Uthibitisho wa Utukufu wa Sulemani
KULINGANA na orodha ya matukio ya Biblia, Mfalme Sulemani alitawala Israeli kuanzia 1037 K.W.K. hadi 998 K.W.K. Kwa kupendeza, kitabu The Archaeology of the Land of Israel, kilichotungwa na Profesa Yohanan Aharoni, chafunua jinsi maendeleo yenye mabadiliko makubwa katika mwerevuko wa Kiisraeli yalivyotukia “karibu 1000 K.W.K.”
Kielelezo kimoja kilichotolewa na Aharoni ni uthibitisho wa kuta imara za jiji zilizojengwa kwa mawe makubwa “yaliyokatwa yakawa bloki za umbo mstatili, zilizounganishwa zikaingiana vizuri kabisa.” Tofauti na hivyo, katika nchi zilizo jirani ya Israeli, sehemu za kuta za jiji ‘zilifanyizwa kwa matufali na mbao.’
Tena, majiji yaliyojengwa karibu na wakati wa Sulemani yatoa uthibitisho wa uangalifu wa kuchora ramani za ujenzi, kukiwa na mistari ya nyumba zilizopangwa kwa unadhifu na barabara zilizopangwa kwa uangalifu. Aharoni achanganua magofu ya “miji minne katika Yuda iliyojengwa kulingana na ramani ile ile moja ya msingi . . . Beer-sheba, Tell Beit Mirsim, Beth-shemeshi, na Mispa.” Hiyo yatofautiana kama nini na kitovu kingine kikubwa cha mwerevuko—Uru jiji lile la mapema zaidi la Mesopotamia! Kwa habari yalo, Sir Leonard Woolley aliandika hivi: “Hakukuwa kumekuwako jaribio lolote la kuchora ramani ya mji . . . Zile barabara zisizolainishwa vizuri, nyingi zazo zikiwa ni njia zenye kukoma ghafula . . . zilikuwa vurugu ambalo mtu angeweza kupotea njia kwa urahisi.”
Aharoni aeleza pia juu ya maendeleo yaliyofanyiwa vyombo vya nyumbani karibu na wakati wa utawala wa Sulemani. “Badiliko la utamaduni wa vitu vya kimwili . . . laweza kuonekana wazi si katika vitu vya anasa tu bali pia hasa katika vyungu vilivyoundwa kwa ustadi . . . Ubora wa ufinyanzi huo na ukaushaji wao wa kutumia moto ulifanyiwa maendeleo yasiyo na kifani . . . Kulitokea kwa ghafula ujumla wa namna mbalimbali za vyombo.”
Sehemu tukufu zaidi ya utawala wa Sulemani ilikuwa lile hekalu lenye fahari nyingi, lile jumba la kifalme, na majengo ya serikali katika Yerusalemu. Dhahabu nyingi sana ilitumiwa kupamba majengo hayo. (1 Wafalme 7:47-51; 10:14-22) Miaka mitano baada ya kifo cha Sulemani, Farao Shishaki wa Misri alikuja akakumba hazina ya Yerusalemu.—1 Wafalme 14:25, 26.
Katika Misri na Palestina pia, nakshi zilizochimbuliwa ardhini zathibitisha kwamba kwa kweli Shishaki alishinda Israeli. Kwa uhakika, wanahistoria wengi hukiri kwamba uporaji wa Shishaki kwa Yerusalemu ulitia nguvu mpya katika uchumi dhaifu wa Kimisri na kumwezesha Shishaki apate pesa za mpanuko mkubwa sana wa hekalu moja la Kimisri ambalo aliandika juu yalo habari za ushindi wake, kama ionwavyo katika ukurasa huu. Shishaki alikufa muda mfupi baada ya hapo, na nakshi nyingine ina habari za kwamba mwana wake aliyachangia mahekalu ya Misri karibu tani 200 za dhahabu na fedha. Nakshi hiyo haifunui chanzo cha utajiri huo, lakini mwanaakiolojia Alan Millard, katika kitabu chake Treasures From Bible Times, hudokeza kwamba “kiasi kikubwa kilikuwa ile dhahabu ambayo Shishaki alichukua kutoka Hekalu la Sulemani na jumba la kifalme katika Yerusalemu.”
Si ajabu kwamba hata chanzo kisichoamini kuna Mungu hukiri uhalisi wa utawala mtukufu wa Sulemani! Bol’shaia Sovetskaia Entsiklopediia (Ensaiklopedia Kubwa ya Kirusi), chini ya habari “Sulemani,” humwita yeye “mtawala wa ufalme wa Israeli na Yudea,” ikiongezea kwamba alitawala wakati wa “ufanisi mkubwa zaidi wa ufalme huo.”