Rebeka—Abarikiwa na Yehova
YEHOVA Mungu aliongoza kuchaguliwa kwa Rebeka awe mke wa mwana wa Abrahamu, Isaka. Lakini sababu gani Rebeka alichaguliwa? Lazima sifa zake ziwe zilikuwa nzuri sana kwa maoni ya Mungu. Lazima awe alifaa kusudi lake la kuwa mama ya taifa ambalo lingekuwa watu kwa ajili ya jina lake.
Baada ya kifo cha mkewe mpendwa Sara, Abrahamu alifanya mipango apate mke kwa ajili ya mwanawe Isaka, ambaye sasa alikuwa na umri wa miaka 40. Akiwa hataki mwanawe aunganishwe na mtu asiye mwabudu wa Yehova, Abrahamu akauliza msimamizi wa nyumba yake, yaelekea sana mtumishi wake mwaminifu Eliezeri, asafiri mbali hadi Mesopotamia. Hakumtajia mtumishi wake maagizo ya kumwongoza. ‘Malaika wa Yehova atafanya hivyo,’ Abrahamu akasema kwa uhakika. Alitumaini Aliye Juu Zaidi ataonyesha ni msichana yupi kati ya watu wa ukoo wake atakayefaa Isaka.—Mwa. 24:1-9.
Mtumishi wa Abrahamu akachukua ngamia 10 waliobeba zawadi za thamani. Akiwa pamoja na watumishi wake, akasafiri kwa siku nyingi, mwishowe akafika kwenye mji wa Nahori katika upande wa juu wa bonde la Mesopotamia. Akiwa amechoka na mwenye kiu, akafika wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake vijana wa mji huo wanakuja kuteka maji kisimani. Hiyo ikawa nafasi kama nini ya kutenda kulingana na agizo la bwana yake! Walakini ajueje msichana wa kuchagua? Akamgeukia Yehova, akiomba kwamba chaguo lionyeshwe kwa dalili—kwamba msichana aliyechaguliwa akiulizwa ampe maji, vilevile ajitolee kunywesha ngamia wake,—Mwa. 24:10-14.
YEHOVA AJIBU SALA
Kabla ya mtumishi huyo kumaliza kuomba, msichana mwenye kuvutia sana akaja akiwa na mtungi wake juu ya bega lake. Hakuwa anajua huyo ni Rebeka, binamu ya kike wa Abrahamu. Mtumishi huyo akamwuliza hivi: “Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe.” Je! mwanamke huyo kijana angekuwa chaguo la Yehova? Kwa huruma, Rebeka akajibu: “Unywe, bwana wangu.” Akashusha mtungi wake haraka na kumpa maji. “Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa,” akasema. Basi haraka Rebeka akamwaga maji yaliyokuwa ndani ya mtungi wake kwenye birika la kunywea naye akakimbia tena na tena kwenye kisima ateke maji kwa ajili ya wale ngamia 10. Kazi nyingi kama nini! Ngamia mmoja anaweza kunywa karibu galani saba (lita 31.8) za maji kwa siku moja.—Mwa. 24:15-20.
Mtumishi huyo akafahamu kwamba kufikia hapo sala yake ya kutaka uongozi imejibiwa. Fikira zake zikavutwa kwa msichana mchanga mwenye sifa nzuri za huruma, nia na bidii ya kazi. Baada ya kumpa pete ya dhahabu ya kuweka puani ya bei kubwa na vikuku viwili vya dhahabu vyenye kuvutia, akauliza juu ya hali ya maisha ya jamaa yake na uwezekano wa kukaa usiku kucha ndani ya nyumba ya babaye. Mara moja, akajitambulisha na kusema hivi: “Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni.” Akimshukuru sana Yehova, mtumishi huyo akainama na kumbariki Aliye Juu Zaidi.—Mwa. 24:21-27.
Hakuna hata shaka dogo moyoni mwa Rebeka kuhusu kumwonyesha mwanaume huyo ukaribishaji wa kutoa vitu. Akakimbia nyumbani na kufanya matayarisho kwa ajili ya mgeni huyo asiyetazamiwa naye akaambia jamaa yake yaliyotokea. Akiisha kusikia jambo hilo, nduguye Labani akakimbia kwenye kisima na kukaribisha mgeni huyo. Karamu ikatayarishwa katika nyumba hiyo. Hakuna ye yote katika jamaa ya Rebeka ambaye amekwisha kuuliza juu ya mgeni huyo ni nani na mgawo wake ni nini. Wamekaza fikira kabisa wamwonyeshe yeye na watumishi wake ukaribishaji na kulisha ngamia wake.—Mwa. 24:28-32.
Hata hivyo, mtumishi wa Abrahamu, ana wazo moja peke yake akilini mwake —kutimiza mgawo wake kwa uaminifu kwa uongozi wa malaika wa Yehova. Kabla ya kukubali kula chakula, mtumishi huyo akajitambulisha na kueleza mgawo wake. Akaeleza juu ya alivyouliza dalili kutoka kwa Yehova na namna Rebeka alivyotenda kulingana na dalili hiyo. —Mwa. 24:33-49.
YEHOVA AONGOZA MAMBO
Jamaa ya Rebeka itaitikiaje? Ni dakika ya kungojea kwa hamu kama nini kwa mtumishi huyo! Wakiwa wamejawa na mshangao na heshima, Labani na Bethueli, ambaye ndiye baba, wakakubali kwamba yote hayo lazima yawe yametoka kwa Yehova. Wakaitikia hivi: “Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema [Yehova].”—Mwa. 24:50, 51.
Kuna msisimuko mwingi katika nyumba hiyo. Mtumishi huyo akaleta zawadi za thamani kwa Rebeka, mamaye na nduguye. Kisha wote wakala chakula kilichotayarishwa. Kulingana na desturi ya wakati huo, mambo hayo yaliyofanywa katika nyumba ya akina Rebeka yalitia ndani mkataba wa ndoa.—Mwa. 24:52-54a.
Lakini, ndipo, mama ya Rebeka na ndugu yake wakasihi wangojee angaa siku 10 kabla ya kumruhusu aende. Mtumishi huyo akasisitiza waondoke mara moja. Mwishowe, wakamruhusu Rebeka aamue. Wakamwita na kuuliza hivi: “Je! utakwenda na mtu huyu?” Kwa dakika hiyo lazima mtumishi huyo awe alikuwa anangojea kwa hamu sana. Je! ataondoka nyumbani mara moja aende kwa mume ambaye hajapata kumwona? Jibu la Rebeka litakuwa nini? Je! ana nia, na kwa hiyo je! atakubaliana na uchaguzi wa Yehova? “Nitakwenda,” akajibu Rebeka. Hakukawia, hakusita, hakutia shaka, hakuweka masharti! Ni msichana mwenye kutokeza kama nini! (Mwa. 24:8, 54b-58) Si kwamba tu anavutia sura, mwenye huruma, mwenye nia, mwenye bidii ya kazi na mkaribishaji; vilevile Rebeka ni mwenye kukata maneno, mwenye kuona wakati ujao na mwenye imani thabiti. Anaona mkono wa Yehova katika jambo hilo, naye hasiti kutenda kulingana na mapenzi Yake. Akiwa anajua kwamba mjomba wake Abrahamu amemzoeza Isaka amwogope Mwenye Nguvu Zote, Rebeka hana sababu ya kuwa na wasiwasi atakavyotendwa akiwa mke.
Mwanamke huyo kijana akaondoka na kupewa baraka na jamaa yake: “[Dada] yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao.” Yaya wake na watumishi wengine wanawake wakaandamana naye juu ya ngamia.—Mwa. 24:59-61.
Siku nyingi baadaye, wakati usio na joto jingi jioni, Isaka akaona msafara wa ngamia ukikaribia. Wakati uo huo,” Rebeka akamwona. Kwa uzuri na mara moja akashuka toka juu ya ngamia. Alipoambiwa mwanamume huyo ni nani, akajifunika uso, hivyo akaonyesha kutii na kuheshimu bwana-arusi. Kweli kweli, msichana ambaye amekuwa na nia ya kufuata uongozi wa Yehova, apande ngamia pamoja na mtumishi aende kwenye nchi asiyoijua ili akutane na bwana-arusi asiyemjua, bila shaka, ni mwanamke anayestahili kuonyeshwa shauku. Masimulizi ya Biblia yanasema hivi: “Akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamaake.”—Mwa. 24:62-67.
Rebeka akajionyesha kuwa mke ambaye Isaka alihitaji. Roho yake ya kutaka sana, shauku, bidii na kutaka kufanya mambo ikamfanya awe mwenye furaha tena maana alijaza vizuri nafasi iliyoachwa maishani mwake na kifo cha mamaye. Miaka mingi baada ya ndoa yao, Isaka aliendelea kupendezwa na Rebeka mpendwa wake. Aliogopa kumpoteza. Wakati njaa ilipomlazimisha akae kati ya Wafilisti, aliwaza juu ya uzuri wa Rebeka. Isaka akaogopa kupoteza uhai wake, akiwaza kwamba huenda mtu fulani akataka kumwua ili amchukue awe mke. Kwa hiyo, akijaribu kuzuia hilo, Isaka akajifanya kuwa ni nduguye.—Mwa. 26:1-11.
REBEKA AKIWA MAMA
Kama vile Sara, Rebeka akaendelea kuwa asiyechukua mimba kwa muda mrefu. Isaka akaendelea kumsihi Yehova kwa bidii kwa ajili yake. Mwishowe, miaka 20 baada ya ndoa yao, akazaa mapacha wake, wavulana Esau na Yakobo. Kabla ya kuzaa, Rebeka alijua kwamba angezaa mapacha. Mimba yake inataabisha sana. “Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini?” akatamka aliposikia vitoto hivyo vikifanya machachari (viking’ang’ana) ndani yake. Rebeka akapokea ahadi ya Mungu kwamba vikundi viwili vya kitaifa vingegawanywa tokea sehemu zake za ndani, kwamba mmoja angekuwa mwenye nguvu kuliko mwingine na kwamba mkubwa angemtumikia mdogo. Yeye hakusahau ahadi hiyo.—Mwa. 25:21-23.
Baada ya wavulana hao wawili kuzaliwa, Rebeka aliweka matumaini na shauku yake yote kwa Yakobo, na muda si muda Esau hata akadharau haki yake ya kuzaliwa. (Mwa. 25:28-34) Miaka ikapita, nayo siku ikaja Rebeka alipochukua hatua za kibinafsi kwa kupatana na ahadi ya kiunabii ya Yehova. Akasikia mumewe mzee na kipofu, Isaka, akimwita mwanawe mzaliwa wa kwanza, Esau. Kabla ya kufa kwake, Isaka anafikiria kuchagua na kubariki mrithi wake. Likiwa jambo la kutangulia kutoa baraka, Isaka akamtuma Esau nje akaue mnyama amtengenezee chakula kitamu.—Mwa. 27:1-4.
Akiwa anajua kwamba Esau siye aliyechaguliwa na Yehova, Rebeka akataka kumpatilia Yakobo baraka hiyo nzuri. Esau alipokuwa akiwinda, Rebeka akamwagiza Yakobo namna angeweza kupata baraka ambayo kwa haki ilikuwa yake. Yakobo akapinga, akiogopa kwamba babaye kipofu angemtambua kwa kumgusa na kisha amlaani. Walakini Rebeka alikuwa ameazimia kabisa. “Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu,” akasema kwa uhakika. “Usikie sauti yangu tu.” Naye Yakobo akasikiliza.—Mwa. 27:5-14.
Baada ya hayo Rebeka akamfanya Yakobo avae nguo za Esau, ambazo zilikuwa zinatoa harufu ya msituni, shambani na ya ardhi. Vilevile akachukua ngozi laini na iliyo kama hariri ya wanambuzi wachanga na kuweka vipande vyake kwenye mikono na shingo laini ya Yakobo, ili akiguswa na mikono ya Isaka awe kama Esau. Akiwa na chakula kitamu kilichotayarishwa na mamaye, Yakobo akaenda mbele ya Isaka. Mpango wa Rebeka ukafanikiwa. Yakobo akapata baraka za babaye, akifanywa kuwa mrithi wa haki wa Isaka na Abrahamu.—Mwa. 27:15-29.
Baadaye, Rebeka alipopata habari juu ya mipango ya Esau ya kumwua Yakobo, kwa mara nyingine alichukua tendo la kukata maneno kwa ajili ya Yakobo. Isaka akampeleka Yakobo kwenye nchi ya kwao ili atafute mke, hicho kikiwa ni kitia-moyo cha Rebeka. Rebeka alithamini maana ya Yakobo kuwa na mke mwema. Isaka pamoja naye walikuwa wamehuzunishwa sana na Esau aliyetwaa wake wawili kutoka kati ya Wakanaani wenye chuki.—Mwa. 26:34, 35; 27:41-46; 28:1-5.
Bila shaka Rebeka alimkosa sana Yakobo baada ya kuondoka kwake. Pengine alitumaini kwamba angerudi baada ya muda usio mrefu. Walakini Yakobo alikaa mbali kwa miaka 20. Hakuna maandishi yo yote katika Biblia juu ya Rebeka akimwona mwanawe mpendwa tena. Iwapo hakumwona tena, ebu wazia furaha ambayo Rebeka na Yakobo watakuwa nayo watakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Itasisimua Rebeka kama nini kujua juu ya pendeleo lake kubwa la kuwa kiunganishi chenye kuongoza kwa Masihi aliyeahidiwa, au Kristo!
Kweli kweli, Rebeka mwenye sura nzuri mwenye kuwa macho na mwenye kukata maneno, aliyepokea kibali ya Yehova ni mfano mwema kwa wasichana, wake na akina mama leo. Imani yake ilikuwa ya kusifika kweli kweli.