Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 3/15 kur. 3-9
  • Siku ya Mwisho ya Maisha ya Yesu ya Kibinadamu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Siku ya Mwisho ya Maisha ya Yesu ya Kibinadamu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Alhamisi Jioni, Nisani 14
  • Mwadhimisho wa Pekee
  • Katika Bustani ya Gethsemane
  • Ijumaa Asubuhi, Nisani 14
  • Kifo Chenye Maumivu Makali
  • Yu Hai Tena!
  • Jinsi Unavyoathiriwa
  • Kuzikumbuka Siku za Mwisho za Yesu Duniani
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Yesu Anauawa
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • “Saa Imekuja!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Kitabu Cha Biblia Namba 43—Yohana
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 3/15 kur. 3-9

Siku ya Mwisho ya Maisha ya Yesu ya Kibinadamu

Ni wakati wa jioni-jioni, Ijumaa, Nisani 14, 33 W.K. Kikundi cha wanaume na wanawake kiko karibu kuzika rafiki mpendwa. Mmoja wa wanaume hao, Nikodemo, ameleta manukato ili kuutayarisha mwili kwa ajili ya maziko. Mwanamume aitwaye Yosefu ametoa kitani safi ya kufungia maiti iliyochubuka kwa kupigwa.

WATU hawa ni nani, nao wanamzika nani? Je, haya yote yanakuathiri? Ili kujibu maswali hayo, acheni turudi nyuma hadi mwanzo wa siku hiyo muhimu.

Alhamisi Jioni, Nisani 14

Mwezi mpevu ulio mwangavu unachomoza polepole juu ya Yerusalemu. Jiji lenye watu wengi linatulia baada ya siku yenye shughuli nyingi. Jioni hii hewa imejaa harufu nzuri ya mwana-kondoo anayechomwa. Naam, maelfu ya watu wanajitayarisha kwa ajili ya tukio la pekee—mwadhimisho wa kila mwaka wa Sikukuu ya Kupitwa.

Katika chumba kikubwa cha wageni, twamkuta Yesu Kristo na mitume wake 12 kwenye meza iliyoandaliwa. Sikiliza! Yesu anazungumza. “Nimetamani sana kula hii sikukuu ya kupitwa pamoja nanyi kabla sijateseka,” yeye asema. (Luka 22:15) Yesu anajua kwamba adui zake wa kidini wanapanga kumuua. Lakini kabla hajauawa, jambo fulani la maana sana litatukia jioni hii.

Baada ya Sikukuu ya Kupitwa kuadhimishwa, Yesu anatangaza: “Mmoja wenu atanisaliti mimi.” (Mathayo 26:21) Jambo hilo linahuzunisha mitume. Huyo anaweza kuwa nani? Baada ya kuzungumza kidogo, Yesu anamwambia Yudasi Iskariote: “Lile unalofanya lifanye upesi zaidi.” (Yohana 13:27) Yudasi ni msaliti ingawa wale wengine hawatambui jambo hilo. Yeye anaondoka kutimiza fungu lake kwa woga katika njama dhidi ya Yesu.

Mwadhimisho wa Pekee

Yesu sasa aanzisha mwadhimisho ulio mpya kabisa—mmoja ambao utakuwa ukumbusho wa kifo chake. Akichukua mkate, Yesu atoa sala ya kushukuru kwa ajili ya huo mkate, kisha anaugawa. “Chukueni, kuleni,” yeye aagiza. “Huu wamaanisha mwili wangu ambao wapasa kutolewa kwa ajili yenu.” Wakati ambapo kila mmoja wao amekula mkate, yeye anachukua kikombe cha divai isiyokolezwa na kushukuru kwa ajili ya hicho. “Nyweni kutoka hicho, nyinyi nyote,” Yesu anawaambia na kueleza hivi: “Kikombe hiki chamaanisha agano jipya kwa msingi wa damu yangu, ambayo yapasa kumwagwa kwa ajili yenu.” Yeye anawaagiza mitume waaminifu 11 wanaobaki hivi: “Fulizeni kufanya hili katika ukumbuko wangu.”—Mathayo 26:26-28; Luka 22:19, 20; 1 Wakorintho 11:24, 25.

Jioni hiyo, Yesu anawatayarisha kwa fadhili mitume wake waaminifu-washikamanifu kwa yale yaliyoko mbele yao na anawathibitishia upendo wake wenye kina kirefu. “Hakuna aliye na upendo mkubwa zaidi kuliko huu,” yeye aeleza, “kwamba mtu fulani aisalimishe nafsi yake kwa niaba ya marafiki wake. Nyinyi ni marafiki wangu ikiwa mwafanya lile ninalowaamuru nyinyi.” (Yohana 15:13-15) Naam, hao mitume 11 wamethibitisha kwamba wao ni marafiki wa kweli kwa kushikamana na Yesu wakati wa majaribu yake.

Usiku—labda baada ya saa sita usiku—Yesu anatoa sala ya kukumbukwa, halafu wanaimba nyimbo za kumsifu Yehova. Kisha, kwa kuangaziwa na mwezi mpevu, wanaondoka jijini na kuvuka Bonde la Kidroni.—Yohana 17:1–18:1.

Katika Bustani ya Gethsemane

Muda mfupi baadaye, Yesu na mitume wake wanawasili kwenye bustani ya Gethsemane. Akiwaacha mitume wanane kwenye kiingilio cha bustani hiyo, Yesu awapeleka Petro, Yakobo, na Yohana ndani zaidi katikati ya mizeituni. “Nafsi yangu ina kihoro sana, hata kufikia kifo,” awaambia hao watatu. “Kaeni hapa na kufuliza kulinda.”—Marko 14:33, 34.

Hao mitume watatu wanangoja huku Yesu akiingia ndani zaidi katika bustani ili kusali. Kwa vilio vyenye kupaazwa kwa nguvu na machozi, yeye aomba kwa bidii: “Baba, ikiwa wataka, ondoa kikombe hiki kutoka kwangu.” Yesu ana daraka kubwa mno. Ni jambo lenye kumhuzunisha kama nini kufikiria yale ambayo maadui wa Yehova watasema wakati Mwana Wake mzaliwa-pekee anapotundikwa mtini kana kwamba yeye ni mhalifu! Kule kufikiria aibu ambayo Baba yake wa kimbingu atapata ikiwa yeye atashindwa na jaribu hili kali ni jambo jingine linalomuumiza sana Yesu. Yesu asali kwa bidii sana na apatwa na maumivu makali kiasi cha kwamba jasho lake lawa kama matone ya damu yanayoanguka ardhini.—Luka 22:42, 44.

Yesu amemaliza tu kusali mara ya tatu. Watu wanaobeba mienge na taa wanakaribia. Yule anayewaongoza si mwingine ila Yudasi Iskariote, ambaye aenda moja kwa moja hadi alipo Yesu. “Siku njema, Rabi!” yeye asema, akimbusu Yesu kwa wororo. “Yudasi,” Yesu aitikia, “je, wewe wamsaliti Mwana wa binadamu kwa busu?”—Mathayo 26:49; Luka 22:47, 48; Yohana 18:3.

Papo hapo, mitume wanang’amua kinachoendelea. Bwana wao na rafiki yao mpendwa yuko karibu kukamatwa! Kwa hiyo, Petro achomoa upanga na kukata sikio la mtumwa wa kuhani wa cheo cha juu. “Achieni hapa,” Yesu asema haraka kwa sauti kubwa. Akijitokeza mbele, Yesu anamponya mtumwa huyo na kumwamuru Petro: “Rudisha upanga wako mahali pao, kwa maana wale wote wauchukuao upanga wataangamia kwa upanga.” (Luka 22:50, 51; Mathayo 26:52) Maofisa na askari-jeshi wanamkamata Yesu na kumfunga. Wakiwa wamepatwa na hofu na wasiwasi, mitume wanamwacha Yesu kisha wanakimbia na kutoweka gizani.—Mathayo 26:56; Yohana 18:12.

Ijumaa Asubuhi, Nisani 14

Sasa ni Ijumaa alfajiri, saa sita ya usiku ikiwa imepita. Yesu anapelekwa kwanza nyumbani kwa aliyekuwa Kuhani wa Cheo cha Juu, Anasi, ambaye angali na uvutano na uwezo mkubwa. Anasi anamhoji Yesu, kisha anaagiza apelekwe nyumbani kwa Kuhani wa Cheo cha Juu, Kayafa, ambako Sanhedrini imekusanyika.

Viongozi wa kidini sasa wanajaribu kutafuta mashahidi ili kutunga kesi ya uwongo dhidi ya Yesu. Hata hivyo, hata hao mashahidi wa uwongo wanashindwa kuafikiana katika ushuhuda wao. Muda huo wote, Yesu anaendelea kukaa kimya. Akibadilisha mbinu, Kayafa adai: “Kwa Mungu aliye hai nakuweka chini ya kiapo utuambie kama wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu!” Hilo ni jambo hakika ambalo haliwezi kukanushwa, kwa hiyo Yesu anajibu kwa ujasiri hivi: “Mimi ndiye; na nyinyi watu mtamwona Mwana wa binadamu ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu akija pamoja na mawingu ya mbinguni.”—Mathayo 26:63; Marko 14:60-62.

“Amekufuru!” Kayafa asema kwa sauti kubwa. “Ni uhitaji gani zaidi tulio nao wa mashahidi?” Sasa wengine wanampiga Yesu makofi usoni na kumtemea mate. Wengine wanampiga kwa ngumi zao na kumtusi. (Mathayo 26:65-68; Marko 14:63-65) Ijumaa, mara tu baada ya mapambazuko, Sanhedrini inakutana tena, labda kuipa uhalali wa namna fulani kesi isiyokuwa halali ambayo walifanya usiku. Kwa ujasiri, Yesu anaonyesha tena kwamba yeye ni Kristo, Mwana wa Mungu.—Luka 22:66-71.

Halafu, makuhani wakuu na wazee wanamburuta Yesu kumpeleka kufanyiwa kesi na Pontio Pilato, gavana Mroma wa Yudea. Wanamshtaki Yesu kwamba anapindua taifa, anakataza watu kulipa kodi kwa Kaisari, na “[ana]sema yeye mwenyewe ni Kristo mfalme.” (Luka 23:2; linganisha Marko 12:17.) Baada ya kumhoji Yesu, Pilato anatangaza hivi: “Mimi sipati uhalifu katika mtu huyu.” (Luka 23:4) Pilato anaposikia kwamba Yesu ni Mgalilaya, anaagiza apelekwe kwa Herode Antipasi, mtawala wa Galilaya, ambaye yumo Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa. Herode hana nia ya kuona haki ikitekelezwa. Yeye anataka tu kumwona Yesu akifanya muujiza fulani. Kwa kuwa Yesu anakosa kutosheleza udadisi wake na abaki kimya, Herode na askari-jeshi wake wanamdhihaki na kumpeleka tena kwa Pilato.

“Ni jambo gani baya alilofanya mtu huyu?” Pilato auliza tena. “Mimi sikupata jambo lolote linalostahili kifo katika yeye; kwa hiyo hakika mimi nitamwadhibu na kumfungua.” (Luka 23:22) Kwa hiyo yeye anaagiza Yesu apigwe kwa mjeledi wenye kanda nyingi ambao unararua mgongo wake kwa uchungu. Kisha askari wanasukuma taji la miiba juu ya kichwa chake. Wanamdhihaki na kumpiga kwa tete imara, wakilisukuma zaidi taji hilo la miiba ndani ya ngozi ya kichwa chake. Katika maumivu hayo yote yasiyoelezeka, pamoja na matusi, Yesu anadumisha hadhi na uthabiti wenye kutokeza.

Pilato amrudisha Yesu mbele ya umati akitumaini kwamba huenda watamhurumia kwa sababu ya namna alivyokuwa amepigwa sana. “Oneni!” Pilato asema kwa mkazo, “namleta nje kwenu kusudi nyinyi mjue kwamba sipati kosa lolote katika yeye.” Lakini makuhani wakuu wapaaza sauti: “Mtundike mtini! Mtundike mtini!” (Yohana 19:4-6) Umati unaposisitiza zaidi na zaidi, Pilato anasalimu amri na anamtoa Yesu atundikwe mtini.

Kifo Chenye Maumivu Makali

Sasa ni asubuhi katikati, labda adhuhuri yakaribia. Yesu anapelekwa nje ya Yerusalemu mahali paitwapo Golgotha. Misumari mikubwa yapigiliwa kwenye mikono na miguu ya Yesu hadi kwenye mti wa mateso. Maumivu makali anayopata hayawezi kuelezeka wakati mwili wake unapozidi kujeruhiwa kwenye majeraha ya misumari mti wa mateso unapoinuliwa. Umati unakusanyika kuangalia Yesu pamoja na wahalifu wawili wakitundikwa mitini. Wengi wanamtusi Yesu. Makuhani wakuu na wengineo wamdhihaki wakisema, “Wengine aliokoa; mwenyewe hawezi kujiokoa!” Hata askari-jeshi na wahalifu wawili waliotundikwa pamoja naye wanamdhihaki Yesu.—Mathayo 27:41-44.

Kwa ghafula wakati wa adhuhuri, baada ya Yesu kuwa kwenye mti wa mateso kwa muda, giza lenye kuogofya, lenye chanzo cha kimungu, linaikumba nchi kwa muda wa saa tatu.a Labda giza hilo ndilo linalomfanya mtenda-maovu mmoja amkemee yule mwingine. Kisha, akimgeukia Yesu, yeye asihi: “Nikumbuke mimi uingiapo katika ufalme wako.” Ni imani yenye kushangaza kama nini ajapokabili kifo kilichokaribia! “Kwa kweli mimi nakuambia wewe leo,” Yesu aitikia, “Utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.”—Luka 23:39-43.

Saa tisa hivi alasiri, Yesu ahisi kwamba mwisho wake umekaribia. “Nina kiu,” yeye asema. Kisha kwa sauti kubwa, alia: “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniachilia mbali?” Yesu anaweza kutambua kwamba Baba yake amemwondolea kinga ili aruhusu uaminifu-maadili wake ujaribiwe hadi upeo, naye ananukuu maneno ya Daudi. Mtu fulani aweka sponji ambayo imeloweshwa divai iliyochacha midomoni mwa Yesu. Baada ya kuonja divai hiyo, Yesu asema kwa kutweta: “Imetimizwa!” Kisha asema kwa sauti kubwa, “Baba, ndani ya mikono yako naikabidhi roho yangu,” kisha anainamisha kichwa chake na kufa.—Yohana 19:28-30; Mathayo 27:46; Luka 23:46; Zaburi 22:1.

Kwa kuwa ni wakati wa jioni-jioni, mipango ya haraka-haraka inafanywa ili kumzika Yesu kabla Sabato haijaanza wakati wa mshuko-jua (Nisani 15). Yosefu wa Arimathea, mshiriki maarufu wa Sanhedrini ambaye amekuwa mwanafunzi wa siri wa Yesu, anapata ruhusa ya kumzika. Nikodemo, ambaye pia ni mshiriki wa Sanhedrini, aliyekiri kisiri imani katika Yesu, anasaidia kwa manemane na udi vyenye uzito wa kilogramu 33. Wanaweka mwili wa Yesu kwa uangalifu katika kaburi la ukumbusho lililoko karibu.

Yu Hai Tena!

Kungali kuna giza, Jumapili asubuhi na mapema, wakati Maria Magdalene na wanawake wengine wanapokaribia kaburi la Yesu. Lakini ona! Jiwe lililokuwa upande wa mbele wa kaburi limeondolewa. Lo, kaburi ni tupu! Maria Magdalene anakimbia kuwaambia Petro na Yohana. (Yohana 20:1, 2) Punde tu baada ya yeye kuondoka malaika anaonekana kwa wanawake wale wengine. Naye asema: “Msiwe na hofu nyinyi.” Pia awahimiza: “Nendeni upesi na waambieni wanafunzi wake kwamba alifufuliwa kutoka kwa wafu.”—Mathayo 28:2-7.

Wanapotembea haraka-haraka, wanakutana na Yesu mwenyewe! “Nendeni, ripotini kwa ndugu zangu,” yeye awaambia. (Mathayo 28:8-10) Baadaye, Maria Magdalene yuko kaburini akilia wakati Yesu anapoonekana kwake. Yeye hawezi kuzuia furaha yake naye anatimua mbio kwenda kuwaambia wanafunzi wengine habari hizo nzuri ajabu. (Yohana 20:11-18) Kwa kweli, Jumapili hiyo isiyoweza kusahaulika, Yesu Kristo aliyefufuliwa aonekana mara tano kwa wanafunzi mbalimbali, akiwaacha bila shaka yoyote kwamba yeye, kwa kweli, yuko hai tena!

Jinsi Unavyoathiriwa

Je, mambo yaliyotukia miaka 1,966 iliyopita yaweza kukuathirije sasa tunapokaribia kuingia karne ya 21? Shahidi aliyejionea mambo hayo aeleza: “Kwa hili upendo wa Mungu ulifanywa dhahiri katika kisa chetu, kwa sababu Mungu alituma Mwana wake mzaliwa-pekee kuingia katika ulimwengu ili tuweze kupata uhai kupitia kwake. Upendo uko hivi, si kwamba sisi tumempenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda akamtuma Mwana wake kuwa dhabihu yenye kufunika kwa ajili ya dhambi zetu.”—1 Yohana 4:9, 10.

Kifo cha Kristo ni “dhabihu yenye kufunika” katika njia gani? Ni yenye kufunika kwa sababu inafanya uhusiano ufaao pamoja na Mungu uwezekane. Mwanadamu wa kwanza, Adamu, aliasi dhidi ya Mungu na kwa hiyo akaurithisha uzao wake dhambi na kifo. Kwa upande mwingine, Yesu alitoa uhai wake kuwa fidia ya kulipia gharama ya dhambi na kifo cha wanadamu, hivyo akiandalia Mungu msingi wa kuonyesha rehema na upendeleo. (1 Timotheo 2:5, 6) Kwa kudhihirisha imani katika dhabihu ya Yesu yenye kufunika dhambi, waweza kuwekwa huru na hatia uliyorithi kutoka kwa Adamu mtenda-dhambi. (Waroma 5:12; 6:23) Kwa upande mwingine, hilo huandaa fursa nzuri ajabu ya kuwa na uhusiano wa kibinafsi pamoja na Baba yako wa kimbingu mwenye upendo, Yehova Mungu. Kwa kifupi, dhabihu ya Yesu iliyo kuu kuliko zote yaweza kumaanisha uhai wa milele kwako.—Yohana 3:16; 17:3.

Mambo hayo na mengine yanayohusiana nayo yatazungumzwa mahali pengi sana ulimwenguni kote siku ya Alhamisi jioni Aprili 1, wakati mamilioni ya watu watakapokusanyika kuadhimisha kifo cha Yesu Kristo. Wewe unaalikwa kuwapo. Mashahidi wa Yehova katika eneo lako watafurahi kukuambia wakati na mahali unapoweza kuhudhuria. Kule kuwapo bila shaka kutaongeza uthamini wako kwa yale ambayo Mungu wetu mwenye upendo na Mwana wake mpendwa walitufanyia katika siku ya mwisho ya maisha ya Yesu ya kibinadamu.

[Maelezo ya Chini]

a Giza hilo haliwezi kuwa lilisababishwa na kupatwa kwa jua kwa sababu Yesu alikufa wakati wa mwezi mpevu. Kupatwa kwa jua hudumu kwa dakika chache tu na hutokea mwezi unapokuwa katikati ya dunia na jua, wakati wa mwezi mpya.

[Chati/Picha katika ukurasa wa 7]

KIFO NA UFUFUO WA YESU

NISANI 33 W.K. MATUKIO MTU MKUU ZAIDIb

14 Alhamisi Kuadhimisha Sikukuu ya Kupitwa; 113, fu. 2

jioni Yesu aosha miguu ya mitume; hadi 117, fu. 1

Yudasi aondoka kwenda kumsaliti Yesu;

Kristo aanzisha Ukumbusho wa kifo chake

(unaoadhimishwa mwaka huu siku ya

Alhamisi, Aprili 1, baada ya mshuko-jua);

himizo la kuwatayarisha mitume kwa ajili

ya kuondoka kwake

Saa sita usiku Baada ya sala na nyimbo za sifa, 117 hadi

hadi kabla ya Yesu na mitume waenda katika 120

mapambazuko bustani ya Gethsemane;

Yesu asali kwa vilio vyenye kupaazwa

kwa nguvu na machozi; Yudasi Iskariote

awasili na umati mkubwa na kumsaliti Yesu;

mitume wakimbia huku Yesu akifungwa

na kupelekwa kwa Anasi; Yesu apelekwa

kwa Kuhani wa Cheo cha Juu, Kayafa,

ili aonekane mbele ya Sanhedrini;

ahukumiwa kifo; atusiwa na kutendwa

vibaya kimwili; Petro amkana Yesu mara tatu

Ijumaa Kwenye mapambazuko, Yesu 121 hadi

asubuhi aletwa tena mbele ya Sanhedrini; 124

apelekwa kwa Pilato; apelekwa kwa Herode;

kisha arudishwa kwa Pilato; Yesu apigwa

mijeledi, atusiwa, na kushambuliwa; chini ya

mkazo, Pilato amtoa ili atundikwe; apelekwa

Golgotha kuuawa, asubuhi ikikaribia kwisha

Adhuhuri Atundikwa mtini muda mfupi 125, 126

na alasiri kabla ya adhuhuri; giza kuanzia

katikati adhuhuri hadi saa tisa hivi, Yesu anapokufa;

tetemeko la dunia lenye nguvu; pazia la hekalu

lapasuliwa vipande viwili

Wakati wa Mwili wa Yesu wawekwa kwenye 127, mafu. 1-7

jioni-jioni kaburi la bustani kabla ya Sabato

15 Ijumaa Sabato yaanza

jioni

Jumamosi Pilato aruhusu walinzi walinde 127, mafu. 8

kaburi la Yesu hadi 9

16 Jumapili Asubuhi na mapema kaburi la Yesu 127, fu. 10

lakutwa likiwa tupu; Yesu aliyefufuka hadi 129,

aonekana kwa (1) kikundi cha wanafunzi fu. 10

wanawake kutia ndani Salome, Yoana, na

Maria mama ya Yakobo; (2) Maria Magdalene;

(3) Kleopasi na mwandamani wake;

(4) Simoni Petro;

(5) kikusanyiko cha mitume na wanafunzi wengine

[Maelezo ya Chini]

b Nambari zilizoorodheshwa hapa zaonyesha sura mbalimbali kwenye kitabu Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi. Ili upate chati yenye marejezo ya Kimaandiko yenye mambo mengi kuhusu huduma ya Yesu ya mwisho, ona “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa,” ukurasa wa 290. Vitabu hivyo vimechapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki