Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w89 10/1 kur. 22-26
  • Kupata Sikuzote Jambo la Kumfanyia Yehova

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kupata Sikuzote Jambo la Kumfanyia Yehova
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Msimamo wa Kutokuwamo
  • Mgawo Wangu Mpya—Gereza
  • Ule Mwondoko
  • Mfungwa wa Vita
  • Kuwahubiria Watu wa Namna Zote
  • Kupanua Huduma Yangu
  • Yehova, Ngome Imara
  • Kupata Mambo Zaidi ya Kumfanyia Yehova
  • Nilikuwa Mwanasiasa Lakini Sasa Mimi Ni Mkristo
    Amkeni!—2002
  • Mwanadamu Hataishi Kwa Mkate Tu—Jinsi Nilivyookoka Kambi za Nazi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Kungoja Ufalme Ambao Si “Sehemu ya Ulimwengu Huu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Kujitahidi Kuwa “Mtenda-kazi Asiye na Lolote la Kuaibikia”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
w89 10/1 kur. 22-26

Kupata Sikuzote Jambo la Kumfanyia Yehova

Kama ilivyosimuliwa na Jean Queyroi

KILIKUWA kiangazi kitukufu kule nyuma katika 1939. Eneo la mashambani lililozunguka Martigny, katika tarafa ndogo ya Kiswisi ya Valais, liling’aa chini ya jua la Agosti. Juu yetu ilikuwako miinuko mikubwa ya baadhi ya vilele vilivyo na kimo kirefu zaidi katika misafa ya milima Alps, kama kile cha Grand Combin chenye theluji kwenye kileleta, kikiwa na kimo cha meta 4,314. Mimi nilikuwa nikiona shangwe ya ukaribishaji wa jamaa moja ya Kikristo kwa siku chache, nasi tulitumia saa nyingi za kutojali sana tukiranda-randa pamoja kwenye vijia vya milimani. Mimi nilihisi kana kwamba tayari nilikuwa katika Paradiso.

Muda ulikwisha haraka mno ukawa ni wakati wa kusema bakini-salama na kurudi Paris. Nilinunua karatasi-habari niisome katika gari-moshi, na habari za kugutusha zilizokuwamo zikaniondolea msisimuko wangu nikarudiwa na fahamu nikauona uhalisi wa mambo. Hali ya ulimwengu ilikuwa imezorota kwa kadiri kubwa, na vita ilikuwa ikikaribia sana.

Nilirudia kazi yangu katika ofisi ya Paris ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, ambako nilikuwa nimekuwa nikitumikia kwa zaidi ya mwaka mmoja. Lakini siku chache baadaye, nilipokea arifa ya kuingia kazi ya jeshi nikaagizwa niripoti kwenye mabweni ya wanajeshi yaliyoko Fort of Vincennes, kidogo tu mashariki mwa Paris. Maisha yangu yalikaribia kubadilika sana.

Msimamo wa Kutokuwamo

Siku ya Septemba 3, 1939, Ufaransa na Uingereza zilijulisha rasmi kwamba zingeipiga vita Ujeremani. Mimi nikaripoti Vincennes nikachukua msimamo wangu kuhusu suala la kutokuwamo kwa Kikristo. Upesi nikajikuta ndani ya kigari kilichounganishwa na pikipiki ya kijeshi yenye kuendeshwa na askari kijana aliyepewa maagizo anipeleke Fort of Charenton iliyokuwa hapo karibu. Ijapokuwa mngurumo wa pikipiki ulikuwa mkubwa kiasi cha kuziba masikio, askari yule kijana, aliyejua sababu yangu ya kupelekwa huko, alijaribu kusababu mambo pamoja nami. Aliniomba sana hivi: “Queyroi, tafadhali usishikilie msimamo wako. Usikatae kupigana, ama sivyo mambo hayatakuendea vizuri.” Nami nikafanya haraka kumhakikishia kwamba sikuwa na woga.

Ndipo ukaja usiku wangu wa kwanza katika kijumba cha gerezani. Kijumba hicho kilikuwa cha meta 2 kwa meta 1.5 na kilichokuwa humo ni blanketi kadhaa na ubao wa kulalia tu. Hamkuwa na taa. Niliwaza ningeweza kumfanyia Yehova nini katika hali yangu iliyopo. Nilipoamka, nikagundua kwamba hata hamkuwa na kidirisha kidogo cha kuingiza kiangaza chochote cha nuru ya mchana. Niliruhusiwa kwenda nje kwa robo-saa kila siku ili nikaoge, huku sajini mwenye bastola ya kufuliza risasi akinisindikiza kwenye bakuli la kuogea, akiwa ameandamwa na askari wawili wenye bunduki. Nilikuwa nikitendwa kama mhalifu hatari!

Askari tofauti-tofauti waliniletea chakula. Walishangazwa sana na msimamo wangu, na hiyo ikanipa fursa ya kumfanyia Yehova jambo fulani. Niliwapa ushahidi mwema, na muda mfupi baada ya hapo baadhi yao walinichangamkia wakaniletea viberiti, mishumaa, na hata chakula cha ziada. Hapo mwanzo nilikuwa nimenyang’anywa Biblia yangu, lakini asante kwa ofisa mmoja, ilirudishwa kwangu. Nilithamini kama nini kuyasoma maneno yayo yenye thamani kubwa kwa kutumia nuru ya mishumaa!

Baadaye nilihamishwa nikapelekwa gereza la kijeshi ambalo halipo tena, katika barabara ya Cherche-Midi, katika Paris. Niliwekwa katika uzuilio mpweke, kwa hiyo nilikuwa na wakati tele wa kuitafakari hali yangu.

Nilikuwa na miaka 27 na nilikuwa nimekuwa nikitumikia Yehova wakati wote kwa miaka miwili. Mwonano wa kwanza wa jamaa yetu pamoja na Mashahidi wa Yehova ulikuwa kupitia habari zilizotangazwa katika Radio Vitus, kituo cha watu binafsi katika Paris. Hiyo ilikuwa katika 1933. Nilichukua msimamo wangu upande wa ukweli katika 1935, baada ya kumaliza utumishi wa kijeshi uliokuwa wa lazima. Nilibatizwa katika Lucerne, Uswisi, katika Agosti 1936.

Wazazi wangu, ndugu yangu, dada yangu, na mimi tulishirikiana na kundi moja tu lililokuwamo Paris. Ndugu Knecht, ambaye wakati huo ndiye aliyesimamia kazi katika Ufaransa, kwa uendelevu aliwatia Mashahidi vijana moyo mkuu wa kuingia huduma ya wakati wote. Tokeo ni kwamba, katika Aprili 1938, ndugu yangu, dada yangu, na mimi tuliamua kuwa mapainia, au wahudumu wa wakati wote. Mgawo wetu ulikuwa Auxerre, mji ulioko kilometa 154 hivi kusini-mashariki mwa Paris. Jeanette dada yangu alitoa ushahidi katika mji wenyewe, na ndugu yangu Marcel na mimi tuliendesha baiskeli kwenda kwenye vijiji vilivyouzunguka katika mwendo wa kilometa 30 hivi kutoka mjini. Huko nyuma kazi ya kuhubiri ilikuwa hasa ya kugawanya fasihi za Biblia, bila kufanya ziara za kurudi. Mimi naweza kukumbuka jinsi jambo hilo lilivyonisumbua mawazo.

Katika Juni 1938 nilialikwa nikafanye kazi katika ofisi ya Paris ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi. Wakati huo wafanya kazi, au jamaa ya Betheli, katika Ufaransa walikuwa washiriki kumi hivi, nami niligawiwa kusaidia katika Idara ya Usafirishaji Fasihi. Humo ndimo nilimokuwa nilipoitwa nikafanye utumishi wa kijeshi na kupokea “mgawo mpya.”

Mgawo Wangu Mpya—Gereza

Kutoka mwanzo mimi niling’amua kwamba kama singetafuta njia za kufanya jambo fulani—hata liwe dogO namna gani—kwa ajili ya Yehova nikiwa gerezani, imani yangu ingedhoofika haraka. Lakini baada ya muda mfupi niliweza kufanyiza fursa za kuongea kuhusu ukweli wa Neno la Mungu. Majuma machache baada ya mimi kuwasili kwenye gereza la Cherche-Midi, nilihamishwa nikapelekwa kwenye chumba cha jumla niwe pamoja na wafungwa wengine. Humo nikakuta mwanafunzi wa sheria aliyekuwa amehukumiwa kuwa gerezani kwa sababu alichelewa siku chache kurudi kutoka kwenye likizo lake la kijeshi. Alikuwamo pia mwanafunzi wa seminari ya Kikatoliki aliyekuwa amehukumiwa kwa kuiba. Sisi watatu tuliona shangwe ya kufanya maongeo marefu mengi kuhusu ukweli wa Biblia.

Siku moja niliona mfungwa akiwa peke yake kabisa katika pembe moja ya ua. Nilipokuwa nikikaribia, ningeweza kuona kwamba alikuwa anasoma. Nilinena naye. Akageuka akanionyesha Biblia yake. Ebu wazia! Yeye alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova! Alikuwa wa uzawa wa Kipolandi, jina lake Ceglarski, na kama mimi, yeye alikuwa gerezani kwa sababu ya kutokuwamo kwake. Lo, ushirika wa Kikristo hatimaye! Waweza kuwazia jinsi sisi wote wawili tulivyofurikwa na shangwe. Sasa tungeweza kuona shangwe ya kuwa na saa nyingi za maongeo yenye kujenga.

Katika gereza hili tuliruhusiwa kuingia uani saa kadhaa kwa siku, kwa hiyo niliweza kunena pamoja na wafungwa kadhaa walioona shangwe ya kuusikia ujumbe wa Biblia. Nyakati fulani hata baadhi ya walinzi walijiunga katika mazungumzo yetu. Nilikuwa nimepata jambo fulani la kumfanyia Yehova. Kwa uhakika, gereza lilikuwa limekuwa mgawo wangu mpya wa kuhubiri, nami sasa nilikuwa ninafanya saa za painia, hata ingawa singeweza kuziripoti. Lakini hilo halikunisumbua.

Ule Mwondoko

Miezi ilipita bila vituko vikubwa hasa—ni ile Vita ya Kusingizia tu. Lakini hiyo iliisha Mei 1940, wakati Wajeremani waliposhambulia Ufaransa. Katika Juni Wafaransa wenye mamlaka walihamisha wafungwa wote katika magereza ya Paris kwa sababu ya vikosi vya Kijeremani vyenye kukaribia. Sisi tulipakiwa ndani ya malori ya kijeshi tukapelekwa Orleans, mji ulioko zaidi ya kilometa 100 kusini mwa Paris. Baada ya kituo kifupi, wafungwa-raia na hata wafungwa-wanajeshi waliwekwa pamoja na kuagizwa waendelee kusonga mbele kusini-mashariki wakitembea kwa miguu kando-kando ya ukingo wa kaskazini wa ule mto Loire. Washika-doria wenye silaha waliulinda msafara huo. Mwendo ulikuwa mgumu chini ya jua kali la Juni.

Miongoni mwetu walikuwamo wahalifu, na washika-doria walikuwa wamepokea maagizo wampige risasi mtu yeyote aliyesimama, aliyeanguka, au asiyeweza kuendelea kutembea. Siku ya tatu, Ndugu Ceglarski alianza kuteseka kutokana na ugonjwa wa kuunguzwa na jua. Kumwacha peke yake kungalimaanisha apatwe na kifo hakika. Washika-doria waliniruhusu mimi, kwa msaada wa wafungwa wengine, tumtie katika blanketi, nasi tukambeba. Siku iliyofuata alihisi vizuri zaidi akaweza kusonga mbele kwa miguu.

Kabla tu ya kuwasili Briare, mji mdogo ulio katika ukingo wa kaskazini wa Loire, kikundi chetu kilikutana na mtiririko wa watu wenye kuchukua mizigo ya kadiri ambayo wangeweza kubeba au kusukuma katika mkokoteni. Walikuwa wakikimbia kwenda kusini kuyaondokea majeshi ya Ujeremani yenye kukaribia. Maelfu ya raia walipokuwa wakikimbia wakaokoe maisha zao akili zetu ziliweza kufahamu mwondoko huo ulikuwa na ukubwa wa kadiri gani,

Ndipo tukagundua kwamba washika-doria wetu walikuwa wametoweka, na kwamba tulikuwa peke yetu. Sasa tufanyeje? Haikuwezekana kuvuka ule mto mpana wa Loire tuendelee na safari yetu kusini kwa sababu madaraja yote yalikuwa yamelipuliwa. Kikundi chetu kidogo (chenye Ndugu Ceglarski, wafungwa wengine wawili, na mimi) kiliamua kurudi Paris.

Tulipata farasi fulani walioachwa peke yao nasi tukaweka matandiko kwa kadiri nzuri tulivyoweza. Mimi nilikuwa nimeumiza goti langu na singeweza kukunja mguu wangu, kwa hiyo ilikuwa lazima waandamani wangu wanisaidie kupanda mgongoni pa farasi. Ndipo tukagundua kwamba farasi wangu alikuwa akichechemea pia! Kwa hiyo mwendo wa kusonga mbele ukawa wa polepole huku farasi wangu akienda chopichopi. Vyovyote vile, baada ya muda mfupi safari yetu ilifikia mwisho wa ghafula. Tulikuwa tumemaliza kilometa chache tu tulipokabiliana uso kwa uso na kikosi kidogo cha jeshi la Ujeremani, na polisi mmoja wa kijeshi akatuagiza tushuke chini. Kumbe hatukufanikiwa kitu ila kuwabadili tu washika-doria wetu!

Mfungwa wa Vita

Muda mfupi baada ya kutekwa kwetu, Ndugu Ceglarski na mimi tulitenganishwa, naye akabaki akiwa mfungwa wa Wajeremani mpaka mwisho wa vita. Baada ya miezi michache katika gereza kwenye mabweni ya kijeshi kule Joigny, katika Ufaransa ya kati, mimi nilihamishwa nikapelekwa Stettin, bandari moja katika iliyokuwa Prussia ya Mashariki. Sasa hiyo ni bandari ya Kipolandi ya Szczecin.

Kwa kuwa kwa kufuata kanuni hasa mimi nilikuwa katika gereza la jeshi la Ufaransa nilipotekwa na Wajeremani, nilitiwa katika kambi ya wafungwa wa vita, ambamo ugumu wa hali haukukaribia hata kidogo kuwa kama zile zilizokuwa katika kambi za mateso. Kambi hiyo ilikuwa bohari kubwa lenye nafasi ya wafungwa 500, likilindwa na washika-doria wenye silaha. Wafungwa walifanya kazi tofauti-tofauti jijini wakati wa mchana na wakarudishwa kambini jioni. Kwa hiyo mimi ningepataje jambo la kumfanyia Yehova, huku wanaume hao wakiwa wameondoka mchana kutwa?

Katika lile bohari kubwa, ulikuwamo ubao mkubwa ambapo habari zingeweza kubandikwa, nami nilipata ruhusa nitumie nafasi ndogo katika ubao huo. Nilipata karatasi fulani, na baada ya kuinyoosha-nyoosha, nikaandika maandishi mafupi kadhaa kuhusu habari za Biblia. Pale chini, nikaeleza mahali ambapo mimi ningeweza kupatwa na wakati ambapo mtu yeyote mwenye kupendezwa na ujumbe wa Ufalme wa Mungu angeweza kuja kuniona.

Kuwahubiria Watu wa Namna Zote

Njia hii ilileta matokeo mema. Baada ya muda mfupi niliweza kufanya mkutano mdogo kila jioni, kukiwa na watu sita, wanane, na nyakati fulani hata watu kumi wenye kuhudhuria. Mara nyingi mazungumzo yetu yaliendelea kwa saa moja au zaidi, ikitegemea maswali yaliyotokezwa. Mara kwa mara, mshika-doria Mjeremani aliyenena Kifaransa alijiunga ndani.

Kwa maana nilikuwa na Biblia moja tu, niliandikia Msalaba Mwekundu katika Geneva, nikiwaomba wanipelekee Biblia za kadiri ambayo wangeweza kupata. Muda ulipita, lakini hatimaye nikapokea furushi langu la kwanza la Biblia zilizotumika. Siku moja niliambiwa niende kwenye ofisi ya kambi kwa sababu mgeni fulani mwenye kuzuru, mwakilishi wa Msalaba Mwekundu, alitaka kuniona. Kumbe alikuwa mhudumu Mprotestanti. Yaonekana alifikiri kwamba mimi pia nilikuwa Mprotestanti. Alitamauka kidogo alipojua kwamba mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova.

Hata hivyo, alikuwa mwenye fadhili na hata akanipongeza kwa nililokuwa nikifanya. Alinihakikishia kwamba ningeweza kuendelea kuagiza Biblia na kwamba ningezipokea. Hiyo ikawa kweli. Hivyo, niliweza kugawanya karibu Biblia 300 katika muda niliokaa katika kambi hiyo. Baada ya vita, ilikuwa shangwe kama nini kujua kwamba mfungwa mmoja Mbelgiji mwenye kuitwa Wattiaux, ambaye nilikuwa nimemtolea ushahidi katika kambi ya Stettin, alikuwa amechukua msimamo wake upande wa ukweli!

Wakati wa utekwa wangu katika Ujeremani, mimi nilipendelewa kupokea vifurushi vya chakula kutoka kwa jamaa yetu. Baada ya muda mfupi niligundua kwamba ndani ya kila kifurushi mlikuwa mmefichwa pia wingi wa chakula cha kiroho chenye thamani kubwa. Dada yangu alichapa kwa taipureta makala za Mnara wa Mlinzi katika karatasi nyembamba sana na kuzificha katika pakiti za makaroni. Washika-doria hawakuzipata kamwe. Hata nilipokea nakala ya kitabu Children katika furushi la chakula. Kilithibitika kuwa msaada mkubwa kwangu katika huduma yangu.

Kupanua Huduma Yangu

Kwa maana nilikuwa mekanika, hatimaye niligawiwa kazi kwenye banda la kutengenezea tingatinga. Wajeremani 20 hivi, walio wengi kati yao wakiwa ni wazee mno wasiweze kuingizwa utumishi wa kijeshi, walifanya kazi humo. Kwa hiyo nilifanya jitihada za kujifunza Kijeremani kidogo. Tamaa niliyohisi moyoni ilikuwa kupanua huduma yangu nisiwe tena nikiwahubiria wafungwa wenye kunena Kifaransa tu.

Hata hivyo, ilikuwa lazima nitende kwa hadhari kwa sababu wafanya kazi Wajeremani waliogopa kusema wazi maoni yao peupe. Kwa hiyo niliongea nao mmoja mmoja. Kwa kawaida, wao waliijua Biblia vizuri sana na walikuwa wamesikia habari za Mashahidi wa Yehova. Baadhi yao hata walijua kwamba Mashahidi wengi walikuwa wamepelekwa kwenye kambi za mateso.

Kila siku katika banda la kutengeneza vilivyoharibika, nilijikuta mwishowe nikizunguka-zunguka kuambia wafanya kazi wenzangu kuhusu ukweli. Baadhi yao walipendelea ujumbe huo, lakini mwanamume aliyekuwa msimamizi wa mahali hapo hakuupendelea. Bila shaka nilizidi mno nilipoandika kwa chokaa Jehovas Zeugen (Mashahidi wa Yehova) katika ubao wake wa kufanyia kazi ili kumsaidia aelewe mimi nilikuwa nani. Mwanamume huyo alionekana mwenye woga mwingi alipoona jina hilo na alilifuta haraka. Lakini hakuniadhibu. Wakati ulipozidi kupita, wafanya kazi wengine wakawa wenye urafiki. Kwa uhakika, waliniletea chakula kingi sana hata nikaweza kukishiriki pamoja na wafungwa wengine kadhaa niliporudi kambini.

Yehova, Ngome Imara

Muda wa miaka iliyopita, nimejifunza kwamba sikuzote sisi twaweza kumfanyia Yehova na mwanadamu mwenzetu jambo fulani, hata hali ziwe ngumu kadiri gani. Stettin ulipigwa makombora mengi mara kadhaa na majeshi ya Wafungamani. Sisi tulijaribu kujificha katika mahandaki yaliyofunikwa kwa magogo na ardhi. Vitu hivi vilitutolea usalama wa kuwazia tu, kwa maana wafungwa wengi walipoteza maisha zao katika mahandaki hayo. Wakati wa yale maparamio ya kushambuliwa angani, nyakati fulani ningehisi mkono ukinishika imara gizani, kisha uniache mara tu paramio lile lilipomalizika. Sikujua kamwe huyo alikuwa nani. Yaonekana kwamba baadhi ya wafungwa walifikiri mimi nilikuwa na ulinzi maalumu kwa sababu niliongea kuhusu Mungu.

Wakati wa paramio moja la angani, kambi yetu iliteketezwa na makombora yenye moto ikawa ardhi tupu. Kwa kuachwa peke yetu katika barabara za mji, tulishuhudia tamasha nyingi za maogofyo. Raia wenye kuteseka kutokana na michomo mikali walijirusha ndani ya mitaro ya Mto Oder ambao hutiririka ukipitia Stettin. Majeruhi hawa wenye michomo walipotoka ndani ya maji yale, ile madini-fosforasi iliendelea kuwachoma. Wengi walikufa.

Kwa sababu ya kukaribia kwa vikosi vya Urusi, sisi tuliagizwa tuondoke Stettin tushike njia kwenda magharibi Neubrandenburg halafu tuendelee mpaka Gustrow. Tukiwa mahali palipoinuka katika tingatinga, tulisafiri kwa kufuata barabara ambayo vikombora vya Warusi vilianguka mara kwa mara. Mwishowe vifaru vya Kirusi vikatufikilia kule Güstrow. Vikosi vya Urusi vya kushtua watu vilitawala mji ule kwa juma moja. Vikosi vya Uingereza vilikuwa vinakaribia, na wakati wenye mamlaka wa Urusi walipokuwa wakingoja majeshi yale yakutane, walitenganisha wafungwa-wanajeshi kutoka kwa wafungwa-raia. Pia waliwaweka kizuizini baadhi ya wafungwa na kuwatia wale wengine (kutia na mimi) mikononi mwa Waingereza.

Huo ulikuwa ndio mwisho wa jinamizi la usiku. Majuma machache baadaye, nilijipata nikiwa nimerudi kwenye jukwaa la kituo cha reli cha Gare du Nord katika Paris. Mchana ulikuwa ndio sasa unaanza kuingia. Ilikuwa katikati ya Mei 1945, nami hatimaye nikawa nimerudi, baada ya miezi 69 ya utekwa.

Kupata Mambo Zaidi ya Kumfanyia Yehova

Katika 1946 Sosaiti ilinialika tena nikatumikie katika Betheli, wakati huo ikiwa katika Montmorency, kiunga kimoja kilicho kaskazini mwa Paris. Miezi michache baadaye, Ndugu Paul Dossman na mimi tuligawiwa kuzuru makundi katika Ufaransa tukiwa waangalizi wa mzunguko. Wakati huo, Mashahidi katika nchi nzima walikuwa hawajatimia vizuri 2,000. Leo, zaidi ya miaka 40 baadaye, kuna wahubiri zaidi ya mia moja elfu.

Baadaye niliitwa nirudi Betheli, wakati huo ikiwa katika sehemu ya makao ya watu Paris. Katika 1949, kwa kutiwa moyo mkuu na ndugu wamisionari wawili kutoka Uingereza, nilianza kujifunza Kiingereza—lakini lazima nikiri kwamba ilikuwa vigumu. Mwaka uliofuata, nilialikwa kwenye Shule ya Biblia ya Gileadi ya Mnara wa Mlinzi.

Niliporudi Ufaransa, kwa muda nilitumikia katika kazi ya mzunguko, halafu Sosaiti ikaniomba nitumikie nikiwa mmisionari katika Afrika. Kwa sasa, nilikuwa nimemwoa Titica, dada wa uzawa wa Kigiriki. Tulikaa Senegali kwa miaka mitano na tukapendelewa kuona kundi la kwanza likifanyizwa katika Dakar. Kwa sababu za afya, baadaye tulilazimika kurudi Ufaransa.

Sasa mimi nimo katika mwaka wangu wa 50 wa utumishi wa wakati wote na miaka yote hii nimekuwa na shangwe ya kusaidia watu zaidi ya mia moja wachukue msimamo wao upande wa ukweli. Yehova ameendelea kuwa mwema na mkarimu kwangu kweli kweli. Nimejifunza kutokana na yaliyonipata maishani kwamba hata hali yetu iwe nini, sikuzote sisi twaweza kupata njia fulani ya kumsifu na kumheshimu Mungu wetu, Yehova.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Jean Oueyroi pamoja na mke wake, Titica

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki