Neno la Mungu Li Hai
Upendo Thabiti wa Msichana
KUNA jambo lililo zuri sana kuhusu upendo thabiti kati ya mwanamume na mwanamke. Upendo huo uendeleapo ijapokuwapo mikazo mikubwa kutokana na vyanzo vingine vya kuvunja mapenzi kama hayo yaliyoimarika sana, hata maono ya moyoni ya watazamaji yanachochewa.
Ebu chukua kisa cha msichana wa Mashariki kutoka Shunemu, au Shulemu. Anampenda mchungaji mwenye umbo zuri. Wakijitahidi kumlinda Mshulami huyo asipatwe na majaribu, ndugu zake wamkataza asikubali mwaliko wa mpenzi wake kwenda matembezi pamoja naye katika siku nzuri ya wakati wa masika. Wamweka akalinde shamba la mizabibu lisiharibiwe na mbweha wadogo.—Wim. 1:6; 2:8-15.
Wakati wa kipindi hiki, Mfalme Sulemani aja na sherehe za kifalme na kupiga kambi karibu na nyumbani kwa yule Mshulami. Mfalme akamwona Mshulami alipokuwa akifanya kazi zake. Kwa sababu ya uzuri wake aletwa katika kambi ya mfalme na kuyakabili maposo yake.—Wim. 6:11, 12; 1:2-4.
Je! Mshulami huyo anavutiwa? Hapana. Bila kuona haya asema namna anavyomtamani sana mpenzi wake mchungaji. Walakini Sulemani hataki kumwachilia aondoke, aendelea na maposo yake na kumwahidi kwamba atamfanyizia mapambo mazuri sana. Hata hivyo, yule Mshulami azungumza tu juu ya namna anavyompenda mchungaji wake kwa upendo usiovunjika. Baadaye, mchungaji huyo apashana habari naye, nao wote wawili wafurahia mazungumzo ya mapenzi.—Wim. 1:7-17; 2:1, 2.
Arudipo Yerusalemu, Mfalme Sulemani amchukua yule Mshulami na kwenda naye. Humo mjini, yule mchungaji apata njia ya kumwona. (Wim. 3:6-11; 4:1-5) Baada ya jitihada zake zote za kumfanya Mshulami huyo ampende kushindwa, mwishowe Sulemani amruhusu arudi nyumbani. (Wim. 8:5a) Loo! ushindi kama nini kwa Mshulami huyo.
Kwa hakika msichana huyo wa mashambani ni mfano bora sana wa upendo wenye kuendelea, upendo ambao haungeweza kupotoshwa. Upendo kama huo ndio walio nao kwa “mchungaji mwema” wao wale washiriki wa kweli wa bibi-arusi wa kiroho wa Kristo, na vilevile wale wa “kondoo wengine” wake.—Linganisha Yohana 10:14, 16; 2 Kor. 11:2; Waefeso 5:25-32.