Ile Kanuni ya Kidhahabu kwa Nini Ingali Halali?
DHAHABU halisi haichujuki kamwe, kwa hiyo johari zilizopakwa dhahabu hutunukwa na kuthaminiwa. Badala ya kutupilia mbali vitu vya kidhahabu vilivyoharibika, wafua-dhahabu huifanya upya metali hiyo yenye thamani kubwa ili wafanyize sanaa mpya kwa sababu dhahabu hudumisha thamani yayo.
Vivyo hivyo, ingawa Yesu alitamka ile Kanuni ya Kidhahabu miaka elfu mbili hivi iliyopita, haijapungua thamani. Kwa kuchanganua, au kutafuta kujua, sababu za uhalali wayo, twaweza kuthamini ina ubora gani kwetu leo.
Yesu alipotupa sisi ile Kanuni ya Kidhahabu, “basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo,” aliongeza: “Maana hiyo ndiyo torati na manabii.” (Mathayo 7:12) Wanafunzi wa Yesu na wengine wenye kumsikiliza walielewaje jambo hilo?
‘Maana ya Torati na Manabii’
“Torati” ilirejezea miandiko ya mapema iliyojumlika kuwa vile vitabu vya kwanza vitano vya Biblia, Mwanzo hadi Kumbukumbu la Torati. Hivi vyafunua kusudi la Yehova kutokeza mbegu ambaye angeondolea mbali uovu. (Mwanzo 3:15) Katika vitabu hivyo vya mapema vya Biblia ilikuwamo pia ile Torati, au fungu la amri, ambalo katika 1513 K.W.K. Yehova alilipa taifa la Israeli kupitia Musa akiwa mpatanishi juu ya Mlima Sinai.
Sheria ya kimungu iliwatenga kando Israeli kutoka kwenye mataifa mapagani yaliyowazunguka, na Waisraeli hawakupaswa kufanya lolote la kuridhiana msimamo wao mbele za Yehova. Walikuwa mali yake pekee na ilikuwa lazima wabaki hivyo ili wapokee baraka zake. (Kutoka 19:5; Kumbukumbu 10:12, 13) Lakini kwa kuongezea wajibu wao mbalimbali kwa Mungu, Torati ya Musa ilitaja wazi daraka la Waisraeli kuwatendea mema wakaaji wa kigeni katika Israeli. Kwa kielelezo, ilitaarifu hivi: “Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi Bwana [Yehova, NW], Mungu wenu.” (Walawi 19:34) Wakati wa kipindi cha wafalme katika Israeli, wakaaji wa kigeni waliona shangwe kuwa na mapendeleo mengi, kama vile kushiriki katika ujenzi wa hekalu la Mungu katika Yerusalemu.—1 Nyakati 22:2.
Sheria waliyopewa Israeli ilikataza uzinzi, uuaji, wizi na choyo. Maamrisho haya, pamoja na ‘amri nyingine yoyote iliyopo,’ yangeweza kujumlishwa katika lile adilisho la kwamba, “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Mtume Paulo aliongeza hivi: “Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.”—Warumi 13:9, 10.
Ikiwa Torati ilipangilia wazi msingi wenyewe wa ile Kanuni ya Kidhahabu, namna gani kuhusu “Manabii”?
Vilevile vitabu vya kiunabii vya Maandiko ya Kiebrania vyathibitisha uhalali wa ile Kanuni ya Kidhahabu. Vyamwonyesha Yehova kuwa Mungu ambaye hutimiza kusudi lake kwa imani. Yeye hubariki watumishi wake wenye imani ambao, ingawa si wakamilifu, hujaribu kufanya penzi lake na kuonyesha toba ya kweli kuhusu vitendo vyao vya kupotoka. “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.”—Isaya 1:16, 17.
Watu wa Mungu walipofanya yaliyokuwa sawa kwa wengine na kwa Mungu, hapo Yehova aliwahakikishia kikamili kwamba angewategemeza. “BWANA [Yehova, NW] asema hivi, Shikeni hukumu [haki, NW], mkatende haki [uadilifu, NW] . . . Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana.”—Isaya 56:1, 2.
Kristo Aelekeza Kundi Lake
Kristo alikuja kutimiza Torati na Manabii, na tangu wakati wake, kusudi la milele la Yehova limeendelea kusonga mbele. (Mathayo 5:17; Waefeso 3:10, 11, 17-19) Mahali pa Torati ya zamani ya Musa pamechukuliwa na agano jipya, ambalo lahusisha ndani Wakristo wapakwa mafuta walio na wasio Wayahudi. (Yeremia 31:31-34) Hata hivyo, kundi la Kikristo la siku yetu lingali lafuata ile Kanuni ya Kidhahabu. Na hii hapa ni sababu zaidi ya kukubali uhalali wa kanuni hiyo: Kristo ndiye Kichwa mtendaji wa kundi la Kikristo la ki-siku-hizi. Yeye hajabadili maagizo yake. Ushauri wake uliovuviwa ungali wenye faida.
Kabla ya kuondoka kwenye dunia hii, Yesu aliamuru wafuasi wake wafanye wanafunzi wa watu wa mataifa yote na kuwafundisha “kushika mambo yote ambayo nimewaamuru nyinyi.” Agizo hilo lilitia ndani ile Kanuni ya Kidhahabu. Yesu alihakikishia wanafunzi wake hivi: “Tazama! mimi nipo pamoja na nyinyi siku zote mpaka umalizio wa mfumo wa mambo.”—Mathayo 28:19, 20, NW.
Kama ilivyoandikwa kwenye Luka 6:31, Yesu aliamuru hivi: “Kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo.” Lo, Yesu aliweka kielelezo kizuri kama nini katika kuchukua hatua ya kwanza kutendea wengine mema!
Katika mwendo wa huduma yake ya kidunia, Yesu alitazama kwa uangalifu mambo ambayo watu walilazimika kuyavumilia, naye akawahurumia. Wakati wa moja ya ziara zake za kuhubiri, yeye aliona umati wa watu na akawasikitikia. Lakini zaidi ya hilo, alifanya mipango ya kuwasaidia. Jinsi gani? Kwa kupanga kitengenezo kampeni nzito ya kuhubiri ambayo iliwaleta wanafunzi kwenye makao ya watu. Kama alivyoelekeza: “Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu [mwenye kustahili, NW]; mkae kwake hata mtakapotoka.” Kwamba kazi hii ilikuwa na utegemezo na baraka ya Yehova yaonwa wazi kutokana na maneno haya zaidi ya Yesu: “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. . . . Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.” —Mathayo 9:36–10:42.
Kwamba ile Kanuni ya Kidhahabu yadokeza kuchukua hatua hakika kwa ajili ya wengine yaonwa kutokana na jinsi Yesu alivyo sababu mambo katika pindi nyingine: “Mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema . . . na thawabu yenu itakuwa nyingi.” (Luka 6:32, 33, 35) Hivyo, kushika ile Kanuni ya Kidhahabu ambayo bado ni halali kutatuharakisha sisi kuchukua hatua ya kwanza kuwatendea mema hata watu tusiowajua kibinafsi.
Ingali Halali, Ingali Yafanya Kazi
Labda uthibitisho ambao ni wenye kukata shauri zaidi kwamba ile Kanuni ya Kidhahabu ingali halali watokana na yaliyoonwa kikweli na wenye kuishi kulingana nayo. Wakristo ambao hujiendesha kila siku kupatana na sheria za Mungu hupata shangwe kubwa na, mara nyingi, baraka zisizotarajiwa. Kwa kuwa mwenye hisani na fadhili kwa wafanya kazi wa kliniki moja ya kitiba aliyoitumia, mwanamke mmoja Mkristo alipata kwamba alinufaika kwa jinsi wauguzi na madaktari walivyojishughulisha sana ili wamtunze.
Mashahidi wa Yehova wenye kuhusika katika miradi ya ujenzi-haraka wa Majumba ya Ufalme waweza pia kuthibitisha uhalali wa ile Kanuni ya Kidhahabu. Mara nyingi wao hupata itikio zuri kwa kufanya ziara zenye fadhili kwa watu wanaoishi karibu na mahali pa ujenzi ili kuwapasha habari wamepanga kufanya nini. Hivyo watu ambao hapo kwanza walipinga Mashahidi huona kwamba wao huwatendea mema jirani zao, nao hujionea wenyewe jinsi watu wa Mungu hufanya ushirikiano katika kazi yao. Tokeo ni kwamba, baadhi yao wamejitolea kusaidia ujenzi, moja kwa moja ama kwa kutoa vifaa walivyo navyo. —Linganisha Zekaria 8:23.
Wakati Shahidi Mwirani anayeishi London, Uingereza, aliponunua chakula kwenye duka moja, mwenye duka alimtusi kwa sababu hakuwa mwananchi. Bila kukata tamaa, Shahidi huyo akaeleza kwa fadhili na busara kwamba yeye, akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, hakuwa na hisia mbaya kuelekea watu wa mataifa mengine. Bali, yeye huzuru watu wote katika ujirani akiwa na ujumbe wa Biblia. Tokeo likawa nini? Mwenye duka huyo aliongeza vitamutamu vya ziada kwenye agizo la chakula cha Shahidi huyo.
Bila shaka, ile Kanuni ya Kidhahabu haihusu hivyo vitendo vidogo tu vya fadhili. Kwa uhakika, wonyesho mkubwa zaidi wa kanuni hiyo ni wema ambao Mashahidi wa Yehova hufanya ulimwenguni pote kwa kuzuru makao ya jirani zao kwa ukawaida wakiwa na ujumbe wa habari njema za Ufalme wa Mungu.
Kuishi Kulingana na ile Kanuni ya Kidhahabu
Kutumia ile Kanuni ya Kidhahabu kwamaanisha kugeuza uangalifu wako uwaelekee wengine. Kanuni hiyo ni mwongozo wa kuchukua hatua hakika. Utahitaji kutafuta pindi za kuwatendea mema wale walio kandokando yako. Jitokeze kuwaonyesha urafiki na hangaikio, huku ukiwaonyesha upendezi wa kibinafsi! (Wafilipi 2:4) Kwa kufanya hivyo, utavuna baraka nyingi. Hapo wewe utakuwa unafuata ushauri huu wa Yesu: “Nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” (Mathayo 5:16) Halafu tena, Yehova atakuwa Mthawabishi wako umtafutapo kwa bidii na kuishi kila siku kulingana na ile Kanuni ya Kidhahabu.—Waebrania 11:6.