William Whiston—Mzushi au Msomi Mwenye Kufuatia Haki?
JE! UNGEDHABIHU kazi-maisha yako kwa ajili ya itikadi zako? William Whiston alifanya hivyo.
Yeye alitokeza ubishi wa kidini mapema katika karne ya 18, alipobishana na Kanisa la Uingereza juu ya mafundisho ya Biblia. Kama tokeo, mwishowe aliitwa mzushi. Hivyo mwendo wake ulimletea dhihaka lakini pia ukamletea staha.
William Whiston alikuwa nani? Naye alitimiza nini?
Msomi wa Biblia
William Whiston alikuwa rafiki mwenye ujuzi wa Sir Isaac Newton katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Ukichunguza chapa ya Kiingereza ya maandishi ya mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza Flavio Yosefo, yaelekea utakuwa ukisoma tafsiri iliyofanywa na Whiston katika 1736. Ingawa tafsiri nyinginezo ziko, tafsiri yake ya usomi, pamoja na maandishi yake na insha, zapita nyingine zote na bado zachapishwa. Wengi huona kitabu hicho kuwa kilele cha matimizo ya Whiston.
Hata hivyo, tafsiri ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ya Whiston iitwayo Primitive New Testament, ni kitabu kisichopaswa kupuuzwa. Kilichapishwa katika 1745, akiwa katika mwaka wake wa 78. Whiston alitafsiri zile Gospeli nne na Matendo ya Mitume kutoka kwa Kodeksi ya Bezae, barua za Paulo kutoka kwa Kodeksi ya Clermont, na sehemu iliyobakia, kutia Ufunuo, kutoka kwa Hati-Kunjo ya Aleksandria. Kwa uangalifu, yeye hakutia ndani ile sehemu isiyo asilia ya 1 Yohana 5:7. Whiston alichagua vyanzo hivyo vitatu vya Kigiriki vya kale vikiwa vyanzo bora zaidi vilivyopatikana wakati huo.
Kichocheo cha yale aliyofanya Whiston kilikuwa ni kupenda Biblia. Kuamini kuwako kwa Mungu, fundisho kwamba kusababu pekee badala ya dini kwatosha kuwa msingi wa kuitikadi katika Mungu ndiko kulikoenea katika siku yake. Kulingana na kitabu William Whiston—Honest Newtonian, yeye alishikilia sana “yale maoni ya kimapokeo kwamba Biblia ni chanzo kimoja kisichobatilika cha historia ya kale.” Neno “Newtonian” hapa larejezea Isaac Newton, aliyejulikana zaidi kwa kitabu chake Principia, ambamo alifafanua juu ya nguvu za uvutano za ulimwengu wote mzima. Njia ya kufikiri ya Newton ilikuwa na tokeo kubwa juu ya William Whiston. Jinsi gani?
Nyutu Zenye Kutofautiana
William Whiston alizaliwa katika 1667, akiwa mwana wa kasisi mmoja wa Kanisa la Uingereza. Baada ya kutawazwa kuwa kasisi katika 1693, yeye alirudi kwenye Chuo Kikuu cha Cambridge ili kujifunza hesabu na kuwa msaidizi wa Newton. Urafiki wa karibu ulikua kati yao. Newton alipoacha cheo chake akiwa Profesa wa Hesabu karibu miaka mitatu baadaye, yeye alihakikisha kwamba Whiston amechaguliwa mahali pake. Akifuatia kazi-maisha yake, Whiston alifundisha elimu-anga na hesabu, lakini uvutano wa Newton ulimchochea pia kuwa na upendezi mkubwa zaidi katika kronolojia na mafundisho ya Biblia.
Newton alikuwa mtu wa kidini. Akiamini kwa uthabiti Miaka Elfu ya Biblia, aliandika mambo mengi juu ya unabii mwingi wa Danieli na Ufunuo. Hata hivyo, ni kama hakuna yoyote ya maandishi hayo yaliyochapishwa wakati wa maisha yake. Yeye alikataa fundisho la Utatu. Lakini wakati ulipofika wa kuchapisha ithibati yake dhidi ya Utatu, “Newton alikataa kuunga mkono fundisho hilo akihofu kwamba maoni yake ya kupinga Utatu yangejulikana,” laonelea The New Encyclopædia Britannica. F. E. Manuel aeleza jambo hilo hivi katika kitabu Isaac Newton, Historian: “Kikundi cha Newton ama kiliweka maoni yacho yakiwa siri ama kikazuia msisimuko wacho. . . . Mahali ambapo Newton alikuwa mwenye usiri, Whiston alisema waziwazi.” Hivyo wanaume hao wawili walitofautiana utu.
Kutengwa
Katika Julai 1708, Whiston aliandikia maaskofu wakuu wa Canterbury na pia wa York, akihimiza kuwe na mabadiliko katika mafundisho ya Kanisa la Uingereza kwa habari ya fundisho la uwongo la Utatu kama lilivyoonyeshwa katika Imani ya Athanasio. Kwa kueleweka, yeye alishauriwa awe mwenye tahadhari. Lakini Whiston alisisitiza. “Nimechunguza mambo hayo kabisa kabisa,” yeye akasema, “na nimesadiki kabisa kabisa kwamba kanisa la kikristo limedanganywa sana katika mambo hayo kwa muda mrefu; na, kwa baraka za Mungu, ikiwa ni katika uwezo wangu, kanisa halitadanganywa tena.”
Newton alihofia cheo chake cha kijamii na kiusomi. Kwa upande ule mwingine, Whiston hakuhofu. Baada ya kufanyiza itikadi zake za kupinga Utatu, yeye aliandika kijitabu chenye maoni yake. Lakini katika Agosti 1708, Chuo Kikuu cha Cambridge kilikataa kumpa Whiston leseni ya kuchapisha kijitabu chake, kwa sababu kilionwa kuwa chenye kupinga dini.
Katika 1710, Whiston alishtakiwa kwa kufundisha mafundisho yaliyo kinyume cha itikadi ya Kanisa la Uingereza. Alipatikana na hatia, akapokonywa uprofesa wake, na kufukuzwa kutoka Cambridge. Hata hivyo, kujapokuwa mashtaka ya mahakamani dhidi yake, ambayo yaliendelea kwa karibu miaka mitano zaidi, Whiston hakuhukumiwa kamwe kuwa mzushi.
Ingawa maoni ya Newton ya kupinga Utatu yalipatana na yale ya Whiston, yeye hakumuunga mkono rafiki yake na hatimaye alimtenga. Hatimaye katika 1754, kitabu cha Newton cha Kibiblia kilichofunua Utatu kilichapishwa—miaka 27 baada ya kifo chake. Lakini huko kulikuwa kuchelewa mno kuweza kumsaidia Whiston, aliyekuwa amekufa miaka miwili mapema.
Newton pia hufikiriwa kuwa ndiye aliyehusika katika kumzuia Whiston asijiunge na Kundi la Kifalme lililokuwa mashuhuri. Lakini Whiston hakuvunjika moyo. Yeye na familia yake walihamia London, ambako alianzisha Kundi la Kuendeleza Ukristo wa Mapema. Alitia nishati zake zote katika uandishi, kitabu chake muhimu zaidi kufikia wakati huo kikiwa kile chenye mabuku manne cha Primitive Christianity Revived.
Awa Mbishi Hadi Mwisho
Akiwa mwanasayansi, Whiston alifanya kazi kwenye njia tofauti kwa ajili ya mabaharia ili kujua longitudo ya bahari. Hata ingawa mawazo yake hayakutumiwa, hatimaye udumifu wake uliongoza kwenye usitawi wa kronometa ya baharini. Ingawa mengi ya maoni ya Whiston juu ya unabii wa Biblia, kama yale ya wenzake wa wakati huo, hayajakuwa sahihi, yeye alijaribu kutafuta kweli kwa kila njia. Trakti zake juu ya mzunguko wa vimondo na nadharia yake juu ya matokeo ya Gharika ya siku ya Noa ni miongoni mwa trakti nyingi alizoandika ili kutetea kweli yake ya kisayansi na Kibiblia. Hata hivyo, maandishi yake yanayofunua fundisho la Utatu kuwa si la kimaandiko yapita ubora yale mengineyo.
Kama kawaida yake, Whiston aliacha Kanisa la Uingereza katika 1747. Yeye aliacha kanisa hilo kihalisi, na pia kitamathali, alipoondoka kanisani wakati kasisi mmoja alipoanza kusoma Imani ya Athanasio. Kitabu A Religious Encyclopædia husema hivi juu ya Whiston: “Ni lazima mtu avutiwe na utu wake wa kusema mambo waziwazi na ukweli kimwanamume, hali ya upatano katika maisha yake, na mwenendo wake wa kufanya mambo kwa njia ya moja kwa moja.”
Kwa habari ya William Whiston, yeye hangeridhiana juu ya kweli, na masadikisho ya kibinafsi yalikuwa ya thamani zaidi ya kibali na sifa ya wanadamu. Ingawa alikuwa mbishi, Whiston alikuwa msomi mwenye kufuatia haki aliyeitetea Biblia bila hofu kuwa Neno la Mungu.—2 Timotheo 3:16, 17.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
Copyright British Museum