Lazima Tuote Ndoto
JE, WEWE huota ndoto? Ni sawa kabisa kudhani kwamba wewe huota ndoto, kwa kuwa sisi sote huota ndoto tunapokuwa usingizini, hata ingawa huenda tukadai kwamba hatuoti ndoto. Imekadiriwa kwamba zaidi ya asilimia 95 ya ndoto zote haikumbukwi. Ni zipi unazokumbuka? Kwa kweli, zile tunazokumbuka kwa kawaida ni zile ambazo tumetoka tu kuota kabla ya kuamka.
Wachunguzaji wa ndoto wamegundua kwamba usingizi ni utaratibu wa hatua kwa hatua ulio mzito zaidi katika saa chache za kwanza kisha huzidi kuwa mwepesi baadaye. Kuota ndoto hutokea hasa wakati wa vipindi vya msogeo wa haraka wa jicho, uitwao usingizi wa REM (Rapid Eye Movement). Kipindi hicho hubadilishana na kipindi cha usingizi usio wa REM. Kila duru ya usingizi usio wa REM na usingizi wa REM hudumu muda wa dakika 90 hivi, na duru hizo hurudiwa mara tano au sita wakati wa usiku, duru ya mwisho ikitukia kabla tu ya sisi kuamka.
Ni kosa kufikiri kwamba ubongo wako uko kwenye kiwango cha chini cha utendaji wakati wa usingizi. Imegunduliwa kwamba ubongo ni wenye kutenda zaidi katika ndoto kuliko ulivyo katika hali fulani za kuwa macho, isipokuwa tu kwa habari ya nyuroni fulani katika shina la ubongo, zinazohusiana na umakini na kumbukumbu. Hizo zaonekana kupumzika wakati wa usingizi wa REM. Lakini kwa ujumla seli za neva katika ubongo huwa na uwasiliano wenye kuendelea wa kati ya seli.
Ubongo wetu ni sehemu ya mwili iliyo tata kwa njia ya ajabu ukiwa na mabilioni ya elementi zinazotokeza ishara kwa mwendo wa karibu mia moja hadi mia mbili au tatu kwa sekunde. Kuna elementi nyingi zaidi katika ubongo mmoja wa binadamu kuliko idadi ya watu duniani. Watafiti fulani hukadiria kwamba huo una elementi bilioni 20 hadi zaidi ya bilioni 50. Utata wao huhakikisha yale aliyosema mwandikaji wa Biblia Daudi kuhusu mwili wa kibinadamu: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu.”—Zaburi 139:14.
Ulimwengu wa Ndoto
Tunapokuwa macho, hisi zetu tano zinawasilisha daima habari na taswira kwa ubongo, lakini haiwi hivyo wakati wa usingizi. Ubongo hutokeza taswira ndani yao wenyewe bila msaada wowote wa hisi za nje. Kwa hiyo, nyakati nyingine yale tunayoona katika ndoto na mambo tunayopatwa nayo katika hizo ni kama maono ya uwongo. Hilo hutuwezesha kufanya mambo yanayopingana na sheria za asili, kama kuanguka kutoka kwenye genge bila kujeruhiwa. Huenda wakati ukapotoshwa hivi kwamba wakati uliopita unaonwa kana kwamba ni wakati uliopo. Au ikiwa tunajaribu kukimbilia mbali, yaonekana hatuwezi kudhibiti mwendo wetu—miguu yetu inakataa kwenda. Bila shaka, mambo na matukio yenye kuathiri sana ambayo huenda tukayaona tunapokuwa macho, yaweza kuathiri ndoto zetu. Watu wengi ambao wamejionea ukatili mbalimbali wenye kuhofisha wa vita hawawezi kuusahau kwa urahisi, wala watu fulani hawawezi kusahau hisia ya kushambuliwa na mhalifu. Mambo hayo yenye kusumbua yaliyoonwa tukiwa macho yaweza kutokea katika ndoto zetu, yakisababisha majinamizi. Mambo ya kawaida tunayofikiria tunapoenda kulala yaweza kutokea katika ndoto zetu.
Nyakati nyingine tunapojaribu kusuluhisha tatizo fulani, tunalipata suluhisho tunapokuwa usingizini. Hilo huenda likaonyesha kwamba si usingizi wote unaotia ndani kuota. Sehemu yao ni kufikiri.
Kitabu fulani juu ya ndoto na ubongo wetu hutaarifu hivi: “Namna ya kawaida zaidi ya utendaji wa akilini katika usingizi si kuota ndoto bali ni kufikiri. Fikira za wakati wa usingizi haziandamani na maono ya kihisia ya uwongo na zisizowazika. Zinaelekea kuwa za kawaida, mara nyingi zikihusu matukio ya maisha halisi ya jana au ya kesho, na kwa kawaida huwa duni, bila ubunifu, na za kurudia-rudia.”
Watu fulani huhisi kwamba habari za ndoto zao zina ujumbe wa pekee kwa ajili yao. Ili ndoto zifafanuliwe, wao huweka kitabu cha kuandikia karibu na kitanda chao ili waweze kuzirekodi wanapoamka. Kuhusiana na faida ya vitabu vinavyojaribu kutoa maana ya mifano ya ndoto, The Dream Game, kilichoandikwa na Ann Faraday, chasema: “Vitabu vya ndoto ambavyo katika hivyo unachunguza maana ya vichwa na mifano ya ndoto havina faida vilevile, viwe ni vya kimapokeo au vinategemea nadharia fulani ya kisaikolojia ya kisasa.”
Kwa kuwa yaonekana kwamba ndoto hutokea katika ubongo hasa, haifai kufikiri kwamba zina ujumbe mbalimbali wa pekee kwa ajili yetu. Twapaswa kuziona kuwa utendaji wa kawaida wa ubongo unaosaidia kuudumisha ukiwa wenye afya.
Lakini namna gani wale wasemao kwamba walikuwa wameota ndoto juu ya kifo cha mtu fulani wa ukoo au cha rafiki kisha wakapata kujua siku ifuatayo kwamba huyo mtu alikuwa amekufa? Je, hilo halionyeshi kwamba ndoto zaweza kutabiri wakati ujao? Katika makala ifuatayo, tutazungumzia ni jambo gani linalosababisha ndoto za kiunabii.