Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 2/1 kur. 3-5
  • Matokeo ya Kiburi—Ni Makubwa Kadiri Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Matokeo ya Kiburi—Ni Makubwa Kadiri Gani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Somo Katika Unyenyekevu
  • Matokeo ya Majivuno
  • Usiache Kiburi Kikuharibu
  • Kujistahi Dhidi ya Majivuno
  • Yafaa Kuzuia Kiburi Chako
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Je, Ni Vibaya Kuwa na Kiburi?
    Amkeni!—1999
  • Je, Unyenyekevu Ni Udhaifu au Ni Sifa Nzuri?
    Amkeni!—2007
  • Unaweza Kumshinda Shetani!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 2/1 kur. 3-5

Matokeo ya Kiburi—Ni Makubwa Kadiri Gani?

JE, UMEPATA kushughulika na mtu aliyejaribu kimakusudi kukufanya uhisi kuwa mtu asiye wa maana? Labda meneja, msimamizi, mwangalizi, au hata mtu wa jamaa aliyekuona kuwa duni na kukudharau kabisa? Ulihisije kuhusu mtu huyo? Je, ulivutiwa na utu wake? Hata kidogo! Kwa nini? Kwa sababu kiburi huleta vizuizi na hukomesha mawasiliano.

Kiburi humfanya mtu adharau kila mtu, ili yeye sikuzote aonekane kuwa bora zaidi. Mtu aliye na mtazamo kama huo, mara nyingi hasemi neno zuri kuhusu wengine. Sikuzote huwa kuna maneno ya kumalizia yasiyojenga—“ndiyo, huenda hilo likawa kweli, lakini ana tatizo hili au kasoro ile.”

Katika kitabu Thoughts of Gold in Words of Silver, kiburi chafafanuliwa kuwa “uovu wenye kushinda sikuzote. Humharibu mtu, kikimwacha bila kutamanika.” Je, ni ajabu kwamba hakuna mtu ambaye huhisi amestareheka akiwa na mtu mwenye kiburi? Kwa kweli, matokeo ya kiburi mara nyingi ni kukosa marafiki wa kweli. “Kinyume cha hilo,” kitabu hichohicho chaendelea kusema, “ulimwengu hupenda wanyenyekevu—si wanyenyekevu ambao wana fahari ya kuwa hivyo, bali wanyenyekevu kikweli.” Kwa kufaa, Biblia husema: “Kiburi cha mtu humletea aibu, yeye ajinyenyekezaye atapata heshima.”—Mithali 29:23, The Jerusalem Bible.

Hata hivyo, zaidi ya urafiki au heshima kutoka kwa watu, kiburi huathirije uhusiano wa mtu pamoja na Mungu? Mungu humwonaje mtu mwenye kiburi, mwenye majivuno, na mwenye kujiamini mno? Kiburi au unyenyekevu—kwani zina umuhimu kwake?

Somo Katika Unyenyekevu

Mwandikaji aliyepuliziwa wa Mithali aandika hivi: “Kiburi hutangulia uangamivu; na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi.” (Mithali 16:18, 19) Hekima ya maneno hayo yahakikishwa katika kisa cha jenerali Msiria Naamani, aliyeishi nyakati za nabii Mwisraeli Elisha.

Naamani alikuwa na ukoma. Katika kutafuta kwake ponyo, alisafiri hadi Samaria akifikiri kwamba angekuwa na mazungumzo rasmi pamoja na Elisha. Badala yake, nabii huyo alimtuma mtumishi wake akiwa na maagizo kwamba Naamani aoge mara saba katika Mto Yordani. Naamani alihisi amedharauliwa kuhusu alivyotendewa na alivyoshauriwa. Kwa nini nabii hangeweza kuja na kusema naye kibinafsi badala ya kumtuma mtumishi? Na kwa kweli, mto wowote wa Siria ulikuwa sawa tu na Yordani! Kiburi ndicho kilichokuwa tatizo lake. Matokeo? Kwa furaha, shauri lenye hekima lilishinda. “Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.”—2 Wafalme 5:14.

Nyakati nyingine mtu hunufaika sana kutokana na kunyenyekea kidogo tu.

Matokeo ya Majivuno

Hata hivyo, matokeo ambayo kiburi hutulazimisha kupata, yaweza kuwa makubwa zaidi kuliko kukosa tu manufaa au faida. Kuna kiwango kingine cha kiburi ambacho chadokezwa katika neno “kujiona,” (hubris) ambalo lafafanuliwa kuwa “kiburi kingi mno au kujitumaini mno ambako mara nyingi hutokeza adhabu.” (Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary) Neno hilo latokana na Kigiriki, na kulingana na msomi Mgiriki William Barclay, “neno hubris [kujiona] limechangamana na kiburi na ukatili . . . , madharau ya majivuno ambayo humfanya [mwanadamu] akanyage-kanyage mioyo ya wanadamu wenzake.”

Kielelezo kilicho wazi cha kiburi kingi mno jinsi hii hupatikana katika Biblia. Nacho ni kile kisa cha Hanuni, mfalme wa Ammoni. Kichapo Insight on the Scriptures hueleza hivi: “Kwa sababu ya fadhili yenye upendo ambayo Nahasi alimwonyesha, Daudi alituma wajumbe wamfariji Hanuni kwa kumpoteza baba yake katika kifo. Lakini Hanuni, akisadikishwa na wakuu wake kwamba hiyo ilikuwa hila ya Daudi ya kupeleleza jiji hilo, aliwafedhehesha watumishi wa Daudi kwa kuwanyoa nusu ya ndevu zao na kukata mavazi yao katikati hata matakoni, kisha akawatoa waende zao.”a Kuhusu kisa hiki, Barclay asema hivi: “Tendo hilo lilikuwa hubris. Lilikuwa matusi, ukatili, aibu ya peupe, yote hayo kwa ujumla.”—2 Samweli 10:1-5.

Naam, mtu mwenye kiburi anaweza kujiona, kuwa mfidhuli, mwenye kuwaaibisha wengine. Yeye hufurahia kumwumiza kwa njia yenye ubaridi, isiyo na hisia, kisha huchekelea hali mbaya na ya kufedhehesha ya yule mtu mwingine. Lakini kushusha au kuharibu staha ya mtu mwingine ni upanga ukatao kuwili. Husababisha kumpoteza rafiki na hata yaelekea sana, kumfanya awe adui.

Mkristo yeyote wa kweli awezaje kuonyesha kiburi hicho chenye kuumiza, kwa kuwa Bwana-Mkubwa wake aliamuru kwamba ‘ampende jirani yake kama yeye mwenyewe’? (Mathayo 7:12; 22:39) Ni kinyume kabisa na vile Mungu na Kristo walivyo. Kwa sababu hiyo, Barclay atoa maoni haya yenye uzito: “Hubris ni kiburi ambacho humfanya mtu asimwogope Mungu.” Ni kiburi ambacho humfanya mtu aseme: “Hakuna Mungu [“Yehova,” NW].” (Zaburi 14:1) Au kama ilivyoelezwa kwenye Zaburi 10:4, Habari Njema kwa Watu Wote: “Mwovu, kwa majivuno yake, hamjali Mungu; fikira zake zote ni: ‘Hakuna Mungu.’” Kiburi hicho, humtenga mtu si na marafiki na watu wa jamaa tu bali pia na Mungu. Hayo ni matokeo makubwa kama nini!

Usiache Kiburi Kikuharibu

Kiburi chaweza kuwa na sehemu nyingi—kiburi ambacho hutokana na utukuzo wa taifa, ubaguzi wa jamii, tofauti ya tabaka na jamii, elimu, utajiri, sifa, na mamlaka. Kwa njia moja au nyingine, kiburi chaweza kukuingia kwa urahisi na kiharibu utu wako.

Watu wengi huonekana kuwa wanyenyekevu wanaposhughulika na wakuu wao au hata watu wa rika lao. Lakini ni nini hutokea wakati anayeonekana kuwa mtu mnyenyekevu apatapo cheo cha mamlaka? Kwa ghafula, yeye huwa dikteta ambaye hufanya maisha yawe yenye taabu kwa watu awaonao kuwa wa hali ya chini! Hilo laweza kutokea kwa watu fulani wanapovaa nguo rasmi au kuwa na beji inayoonyesha mamlaka. Hata wafanyakazi wa serikali wanaweza kuwa na kiburi wanaposhughulika na umma, wakifikiri kwamba umma wapaswa kuwatumikia, badala ya wao kuutumikia. Kiburi chaweza kukufanya uwe mkali, bila hisia; unyenyekevu waweza kukufanya uwe mwenye fadhili.

Yesu angeweza kuwa na kiburi na mkali alipokuwa na wanafunzi wake. Yeye alikuwa mwanamume mkamilifu, Mwana wa Mungu, aliyeshughulika na wafuasi wasio wakamilifu, wenye harara, wenye kutenda kwa msukumo. Lakini, yeye aliwapa mwaliko gani wale waliosikiliza? “Njoni kwangu, nyinyi nyote mnaomenyeka na kulemezwa mizigo, nami hakika nitawaburudisha nyinyi. Chukueni nira yangu juu yenu na mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mwenye tabia-pole na wa hali ya chini moyoni, nanyi mtapata burudisho kwa ajili ya nafsi zenu. Kwa maana nira yangu ni ya fadhili na mzigo wangu ni mwepesi.”—Mathayo 11:28-30.

Je, sisi hujitahidi sikuzote kufuata kielelezo cha Yesu? Au sisi hujipata tukiwa wakali, wagumu, madikteta, wasio na huruma, wenye kiburi? Kama Yesu, jaribu kuburudisha, si kukandamiza. Kinza matokeo yenye kuharibu ya kiburi.

Kuhusu yaliyotoka kutajwa, je, aina yote ya kiburi ni mbaya?

Kujistahi Dhidi ya Majivuno

Fahari ni “kujistahi kufaako au kwenye haki.” (Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary) Kujistahi humaanisha kujiheshimu wewe mwenyewe. Humaanisha kwamba unajali yale ambayo watu wengine hufikiri juu yako. Unajali sura yako na sifa yako. Methali hii ya Kihispania ni ya kweli, “Niambie ni nani ambao wewe hutembea nao nami nitakwambia jinsi ulivyo.” Ukipendelea kushirikiana na watu walio na mazoea ovyoovyo, wavivu, watovu wa adabu, na wenye maneno machafu, basi utakuwa kama wao. Mitazamo yao itakuambukiza, na kama wao, utakosa kujistahi.

Bila shaka, kuna kule kupita kiasi—kiburi ambacho huongoza kwenye majivuno na ubatili. Waandishi na Mafarisayo katika siku ya Yesu walijivunia mapokeo yao na kuonekana kwao kuwa watu wa kidini zaidi kupita wengine. Yesu alionya juu yao hivi: “Kazi zote wazifanyazo wao huzifanya ili watazamwe na watu; kwa maana wao hupanua vibweta vyenye maandiko ambavyo wao huvaa kama ulinzi, na kuongeza ukubwa wa pindo zenye matamvua za mavazi yao [waonekane kuwa wacha-Mungu]. Wao hupendezwa na mahali penye kutokeza zaidi sana kwenye milo ya jioni na viti vya mbele katika masinagogi, na salamu katika mahali pa masoko na kuitwa Rabi na watu.”—Mathayo 23:5-7.

Basi, fahari inayofaa ni mtazamo wenye usawaziko. Pia, kumbuka kwamba Yehova huona moyo si sura ya nje tu. (1 Samweli 16:7; Yeremia 17:10) Kujiona kuwa mwadilifu si uadilifu wa Mungu. Hata hivyo, swali ni, Twaweza kusitawishaje unyenyekevu wa kweli na kuepuka kupatwa na matokeo makubwa ya kiburi?

[Maelezo ya Chini]

a Kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Unyenyekevu kidogo ulimletea Naamani manufaa kubwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki