Je! Kweli Ainabinadamu Inahitaji Mesiya?
“ULIMWENGU WAHITAJI MESIYA, ASEMA OFISA”
Kichwa kikuu hicho kilitokea katika gazeti The Financial Post la Toronto, Kanada, katika 1980. Ofisa huyo aliyenukuliwa alikuwa Aurelio Peccei, msimamizi na mwanzilishi wa shirika mashuhuri la utafiti liitwalo Club of Rome. Kulingana na Post, Peccei aliamini kwamba “kiongozi mwenye uwezo wa kuwavutia watu—mwanasayansi, mwanasiasa, au mtu wa kidini—angekuwa ndiye wokovu wa pekee wa ulimwengu kutoka katika michafuko ya kijamii na ya kiuchumi inayotisha kuuharibu ustaarabu.” Wewe unafikirije? Je! ulimwengu huu umo katika hali mbaya sana hivi kwamba ainabinadamu inahitaji Mesiya? Fikiria tatizo moja tu ambalo ulimwengu huu unakabili—njaa.
MACHO mawili makubwa ya kahawia yakutazama kutoka picha iliyomo katika nyusipepa au gazeti. Hayo ni macho ya mtoto, msichana mdogo ambaye hata hajafikia umri wa miaka mitano. Lakini macho hayo hayakufanyi utabasamu. Hayana uchangamfu wa kitoto, hayana ule mshangao wenye furaha, hayana tumaini lolote. Badala ya hivyo, yamejaa uchungu mkali, maumivu, njaa isiyo na tumaini. Mtoto huyo anakufa njaa. Maumivu na njaa ni mambo pekee ambayo amepata kujua.
Labda, kama wengi, wewe hupendi kuzitazama picha hizo kwa muda mrefu, kwa hiyo unageuza ukurasa huo upesi. Si kwamba hujali, lakini unahisi umefadhaika kwa sababu unadhani kumekuwa kuchelewa mno kwa msichana huyo. Viungo vilivyodhoofika na tumbo lililofura ni ishara kwamba mwili wake umeanza tayari kujimeza wenyewe. Kufikia wakati uonapo picha yake, huenda ikawa amekwisha kufa. Kwa ubaya hata zaidi, wajua ya kwamba kisa chake si cha pekee.
Tatizo hilo limeenea kadiri gani hasa? Je! waweza kuwazia watoto milioni 14? Wengi wetu hatuwezi; hesabu hiyo ni ya juu sana kuweza kuwazia. Ebu wazia, basi, stediamu itoshayo watu 40,000. Sasa iwazie ikiwa imejaa tele watoto—safu baada ya safu, tabaka baada ya tabaka, bahari ya nyuso. Hata hilo si rahisi kuwazia. Hata hivyo, ingechukua stediamu 350 za jinsi hiyo zilizojaa watoto ili kufikia jumla ya watu milioni 14. Kulingana na UNICEF (Hazina ya Umoja wa Mataifa Kwa Ajili ya Watoto), hiyo ndiyo hesabu yenye kuhofisha ya watoto katika nchi zinazositawi, walio na umri ulio chini ya miaka mitano ambao hufa kila mwaka kwa ajili ya utapiamlo (ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa chakula kinachofaa) na magonjwa yawezayo kukingwa kwa urahisi. Hilo lajumuika kuwa karibu stediamu moja ya watoto wakifa kila siku! Ongezea hiyo hesabu ya watu wazima wenye njaa, na unapata jumla ya ulimwenguni pote ya watu bilioni moja hivi wanaokosa chakula kinachofaa daima.
Kwa Nini Kuna Njaa Hiyo Yote?
Kwa sasa sayari hii hutokeza chakula kingi zaidi ya kile ambacho wanadamu hula sasa, na ina uwezo wa kutokeza zaidi. Hata hivyo, kila dakika, watoto 26 hufa kutokana na utapiamlo na ugonjwa. Katika dakika hiyohiyo, ulimwengu hutumia karibu dola 2,000,000 kutayarishia vita. Je! waweza kuwazia lile ambalo pesa hizo zote—au sehemu yazo tu—zaweza kuwafanyia watoto hao 26?
Kwa wazi, njaa ya ulimwengu haiwezi kulaumiwa kwa ukosefu wa chakula au pesa tu. Tatizo ni lenye kina kirefu zaidi. Kama vile Jorge E. Hardoy, profesa wa Argentina, alivyoeleza, “ulimwengu kwa ujumla hauwezi hata kidogo kushiriki faraja, nguvu, wakati, nyenzo na maarifa pamoja na wale wanaohitaji mambo hayo zaidi.” Naam, tatizo limo, si katika nyenzo za mwanadamu, bali katika mwanadamu mwenyewe. Pupa na ubinafsi vyaonekana kuwa ndivyo uvutano mkuu katika jamii ya kibinadamu. Sehemu moja kwa tano ya wakazi wa dunia wenye utajiri mwingi zaidi huonea shangwe mali na utumishi wa mara 60 hivi kuliko ile sehemu moja kwa tano ya wale wenye umaskini kabisa.
Ni kweli, wengine wanajaribu kwa unyoofu kuwapelekea chakula wenye njaa, lakini jitihada zao nyingi huzuiwa na visababishi wasivyoweza kudhibiti. Njaa kuu mara nyingi huzipata nchi ambazo zimefarakishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe au na uasi, na si jambo lisilo la kawaida kwa majeshi yanayopigana kuzuia ugavi wa msaada usiwafikie wale wenye uhitaji. Pande zote mbili huhofu kwamba kwa kuruhusu chakula kiwafikie raia wanaokufa njaa katika eneo la adui, watakuwa wakiwalisha adui zao. Serikali zenyewe hutumia njaa kali kuwa silaha ya kisiasa.
Hakuna Suluhisho?
Kwa kusikitisha, tatizo la mamilioni wanaokufa njaa si tatizo la pekee linalompata mwanadamu wa ki-siku-hizi. Uharibifu na utiaji sumu wa mazingira unaoenea, lile pigo la vita lenye kudumu linaloharibu mamilioni ya uhai, na uhalifu wenye jeuri wenye kuenea unaosababisha hofu na kutoaminiana kila mahali, na hali ya maadili yanayoendelea kupungua ambayo huonekana kuwa ndio msingi wa mengi ya matatizo hayo—matatizo hayo yote ya tufeni pote, ni kana kwamba huunganika na kuyakinisha ile kweli isiyoweza kukanushwa—mwanadamu hawezi kujiongoza mwenyewe kwa mafanikio.
Bila shaka hiyo ndiyo sababu watu wengi wamekata tamaa ya kuona suluhisho la matatizo ya ulimwengu. Wengine huhisi kama Aurelio Peccei, yule mwanachuo Mwitaliano aliyetajwa mwanzoni. Ikiwa kutakuwako suluhisho, wao huwaza, ni lazima lije kutoka kwa chanzo kisicho cha kawaida—labda kipitacho uwezo wa kibinadamu. Hivyo wazo la mesiya lina uvutano wenye nguvu. Lakini je, ni jambo la kihalisi kutumaini katika mesiya? Au tumaini la jinsi hiyo ni matamanio ya kimawazo tu?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Picha za jalada Juu: Picha ya U.S. Naval Observatory; Chini: Picha ya NASA
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Picha ya WHO iliyopigwa na P. Almasy
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
Picha ya WHO iliyopigwa na P. Almasy
Picha ya U.S. Navy