagiriki pia.’​—Rum. 2:10.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki