Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w86 3/1 kur. 10-15
  • Ukamilifu wa Ayubu—Kwa Sababu Gani Unastaajabisha Sana?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ukamilifu wa Ayubu—Kwa Sababu Gani Unastaajabisha Sana?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maarifa ya Ayubu Yenye Kikomo
  • Suala la Ukamilifu wa Ayubu
  • Namna Nyingine ya Shambulio
  • Kujitetea kwa Ayubu na Kusahihishwa Kwake
  • “Sitaukana Utimilifu Wangu!”
    Igeni Imani Yao
  • Ayubu Alivumilia—Hata Sisi Twaweza!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Ayubu Alilitukuza Jina la Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Kitabu Cha Biblia Namba 18—Yobu
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
w86 3/1 kur. 10-15

Ukamilifu wa Ayubu​—Kwa Sababu Gani Unastaajabisha Sana?

“Mpaka nitakapokufa mimi sitaondoa ukamilifu kwangu mwenyewe!”​—AYUBU 27:5, Biblia ya New World Translation.

1. Ayubu alikuwa nani, na tunajuaje kwamba yeye alikuwa mtu halisi?

AYUBU alikuwa mwanamume wa kutokeza katika historia. Hakuwa na utajiri mwingi tu wa vitu vya kimwili, bali pia aliheshimiwa kuwa mwamuzi na kiongozi mwenye huruma. Biblia inasema kwamba alikuja kuwa “mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.” (Ayubu 1:3; 29:12-25) Yeye, pamoja na Noa na Danieli, anajulikana sana kuwa mtu mwenye uadilifu mwingi. (Ezekieli 14:14, 20) Pia Biblia inamwonyesha Ayubu kuwa mfano unaopasa kufuatwa na Wakristo, hivyo ikionyesha kwamba yeye alikuwa mtu wa kweli katika historia.​—Yakobo 5:11.

2. Tunaweza kukadiriaje ni wakati gani Ayubu alijaribiwa na Shetani?

2 Ayubu aliishi katika nchi ya Usi, katika ile sasa inayoitwa Uarabu. Ingawa hakuwa Mwisraeli, Ayubu alikuwa mwabudu wa Yehova, na Yehova alimweleza Shetani jambo hilo. Maneno ya Mungu kwamba “hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu” yanafunua kwamba hakukuwa na mtumishi mwingine wa Mungu mwenye kutokeza aliyekuwa akiishi wakati huo. (Ayubu 1:8) Hivyo, pasipo shaka kujaribiwa kwa Ayubu na Shetani kulitukia wakati binamu zake wenye uhusiano wa mbali naye, yaani Waisraeli, walipokuwa utumwani Misri​—wakati fulani katika ile miaka iliyofuata kifo cha mshika-ukamilifu wa kutokeza Yusufu mwaka 1657 K.W.K.. na kabla Musa hajauanza mwendo wake wa ukamilifu.

3. Ni nani aliyeandika kitabu cha Ayubu, na kwa sababu gani aliweza kupata habari hizo?

3 Kwa wazi Musa ndiye aliyekiandika kitabu cha Ayubu. Angeweza kuwa alipataje habari za kujaribiwa kwa Ayubu? Basi, Musa alipokwisha kulazimika kuondoka Misri mwaka 1553 K.W.K. alikaa Midiani, nchi isiyokuwa mbali na nchi ya Uzi. (Kutoka 2:15-25; Matendo 7:23-30) Wakati huo, Ayubu alikuwa akiimalizia miaka 140 ya mwisho ya maisha yake aliyobarikiwa na Yehova. (Ayubu 42:16) Baadaye, wakati Waisraeli walipokuwa karibu na Usi kuelekea mwisho wa safari yao ya jangwani, Musa angeweza kuwa alisikia habari za miaka ya mwisho ya maisha na kifo cha Ayubu.

Maarifa ya Ayubu Yenye Kikomo

4. (a) chanzo cha maarifa ya Ayubu ya kumjua Yehova kilikuwa nini, na kwa sababu gani bila shaka yeye angekuwa amekuwa akiwasiliana na Abrahamu na wazao wa Isaka? (b) ayubu alipataje kuwa mtu mwenye ukamilifu wa kutokeza?

4 Ayubu alipojaribiwa, maarifa yake ya kumjua Mungu na makusudi yake yalikuwa yenye kikomo, kwa kuwa hakuna sehemu ya Biblia iliyokuwa imekwisha kuandikwa. Lakini, Ayubu bila shaka alijua mambo fulani juu ya shughuli za Yehova pamoja na Abrahamu, Isaka, Yakobo, na Yusufu. Hiyo ni kwa sababu kwa wazi Ayubu alikuwa mzazo wa Nahori ndugu ya Abrahamu, kupitia Usi mwana mzaliwa wa kwanza wa Nahori. Tena, ndugu yake Usi alikuwa Bethueli, aliyekuwa baba ya Rebeka mke wa Isaka na pia babu mkuu wa Yusufu. (Mwanzo 22:20-23) Bila shaka Ayubu alipata kuyahifadhi sana maarifa yo yote aliyokuwa nayo juu ya mawasiliano ya Yehova na Abrahamu na wazao wake, naye alitaka sana kumpendeza Yehova. Hivyo Ayubu akawa mtu wa ukamilifu wenye kutokeza, mtu asiye na lawama na mwenye kujitoa kabisa kwa Yehova.

5. Ni jambo gani hasa linalofanya ukamilifu wa Ayubu uwe wa kutokeza sana?

5 Muda mfupi baada ya kifo cha Yusufu katika Misri, ukamilifu wa Ayubu ukawa jambo la kubishaniwa kati ya Yehova Mungu na Shetani katika mbingu zisizoonekana. Hata hivyo Ayubu hakujua lo lote juu ya ubishi uliotegemea ukamilifu wake. Na hasa kutokujua sababu yake ya kutaabika ndiko kunakofanya ukamilifu wa Ayubu usiovunjika uwe wa kustaajabisha sana. Lakini, kwa faida ya watumishi wote wa Mungu baadaye Yehova alimwagiza Musa aandike mambo yote ya ubishi uliohusu ukamilifu wa Ayubu.

Suala la Ukamilifu wa Ayubu

6. (a) Kusanyiko moja katika mbingu lilifunuaje kuwako kwa suala fulani kati ya Mungu na Shetani? (b) Ni wakati gani suala hilo lilipoanza, nalo lilitia ndani nini?

6 Kitabu cha Ayubu kinalifungua pazia la mambo yasiyokuwa yanaonekana halafu tunapewa maono ya mkutano wa malaika waliokusanyika mbele za Yehova Mungu. Humo Yehova anamkumbusha Shetani, ambaye pia yupo, kwamba “hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.” (Ayubu 1:8) Kwa wazi, kuna suala fulani linalotia ndani ukamilifu wa Ayubu. Lakini si suala jipya. Suala hilo liligusiwa wakati Shetani alipogeuza Adamu na Hawa, wakamwacha Mungu, kwa njia hiyo akawa ni kama anasema: ‘Wewe nipe tu nafasi nami naweza kugeuza mtu ye yote asikutumikie.’​—Mwanzo 3:1-6.

7. Shetani alilazimika kutoa madokezo gani juu ya ukamilifu wa Ayubu, na Shetani alimtolea Mungu mwito gani wa ushindani?

7 Sasa, wakati wa mkutano huu rasmi mbinguni, Shetani analazimika kutoa maelezo kuhusu ulio msingi wa ukamilifu wa Ayubu. “Je! huyo Ayubu yuamcha [Yehova] bure?” anauliza. “Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake. Na vitu wote alivyo navyo? . . . Lakini nyosha mkono wako sasa,” Shetani anatokeza mwito wa ushindani, “uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.”​—Ayubu 1:9-11.

8. (a) Yehova aliitikiaje mwito wa ushindani wa Shetani? (b) Shetani alimwangushia Ayubu dharuba gani kali kali?

8 Yehova anaukubali mwito wa ushindani unaotokezwa na Shetani. Yeye anautumaini kabisa ukamilifu wa Ayubu, akimjibu Shetani: “Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe.” (Ayubu 1:12) Shetani anampiga Ayubu haraka. Waseba wavamizi wanatoroka na ng’ombe 1,000 na punda-jike 500 wa Ayubu, wakiwaua watunzaji wao wote isipokuwa mmoja. Ndipo Shetani anapeleka moto kutoka mbinguni ukawale kondoo 7,000 wa Ayubu pamoja na watunzaji wao, wakiachilia mmoja tu. Halafu anavifanya vikosi vitatu vya Wakaldayo vitoroke vikiwa na ngamia 3,000 wa Ayubu, navyo vinaua watunzaji wote isipokuwa mmoja. Mwishowe, Shetani anapeleka upepo mkubwa unaopiga nyumba walimo watoto kumi wa Ayubu wanaokula karamu, na wote wanakufa. Baadaye, kwa mfuatano wa haraka, waokokaji wa misiba hiyo wanamletea Ayubu habari hizo zilizo mbaya sana.​—Ayubu 1:13-19.

9. Ni jambo gani lililofanya misiba ya Ayubu iwe migumu zaidi kuvumiliwa, hata hivyo Ayubu alitendaje alipopatwa nayo?

9 Loo, maafa yaliyoje! Hata kama Ayubu angefahamu ni nani mwenye kuyatokeza, bado ingekuwa vigumu kuyavumilia. Lakini yeye hafahamu! Yeye hajui kwamba ni kumhusu yeye hasa kwamba ubishi ulitokea mbinguni na kwamba Yehova alikuwa akimtumia yeye ili aonyeshe kwamba kuna watu watakaoshika ukamilifu wao zijapokuwa taabu zote za udhalimu ambazo Shetani anaweza kuwaletea. Hata hivyo, kwa kupigwa na kihoro na hata akifikiri kwamba kwa njia fulani Mungu amehusika katika kuleta hasara zilizompata, Ayubu anapaaza sauti: “[Yehova] alitoa, na [Yehova] ametwaa; jina la [Yehova] na libarikiwe.” Ndiyo, “katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.”​—Ayubu 1:20-22.

10. (a) Ni ruhusa gani nyingine ambayo Shetani aliomba apewe kuhusiana na Ayubu, na kwa sababu gani Yehova alikuwa na nia ya kumpa ruhusa hiyo? (b) Matokeo yalikuwa nini kwa Ayubu juu ya hali yenye kusikitisha aliyoingizwa ndani?

10 Kwenye mkutano mwingine wa malaika, Shetani alishushiwa heshima kama nini kwa kukumbushwa na Yehova hivi juu ya Ayubu: “Hata sasa bado anashika sana ukamilifu wake”! Lakini Shetani hachoki. Sasa anatoa mwito wa ushindani kwa kusema kwamba akipewa nafasi ya kumpiga Ayubu kimwili, Ayubu atamlaani Mungu mbele ya uso wake. Kwa kuutumaini ukamilifu wa Ayubu kwa kadiri hiyo, Yehova anatoa ruhusa. Onyo moja tu analompa Shetani ni kwamba asiondoe uhai wa Ayubu. Kwa hiyo Shetani ‘anampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa.’ (Ayubu 2:1-8) Hali ya Ayubu inazorota vibaya sana mpaka watu wa ukoo na marafiki wanamkwepa, nao waliokuwa wanafahamiana naye wanamdhihaki.​—Ayubu 12:4; 17:6; 19:13-19; 30:1, 10-12.

11. Ni dharuba gani nyingine ambayo Ayubu alipaswa kuvumilia, na ni jambo gani jingine lililofanya ushikaji ukamilifu wake uwe wa kusifika sana katika taabu zake zote?

11 Halafu pigo jingine tena! Imani ya mke wa Ayubu inadhoofika. Yeye anamwambia “Je! wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? umkufuru Mungu, ukafe”! Lakini yeye anamwambia mkeye: “Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya?” Kama yanavyosema masimulizi, “Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.” (Ayubu 2:9, 10) Nawe unapokumbuka kwamba sababu ya Ayubu kutaabika imefichwa asiijue, ukamilifu wake unaonekana kuwa wa kustaajabisha kama nini!

Namna Nyingine ya Shambulio

12. (a) Wanaume waliokuja kumfariji Ayubu walikuwa akina nani? (b) Shetani aliwatumiaje wanaume hao kuzidi kumjaribu Ayubu?

12 Lakini Shetani hajamaliza mambo yake. Anainua wanaume watatu wanaosemekana kuwa wenye hekima ambao ama walimjua Ayubu kibinafsi, ama walipata habari za sifa yake, kwamba “alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa mashariki.” Kwa wazi wao ni wazee sana kwa umri kuliko Ayubu. (Ayubu 1:3; 15:10; 32:6) Wawili kati yao ni watu wa ukoo ulio wa mbali. Elifazi Mtemani ni mzao wa Abrahamu kupitia Temani, mjukuu wa Esau, na Bildadi Mshuhi ni mzao wa Shua mwana wa Abrahamu. (Ayubu 2:11; Mwanzo 36:15; 25:2) Ukoo wa Sofari haujulikani kwa uhakika, Wanasingizia kwamba wamekuja kumfariji Ayubu, lakini kwa kweli Shetani anawatumia katika jitihada ya kubomoa ukamilifu wa Ayubu. Sawa na vile wanasiasa wenye kuuliza wafungwa maulizo ya kuwachunguza wamewafanya wabomoe ushikamanifu wao na kuwapinganisha na serikali zao wenyewe, ndivyo Shetani alivyotumainia kuwatumia “wafariji” wake wampinganishe Ayubu na Mungu.​—Ayubu 16:2, 3.

13. (a) Wageni wa Ayubu walifanya nini walipofika? (b) Wakati maneno yalipoanza kusemwa, yalichukua mwendo gani?

13 Wanapofika, wageni watatu hao wanakaa siku saba na mausiku saba wakichungua kwa ukimya maumivu makali na matwezo mengi mno ya Ayubu. (Ayubu 2:12, 13) Elifazi, ambaye kwa wazi ndiye aliyekuwa na umri mkubwa kuliko wote, mwishowe anaongoza katika kunena, akianzishia wale wengine maoni na habari ya ujumla ya majadiliano ya vipindi vitatu. Hotuba ya Elifazi, na pia zile zinazofuata za wenzake, ni za mashtaka hasa. Baada ya kila mmoja wa washtaki wake kunena, naye Ayubu anajibu akikanusha hoja zao. Sofari hashiriki kipindi cha tatu cha majadiliano, kwa wazi akijisikia kwamba amekwisha sema ya kutosha. Hivyo Sofari anatoa hotuba mbili tu, hali Elifazi na Bildadi wanatoa tatu kila mmoja.

14. Ni hoja za namna gani ambazo wanaume hao watatu walitumia dhidi ya Ayubu, na Shetani alitumiaje mbinu kama hiyo kuhusiana na Yesu?

14 Hotuba za Elifazi ni ndefu zaidi, na maneno anayotumia ni mapole kidogo. Maneno ya Bildadi yanauma kama meno, nayo ya Sofari ni zaidi. Hoja zao zimetungwa kwa ujanja kutimiza kusudi la Shetani la kuvunja ukamilifu wa Ayubu. Mara nyingi wao wanataja mambo ya hakika, lakini hali na njia ya kuyatumia haifai. Shetani alitumia mbinu iyo hiyo dhidi ya Yesu. Akinukuu andiko linalosema malaika wa Mungu angemlinda mtumishi wake asipatwe na dhara. Shetani alimwalika Yesu athibitishe ni mwana wa Mungu kwa kujitupa chini kutoka juu hekaluni. (Mathayo 4:5-7; Zaburi 91:11, 12) Kwa kipindi kirefu, Ayubu alikabili wazo la kishetani la mfano huo.

15. Elifazi alitoa hoja ya kwamba chanzo cha taabu za Ayubu kilikuwa nini?

15 Katika hotuba yake ya kufungua, Elifazi anabisha kwamba matata ya Ayubu ni malipo ya Mungu kwa dhambi zake. “Ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? anauliza. “Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.” (Ayubu 4:7, 8) Akiendelea kusema, Elifazi anadai kwamba Mungu hawatumaini watumishi wake. “Katika watumishi wake hana imani,” Elifazi anasema, “na [malaika] zake anawashtakia ukosaji. Si zaidi sana wale wanaokaa katika nyumba za udongo.”​—Ayubu 4:18, 19, NW.

16. Bildadi aliendelezaje ushambulizi wa Elifazi, naye alitumia mfano gani usiofaa?

16 Bildadi anauendeleza ushambulizi huo wa maneno. “Ikiwa wewe umetakata na u mnyofu,” anasema, “kufikia sasa [Mungu] angeamka kwa ajili yako naye hakika angekurudishia kao lako lenye uadilifu.” Bildadi anasema kwamba mafunjo na matete yanakauka na kunyauka yakikosa maji, kisha anakata shauri kikweli kwamba ndivyo pia itakavyokuwa kwa “wote wale wanaomsahau Mungu.” Lakini ni kosa kama nini kutumia mfano huo umhusu Ayubu, kisha kuongeza, “Hata lile tumaini alilo nalo mwasi-imani litatoweka”!—Ayubu 8:6, 11-13, NW.

17. Ni maelezo gani makali ambayo Sofari alitoa?

17 Maneno ya Sofari ni yenye nguvu hata zaidi. Anasema jambo kama hili, ‘Laiti Mungu angenena akuambie anavyofikiri! Mungu anajua lile ambalo umefanya. Yeye anakuadhibu kwa kipimo kilicho kidogo sana kuliko kile unachostahili. Ondolea mbali dhambi zako na kuacha ubaya wako wote, kisha utakuwa na usalama na rafiki wengi.’​—Ayubu 11:4-6, 14-20.

18. Katika kipindi cha pili cha majadiliano yale, wanaume hao watatu waliendelezaje ushambulizi wao juu ya Ayubu?

18 Katika kipindi cha pili cha majadiliano, Elifazi anaendeleza ushambulizi juu ya ukamilifu wa Ayubu. ‘Ala, Mungu hata hawatumaini malaika, sembuse mtu kama wewe! Mtu mwovu sikuzote anakuwa matatani.’ (Ayubu 15:14-16, 20, NW) Kwa kukasirishwa na upinzani thabiti wa Ayubu kwa hoja zao, Bildadi anasema jambo kama hili: ‘Nuru yako itazimishwa. Kumbukumbu lote la kuwako kwako litafifia liishe. Hilo ndilo linalowapata wale wanaomsahau Mungu.’ (Ayubu 18:5, 12, 13, 17-21) Sofari anagusia ufanisi ambao Ayubu alikuwa nao, na kuuliza: Wewe hujui kwamba shangwe ya mwovu ni fupi, na kufurahi kwa mwasi-imani ni kwa dakika? Mbingu inafunua makosa ya mwovu.’​—Ayubu 20:4, 5, 26-29, NW.

19. (a) Kulingana na Elifazi, Mungu anaona kuna thamani gani ya mwanadamu kuwa na ukamilifu? (b) Bildadi alimaliziaje ushambulizi wa maneno juu ya Ayubu?

19 Akifungua kipindi cha tatu cha majadiliano, Elifazi anauliza: ‘Je! mwanadamu ye yote anaweza kuwa mwenye thamani kwa Mungu? Hata kama ungekuwa asiye na lawama, je, Mungu angefaidika kutokana na jambo hilo? Mrudie Mungu,’ anasema, ‘nawe unyooshe mambo yako, Ndipo utakapoponywa.’ (Ayubu 22:2, 3, 21-23, NW) Bildadi anamalizia ushambulizi huo wa maneno. ‘Ni nani duniani anayeweza kujisifu kuwa ni safi?’ anauliza. ‘Mungu ni mtukufu sana kwamba hata mwezi na nyota si kitu kabisa mbele yake. Sembuse mwanadamu, ambaye ni mdudu tu machoni pake!’​—Ayubu 25:2-6, NW.

Kujitetea kwa Ayubu na Kusahihishwa Kwake

20. (a) Ayubu alijibuje hoja ya kwamba kutaabika ni adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya dhambi? (b) Ayubu aalikaza moyo afanye nini, nasi tunajuaje kwamba kwa kweli Mungu aliuona ukamilifu wake kuwa jambo lenye thamani?

20 Ijapokuwa anataabika vibaya sana, Ayubu hajiachi kamwe akubaliane na hoja za udanganyifu za hao wenye kumtesa-tesa. Ikiwa kutaabika ni adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya dhambi zake, yeye anauliza: “Mbona waovu wanaishi, na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu [katika utajiri]”? (Ayubu 21:7-13) Na kinyume cha vile washtaki wa Ayubu wanavyosema, Yehova anawathamini washika-ukamilifu ambao kwa njia hiyo wanamwandalia jibu kwa madharau ya Shetani kwamba yeye anaweza kugeuza mtu ye yote aache kumtumikia Mungu. (Mithali 27:11; Zaburi 41:12) Ayubu ana uhakika juu ya ukamilifu wake mwenyewe, akipaaza sauti hivi: “Mpaka nitakapokufa mimi sitaondoa ukamilifu kwangu mwenyewe!” (Ayubu 27:5, NW) Hapana, yeye hakufanya jambo lo lote hata astahili yaliyompata.

21. Elihu aliwaambia nini wafariji wa uwongo wa Ayubu, naye alimpa Ayubu sahihisho gani lililohitajiwa?

21 Kijana Elihu anasikiliza kwa makini kila neno la majadiliano hayo marefu. Sasa yeye, ananena akiwafariji wa uwongo wa Ayubu hakuna lo lote ambalo wamesema limemthibitisha Ayubu kuwa mtenda dhambi (Ayubu 32:11, 12) Halafu, akimgeukia Ayubu, Elihu anasema: “Nimesikia sauti ya maneno yako, ukisema, Mimi ni safi, sina makosa; sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu. Tazama, yuaona sababu za kufarakana nami, hunihesabu kuwa ni adui yake . . . Katika neno hili [umekosea].” (Ayubu 33:8-13; 6:29; 13:24, 27; 19:6-8) Ndiyo, Ayubu alihangaikia mno kuondoa malawama juu ya ukamilifu wake mwenyewe. Hata hivyo, wakati uo huo, yeye hakumlaumu Mungu kamwe wala hakupoteza tumaini hakika la kwamba Mungu angetenda linalofaa.

22. (a) Baada ya kumsikiliza Yehova, itikio la Ayubu lilikuwa nini? (b) Mungu alitaka nini kwa wafariji wa uwongo wa Ayubu, na matokeo ya mwisho kwa Ayubu yalikuwa nini?

22 Upepo unaanza kupiga kwa nguvu wakati Elihu anapomaliza hotuba yake, na Yehova mwenyewe ananena kutoka kwa upepo wa kisulisuli: “Ni nani huyu atiaye mashauri giza kwa maneno yasiyo na maarifa? Basi jifunge viuno . . . Maana nitakuuliza neno, nawe niambie.” Baada ya kumsikiliza Yehova, Ayubu anatambua kwamba alinena haraka haraka, bila maarifa kamili, kisha anatubu “katika mavumbi na majivu.” Halafu Yehova anamkanusha vikali Elifazi na wenzi wake wawili, na kumwagiza Ayubu awaombee. Baada ya hapo Ayubu anarudishwa kwenye hali yake ya kwanza, naye anabarikiwa akiwa na watoto saba wa kiume na binti watatu warembo na mifugo iliyo mara mbili ya ile aliyokuwa nayo zamani. Ayubu anaishi muda wa miaka 140 zaidi, na anakufa “mzee sana mwenye kujawa na siku.”​—Ayubu 38:1-4; 42:1-17.

23. Ukamilifu wa Ayubu unapasa kuwa na matokeo gani juu yetu?

23 Kweli Ayubu alikuwa mtu wa kusifika mwenye ukamilifu! Yeye hakuwa na njia ya kujua kwamba alikuwa akifanywa awe lengo la shtaka bovu la Shetani. Jambo hilo linaukazia hata zaidi ukamilifu wake kwa sababu ingawa aliamini kwamba taabu zote zilizompita zilitoka kwa Mungu, bado yeye hangemkana Mungu wala kumlaumu. Ni somo lililoje kwetu, kwa kuwa sisi tunajua chanzo cha majaribu ya ukamilifu wetu! Hakika tunapaswa kusukumwa na moyo tuige mfano wa Ayubu na kusonga mbele katika kazi ya Yehova hata Adui ya Mungu alete jambo liwalo lote dhidi yetu.

Wewe Unaweza Kujibu?

◻ Ni mambo gani yanayoufanya ukamilifu wa Ayubu uwe wa kusifika sana?

◻ Ni nani waliomtembelea Ayubu, naye Shetani alitumaini kwamba wangetimiza nini?

◻ Ni hoja gani ambazo hao watatu walitumia kinyume cha Ayubu?

◻ Ayubu alijitetea kwa kusema nini, lakini alisahihishwaje?

◻ Matokeo yalikuwa nini, na yanapasa kutuhusuje sisi?

[Picha katika ukurasa wa 13]

Shetani alipeleka “wafariji” watatu wakamgeuze Ayubu kinyume cha Mungu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki