Yehova Amekuwa Kimbilio Langu na Ngome Yangu
Kama ilivyosimuliwa na Margaret West
WAZIA ukiwa unaishi katika ngome ya kifalme ambapo Malkia Anna Sophie wa Denmark alitawazwa katika mwaka 1721. Kao hilo la mapumziko ya kiangazi ya jamaa ya kifalme ya Denmark, lililo katikati ya bustani za kupendeza, lilikuwa maskani yangu ya utotoni. Wakati huo vile vyumba vya anasa nyingi, vile vidato vyenye fahari ya kudumu, zile dari zilizopakwa rangi na wastadi wa kale Wafaransa, vilionekana kuwa vya uvutio mkubwa sana.
Mwendo mfupi wa miguu kutoka kwenye hiyo ngome ya kifalme lilikuwako jengo jingine, la kiasi zaidi, lakini miaka yangu 30 ya kuwa katika jengo hilo ilitajirisha maisha yangu kwa kadiri kubwa zaidi. Hilo lilikuwa Betheli ya Denmark, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Denmark.
Lakini kwanza acha nikueleze jinsi nilivyokuja kuishi katika Ngome ya Kifalme ya Frederiksberg katika Copenhagen. Baba yangu, kanali katika jeshi la Denmark, ndiye alielekeza chuo cha ustadi wa kijeshi ambacho makao makuu yacho yalikuwa katika ngome hiyo. Cheo hicho kilistahilisha yeye na jamaa yake kuishi katika mazingira hayo yenye pendeleo. Kwa msichana mchanga, hayo yalikuwa maisha ya raha mustarehe, yaliyokingwa madhara katika mipaka ya kikao hicho cha kupendeza. Mimi nilifikiri kwamba siku hizo za utoto wenye furaha na msisimuko hazingeisha kamwe. Lakini ndoto hiyo ilivunjika-vunjika siku moja isiyosahaulika katika 1921.
Sisi watoto tuliitwa kwenye chumba cha baba. Niliweza kumwona amelala pale, akionekana mweupe sana, mikono yote miwili ikiwa juu ya shuka. Mama alituzungushia mikono. Daktari wetu, ambaye pia alikuwa kando ya kitanda, alionekana mwenye uso mzito sana. Mama akasema kwa sauti ya chini: “Baba amekufa.” Fikira yangu ya kwanza ilikuwa: ‘Haiwezekani! Yeye hakuwa mgonjwa hivyo.’ Lilikuwa tukio la kulemea hisia kwa mtoto wa miaka kumi. Wakati huo sikung’amua sana kwamba kifo hicho chenye msiba kingeniongoza kuelewa kusudi la maisha.
Kifo cha baba kilimaanisha badiliko kubwa sana katika maisha zetu. Hiyo ngome ya kifalme ilikuwa kao rasmi, kwa hiyo ilikuwa lazima Mama atafute mahali pengine pa sisi kuishi. Ulikuwa wakati mgumu, na ili kutusaidia kujimudu katika tanzia hiyo, alifanya jambo lililogutusha jamaa na rafiki zetu. Alituondoa sote shuleni, nasi tukaanza safari ya kutalii Ulaya muda wa mwaka mzima.
Utafutaji Wathawabishwa
Hata hivyo, tuliporudi Denmark fikira za kifo cha Baba zilikaakaa juu yetu, na Mama akaendelea kujiuliza-uliza, Kwa nini? Kwa nini? Kwa nini? Ili kupata jibu, alianza kuchunguza-chunguza falsafa za Mashariki, lakini hazikuridhisha akili yake yenye kufikiria mambo kwa akili nzuri. Ndipo alipoamua kugeukia Biblia, akifikiri kwamba huenda ikawa na majibu fulani. Alipokuwa akinyosha mkono kuchukua Biblia kwenye rafu ya vitabu, aliona kitabu chekundu kando yayo, kitabu asichopata kukiona. Kiliitwa The Divine Plan of the Ages. Ndugu yangu alikuwa ndiyo sasa tu amekinunua kwa Mwanafunzi wa Biblia aliyetutembelea.
Mama alianza kusoma kitabu hicho na muda si muda akasadiki kwamba alikuwa amepata majibu kwa maswali yake. Wakati huo, mimi nilikuwa nikihudhuria shule Ufaransa, lakini niliporudi nyumbani wakati wa likizo miezi michache baadaye, Mama aliniambia kwa bidii ya moyoni juu ya hazina yake aliyoipata majuzi. Aliniambia juu ya Ufalme wa Mungu—Ufalme ambao ungetawala dunia yote na kukomesha vita vyote, Ufalme ambao ungeletea aina ya binadamu baraka zisizoelezeka, kutia na ufufuo wa wafu. Ilikuwa vizuri ajabu. Hatimaye tukawa tumepata kimbilio kutoka kwenye mashaka na wasiwasi.
Jioni hiyo nilipoenda kulala, nilisali kwa mara ya kwanza maishani mwangu. Sisi hatukuwa tumekuwa kamwe jamaa ya kidini, lakini shuleni tulikuwa tumefundishwa Sala ya Bwana. Kwa hiyo kwa kusita-sita nikaanza kukariri maneno ya sala hiyo. Nilipoyafikia maneno, “Ufalme wako uje . . . ,” karibu moyo wangu upasuke kwa shangwe. Hatimaye nikawa nimeelewa nilichokuwa nikiomba! Miaka 60 imepita, lakini ningali nakumbuka wazi-wazi shangwe isiyoelezeka niliyohisi usiku huo.
Baada ya kumaliza masomo yangu katika Ufaransa, nilienda Uingereza kwa mwaka mmoja kufanya mazoezi ya Kiingereza changu. Mama alikuwa amesisitiza hivi: “Msichana apaswa kujifunza lugha mbalimbali, na mvulana hesabu.” Mwishowe, nilijifunza lugha tano, na zote zimekuwa za thamani kubwa sana, na katika miaka ya baadaye nilimshukuru Mama mara nyingi kwa kunipa fursa hiyo.
Nilipowasili Uingereza, nilipata kwamba Mama alikuwa ametia kitabu The Harp of God (Kinubi cha Mungu) katika mkoba wa nguo zangu. Nilijifunza kitabu hicho kwa uangalifu na kuipa jamaa ya Kiingereza niliyokaa nayo ushuhuda wa mambo niliyokuwa nimejifunza. Mwanamke wa ukoo wa jamaa hiyo alizuru nyumba hiyo pindi moja, kwa hiyo nikampa ushuhuda yeye pia. (Nilikuwa nikianza kuwa stadi sana katika ‘kupiga zile nyuzi kumi’ za “kinubi” hicho.) Kwa kuwa bibi huyo alitaka kitabu chake mwenyewe, niliandikia ofisi ya tawi ya London ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, nao wakanielekeza kwa akina ndugu wa mahali petu.
Hivyo nikaanza kufanya ushirika pamoja na kikundi hicho kidogo katika Wickford, Essex, kilichokutana nyumbani mwa mmoja wa Wanafunzi wa Biblia. Kwenye mkutano mmoja, ilitangazwa kwamba Jumapili inayofuata kungekuwa na “safari ya burudiko,” nami pia nilialikwa. Nilitazamia safari ya kupendeza ya kwenda nje sehemu za kwetu mashambani, lakini nilipowasili, sala ilitolewa, nami nikapewa fasihi (vitabu) fulani na kuambiwa niende zangu pamoja na dada mzeemzee ili tukahubiri!
Baada ya kurudi Denmark, niliendelea kushirikiana pamoja na Wanafunzi wa Biblia, na katika 1929 nikabatizwa. Tukio lisilosahaulika lilikuwa kusanyiko katika Copenhagen katika 1931. Kwenye kusanyiko hilo ndiko sisi tulitwaa jina Mashahidi wa Yehova. Ili kujulisha watawala jambo hilo, hotuba ya Ndugu Rutherford na azimio lililopitishwa baadaye kwenye kusanyiko hilo vilitangazwa kwa chapa katika kijitabu The Kingdom, the Hope of the World. Sisi tulipaswa kuwapelekea binafsi watu wote mashuhuri katika jumuiya, kutia na mahakimu, washiriki wa serikali, wanabiashara wenye kujulikana sana, na pia makasisi wote.
Bibi Mdogo na Askofu
Mfalme wa Denmark alipokea nakala yake katika maongezi ambayo mwangalizi wa tawi aliruhusiwa kufanya naye. Mimi nilipewa fungu la vijitabu, pamoja na bahasha zilizokuwa na majina na anwani za watu niliopaswa kuwazuru katika kampeni hiyo. Jina la kwanza orodhani lilinishtua kweli kweli. Alikuwa ni askofu mashuhuri Mlutheri aliyejulikana sana kwa kupinga Mashahidi wa Yehova.
Askofu huyo aliishi katika sehemu isiyoendwa sana ya Copenhagen, na nilipopiga kengele, lazima nikiri kwamba nilihisi nikiwa mdogo hata kuliko kile kimo changu kidogo cha meta 1.5. Mjakazi alifungua mlango, akanitazama juu-chini kwa shuku, na kuuliza: “Wewe wataka nini, tafadhali?” “Asante, mimi nataka kunena na askofu,” nikajibu kwa imara. Mama alikuwa ameniazima koti zuri sana la manyoya-nyoya ya kondoo kwa ajili ya pindi hiyo, na labda lilisadikisha mjakazi huyo kwamba apaswa kunipa ombi langu, kwa maana baada ya kituo kirefu kilichoonekana kama umilele, yeye alisema: “Ngoja kidogo.” Muda si muda akarudi na kuniingiza ndani akinipitisha katika kijia kirefu cha ndani, akafungua mlango, na pale nyuma ya dawati kubwa alikuwa ameketi askofu huyo. Alikuwa mwanamume mrefu, mnene wa maungo. Aliinua kichwa na kutabasamu kwa uanana.
Nilijikumbusha kwamba yule Mmoja mwenye kunitegemeza alikuwa mkuu kuliko yule mmoja aliye mbele yangu, nami nikamweleza kusudi la ziara yangu, na kumpa bahasha ile. Aliichukua halafu akaitupa juu ya dawati lile kana kwamba ilikuwa imewaka moto. Akainuka haraka, akanishika mkono, na kwenda na mimi nikipiga miguu nyuma-nyuma kwa kufuata kijia kile kisichofikia mwisho hadi kwenye mlango wa mbele. Mlango ulifungwa kwa kishindo, lakini mimi nikatabasamu. Kijitabu kilikuwa juu ya dawati lake; kazi yangu ilikuwa imetekelezwa.
Katika 1933 nilianza kupainia, kwa maana nilihisi hiyo ilikuwa njia bora kabisa ya kutumikia Yehova kikamili zaidi. Mwaka mmoja baadaye niliolewa na Ndugu Albert West, ndugu Mwingereza aliyekuwa amepewa mgawo Denmark miaka kadhaa mapema kidogo. Tulitumikia pamoja katika Betheli ya Denmark kwa miaka 30.
Kukaliwa kwa Nchi na Wanazi
Aprili 9, 1940, ilikuwa siku ambayo sitasahau kamwe. Niliamshwa saa kumi na mbili asubuhi na mvumo wa ndege iliyosikika kana kwamba ilikuwa ikiruka pale pale juu ya kichwa changu. Kulikuwa nini? Denmark ilikuwa nchi isiyofungamana. Nje, watu walikuwa wakikusanyika barabarani, uvumi ulienea, wasiwasi ukiwa mwingi. Ndipo redio ikatangaza: “Denmark imekaliwa na majeshi ya Kijeremani.”
Tatizo la papo hapo lilikuwa jambo la kufanya na fasihi yote tuliyokuwa tumeweka akibani katika jengo. Akina ndugu katika Copenhagen walionyesha muono-mbele na busara nzuri ajabu. Muda si muda vitabu hivyo vikagawanywa kwa akina ndugu wa kwetu, na maandishi ya tawi yakawekwa salama kwa dada mmoja mzee-mzee aliye chonjo, aliyeviweka chini ya kitanda chake kwa muda ambao vita iliendelea.
Tatizo jingine lilikuwa jambo la kufanya na vijitabu 350,000 vilivyokuwa vimetoka kuwasili sasa hivi. Iliamuliwa kuvigawanya mara hiyo. Kabla ya hapo nisingaliitikadi kamwe kwamba mtu angeweza kupanda vidato vingi jinsi ile katika muda wa siku mbili tu. Yote hayo yalifanywa bila kuamsha shuku za askari Wajeremani waliokuwa wakitembea-tembea kwenye barabara ili kuzikagua. Walipopita pale kando, sisi tulijaribu kuwapa wazo la kwamba tulikuwa tukitazama vinunuliwa vilivyopangwa katika madirisha ya maduka. Ndugu wote, vijana kwa wazee, walishiriki ugawanyaji huo wenye haraka ya umeme, na baada ya kampeni hiyo moto-moto ya saa 48, vijitabu vyote vikawa mikononi mwa hadhara ya watu.
Uvamizi ulipotokea, mawasiliano yote pamoja na makao makuu katika Brooklyn yalikatizwa, lakini chakula cha kiroho hakikukoma. Kulikuwako ndugu mmoja au wawili wenye kufanya kazi katika utumishi wa kibalozi, na vifurushi vyao havikupekuliwa. Walipoenda Sweden kwa ukawaida, waliweza kutuletea Mnara wa Mlinzi wa Kisweden. Mimi nilijua Kisweden kwa kiasi fulani, kwa hiyo niligawiwa kazi ya kutafsiri kila toleo katika Kidenmark. Ilikuwa kazi ya kutatiza sana, lakini nilijishughulisha kujifunza mengi kwa kadiri ambavyo ningeweza. Kwa njia hiyo, sisi tukawa na gawio la ukawaida la Mnara wa Mlinzi muda wote wa vita.
Kwa uhakika, hata tuliweza kuwapelekea akina ndugu katika Norowei nakala fulani za Kidenmark. Vibweta vya mayai vilivyokusudiwa kuendea maofisa Wanazi vilipelekwa Norowei kwa ukawaida kutoka Denmark. Tuliweza kufunga mayai katika kurasa za magazeti ya Mnara wa Mlinzi wa Kidenmark, nao ndugu Wanorowei wakazifungua kwa uangalifu kabla Wajeremani hawajapewa mayai hayo.
Mkabiliano Usio wa Kawaida
Wakati wa vita, Ndugu Eneroth, aliyekuwa mtumishi wa tawi katika Sweden, alipata ruhusa ya kuzuru Denmark, na Albert akaenda kwenye kivuko kukutana naye. Ndugu Eneroth aliposhuka kwenye daraja la kivuko, maofisa wawili Wajeremani walitokea wakaambia Albert na Ndugu Eneroth waandamane nao.
Walipelekwa Hotel Cosmopolite, moja la makao makuu ya jeshi la Kijeremani, na wakasindikizwa kwenye ofisi moja katika ghorofa ya pili, ambako walilakiwa na Mjeremani aliyevaa nguo za kiraia. Akisema nao kwa Kiingereza kizuri kabisa, yeye akasema: “Kama mjuavyo sana, vita inaendelea. Mimi ni mfanya biashara kutoka Hamburg, na nimepewa mgawo kuja hapa nikiwa mkaguzi wa vitu vinavyoingia nchini. Ninakagua barua zote za Sosaiti ya Biblia ya Mnara wa Mlinzi [kati ya Denmark na Sweden]. Mimi sifurahii sana kufanya hivyo, lakini sina hiari. Ningependa kuwapongeza nyinyi kwa barua mnazoandikiana, ambazo zinafuata haki na inaburudisha kuzisoma. Udanganyifu ninaoupata katika barua za mashirika fulani ni mkubwa kwa kadiri kubwa ajabu.”
Akawauliza swali ndugu hao. “Rudio ni kitu gani?” Albert akafuliza kutoa wonyesho mfupi wa rudio, au ziara ya kurudia, akimtumia Ndugu Eneroth kama mwenye nyumba wake. Ndipo ofisa akamalizia hoji lile, akisema: “Asanteni, nyinyi waungwana, ni hayo tu niliyotaka kujua.” Labda hiyo ilikuwa njia yake ya kuonya akina ndugu wawe waangalifu juu ya mambo waliyoandika katika barua zao.
Mwaliko wa Kwenda Gileadi
Mwishoni mwa 1945, tulipokea ziara ya uchangamshi sana kutoka kwa Ndugu Knorr na Henschel. Wakati wa ziara hiyo, Albert na mimi tulialikwa kwenda Shule ya Biblia ya Gileadi ya Mnara wa Mlinzi, nasi tukahudhuria darasa la 11 la shule hiyo ya kimisionari katika 1948. Baada ya mazoezi yetu ya Gileadi, nilitumikia pamoja na mume wangu aliyegawiwa kazi ya mzunguko kwa miezi sita katika Maryland, Virginia, na Washington, D.C., kabla ya kurudi Denmark.
Miaka michache baadaye, Albert akawa mgonjwa, na ugonjwa huo ukapimwa mwishowe na kuonekana kuwa kansa. Nilimuuguza kwa miaka kumi huku nikifanya kadiri ambayo ningeweza nikiwa mtafsiri, mpaka alipokufa katika 1963. Mwaka uliofuata, nilikabiliwa na daraka jingine la kufikiria. Sasa mama yangu alikuwa na umri wa miaka 88 na alihitaji mtu wa kumtunza. Hivyo, nikiwa na majuto, nikalazimika kuacha utumishi wa wakati wote. Mama aliishi mpaka alipokuwa na miaka 101 na aliendelea kuwa mwaminifu moja kwa moja mpaka mwisho.
Kustaafu Kwenye Shughuli Nyingi
Wakati wa miaka ya mwisho ya maisha ya mama yangu, tulitumia miezi ya kipupwe katika Hispania. Hivyo basi alipokufa, niliamua kukaa huko. Nilikuwa nimejifunza Kihispania na nilihisi pia kwamba kwa njia hiyo ningekuwa nikitumikia katika shamba la kigeni. Ingawa siwezi kufanya mengi kwa kadiri ambayo ningependa, kwa sababu ya umri na madaraka yangu mengine, bado naweza kufanya upainia msaidizi kwa ukawaida.
Zaidi ya miaka 20 ya maisha yangu imetumiwa kwa kutunza mume mgonjwa na mama mzee-mzee. Hata hivyo, sikuliona hilo kuwa lemeo kamwe. Sikuzote nilihisi kwamba wote wawili walistahili utunzaji na ufikirio huo, nami nikawa na rai ya kwamba hiyo ilikuwa sehemu ya utumishi wangu kwa Yehova, ambaye sikuzote alinisaidia kukabiliana na huzuni na majaribu ambayo ni lazima yavumiliwe chini ya hali za jinsi hiyo.
Sasa ninaishi katika nyumba ndogo, inayotofautiana sana na ile ngome ya kifalme ya kuvutia sana nilimozaliwa. Lakini majengo hayawezi kamwe kutoa usalama, kama nilivyogundua mapema maishani. Kwa upande ule mwingine, niligundua kimbilio na ngome kubwa zaidi, ambayo haijanikosesha kamwe mafanikio. Kama mtunga zaburi, mimi naweza kusema kikweli: “Wewe ndiwe kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ambaye katika yeye mimi nitaitibari.”—Zaburi 91:2, NW.