Yehova Amenitegemeza Kama Rafiki
Kama ilivyosimuliwa na Maria Hombach
NIKIWA kisichana cha miaka sita, nilijifunza shuleni ule wimbo mzuri wa utamaduni wa Kijeremani: “Wajua anga samawati lina nyota ngapi? . . . Mungu, Bwana, kahesabu zote, hakuna isiyokuwapo . . . Akujua wewe pia na akupenda sana.” (Umetafsiriwa kutoka Kijeremani.) Mimi nilikuwa nikiuimba siku moja wakati mama yangu aliposema: “Yeye anakujua wewe na kukupenda pia.” Tangu hapo,Mungu akawa kama rafiki kwangu. Nami nikaamua kumpenda pia. Hiyo ilikuwa kabla ya Vita ya Ulimwengu 1 tulipoishi katika Bad Ems kwenye mto wa Lahn.
Miaka kumi na saba baadaye, nikiwa likizoni 1924, nilikutana na msichana wa umri wangu. Alikuwa mmoja wa Wanafunzi wa Biblia, ambao leo wanajulikana kuwa Mashahidi wa Yehova. Kwa majuma manne, tukawa na mazungumzo makali juu ya dini. Halafu habari ya “helo” (moto wa mateso) ikatokea. “Wewe hungeingiza paka aliye hai katika joko lenye moto, sivyo?” yeye akauliza. Jambo hilo likanigutusha sana, nikatambua kwamba nilikuwa nimedanganywa vibaya sana. Sasa ningeweza kujifunza yote juu ya Mungu—jinsi alivyo hasa, kwa uhakika, kila jambo nililokuwa nimetaka kujua juu yake tangu nilipokuwa mtoto!
Kwangu ilikuwa kama kugundua “hazina iliyofichwa shambani.” (Mathayo 13:44, ZSB) Niliporudi nyumbani, nikaenda mbio kwa majirani nikiwa na shauku, moyo wangu ukibubujika kwa kutaka kushiriki mambo mapya niliyojifunza. Muda mfupi baadaye, nilihamia mji wa Sindelfingen kusini mwa Ujeremani, kilikoishi kikundi cha Wanafunzi wa Biblia karibu 20. Nikajiunga nao kwa bidii katika utendaji huu mpya wa kupeleka evanjeli nyumba kwa nyumba.
Mara yangu ya kwanza kusikia juu ya utumishi wa painia ilikuwa 1929 wakati wa hotuba ya ndugu aliye mhudumu msafiri. Aliuliza nani angenuia kuwa painia. Nikainua mkono moja kwa moja. Sikuwa na mashaka-mashaka. “Mimi hapa, nitume mimi,” moyo wangu ukasema,—Isaya 6:8.
Bila kukawia nilijiuzulu kazi yangu ya ofisi na Oktoba 1, 1929, nikaanza utumishi wa painia wa pekee, kama unavyoitwa leo, katika kusini-magharibi mwa Ujeremani. Katika Limburg, katika Bonn, tulipanda mbegu ya ukweli ikiwa kwa maandishi yaliyopigwa chapa, tukiwa tumepanda mashua-mikokoteni ya kimataifa katika bandari ya Cologne, na mahali penginepo.—Mhubiri 11:1.
Kupata Urafiki wa Mungu
Adolf Hitler aliposimamisha imara utawala wake wa kimabavu katika Ujeremani katika 1933, nililazimika kuacha utumishi wa painia nikarudi Bad Ems. Upesi wenye mamlaka wakagundua sikuwa nimepiga kura katika uchaguzi. Siku mbili baadaye, polisi kadhaa walikuja kupekua chumba changu. Kona moja ilikuwa na kikapu cha takataka ambamo, dakika moja tu kabla ya hapo, nilikuwa nimetupa anwani zote za Mashahidi wenzangu. Hakuna wakati wa kuziondoa humo! Polisi walipekua-pekua kila kitu—isipokuwa kikapu hiki.
Nilithamini kama nini jambo la kwamba, wakati huo Anna dada yangu alikuwa pia amekubali kuwa na urafiki pamoja na Mungu wa kweli! Katika 1934 tukahama pamoja kwenda mji wa Freudenstadt na huko tukaanza kueneza fasihi za Biblia kwa uangalifu. Wakati mmoja, tukiwa likizoni, tuliweza kwenda haraka sana kwa garimoshi ili kuzuru mji wa nyumbani kwetu wa Bad Ems, tukaeneza haraka-haraka broshua 240 zilizojaa sandukuni, kisha tukatoweka. Usumbufu wa polisi wa siri katika Freudenstadt ulitusadikisha tuhamie jiji jingine, na katika 1936 tukaenda Stuttgart. Huko, nikatafuta kuwasiliana na wenye kusimamia kazi yetu ya siri—na moja kwa moja nikapewa “kazi.” Nilipokea kwa ukawaida picha za postikadi zenye salamu. Kwa kweli, zilikuwa jumbe zilizofichwa. Kazi yangu ilikuwa kuzileta mahali pa siri jijini. Ili nisihatarishe utendaji huo, niliambiwa nisieneze fasihi zozote. Kila jambo liliendelea kwa ulaini mpaka Agosti 1938.
Siku moja, nilipokea kadi ikiagiza kwamba jioni fulani nikasimame mbele ya kanisa lililojulikana. Hapo ningepokea habari zaidi. Nikaenda mahali hapo pa kukutania. Palikuwa na giza tiii. Mwanamume mmoja akajijulisha ya kuwa yeye ni Julius Riffel. Mimi nilijua hilo lilikuwa jina la ndugu mwaminifu aliyefanya kazi ile ya siri. Aliniambia haraka-haraka nisafiri kwenda Bad Ems tarehe fulani ili nikakutane na mtu fulani. Ndipo akatoweka haraka.
Hata hivyo, jukwaani katika Bad Ems, polisi wa siri peke yao ndio walioningojea. Ni kasoro gani iliyokuwa imetokea? Yule mwanamume aliyekuwa mbele ya kanisa—hapo kwanza akiwa kwa kweli ni ndugu kutoka Dresden, Hans Muller, aliyejua kila jambo juu ya kazi ya siri katika Ujeremani na akaanza kushirikiana na polisi wa siri—alikuwa amenitega mtego. Lakini wapi. Muda mfupi kabla ya hapo, mama yangu alikuwa ameniarifu kwamba amepatwa na ugonjwa kidogo wa kupoozesha mwili kwa muda, nami, kwa kumjibu, nikaahidi kumzuru katika Bad Ems tarehe fulani. La kufurahisha ni kwamba hiyo ililingana na ule “uvamizi,” na kwenye kesi ya baadaye mahakamani, barua zetu zikaandaa kithibiti cha kwamba mimi nilikuwa mahali penginepo. Nilishangaa kwa kuondolewa hatia. Ndiyo, katika Februari 1939, baada ya miezi mitano na nusu ya kutiwa kizuizini, nikawa huru tena!
Kuitikia Urafiki Wake
Bila shaka, sikupanga kubaki nikiwa si mtendaji, hasa kwa kuwa walio wengi wa akina ndugu walikuwa wakiteseka katika kambi za mateso au walikuwa wamekamatwa mahali penginepo.
Baada ya ndugu Wajeremani wenye madaraka kukamatwa kwa msaada wa Muller, Ludwig Cyranek akachukua daraka la ugawa-nyaji wa chakula cha kiroho. Ndugu huyu, aliyekuwa mfanya kazi wa Betheli katika Magdeburg, alikuwa ametoka tu kufunguliwa kizuizini, naye alinizuru katika Bad Ems. “Haya, basi, Maria! Na tuendelee kufanya kazi,” akasema. Akanirudisha Stuttgart, nami nikapata kazi ya kimwili huko. Hata hivyo, kazi yangu halisi kuanzia Machi 1939 ilikuwa kugawanya katika Stuttgart na mazingira yayo magazeti ya Mnara wa Mlinzi yaliyojaa katika mikoba ya nguo. Mashahidi wengine walishiriki kishujaa katika kazi hii.
Kwa sasa, Ndugu Cyranek alimaliza eneo lote isipokuwa sehemu ya kaskazini-mashariki mwa nchi. Kwa kuwa makao ya Mashahidi yalikuwa yakichunguliwa, alilazimika kuenda-enda kwa hadhari kubwa na nyakati fulani alilazimika hata kulala miituni. Magari-moshi ya moja kwa moja yalimleta Stuttgart mara kwa mara, ambako yeye aliniagiza-agiza juu ya ripoti maalumu juu ya hali yetu katika Ujeremani. Mimi niliandika barua za kikawaida, nikiandika jumbe hizo kati ya mistari kwa wino isiyoonekana na kuzipeleka Betheli ya Uholanzi, kwa kutumia anwani ya maficho.
La kuhuzunisha ni kwamba, ndugu wa pili alikuwa amegeuka kuwa msaliti kwa matumaini ya kuponyoka kizuizini. Mwaka mmoja baadaye, alivisaliti kwa polisi wa siri vikundi vilivyoshirikiana kazi katika Stuttgart na mahali penginepo. Siku ya Februari 6, 1940, tulikamatwa. Ludwig Cyranek alienda kwenye kijumba cha Muller katika Dresden—akifikiri Miiller angali Shahidi mwenzake—akashikiwa hapo. Baadaye Ndugu Cyranek alihukumiwa kifo akakatwa kichwa siku ya Julai 3, 1941.a
Sasa adui zetu waliamini kwamba walikuwa wamepoozesha utendaji wetu wote katika Ujeremani. Lakini mipango ilikwisha fanywa kuhakikisha kwamba maji ya ukweli yangeendelea kutiririka, hata yakipunguzwa yawe kitiririko tu. Mathalani, kikundi katika Holzgerlingen kiliweza kuendelea na utendaji mpaka mwisho wa vita katika 1945.
Yeye Hawaachi Kamwe Rafiki Zake
Anna na mimi pia, pamoja na dada wengine waaminifu, tulikuwa tumepelekwa jela ya Stuttgart. Mara nyingi niliweza kusikia wafungwa wakipigwa. Kufungiwa mahali ukiwa peke yako bila jambo lolote la kufanya ni tukio baya sana. Lakini kwa sababu tulikuwa hatujakosa mkutano wowote wa Kikristo na tulikuwa tungali wachanga, tuliweza kukumbuka karibu makala zote za Mnara wa Mlinzi. Kwa hiyo, imani yetu iliendelea kuwa imara, nasi tukaweza kuvumilia.
Siku moja, polisi wawili wa siri walitoka Dresden wamchukue mfungwa mwenzangu Gertrud Pfisterer (sasa Wulle) na mimi ili tukatambulishwe. Kwa kawaida, wafungwa waliruhusiwa kusafiri katika magari-moshi ya polepole tu, yaliyochukua siku kadhaa. Lakini sisi tuliwekewa akiba ya chumba kizima katika gari-moshi la moja kwa moja, ijapokuwa lilikuwa limesongamana watu. “Nyinyi ni wa maana sana kwetu. Hatutaki kuwapoteza,” maofisa hao wakaeleza.
Katika Dresden, polisi wa siri walinikabili wakiwa na msaliti wa tatu kutoka miongoni mwetu. Nikahisi kuna kasoro, basi nikanya-maza, hata nisimsalimu. Halafu nikakabilishwa uso kwa uso na mwanamume mrefu wa maungo mapana aliycvaa mavazi ya askari: yule Muller msaliti, niliyekuwa nimekutana naye mbele ya kanisa. Mimi niliondoka chumba hicho bila kusema neno. Polisi wa siri hawakupata habari zozote kwangu.
Kila mmoja wa wasaliti hao alifikia mwisho mbaya. Kama walivyosema Wanazi, kile ambacho wao walikipenda ni usaliti wenyewe wala si msaliti mwenyewe. Wote watatu walipelekwa ukingo wa mashariki wasirudi kamwe. Ikawa tofauti kama nini kwa wale wasioacha kamwe urafiki pamoja na Mungu na watu wake! Wengi wa washikamanifu, miongoni mwao wakiwamo Erich Frost na Konrad Franke, walioteseka sana kwa ajili ya Bwana na baadaye wakawa waangalizi wa tawi katika Ujeremani, walirudi wakiwa hai kutoka tanuri la moto wa mnyanyaso.b
Polisi wa siri katika Stuttgart—kwa kujivunia sana “pato” lao—waliwaomba wenzao katika Dresden katika Mei 1940 waturudishe. Kesi zetu zingejaribiwa kusini mwa Ujeremani. Lakini yaonekana polisi wa siri kaskazini na kusini hawakuwa wakisikilizana, basi ofisi ya Dresden ikakataa, na hapo wale wa Stuttgart wakaja na kutuburuta wao binafsi. Sasa iweje? Tulifurahia kupelekwa stesheni kwa gari kwa kupita kandokando ya mto wa Elbe; kwa muda mrefu tulikuwa hatujaona miti ya kijani na anga samawati tukiwa katika vijumba vyetu jela. Kama hapo kwanza, chumba kizima cha gari-moshi kiliwekwa akiba kwa ajili ya sisi tu, hata tukaruhusiwa kuimba nyimbo za Ufalme. Tulipobadili magari-moshi, tulipewa mlo katika mkahawa wa stesheni. Ebu wazia, asubuhi tulikuwa tumepata kipande kikavu tu cha mkate, na sasa ebu ona!
Kesi yangu ililetwa mahakamani Stuttgart siku ya Septemba 17, 1940. Kwa kuandika na kupeleka barua za Ludwig Cyranek, nilikuwa nimearifu watu wanaoishi nchi za kigeni juu ya utendaji wetu wa siri na mnyanyaso wetu. Huo ulikuwa usaliti mkubwa kwa serikali, wenye adhabu ya kifo. Kwa hiyo ulionekana kuwa muujiza kwamba mimi, mshtakiwa mkuu katika Stuttgart, nilihukumiwa kifungo cha kuzuiliwa nikiwa mpweke kwa miaka mitatu na nusu tu! Ni wazi kwamba ofisa mmoja wa polisi wa siri jina lake Schlipf, ambaye alipendezwa nasi na kusumbuliwa na dhamiri yake, alikuwa ametumia mamlaka yake. Wakati mmoja alitaja kwamba alikuwa halali tena usingizi kwa sababu ya sisi “akina mama.” Dresden hapakuwa mahali ambapo ningaliweza kuponyoka kwa urahisi hivyo.
Kunufaika na Urafiki wa Kudumu
Ingawa chakula gerezani hakikuwa kibaya kama katika kambi za mateso, nilipungua uzito sana na mwishowe nikawa kimba-ombao. Miaka 1940 hadi 1942 ikapita, nami nikawa nikiwaza hivi: ‘Kifungo chako kimalizikapo, watakutia katika kambi ya mateso uweze kupata uandamani wa akina dada usiwe peke yako tena.’ Kumbe nilikosea kufikiri hivyo.
Walinzi walishangaa kabisa wakati ombi la kufunguliwa kwangu, lililofanywa na wazazi wangu Wakatoliki, lilipokubaliwa. (Nilikuwa nimekataa-kataa kufanya ombi hilo mimi binafsi.) Jamani, ilikuwa ajabu kwamba mimi—niliyehukumiwa usaliti mkubwa kwa serikali—ningeponyoka kwa urahisi hivyo, tena bila kuacha kamwe msimamo unaofaa—na hali waamini wenzangu walitupwa ndani ya kambi za mateso! Basi nikawa huru tena katika 1943 na hivyo nikawa naweza kuchukua habari za kitheokrasi kutoka Holzgerlingen, nikitumia uangalifu mwingi sana. Baada ya kuzinakili, nilizificha katikati ya kuta za chupa ya chai iliyojaa kahawa na kuwapelekea akina ndugu walioishi kandokando ya Mto Rhine na katika kisehemu cha Westerwald cha Ujeremani. Tangu hapo hadi mwisho wa vita, niliweza kufanya kazi bila kusumbuliwa. Baadaye nikapata habari kwamba maofisa-polisi wenye urafiki waliopokea taarifa za kutulaumu wazi hawakuzipeleka kwa polisi wa siri.
Ikawaje baada ya 1945? Nilikuwa na tamaa ya kupainia tena mara ikiwezekana. Bila kutarajia hata kidogo ukaja mwaliko mzuri zaidi niliowahi kupokea. Nilikuwa sijapata kuwazia kwamba ningealikwa kufanya kazi Betheli katika Wiesbaden!
Na tangu Machi 1, 1946, humo ndimo nimekuwa, katika Betheli (sasa katika Selters/Taunus). Kwa miaka mingi nilifurahia kufanya kazi katika ofisi moja iliyosimamiwa na aliyekuwa mwangalizi wa tawi, Konrad Franke. Pia nilifanya kazi kwa shangwe katika idara nyinginezo, kama vile katika mahali pa kufulia nguo. Hata leo, nikiwa na miaka 87, ningali nafanya kazi saa kadhaa kwa juma nikikunja taulo. Ikiwa wewe umepata kutalii Betheli yetu, labda tumeonana.
Katika muda huo uliopita, nilikuwa na pendeleo la kusaidia watu wengi wakubali ukweli, kutia ndani mama yangu na dada mwingine wa kimnofu. Maneno ya Mama, “Yeye anakujua wewe na kukupenda,” nimeyaona kuwa ya kweli, sawa na yalivyokuwa maneno ya mtunga zaburi, “Naye atakutegemeza.” (Zaburi 55:22) Lo, imekuwa shangwe iliyoje kumpenda Yehova huku nikitegemezwa naye kama rafiki!
[Maelezo ya Chini]
a Ona 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses, kurasa 179-80.
b Ona Mnara wa Mlinzi, Aprili 15, 1961 (Kiingereza), kurasa 244-9, na Machi 15, 1963, kurasa 180-3