Imani Katika Mungu Ilinitegemeza
Kama ilivyosimuliwa na Harald Abt
KATIKA SEPTEMBA mwaka 1940 nilipelekwa kwenye kambi ya mateso ya Sachsenhausen katika Ujeremani. Maafisa wa SS (Askari kanzu wa Hitler) walinikaribisha ‘kwa uchangamfu’; nikapigwa mara nyingi kisha nikaogopeshwa. Akielekeza kidole kwenye bomba la moshi la mahali karibu pa kuchomea maiti za watu, afisa mmoja akanionya akisema: “Kabla hazijamalizika siku 14, utakuwa ukipaa kwa Yehova wako ikiwa unashikamana na imani yako.”
Halafu nikapelekwa mahali ambako ndugu zangu Wakristo, Mashahidi wa Yehova walikuwa. Niliamriwa kuchuchumaa na mikono yangu ikiwa imenyoshwa mbele yangu. Nililazimika kuchuchumaa hivyo muda wa saa nne. Nilifurahi kama nini ilipofika saa 12 za jioni kuwaona Mashahidi wakirudi kutoka kwenye kazi yao ngumu waliyofanya siku hiyo!
Mashahidi hao—mwanzoni wakiwa idadi ya 400—waliniambia ya kwamba ndugu zao karibu 130 walikuwa wamekufa kwa sababu ya kuteswa kikatili wakati wa majira ya baridi yaliyokuwa yametangulia. Je! kuteswa huko kulikuwa kumewaogopesha wale waliosalia? Hata kidogo, walikuwa thabiti vilevile kama mimi kuendelea kushikamana na Mungu.
Lakini kabla ya kusimulia mengi zaidi yaliyonipata muda wa miaka karibu mitano katika kambi za mateso za Sachsenhausen na Buchenwald, acha nisimulie kifupi namna ilivyokuwa hata nikapelekwa huko.
WAKRISTO KATIKA NYAKATI ZA TAABU
Mimi nilizaliwa katika upande wa kusini wa Poland, katika sehemu ambayo zamani ilikuwa ya Austria; basi nikakua nikiwa ninasema lugha ya Poland na Kijeremani vilevile. Katika mwaka 1931, nikiwa mwenye umri wa miaka 19, niliingia Chuo cha Kazi za Ufundi katika Danzig (Kipoland ni Gdansk), kisha ‘Mji Huru’ usemao Kijeremani katika Bahari ya Baltic. Huko ndiko nilikokutana na Elsa mwaka 1934, mwanamke kijana ambaye angegeuza sana maisha yangu.
Katika mwaka 1936, nilipokuwa nikijitayarisha kufanya mitihani yangu ya mwisho, Elsa alianza kwenda kwenye mikutano ya Mashahidi wa Yehova. Mikutano hiyo ilifanywa kwa siri, kwa kuwa Mashahidi wengine wakati huo walikuwa wamekwisha kukamatwa. Nikataka kumjulisha Elsa nilivyoona kuwa upumbavu kwake kujitia katika mambo ya watu hao. Lakini mwishowe akanishawishi nifuatane naye kwenye mkutano. Badala ya kutafuta makosa, nilivutiwa na maarifa ya Biblia waliyokuwa nayo Mashahidi hao.
Nilipomaliza masomo yangu katika chuo kikuu, hazikuwako nafasi nzuri zo zote za kupata kazi katika Poland. Basi nikafikiria kwenda Ujeremani nikatafute kazi huko. Lakini Elsa akasema: “Ukienda huko, basi utakwenda peke yako.” Mashahidi wa Yehova walikuwa wakiteswa vikali sana katika Ujeremani, naye Elsa hakutaka ajihatirishe bure. Jambo hilo likanifanya nifikiri, hivyo nikaanza kujifunza Biblia kwa kawaida zaidi. Katika Juni 1938 tukaoana. Kisha mapema mwa mwaka 1939 Elsa na mimi wawili tukabatizwa, tukionyesha kwa njia hiyo kujiweka kwetu wakf kwa Yehova Mungu.
Wakati huo nikawa nimekwisha kupata kazi nzuri ya uhandisi (engineer) katika idara ya usimamizi wa bandari ya Danzig. Tulikuwa na nyumba nzuri iliyopambwa na kuwekwa viti ndani, nayo ilitumiwa kwa ajili ya mikutano ya Biblia. Wakati kama huo, vitabu vyetu vya kujifunzia Biblia, vilivyopelekwa kutoka afisi ya tawi ya Poland katika Loz, vilikuwa vikizuiwa katika Danzig. Nikiwa na hakika kwamba lazima nijaribu jambo fulani, nikawaandikia ndugu zetu Wakristo katika Loz, nikishauri wapeleke vitabu kwenye anwani iliyo nje ya Danzig. Huko ndiko Elsa nami tungekwenda kuvichukua na kuviingiza kisiri mjini.
Wakati huo Elsa alikuwa mjamzito (mwenye mimba), na mara nyingine alikuwa akifunga magazeti 100 ya Mnara wa Mlinzi kuzunguka kiuno chake, chini ya mavazi yake. Wakati mmoja afisa wa forodha (duane) alimwambia hivi kwa dhihaka: “Mama wee! bila shaka utazaa watoto watatu wewe!” Lakini hakuchunguzwa ‘hata kidogo. Basi tukaendelea kuingiza vitabu kwa siri mpaka Wajeremani waliposhambulia nchi ya Poland mwezi wa Septemba 1, 1939, ndipo uhuru wetu wa kuingia na kutoka katika Danzig ukazuiwa. Binti yetu Jutta alizaliwa Septemba 24.
KUMHESHIMU HITLER?
Askari walinzi wa Poland walipokwisha kujitoa kwa Wajeremani, niliweza kuirudia kazi yangu. Salamu yangu ya kusema, “Habari za asubuhi,” iliwafanya wenzangu niliokuwa nikifanya kazi nao wanikodolee macho; sasa kila mtu alitakiwa aseme, “Heil Hitler” (“Wokovu Watokana na Hitler”).
Nikaomba ruhusu niseme na msaidizi wa mkurugenzi wa bandari na kueleza kwamba mimi ni Mkristo, nami siwezi kusalimu namna hiyo. “Basi, mimi vilevile ni Mkristo,” akajibu. Hata hivyo nikamwambia kwamba, mimi ni Mkristo halisi, na sioni yafaa kumpa mwanadamu utukufu kama huo. Nikafutwa kazi papo hapo na kuambiwa kwamba nisipomsalimu Hitler namna hiyo, ningefungwa gerezani.
Baadaye mwezi huo wa Septemba, majeshi ya Wajeremani yalipokwisha kushinda Poland, Hitler akaja Danzig. Akatoa hotuba yake kali ya ushindi katika uwanja mkubwa wa mji. karibu na nyumba tulimokuwa tukiishi. Kila mtu alitakiwa kupeperusha bendera nje ya dirisha, lakini nyumba yetu haikuonyesha bendera!
Ili tupate usalama, ndugu wakatushauri tuhamie sehemu ya mashariki ya Poland. Hiyo ilimaanisha kuacha mali zetu zote. Tukichukua sanduku la mavazi, kigari cha kuchukulia mtoto naye Jutta tukimfunga katika mto, tukaanza safari ndefu mwezi wa Desemba. Magari ya moshi yalisongamana watu, tena hayakuwa na utaratibu wa kusafiri.
Mwishowe, tukaifikia nyumba katika Lodz mahali ilipokuwa afisi ya tawi. Dada aliyefungua mlango alipoona mtoto mikononi mwa Elsa hasongisongi, aliondoka mbio mlangoni akaenda akilia. Zilipopita dakika chache akarudi, alipomwona mtoto akisongasonga, alipaza sauti hivi: “He! Kumbe yu hai! Yu hai!” Hapo ndipo alipotukaribisha tuingie ndani. Watoto wengi walikuwa wamekufa njiani kwa sababu ya baridi; hivyo akadhani Jutta naye amekufa.
KUKAMATWA NA KUFUNGWA GEREZANI
Mume wa dada huyo alikuwa amekwisha kufungwa tayari gerezani. Wakati huo ulikuwa wa baridi kali kwetu. Hatukuwa na makaa yo yote ya kupashia nyumba moto wala ya kupikia chakula kidogo tulichokuwa nacho. Mwishowe, nikaweza kupata kazi. Lakini siku moja katika Julai 1940, Gestapo (kachero, polisi wa siri wa Nazi) wakatukuta nyumbani, wakati walipokuwa wakimtafuta mtu mwingine. Elsa nami tukaagizwa tupige ripoti kwenye afisi ya Gestapo.
Asubuhi yake mimi nikaenda kazini, nikavikusanya vitu vyangu, nikamwambia mkubwa wa kazi kwamba ninalazimika kupiga ripoti kwa Gestapo na huenda nisirudi. “Aa-aa, huu ni upuzi tu,” akajibu. “Utarudi saa sita za mchana. Usihangaike.” Baadaye, dakika chache nikamkuta Elsa akiwa mbele ya afisi ya Gestapo, tukapanda pamoja kwenye chumba cha juu.
“Tafadhali ketini,” afisa akasema. “Twajua sababu iliyowaleta huku.” Kisha akatukumbusha kwamba sasa nchi ya Poland iko chini ya utawala wa Nazi, chama cha Ujeremani, na juu ya yaliyokwisha kuwapata Mashahidi wa Yehova katika Ujeremani. “Mkiendelea kusema juu ya imani yenu,” akasema, “mtapelekwa kwenye kambi ya mateso.”
Kisha akaenda kwenye taipuraita na kuanza kuandika. Aliporudi, alinipa karatasi iliyoandikwa. Ilisema hivi, sehemu yake: ‘Mimi, Harald Abt, naahidi kuacha kusema juu ya ufalme wa Mungu.’ Nikamwambia: “Nasikitika, siwezi kutia sahihi juu ya hayo.”
Nilipokwisha kuambiwa jinsi nilivyokuwa mpumbavu kwa kukataa kutia sahihi juu ya karatasi hiyo, nikatwaliwa. Elsa akahojiwa zaidi. Wakati wa kuhojiwa, Elsa alitaja kwamba tuna mtoto nyumbani mwenye umri wa miezi 10. “Hakuna mwingine awezaye kumlisha mtoto huyo,” Elsa akasema, “kwa sababu mimi namnyonyesha maziwa yangu.” Akihurumia mtoto huyo mchanga, afisa ‘huyo akasema: “Basi nitafanya kifupi.”
Maneno aliyoandika haraka yalikuwa tofauti na yale niliyokuwa nimekataa kutia sahihi yangu. Yalisema kwamba Elsa alijua ya kwamba kama angeendelea kufuata dini yake angepelekwa kwenye kambi ya mateso. Elsa akaona angeweza kutia sahihi juu ya hayo, kwa kuwa alikuwa anajua hivyo. Lakini alipokwisha kutia sahihi, aliogopa. Kwa sababu gani? Kwa sababu kama angeachiliwa huenda mimi ningedhani kwamba ameikana imani yake. Basi alipotoka kwenye afisi hiyo, aliniita kwa sauti kuu nikiwa kwenye pembe ya mbali ya jumba akisema: “Sikukana imani! Sikukana imani!”
Nilipokwisha kuzuiwa kwa muda wa juma chache, nikapelekwa gerezani katika Berlin na kutoka huko nikasafirishwa mpaka Sachsenhausen.
MAISHA KATIKA SACHSENHAUSEN
Baada ya kukaribishwa ‘kwa uchangamfu,’ maafisa wa SS walituchukua twende tukapokee mavazi ya gerezani. Nywele zetu zilinyolewa. Kisha tukapewa namba zetu—namba yangu ilikuwa 32,771. Kipande chenye umbo la pembe tatu, cha rangi ya urujuani, kilichotambulisha Mashahidi wa Yehova, kilitolewa kwangu nikishone kwenye mavazi yangu. Wafungwa wengine walitambulishwa kwa vipande vyenye umbo la pembe tatu vya rangi nyingine—wafungwa wa kisiasa walivaa chekundu, Wayahudi walivaa chenye rangi manjano, wahalifu walivaa cha rangi kijani, walawiti walivaa cha rangi nyeupe-nyekundu, na vivyo hivyo. Mimi ndiye Shahidi pekee niliyekuwa katika kikundi hicho.
Mashahidi wa Yehova walipewa nyumba yao peke yao. Nyumba hizo katika Sachsenhausen zilikuwa katika nusu mviringo kuzunguka uwanja mkubwa wa kuitia majina. Katika sehemu ya ukuta wa nyumba za wafungwa kuelekea uwanja huo kulikuwa na maneno yaliyoandikwa kama hivi: ‘Kuna njia inayoongoza kwenye uhuru: Imani, bidii, kazi na kupenda Nchi ya Uzalendo.’ Katika kila sehemu ya nyumba za wafungwa kulikuwako neno moja au mawili yenye kusema hivyo. Neno hili UPENDO lilikuwa kwenye nyumba za wafungwa ambazo Mashahidi waligawiwa. Huko ndiko nilikochuchumaa muda wa saa nne katika baridi.
Nyumba hizo kubwa mno—zikiwa zaidi ya 60—kila moja iligawanywa katika maeneo mawili ya kulala. Katikati yake kulikuwako eneo la kulia chakula, vyoo na maliwato (mahali pa kuogea). Sehemu za kulala zilizokuwa upande huu na upande huu zilikuwa zisizopashwa moto; vitanda vilifanywa katika safu tatu kwenda juu. Wakati wa majira ya baridi, hali ya baridi ilikuwa ikifika kwenye kipimo cha sentigredi 18, nasi tulikuwa na blanketi mbili tu nyembamba. Ile hewa iliyokuwa ikitolewa na watu wenye kupumua iliganda juu ya dari kisha maji yakadondoka chini na kufanyiza barafu juu ya blanketi za watu waliolala katika safu ya juu.
Sana sana, vyakula vyetu vilikuwa mchuzi uliofanyizwa kwa mboga, mara nyingine ukichemshwa pamoja na vichwa vya farasi. Pindi kwa pindi, tulikuwa tukipata mchuzi wa samaki wenye kunuka sana hata kambi nzima ikawa harufu tupu! Wakati wa usiku tulikuwa tukipewa mkate. Kwa kuwa kiamshakinywa kilikuwa ni kahawa ya kubandia tu, mimi nilikuwa nikiweka akiba ya mkate kidogo ili nile asubuhi, kwa sababu nilikuwa mwepesi wa kuona njaa.
Tulikuwa tukilazimika kuamka asubuhi saa kumi na mbili, tutandike vitanda vyetu, tuoge na kuvaa; kisha twende kwenye uwanja tukaitwe majina na kusafiri kwenda kazini. Sehemu kubwa ya kazi tuliyokuwa tukifanya ilifanywa nje ya kambi. Mgawo wangu wa kwanza ulikuwa kujenga barabara. Baadaye, kwa sababu ya mazoezi niliyopewa ya uhandisi, nilipewa kazi ya kusimamia ujenzi wa viwanda vipya vya kazi.
Maafisa wengi wa SS walikuwa wakatili sana, mara nyingi walikuwa wakitafuta tu njia za kututesea. Mara nyingine mmoja alikuwa akija wakati tulipokuwa kazini na kutafuta-tafuta mavumbi katika nyumba za kulala. Kwa kawaida aliweza kuyaona katika makombamoyo, ambayo si ajabu kwani vilikuwako vitanda vya majani makavu katika chumba kimoja karibu 80. Tuliporudi nyumbani kutoka kazini, alikuwa akitangaza hivi: “Niliona mavumbi katika nyumba yenu asubuhi hii, kwa hiyo hamtapata chakula cha mchana leo.” Ndipo walipokuwa wakiziondoa funiko, ili kila mmoja aone harufu ya chakula, na kuondoa mabirika. Lalamiko lo lote lingetokeza adhabu ya kifo.
Hakuna mtu aliyekuwa na hakika ya kuwa hai katika Sachsenhausen. Kama ungevuta fikira za askari walinzi katika njia ndogo, ungeweza kuadhibiwa. Huenda mtu akalazimishwa kusimama mbele ya nyumba za kulala mchana wote katika baridi kali ya kipupwe (majira ya baridi). Ikiwa angeshikwa na homa—wengi walishikwa na ugonjwa wa mapafu—asiweze kufanya kazi, askari SS angesema hivi: “O, ana homa! Vema sana, mwache asimame nje katika baridi kisha apoe.” Mateso hayo yaliua wengi.
Wengine waliuawa kwa njia hii: Waliamriwa kukaa katika bakuli kubwa la maji baridi wakati wa majira ya baridi kali sana, na bomba la maji baridi lililengwa moyoni mwao. Kwa sababu ya mateso kama hayo ya unyama, hatukujua kamwe kama tungeokoka mpaka kwenye masika yanayofuata.
Wengi wameniuliza hivi, “Hukuogopa?” Hapana, unapokuwa katika hali hiyo, unasitawisha nguvu kupitia kwa imani yako. Yehova anakusaidia uvumilie. Penye meza za chakula tulikuwa tukisali pamoja na hata kuimba kwa sauti ndogo wakati wengine walipokuwa mbali wasiweze kusikia. Kwa mfano, tuliposikia kwamba mmojawapo wa ndugu zetu amekufa kwa kuteswa kinyama au kwa kuachwa bila kupewa chakula, tuliimba wimbo kwa roho ya kupigana vita. Maoni yetu yalikuwa: Endelea kishujaa! Uwe hodari! Tulijua huenda tukafa hivi karibu, pia, nasi tulitaka tuonyeshe azimio letu thabiti la kuendelea kuwa waaminifu.
KULISHWA KIROHO NA KUHUBIRI
Tukapata nafuu kidogo (hali ikawa afadhali) katika mwaka 1942. Akaja mwingine mkuu wa kambi, nasi tukapata uhuru zaidi kidogo. Hatukulazimishwa tena kufanya kazi siku za Jumapili. Tena, wakati kama huo matoleo saba ya Mnara wa Mlinzi yaliyokuwa yakizungumza juu ya unabii wa Danieli, yalipenyezwa kambini. Vilevile, tulipata nakala chache za Biblia. Basi, alasiri za Jumapili tulikuwa tukikusanyika pamoja katika pembe moja ya nyumba za kulala ili tujifunze Biblia; tukifikia hesabu ya watu 200. Wachache walikuwa wakiwekwa nje ili watoe ishara ya kuonya iwapo askari SS ye yote angekaribia. Mikutano hiyo ilikuwa ya maana na yenye kutia imani nguvu, nisiyoweza kusahau.
Huenda ukasema, ‘Minara ya Mlinzi ikapenyezwa kambini.’ Hilo nalo ni jambo la imani na uhodari. Mashahidi wafungwa fulani walikuwa wakifanya kazi nje ya kambi nao walikuwa wakionana na ndugu waliokuwa bado kukamatwa. Kwa njia hiyo waliweza kupata vitabu kwa siri na kuvipenyeza kambini wanaporudi. Ndugu Seliger, aliyekuwa kama mwangalizi wetu kambini, alikuwa akifanya kazi katika hospitali ya gerezani, naye alikuwa akificha vitabu vya kujifunza Biblia vilivyopenyezwa nyuma ya kigae katika maliwato (chumba cha kuogea) huko.
Walakini, mwishowe tulijulikana namna tulivyokuwa tumejipanga kwa utaratibu sana. Vilevile, nakala fulani za Biblia zilipatikana katika nyumba yetu. Hivyo ndugu kama 80 hivi walitiwa katika kikosi cha kazi wakapelekwa mbali na Sachsenhausen. Mashahidi wale waliobaki walitawanywa katika nyumba mbalimbali za kambi. Ijapokuwa hiyo ilivunja mikutano yetu mikubwa, ilitoa nafasi nyingi zaidi za kuwahubiri wafungwa wenzetu.
Vijana wachache Warusi, Waukrainia na Wapoland waliitikia wakawa Mashahidi. Wengine kati yao walibatizwa kisiri mle mle kambini—ndani ya birika la kuogea katika hospitali ya kambi. Nawakumbuka sana sana vijana wawili wa kiume Waukrainia. Siku moja walisikia ndugu akiimba wimbo wa Ufalme kwa kupiga mbinja, wakamwuliza habari za wimbo huo. “Huu ni wimbo wa kidini,” ndugu huyo akasema. Walistaajabu sana kujua kwamba watu waliwekwa kambini kwa sababu ya imani zao za kidini. Baada ya kukombolewa, mmojawapo hao vijana aliongoza katika kazi ya kutoa ushuhuda katika sehemu ya mashariki ya Poland. Aliuawa na adui za Mashahidi wa Yehova alipokuwa njiani kuelekea kuongoza mkutano wa Kikristo.
Siku moja katika mwaka 1944, nilipokuwa nikienda kiaskari pamoja na kikosi changu cha kazi kwenye chakula cha mchana, nikawaona ndugu zangu wamesimama katika uwanja wa kambi. Nilipojulikana kuwa Shahidi, nikaambiwa niungane nao. Yaonekana kama askari SS walikuwa wamejua namna tunavyopokea na kupeleka barua kambini (na kutoka kambi kwa kambi), vilevile namna ambavyo tungekutana katika vikundi vidogo vya watu wawili au watatu katika uwanja wa kuitia majina kisha tuzungumze andiko la siku juu ya Biblia. Tuliamriwa tuache shughuli hiyo haramu, lakini sisi tuliungana katika azimio letu la kuendelea kutiana nguvu kiroho. Wakati Ndugu Seliger, aliyekuwa njia kuu ya kuwasilia barua kisiri, alipoulizwa kama ataendelea kuhubiri kambini, alisema hivi: “Ndiyo, hivyo ndivyo nitakavyofanya hasa, wala si mimi peke yangu, bali na ndugu zangu wote pia.” Roho hiyo ya imani na uhodari waliyokuwa nayo Mashahidi wa Yehova, ilionekana wazi kwamba haikuwa imevunjwa, nao wafuasi wa chama cha Nazi wakapata kuona tena kwamba hakuna lo lote ambalo wangeweza kufanya ili wavunje ukamilifu wetu kwa Mungu.
BUCHENWALD NA KUKOMBOLEWA
Kuelekea mwisho wa Oktoba 1944 nilipelekwa kwenye kambi ya mateso ya Buchenwald, pamoja na kikosi cha wataalamu wa ujenzi. Tulitakiwa tujenge upya viwanda fulani vya kazi vilivyokuwa vimeharibiwa kwa makombora yaliyolipuliwa na ndege za Kiamerika. Upesi ndugu waliokuwa katika Buchenwald walipata habari zangu wakanikaribisha nishiriki nao ushirika wa kiroho. Namba yangu huku ikawa 76,667.
Karibu na mwanzo wa mwaka 1945 ikaonekana wazi kwamba utawala wa Nazi ulikuwa ukikaribia kuanguka. Ndege za vita za Waingereza ziliporuka juu ya kambi, zilitusalimu kwa kuinamisha mabawa yazo upande na upande, zikijaribu kututia moyo. Juma mbili za mwisho kabla ya kukombolewa kwetu, wafungwa hawakwenda tena hata kazini.
Jumatano, Aprili 11, 1945, tulikusanyika tumsikie ndugu akitoa hotuba kusimulia Maandiko yote ya mwaka tangu mwaka 1933, wakati Hitler alipoanza kutawala, mpaka mwaka 1945. Mkutano ulipoendelea, tuliweza kusikia mshindo wa vita ukikaribia zaidi na zaidi. Kisha, hotuba ilipofika katikati, mfungwa mmoja alifungua mlango wazi akapaza sauti akisema: “Tuko huru! Tuko huru!” Kukawa na fujo kambini, lakini sisi tukatoa sala ya kumshukuru Yehova, kisha tukaendelea na mkutano wetu.
Bado kulikuwako wafungwa zaidi ya 20,000 katika Buchenwald. Wale askari SS walivua mavazi yao ya kiaskari na kujaribu kutoroka, na huku wafungwa wengi wakijilipiza kisasi juu yao. Baadaye mfungwa mmoja aliniambia namna alivyokuwa amemchoma kisu SS mmoja tumboni mwake. Lakini, Mashahidi wa Yehova hawakushiriki jeuri hiyo.
Ilikuwa karibu baada ya mwezi mmoja ndipo nikamwona Elsa mwishowe. Alikuwa ameokoka kuishi katika Auschwitz na kambi nyingine za matesi. Katika Agosti 1945 tukarudi nyumbani na kumkuta binti yetu akiwa pamoja na ndugu fulani waliokuwa wamemlinda. Wakati huo alikuwa mwenye umri wa miaka sita naye hakututambua.
BILA KUKANA IMANI KAMWE
Baada ya kukombolewa katika kutwaliwa na jeshi la Kijeremani, Poland ikawa Jamhuri ya Watu. Mara hiyo Elsa na mimi tulijaza ombi la kufanya kazi katika afisi ya tawi ya Sosaiti katika Lodz. Tulifanya ‘kazi huko muda wa miaka mitano, tukifurahi kuona hesabu ya Mashahidi wa Yehova ikiongezeka kutoka 2,000 katika mwaka 1945 kufika karibu 18,000 katika mwaka 1950. Kwa muda wa miaka mingi tangu mwaka 1950, tumeendelea kutumikia katika migawo mbalimbali tuliyopewa na tengenezo la Yehova, tukiazimia sikuzote kuwa hodari katika imani.
Kwa jumla, nimetumia miaka 14 ya maisha yangu katika kambi za mateso na magereza kwa sababu ya kumwamini Mungu. Nimeulizwa hivi: “Je! mke wako alikuwa msaada kwako katika kuvumilia yote ‘hayo?” Amekuwa hivyo kweli kweli! Nilijua tangu mwanzoni kwamba hangekana imani yake kamwe, na ujuzi huo ulinisaidia kunitegemeza. Nilijua kwamba ingekuwa afadhali kwake kuona nimekufa katika machela kuliko kujua kwamba nimeachiliwa kwa sababu ya kukana imani yangu. Ni msaada kweli kweli kuwa na mwenzi hodari kama huyo. Elsa alivumilia taabu nyingi wakati wa miaka yake ya kuwa katika kambi za mateso za Ujeremani, nami nina hakika kwamba utatiwa moyo kusoma mambo aliyoona katika toleo linalokuja la Mnara wa Mlinzi.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Sachsenhausen
SS Barracks
Roll-Call Square
Gas Chamber
Cell Building
Isolation
Delousing Station
Place of Execution