Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 10/15 kur. 21-26
  • Je, Wewe Husamehe Kama Afanyavyo Yehova?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Wewe Husamehe Kama Afanyavyo Yehova?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Musa Asihi—Yehova Asikiliza
  • Ibada-Sanamu ya Manase na Uzinzi wa Daudi
  • Kuwekwa Wakfu kwa Hekalu na Sulemani
  • Msamaha Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo
  • ‘Endeleeni Kusameheana kwa Hiari’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Yehova, Mungu Aliye “Tayari Kusamehe”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Yehova—Mfano Bora wa Kusamehe
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2022
  • Kwa Nini Uwe Mwenye Kusamehe?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 10/15 kur. 21-26

Je, Wewe Husamehe Kama Afanyavyo Yehova?

“Mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.”—MATHAYO 6:14, 15.

1, 2. Twahitaji Mungu wa aina gani, na kwa nini?

“BWANA amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”—Zaburi 103:8-14.

2 Tukiwa tumetungwa mimba katika dhambi na kuzaliwa na makosa, huku kutokamilika kulikorithiwa sikuzote kukijaribu kutuongoza kwenye sheria ya dhambi, twahitaji sana Mungu ‘akumbukaye ya kuwa sisi tu mavumbi.’ Miaka 300 baada ya Daudi kumfafanua Yehova vizuri sana katika Zaburi ya 103, mwandikaji mwingine wa Biblia, Mika, alimhimidi Mungu uyo huyo kwa njia iyo hiyo kwa sababu ya njia yake ya rehema ya kusamehe dhambi zilizofanywa: “Ni mungu yupi awezaye kulingana na wewe: anayeondolea mbali makosa, anayesamehe uhalifu, asiyekuwa na hasira ya daima lakini afurahiaye katika kuonyesha rehema? Uturehemu tena mara moja, achilia mbali makosa yetu, uzitupe dhambi zetu zote chini ya bahari.”—Mika 7:18, 19, The Jerusalem Bible.

3. Yamaanisha nini kusamehe?

3 Katika Maandiko ya Kigiriki, neno “samehe” lamaanisha “kuachilia.” Ona kwamba Daudi na Mika, waliotoka kunukuliwa, wawasilisha maana iyo hiyo katika maneno ya kupendeza na yenye ufafanuzi sana. Ili tuelewe kabisa kadiri kubwa ya msamaha wa Yehova, ebu tupitie vichache kati ya vielelezo vingi vya msamaha ukionyeshwa. Kielelezo cha kwanza chaonyesha kwamba akili ya Yehova yaweza kubadilika kutoka mwendo wa kuleta uharibifu hadi wa msamaha.

Musa Asihi—Yehova Asikiliza

4. Ni baada ya maonyesho yapi ya uwezo wa Yehova Waisraeli bado waliogopa kuingia katika Bara Lililoahidiwa?

4 Yehova alileta taifa la Israeli kwa usalama kutoka Misri na karibu na bara alilokuwa amewaahidi kuwa makao yao, lakini wao walikataa kusonga mbele, wakiogopa wanadamu duni tu wa Kanaani. Baada ya kuona Yehova akiwakomboa kutoka Misri akitumia mapigo kumi yenye uharibifu mwingi, akiwafungulia njia ya kuponyokea kupita Bahari Nyekundu, akiwaharibu majeshi ya Misri yaliyojaribu kuwafuata, akianzisha pamoja nao katika Mlima Sinai lile agano la Sheria lililowafanya kuwa taifa teule la Yehova, na kuwaandalia kimwujiza mana ya kila siku ili kuwategemeza, waliogopa kuingia katika Bara Lililoahidiwa kwa sababu ya Wakanaani fulani wenye miili mikubwa!—Hesabu 14:1-4.

5. Wapelelezi wawili waaminifu walijaribuje kutia moyo Israeli?

5 Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi kwa mfadhaiko. Yoshua na Kalebu, wapelelezi wawili waaminifu, wakajaribu kutia moyo Israeli: ‘Nchi hiyo ni njema mno ajabu, nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Msiwaogope wale wenyeji, BWANA yu pamoja nasi!’ Badala ya kutiwa moyo na maneno hayo, watu hao waoga, wenye kuasi walijaribu kuwapiga Yoshua na Kalebu kwa mawe.—Hesabu 14:5-10.

6, 7. (a) Yehova aliamua kufanya nini Israeli lilipokataa kuingia katika Bara Lililoahidiwa? (b) Kwa nini Musa alikataa hukumu ya Yehova juu ya Israeli, na matokeo yakawa nini?

6 Yehova alikasirika! “BWANA akamwuliza Musa, Je! watu hawa watanidharau hata lini? wasiniamini hata lini? nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao. Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao. Basi Musa akamwambia BWANA, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao; kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii. . . . Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena, na kusema, Ni kwa sababu yeye BWANA hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani.”—Hesabu 14:11-16.

7 Musa alisihi wapate msamaha, kwa ajili ya jina la Yehova: “Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema zako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa.”—Hesabu 14:19, 20.

Ibada-Sanamu ya Manase na Uzinzi wa Daudi

8. Mfalme Manase wa Yuda alijiwekea rekodi ya aina gani?

8 Kielelezo kizuri zaidi cha msamaha wa Yehova ni kile kisa cha Manase, mwana wa Mfalme mzuri Hezekia. Manase alikuwa na umri wa miaka 12 alipoanza kutawala katika Yerusalemu. Yeye alijenga mahali pa juu, akazisimamisha madhabahu kwa ajili ya Mabaali, akafanyiza mti mtakatifu, akasujudia nyota za mbingu, akafanya uganga na uchawi, akafanyiza wawasiliani-roho na wabashirio mambo, akaweka sanamu iliyochongwa katika hekalu la Yehova, naye akawapitisha wanaye mwenyewe motoni katika Bonde la Hinomu. “Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA” naye ‘akaendelea kuwakosesha Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, hata wakazidi kufanya mabaya kuliko mataifa, aliowaharibu BWANA mbele ya wana wa Israeli.’—2 Mambo ya Nyakati 33:1-9.

9. Yehova alitulizwaje kumwelekea Manase, na matokeo yakawa nini?

9 Hatimaye, Yehova alileta Waashuru dhidi ya Yuda, nao walimkamata Manase na kumpeleka Babiloni. “Hata alipokuwa katika taabu, akamsihi BWANA, Mungu wake, akajinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake. Akamwomba; naye akamtakabali, akayasikia maombi yake; akamrudisha tena Yerusalemu katika ufalme wake.” (2 Mambo ya Nyakati 33:11-13) Kisha Manase akaondoa miungu ya kigeni, sanamu, na madhabahu na kuzitupa nje ya jiji. Akaanza kutoa dhabihu katika madhabahu ya Yehova na kuanzisha Yuda kuanza kumtumikia Mungu wa kweli. Huo ulikuwa wonyesho wa ajabu wa utayari wa Yehova kusamehe wakati unyenyekevu, sala, na hatua za kurekebisha hali zinapotokeza matunda yaonyeshayo toba!—2 Mambo ya Nyakati 33:15, 16.

10. Daudi alijaribu kufunikaje dhambi aliyofanya na mke wa Uria?

10 Dhambi ya uzinzi ambayo Mfalme Daudi alifanya pamoja na mke wa Uria Mhiti yajulikana sana. Yeye hakufanya uzinzi tu pamoja naye bali pia alitunga hila ya kuufunika mwanamke huyo aliposhika mimba. Mfalme huyo akampa Uria likizo atoke vitani, akimtarajia kwenda nyumbani kwake na kulala na mkeye. Lakini, kwa sababu ya kustahi wanajeshi wenzake waliokuwa vitani, Uria alikataa. Kisha Daudi akamwalika kwa mlo na kumfanya alewe, lakini Uria bado hakuenda kulala na mkeye. Kisha Daudi akampelekea jemadari wake ujumbe wa kumweka Uria mahali vita imewaka zaidi ili Uria auawe, na ikawa hivyo.—2 Samweli 11:2-25.

11. Daudi aliletwaje kwenye toba ya dhambi yake, lakini alipatwa na nini?

11 Yehova alimtuma nabii wake Nathani kumwendea Daudi ili afichue dhambi ya mfalme huyo. “Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.” (2 Samweli 12:13) Daudi alihisi kuwa na hatia sana juu ya dhambi yake naye akaeleza toba yake katika sala yake itokayo moyoni kwa Yehova: “Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.” (Zaburi 51:16, 17) Yehova hakudharau sala ya Daudi iliyotolewa kwa moyo uliovunjika. Na bado, Daudi aliadhibiwa vikali, kwa kupatana na taarifa ya Yehova kuhusu msamaha kwenye Kutoka 34:6, 7: “Si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe.”

Kuwekwa Wakfu kwa Hekalu na Sulemani

12. Sulemani aliomba nini wakati wa kuwekwa wakfu kwa hekalu, na Yehova aliitikiaje?

12 Sulemani alipomaliza kujenga hekalu la Yehova, yeye alisema hivi katika sala yake ya kuweka wakfu: “Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.” Yehova akajibu: “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”—2 Mambo ya Nyakati 6:21; 7:13, 14.

13. Ezekieli 33:13-16 yaonyesha nini kuhusu maoni ya Yehova juu ya mtu?

13 Yehova akutazamapo, yeye akupa kibali kwa kile ulicho sasa, si kile ulichokuwa zamani. Itakuwa kama vile Ezekieli 33:13-16 isemavyo: “Nimwambiapo mwenye haki, ya kwamba hakika ataishi; kama akiitumainia haki yake, akatenda uovu, basi katika matendo yake ya haki, hata mojawapo halitakumbukwa; bali katika uovu wake alioutenda, atakufa katika uovu huo. Tena, nimwambiapo mtu mwovu, Hakika utakufa; kama akighairi, na kuiacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki; kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang’anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa. Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki; hakika ataishi.”

14. Ni jambo gani lililo tofauti kuhusu njia ya Yehova ya kusamehe?

14 Msamaha ambao Yehova Mungu atuandalia una pande fulani iliyo tofauti, ambayo ni vigumu kwa viumbe vya kibinadamu kutia ndani ya msamaha wanaotoleana—yeye husamehe na kusahau. Watu fulani watasema kwamba, ‘Naweza kusamehe jambo ulilotenda, lakini siwezi kulisahau (au sitalisahau).’ Tofauti na hilo, ona yale Yehova asemayo atafanya: “Nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.”—Yeremia 31:34.

15. Yehova ana rekodi gani ya msamaha?

15 Yehova amekuwa akisamehe waabudu wake duniani kwa maelfu ya miaka. Yeye amekuwa akisamehe dhambi walizofanya wakijua na pia nyingi ambazo hawakujua wakizitenda. Andalio lake la rehema, ustahimilivu, na msamaha limekuwa jingi mno. Isaya 55:7 yasema: “Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; na amrudie BWANA, naye atamrehemu; na arejee kwa Mungu wetu, naye atamsamehe kabisa.”

Msamaha Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo

16. Kwa nini twaweza kusema kwamba mazoea ya Yesu ya kusamehe yapatana na ya Yehova?

16 Habari ya msamaha wa Mungu zimejaa katika maandishi ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Yesu huutaja mara nyingi, akionyesha kwamba anapatana na akili ya Yehova kwa habari hiyo. Kufikiri kwa Yesu kwatoka kwa Yehova, yeye ni mng’ao wa Yehova, naye ni chapa halisi ya utu wenyewe wa Yehova; kumwona ni kumwona Yehova.—Yohana 12:45-50; 14:9; Waebrania 1:3.

17. Yesu alitoaje kielelezo juu ya ‘kusamehe sana’ kwa Yehova?

17 Jambo la kwamba Yehova husamehe sana laonyeshwa katika mojapo ya vielelezi vya Yesu, kile cha mfalme aliyesamehe deni ya talanta 10,000 (karibu dola 33,000,000, za Marekani). Lakini mtumwa huyo alipokataa kumsamehe mtumwa mwenzake deni ya dinari mia moja (dola zipatazo 60 za Marekani), mfalme huyo alighadhabika. “Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhabika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.” Kisha Yesu akaonyesha matumizi: “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.”—Mathayo 18:23-35.

18. Maoni ya Petro juu ya msamaha yatofautianaje na maoni ya Yesu?

18 Kabla tu Yesu atoe kielezi hicho, Petro alimjia Yesu na kumwuliza: “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? hata mara saba?” Petro alifikiri kuwa alifanya vizuri sana. Ingawa waandishi na Mafarisayo waliweka kiwango cha kusamehe, Yesu alimwambia Petro: “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.” (Mathayo 18:21, 22) Mara saba hata hazitoshi kwa siku moja, kama asemavyo Yesu: “Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.” (Luka 17:3, 4) Yehova anaposamehe, yeye hahesabu—jambo la kutufurahisha.

19. Ni lazima tufanye nini ili tusamehewe na Yehova?

19 Kama tuna unyenyekevu wa kutubu na kuungama dhambi zetu, Yehova hukubali kutupa kibali chake: “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”—1 Yohana 1:9.

20. Ni utayari gani wa kusamehe dhambi ulioonyeshwa na Stefano?

20 Mfuasi wa Yesu Stefano, akionyesha mtazamo wa ajabu wa kusamehe, alitoa ombi hili huku umati wenye ghadhabu ukimpiga kwa mawe: “Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala.”—Matendo 7:59, 60.

21. Kwa nini utayari wa Yesu wa kusamehe askari Waroma ulistaajabisha sana?

21 Yesu naye aliweka kielelezo cha ajabu hata zaidi ya kuwa tayari kusamehe. Maadui wake walikuwa wamemkamata, wakamjaribu kinyume cha sheria, wakamhukumu, wakamdhihaki, wakamtemea mate, wakamchapa kwa mjeledi wenye kamba nyingi ambazo zaelekea ziliwekewa vipande vya mifupa na vyuma, na hatimaye wakimwacha akiwa ametundikwa mtini kwa muda wa saa nyingi. Waroma walihusika katika mengi ya mambo hayo. Na bado, Yesu alipokuwa akifa katika mti huo wa mateso, akamwambia Baba yake wa mbinguni kuhusu askari waliokuwa wamemtundika: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.”—Luka 23:34.

22. Ni lazima tujaribu kutumia maneno yapi katika Mahubiri ya Mlimani?

22 Katika Mahubiri yake ya Mlimani, Yesu alikuwa amesema: “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi.” Kufikia mwisho wa huduma yake ya duniani, alitii kanuni hiyo yeye mwenyewe. Je, hilo ni takwa gumu sana kwetu, sisi tunaoshindana na udhaifu mbalimbali wa mwili wetu wenye dhambi? Angalau twapaswa kujaribu kutumia maneno ambayo Yesu alifundisha wafuasi wake baada ya kuwapa sala ya kiolezo: “Mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi makosa yenu. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.” (Mathayo 5:44; 6:14, 15) Tukiwa wenye kusamehe kama anavyosamehe Yehova, tutasamehe na kusahau.

Je, Wakumbuka?

◻ Yehova hushughulikaje na dhambi zetu, na kwa nini?

◻ Kwa nini Manase alirudishwa kwenye ufalme wake?

◻ Ni pande gani iliyo tofauti ya msamaha wa Yehova iliyo ngumu sana kwetu wanadamu kuiga?

◻ Utayari wa Yesu wa kusamehe ulistaajabishaje sana?

[Picha katika ukurasa wa 24]

Nathani alimsaidia Daudi aone uhitaji wa msamaha wa Mungu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki