Maisha na Huduma ya Yesu
Makimbio ya Kuepa Mtawala wa Kutumia Mabavu
NI KWA sababu gani Yusufu anamwamsha Mariamu katikati ya usiku? ‘Malaika wa Yehova amenitokea muda mfupi tu uliopita,’ Yusufu anamwambia Mariamu. ‘Naye akaniambia nikuchukue wewe na mtoto tukimbilie Misri, kwa maana Herode karibuni atamwinda Yesu ili amuue.’
Wakiwa watatu, wanakimbia. Nao wanafanya hivyo wakati unaofaa kwa sababu Herode amejua kwamba wale wanajimu wamefanya ujanja na kuondoka nchini. Unakumbuka, walipaswa kurudi kwake wakiisha kumpata Yesu. Herode amechemka kwa hasira. Kwa hiyo katika jaribio la kumuua Yesu, anatoa maagizo wauawe katika Bethlehemu na wilaya zake wavulana wote wenye umri wa miaka miwili na chini. Msingi wa kupiga kwake hesabu ya umri huo ni habari aliyopokea mapema kwa wale wanajimu.
Machinjo ya watoto wote wavulana ni jambo linalochukiza sana kuona! Askari wa Herode wavunja na kuingia nyumba moja baada ya nyingine. Nao wakimkuta mtoto mvulana, wanamnyakua mikononi mwa mamaye. Hatujui ni watoto wangapi wanauawa, lakini kilio na majonzi makubwa ya akina mama yanatimiza unabii wa Yeremia, nabii wa Mungu.
Wakati huu, Yusufu na jamaa yake wamekwisha kufika Misri salama, nao wanaishi huko sasa. Lakini usiku mmoja kwa mara nyingine malaika wa Yehova anamtokea Yusufu katika ndoto. ‘Amka umchukue Yesu na mamaye mrudi Israeli,’ asema malaika huyo, ‘kwa maana wale waliokuwa wakitaka kumuua wamekwisha kufa.’ Kwa hiyo, kwa kutimiza unabii mwingine wa Biblia unaosema Mwana wa Mungu angeitwa atoke Misri, jamaa hiyo inarudi nchi ya kwao.
Bila shaka Yusufu anakusudia kufanya makao katika Yudea, walikokuwa wakiishi kabla ya kutorokea Misri. Lakini anapata habari kwamba mwana mwovu wa Herode, Arkelao, sasa ni mfalme wa Yudea, na katika ndoto nyingine Yehova anamwonya juu ya hatari hiyo. Kwa hiyo Yusufu na jamaa yake wanasafiri kaskazini na kufanya makao katika mji wa Nazareti. Yesu anakulia katika mtaa huo, mbali na makao makuu ya maisha ya kidini ya Kiyahudi. Mathayo 2:13-23; Yeremia 31:15; Hosea 11:1.
◆ Wanajimu walipokosa kurudi, Mfalme Herode alifanya jambo gani baya Sana, lakini Yesu alilindwaje?
◆ Aliporudi kutoka Misri, ni kwa sababu gani Yusufu hakukaa tena katika Bethlehemu?
◆ Ni unabii gani mbalimbali wa Biblia uliotimizwa wakati wa kipindi hicho?