Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w97 6/15 kur. 14-19
  • “Mwanamume na Mwanamke Aliwaumba”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Mwanamume na Mwanamke Aliwaumba”
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ukiume wa Kweli na Ukike wa Kweli
  • Sura ya Nje
  • Wanaume na Wanawake Wakristo —Wanaume na Wanawake Halisi
  • Je, Wanawake Wanapaswa Kuficha Urembo Wao?
    Amkeni!—2005
  • Cheo cha Mwanamke Kinachoheshimiwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Daraka la Mwanamke Katika Maandiko
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Wanawake
    Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
w97 6/15 kur. 14-19

“Mwanamume na Mwanamke Aliwaumba”

“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.”—MWANZO 1:27.

1. Kweli ni baraka jinsi gani kwa wanaume na wanawake Wakristo?

INAFURAHISHA kama nini kuwa miongoni mwa watu wa Yehova na kushirikiana pamoja na wanaume na wanawake, na vilevile wavulana na wasichana, ambao jambo wanalotanguliza maishani mwao ni kumpenda na kumtii Mungu! Kweli hutuweka huru pia na mitazamo na mwenendo usiompendeza Yehova Mungu, nayo hutufundisha kuishi itupasavyo tukiwa Wakristo. (Yohana 8:32; Wakolosai 3:8-10) Kwa kielelezo, watu kila mahali wana mapokeo au dhana kuhusu namna ambavyo wanaume wanapaswa kudhihirisha ukiume wao, na wanawake ukike wao. Je, ni kwamba tu wanaume huzaliwa wakiwa na sifa ya kiume, na wanawake wakiwa na sifa ya kike? Au kuna mambo mengine ambayo ni lazima yafikiriwe?

2. (a) Ni nini kinachopaswa kuamua maoni yetu juu ya ukiume na ukike? (b) Maoni juu ya jinsia yamepatwa na nini?

2 Kwa Wakristo, Neno la Mungu, ndilo mamlaka tunayojinyenyekeza kwayo, bila kujali maoni ya kibinafsi, ya kitamaduni, au ya kimapokeo ambayo huenda tukawa tumepata. (Mathayo 15:1-9) Biblia haielezi kwa kina juu ya sehemu zote za ukiume na ukike. Badala ya hivyo, hiyo huacha nafasi ya kudhihirisha ukiume na ukike katika njia za unamna-namna, kama tunavyoona katika tamaduni tofauti. Ili kuwa vile ambavyo Mungu aliwaumba wawe, ni lazima wanaume wawe na sifa za kiume, na wanawake wawe na sifa za kike. Kwa nini? Kwa sababu zaidi ya mwanamume na mwanamke kuumbwa wakamilishane kimwili, walipaswa kukamilishana kupitia sifa za kiume na za kike. (Mwanzo 2:18, 23, 24; Mathayo 19:4, 5) Hata hivyo, maoni kuhusu jinsia yamepindwa na kupotoshwa. Watu wengi huhusianisha ukiume na utawala usio na huruma, ukatili, au kiburi cha kiume. Katika tamaduni fulani ingekuwa nadra au jambo la aibu kwa mwanamume kulia, hadharani au faraghani. Hata hivyo, akiwa kati ya umati nje ya kaburi la Lazaro, ‘Yesu alitokwa na machozi.’ (Yohana 11:35) Hilo halikuwa jambo lisilofaa kwa Yesu, ambaye ukiume wake ulikuwa mkamilifu. Wengi leo wamekosa usawaziko juu ya ukike, wakiuona kuwa uvutio wa kimwili na wa kingono tu.

Ukiume wa Kweli na Ukike wa Kweli

3. Wanaume na wanawake wanatofautianaje?

3 Ukiume wa kweli ni nini, nao ni nini ulio ukike wa kweli? Kichapo The World Book Encyclopedia hutaarifu hivi: “Wanaume na wanawake wengi hutofautiana si katika mfanyizo tu, bali katika mwenendo na mapendezi vilevile. Baadhi ya tofauti hizi huamuliwa na mfanyizo wetu wa tabia za urithi. . . . Lakini tofauti nyingi zisizo za mfanyizo wa kimwili yaonekana zategemea namna ya mwenendo wa kijinsia ambayo kila mtu hujifunza. Watu huzaliwa wakiwa wanaume au wanawake, lakini hujifunza kuwa na sifa za kiume au za kike.” Huenda mfanyizo wetu wa tabia za urithi ukasababisha mambo mengi, lakini ukuzi wa ukiume au ukike ufaao hutegemea kujifunza kwetu kile ambacho Mungu anataka tufanye na kile ambacho tunachagua kufuatia maishani.

4. Biblia hufunua nini juu ya madaraka ya mwanamume na mwanamke?

4 Historia ya Biblia hufunua kwamba daraka la Adamu lilikuwa kuongoza akiwa kichwa cha mke na watoto wake. Yeye pia alipaswa kujipatanisha na mapenzi ya Mungu ya kuijaza dunia, kuitiisha, na kutiisha uumbaji wa hali ya chini wa kidunia. (Mwanzo 1:28) Daraka la kike la Hawa lilipasa kuwa “msaidiaji” na “kikamilisho” cha Adamu, akinyenyekea ukichwa wake, akishirikiana naye katika kutimiza kusudi la Mungu walilotangaziwa.—Mwanzo 2:18; 1 Wakorintho 11:3.

5. Uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke uliharibiwaje?

5 Lakini Adamu hakuishi kupatana na daraka lake, naye Hawa alitumia ukike wake katika njia ya ubembelezi ili kumtongoza Adamu ajiunge naye katika kutomtii Mungu. (Mwanzo 3:6) Kwa kujiruhusu kufanya lile alilojua kuwa lilikuwa kosa, Adamu alikosa kudhihirisha ukiume wa kweli. Yeye alichagua kwa udhaifu kukubali neno la mwenzi wake aliyedanganywa badala ya lile ambalo Baba na Muumba wake alikuwa amesema. (Mwanzo 2:16, 17) Punde si punde wenzi hao wa kwanza wakaanza kujionea lile ambalo Mungu alikuwa ameona kimbele kuwa lingekuwa tokeo la kutotii. Adamu, ambaye hapo mwanzoni alikuwa amemfafanua mke wake kwa maneno yenye uchangamfu, ya kishairi, sasa kwa ubaridi alimrejezea mke wake kuwa ‘huyo mwanamke uliyenipa.’ Sasa kutokamilika kwake kuliharibu na kulielekeza vibaya ukiume wake, hilo likimfanya ‘amtawale mke wake.’ Hawa naye angekuwa na “tamaa” kwa mume wake, yaelekea katika njia ya kupita kiasi au isiyosawazika.—Mwanzo 3:12, 16.

6, 7. (a) Ni kupotolewa kupi kwa ukiume kulikositawi kabla ya Furiko? (b) Twaweza kujifunza nini kutokana na hali ya kabla ya Furiko?

6 Utumizi mbaya wa ukiume na ukike ukawa dhahiri sana kabla ya Furiko. Malaika walioacha vyeo vyao vya awali mbinguni walivaa miili ya kibinadamu ili wafurahie mahusiano ya kingono na wanawake. (Mwanzo 6:1, 2) Rekodi yataja kuwa wenzi hao wasio wa kiasili walizaa wanaume tu. Na yaonekana kwamba wazao hao walikuwa mivyauso, wasioweza kuzaana. Walikuja kujulikana kuwa wenye uweza, Wanefili, au Waangushaji, kwa kuwa wangesababisha watu wengine waanguke. (Mwanzo 6:4; NW, kielezi-chini) Kwa wazi walikuwa wenye jeuri, wakali, wasioonyesha huruma nyororo kwa wengine.

7 Kwa wazi urembo wa kimwili, umbo la mwili, ukubwa, au nguvu pekee hazitoi ukiume au ukike unaokubalika. Malaika waliovaa miili ya kibinadamu yamkini walikuwa wenye sura nzuri. Nao Wanefili walikuwa wakubwa na wenye misuli, lakini mtazamo wao wa kiakili ulikuwa umepotoka. Malaika hao wasiotii pamoja na wazao wao waliijaza dunia na ukosefu wa adili katika ngono na jeuri. Kwa sababu hiyo, Yehova aliumaliza ulimwengu huo. (Mwanzo 6:5-7) Ingawa hivyo, Furiko hilo halikumaliza uvutano wa roho waovu, wala halikufuta matokeo ya dhambi ya Adamu. Kupotoshwa kwa ukiume na ukike kulitokea tena baada ya Gharika, na kuna vielelezo katika Biblia, vyema na vibaya vilevile, ambavyo twaweza kujifunza kutokana navyo.

8. Yosefu aliweka kielelezo kipi chema cha ukiume unaofaa?

8 Simulizi la Yosefu pamoja na mke wa Potifa hutoa tofauti kubwa kati ya ukiume ufaao ukikabili ukike wa kilimwengu. Mke wa Potifa akiwa ameshikwa na upendo wa kupumbazwa kumwelekea Yosefu mwenye sura nzuri, alijaribu kumshawishi. Wakati huo, hakukuwa na sheria ya kimungu iliyoandikwa yenye kukataza uasherati au uzinzi. Hata hivyo, Yosefu alimkimbia mwanamke huyo asiye na adili akajithibitisha kuwa mwanamume halisi wa Mungu, mwanamume aonyeshaye ukiume ambao ulikuwa na kibali cha Mungu.—Mwanzo 39:7-9, 12.

9, 10. (a) Malkia Vashti aliutumiaje vibaya ukike wake? (b) Esta alituwekea kielelezo kipi chema cha ukike?

9 Esta na Malkia Vashti huandaa tofauti yenye kutokeza kwa ajili ya wanawake. Kwa wazi Vashti alifikiri kwamba alikuwa mrembo sana hivi kwamba Mfalme Ahasuero angekubali sikuzote matakwa yake. Lakini urembo wake ulikuwa wa kijuujuu tu. Alikosa kiasi na ukike, kwa sababu alishindwa kuonyesha ujitiisho kwa mume wake aliyekuwa mfalme. Mfalme alimkataa, akamchagua kuwa malkia wake, mwanamke aliyekuwa na sifa ya kike kikweli ambaye, kwa hakika alimhofu Yehova.—Esta 1:10-12; 2:15-17.

10 Esta atumika akiwa kielelezo chema ajabu kwa wanawake Wakristo. Alikuwa “wa umbo mzuri na uso mwema,” na bado alidhihirisha mapambo ya “mtu wa siri wa moyoni katika vao lisilofisidika la roho ya utulivu na ya upole.” (Esta 2:7; 1 Petro 3:4) Yeye hakuona mapambo ya kujionyesha kuwa ndilo jambo kuu. Esta alionyesha busara na kujidhibiti akiwa mwenye kujitiisha kwa mume wake, Ahasuero, hata wakati ambapo uhai wake na wa watu wake ulipokuwa hatarini. Esta alinyamaza ilipokuwa jambo la hekima kufanya hivyo lakini akasema bila hofu ilipokuwa lazima na ulipokuwa wakati ufaao. (Esta 2:10; 7:3-6) Alikubali shauri kutoka kwa binamu yake aliyekomaa, Mordekai. (Esta 4:12-16) Alionyesha upendo na uaminifu-mshikamanifu kuwaelekea watu wake.

Sura ya Nje

11. Twapaswa kukumbuka nini kuhusu sura ya nje?

11 Ni nini ulio ufunguo wa ukike ufaao? Mama mmoja alisema hivi: “Urembo huenda ukawa wa bandia, na sura nzuri huenda ikawa ubatili; lakini mwanamke ambaye humhofu Yehova ndiye mmoja ambaye hupata sifa kwa ajili yake mwenyewe.” (Mithali 31:30, NW) Kwa hiyo hofu yenye staha kwa Mungu ni muhimu, na fadhili-upendo, upendezo, kiasi, na ulimi mpole huchangia zaidi sana ukike kuliko jinsi urembo unavyochangia.—Mithali 31:26.

12, 13. (a) Kwa kuhuzunisha, ni nini kinachotia alama usemi wa watu wengi? (b) Maana ya Mithali 11:22 ni nini?

12 Kwa kusikitisha, wanaume na wanawake wengi hawafumbui vinywa vyao kwa hekima, wala fadhili-upendo hazimo katika ndimi zao. Usemi wao ni wenye kuudhi, wenye kukejeli, mchafu, na usio na ufikirio. Wanaume fulani hufikiria kwamba lugha chafu ni alama ya ukiume, nao wanawake fulani huwaiga kipumbavu. Hata hivyo, ikiwa mwanamke ni mrembo lakini anakosa busara na ni mwenye kubishana, mwenye kukejeli, au mwenye kujigamba, je, aweza kikweli kuwa mrembo katika maana iliyo bora zaidi, mwenye sifa za kike kikweli? “Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, kadhalika mwanamke mzuri [“mrembo,” NW] asiye na akili [“busara,” NW].”—Mithali 11:22.

13 Urembo pamoja na usemi usio safi, kejeli, au ukosefu wa busara, haungepatana na sura ya kike ambayo huenda mtu akaionyesha. Kwa hakika, mwenendo huo usio wa kimungu ungeweza hata kufanya mtu mwenye kuvutia kimwili aonekane akiwa mwenye sura mbaya. Twaweza kutambua kwa urahisi kwamba sura ya kimwili ya mwanamume au mwanamke haiwezi yenyewe tu kulipia au kufanya mifoko ya hasira, kupiga kelele, au usemi wenye kuudhi ufae. Wakristo wote wanaweza na wanapaswa kujifanya wenyewe kuwa wenye kuvutia kwa Mungu na kwa wanadamu wenzao kwa usemi na mwenendo wao wenye kutegemea Biblia.—Waefeso 4:31.

14. Ni mapambo ya aina gani yanayosifiwa kwenye 1 Petro 3:3-5, nawe wahisije juu ya hilo?

14 Ingawa ukike na ukiume halali hutegemea sifa za kiroho, tabia na sura ya kimwili, kutia ndani mavazi tunayovaa na jinsi tunavyoyavaa, hutoa ujumbe kutuhusu sisi. Mtume Petro bila shaka alikuwa akiwaza juu ya mitindo fulani-fulani ya mavazi na mapambo katika karne ya kwanza aliposhauri wanawake Wakristo: “Msiache urembo wenu uwe ule wa kusuka nywele kwa nje na wa kuvalia madoido ya dhahabu au kuvalia mavazi ya nje, bali acheni uwe yule mtu wa siri wa moyoni katika vao lisilofisidika la roho ya utulivu na ya upole, ambayo ni ya thamani kubwa machoni pa Mungu. Kwa maana, pia, ndivyo wanawake watakatifu hapo zamani waliokuwa wakitumaini katika Mungu walivyokuwa na kawaida ya kujiremba, wakijitiisha wenyewe kwa waume zao wenyewe.”—1 Petro 3:3-5.

15. Wanawake Wakristo wapaswa kujitahidi kuonyesha nini katika mavazi yao?

15 Kwenye 1 Timotheo 2:9, 10, twapata maelezo ya Paulo kuhusu mavazi ya kike: “Natamani wanawake wajirembe wenyewe katika mavazi yenye mpangilio mzuri, pamoja na kiasi na utimamu wa akili . . . katika njia inayofaa wanawake wanaodai kumstahi Mungu, yaani, kupitia kazi zilizo njema.” Hapo alikazia uhitaji wa kuwa na kiasi na mavazi yenye mpangilio mzuri ambayo huonyesha utimamu wa akili.

16, 17. (a) Leo wanaume na wanawake wengi wametumiaje mavazi vibaya? (b) Twapaswa kufikia mkataa gani kutokana na shauri lipatikanalo kwenye Kumbukumbu la Torati 22:5?

16 Haileti heshima kwa Mungu hata kidogo ikiwa mwanamume au mwanamke, mvulana au msichana, angeenenda au kuvalia katika njia yenye kuchochea hisia za kingono wala hilo halingeboresha ukiume au ukike wa kweli. Watu wengi ulimwenguni hupita mipaka ili kuonyesha kwa kupita kiasi hali ya kingono ya kiume au ya kike katika mavazi au katika mwenendo. Wengine huficha tofauti kati ya jinsia hizo mbili kwa sababu ya malengo yasiyo ya adili. Sisi Wakristo twaweza kuwa wenye shukrani kama nini kwa sababu Biblia hufunua kufikiri kwa Mungu! Yehova alitangaza kwa Israeli la kale hivi: “Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA.”—Kumbukumbu la Torati 22:5.

17 Kwa habari hii, yamkini utafurahia kupitia kile ambacho Mnara wa Mlinzi la Agosti 15, 1988, lilisema kwenye ukurasa wa 17: “Suala si kama mtindo fulani ni wa kisasa kupita kiasi bali ni kama unafaa kwa mmoja anayedai kuwa mhudumu wa Mungu. (Warumi 12:2; 2 Wakorintho 6:3) Nguo za kivivi-hivi mno au zenye kubana zinaweza kuondoa fikira kwenye ujumbe wetu. Ni wazi kabisa kwamba mitindo inayofanya kwa utovu wa adabu na kwa makusudi ili wanaume waonekane kama wanawake au kufanya wanawake waonekane kama wanaume haifai. (Linganisha Kumbukumbu la Torati 22:5.) Bila shaka, huenda desturi za mahali zikatofautiana, kulingana na hali ya hewa, mahitaji ya kikazi, na kadhalika, hivi kwamba kundi la Kikristo halifanyi sheria ngumu-ngumu na zilizokazwa sana ili zihusu udugu mzima wa ulimwenguni pote.”

18. Twaweza kuchukua hatua gani katika kutumia shauri la Biblia juu ya mavazi na mapambo?

18 Ni shauri lenye usawaziko na linalofaa kama nini! Kwa kuhuzunisha, Wakristo fulani, wanaume na wanawake, hufuata kiupofu-upofu chochote kile ambacho ulimwengu hutokeza katika mavazi na mapambo bila kufikiria ile picha ambayo hilo laweza kuonyesha kuhusu Yehova na kutaniko la Kikristo. Kila mmoja wetu aweza kujichunguza na kuona ikiwa amepatwa na uvutano wa kuwaza kilimwengu. Au twaweza kumfikia ndugu au dada mwenye kuheshimika na mwenye uzoefu na kumwuliza maoni juu ya marekebisho ambayo tungeweza kufanya katika mtindo wetu wa mavazi kisha tuyafikirie madokezo hayo kwa uzito.

Wanaume na Wanawake Wakristo —Wanaume na Wanawake Halisi

19. Twahitaji kupigana na uvutano gani usiopendeza?

19 Mungu wa ulimwengu huu ni Shetani, na uvutano wake waweza kuonwa katika utatanishi kuhusu jinsia, na waonekana katika mambo mengine zaidi ya mavazi. (2 Wakorintho 4:4) Katika nchi fulani wanawake wengi hushindana na wanaume juu ya ukichwa, wakipuuza kanuni za Biblia. Kwa upande ule mwingine, idadi kubwa ya wanaume huacha tu madaraka yao ya ukichwa, kama alivyofanya Adamu. Kuna wale ambao hata hujaribu kubadili madaraka yao ya kijinsia maishani kwa kugeuka kuwa wagoni-jinsia-moja na kuwa misago. (Waroma 1:26, 27) Biblia haiweki mitindo-maisha yoyote ya badala inayokubaliwa na Mungu. Na wowote ambao, kabla ya kuwa Wakristo, walichanganyikiwa juu ya madaraka yao tofauti wakiwa wanaume au wanawake au juu ya mapendezi yao ya kingono wanaweza kuwa na uhakika kwamba itakuwa kwa faida yao idumuyo milele kuishi kulingana na kiwango cha Mungu, kiwango ambacho bila shaka kitathaminiwa na wote wanaofikia ukamilifu wa kibinadamu.

20. Andiko la Wagalatia 5:22, 23 lapaswa kuwa na matokeo gani juu ya maoni yetu kuhusu ukiume na ukike?

20 Maandiko yaonyesha kwamba wanaume na wanawake Wakristo wanahitaji kukuza na kudhihirisha tunda la roho ya Mungu—upendo, shangwe, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani, upole, na kujidhibiti. (Wagalatia 5:22, 23) Katika hekima yake kubwa, Mungu aliwawezesha wanaume kuboresha ukiume wao, na wanawake kuboresha ukike wao, kwa kukuza sifa hizo. Ni rahisi kumstahi mwanamume anayeonyesha tunda la roho, na ni rahisi kumpenda mwanamke anayefanya hivyo.

21, 22. (a) Yesu aliweka kiolezo kipi kwa habari ya mitindo-maisha? (b) Yesu alidhihirishaje ukiume wake?

21 Yule mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi alikuwa Yesu Kristo, na Wakristo wanapaswa kuiga mtindo-maisha wake. (1 Petro 2:21-23) Kama alivyofanya Yesu, wanaume na wanawake vilevile wapaswa kuthibitika kuwa waaminifu-washikamanifu kwa Mungu na watiifu kwa Neno Lake. Yesu alidhihirisha sifa nzuri ajabu za upendo, wororo, na rehema. Tukiwa Wakristo wa kweli, twatarajiwa kumwiga ili kuthibitisha kwamba sisi ni wanafunzi wake.—Yohana 13:35.

22 Yesu Kristo alikuwa mwanamume halisi, na twaweza kuona sifa zake za kiume tujifunzapo rekodi yake ya maisha inayoonyeshwa katika Maandiko. Yeye hakuoa kamwe, lakini Biblia huonyesha kwamba alifurahia ushirika wenye usawaziko pamoja na wanawake. (Luka 10:38, 39) Mahusiano yake pamoja na wanaume na wanawake sikuzote yalikuwa safi kiadili na yenye kuheshimika. Yeye ndiye kigezo kikamilifu cha ukiume. Hakuruhusu mtu yeyote—mwanamume, mwanamke, au malaika aliyekosa kutii—ampokonye ukiume wake wa kimungu na uaminifu wake kwa Yehova. Yeye hakusita kukubali madaraka yake, naye alifanya hivyo bila kulalamika.—Mathayo 26:39.

23. Kwa habari ya madaraka ya jinsia tofauti, Wakristo wa kweli wanabarikiwaje kwa njia tofauti-tofauti?

23 Ni jambo lenye kufurahisha kama nini kuwa miongoni mwa watu wa Yehova na kushirikiana pamoja na wanaume na wanawake, na vilevile wavulana na wasichana, ambao jambo wanalotanguliza maishani mwao ni kumpenda na kumtii Yehova Mungu! Hatufungwi kwa kutii Neno la Mungu. Badala ya hivyo, tunawekwa huru na ulimwengu huu na njia zao ambazo hupotosha urembo, kusudi, na madaraka tofauti yanayotimizwa na jinsia mbalimbali. Twaweza kupata furaha ya kweli inayokuja kutokana na kutimiza daraka letu tulilopewa na Mungu maishani, tuwe wanaume au wanawake. Ndiyo, tuna shukrani kama nini kwa Yehova Mungu, Muumba, kwa maandalizi yake yote yenye upendo kwa ajili yetu na kwa kutuumba tukiwa wanaume na wanawake!

Ungejibuje?

◻ Biblia hufafanua madaraka gani yanayowafaa wanaume na wanawake?

◻ Ukiume ulipotoshwaje kabla ya Furiko, na mtazamo kuuelekea na kuelekea ukike umepotoshwaje katika wakati wetu?

◻ Wewe utajaribu kutumia shauri gani la Biblia juu ya sura?

◻ Wanaume na wanawake Wakristo wanaweza kujithibitishaje kuwa wanaume na wanawake halisi?

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ingawa alikuwa mrembo, Esta hukumbukwa hasa kwa sababu ya kiasi chake na roho yake ya utulivu na ya upole

[Picha katika ukurasa wa 18]

Elekeza uangalifu ufaao kwenye mapambo huku ukikazia zaidi uzuri wa ndani

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki