Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 8/15 kur. 8-9
  • Zuia Hasira Isikukwaze

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zuia Hasira Isikukwaze
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Hasira?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Hasira
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Kuweza Hasira Yako na ya Wengine
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Je! Ni Vibaya Nyakati Zote Kuwa na Hasira?
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 8/15 kur. 8-9

Zuia Hasira Isikukwaze

“TULIA!” “Usiwe na haraka!” “Kaa kimya!” Je, wayafahamu mafungu haya ya maneno? Labda wewe huyakariri ili kutuliza fadhaiko la moyoni. Watu wengine hutoka kwenda kutembea katika jitihada ya kuzuia mfoko wa hasira. Hizo ni njia sahili za kutuliza hasira na kudumisha mahusiano na wengine.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, mashauri yenye kuhitilafiana kutoka kwa wataalamu juu ya kama hasira yapaswa kudhibitiwa au kuzuiwa huwaacha wengi wakiwa wametatanika. Kwa mfano, wanasaikolojia fulani wamependekeza nadharia ya kwamba “ikiwa [kulipua hasira yako] kwakufanya uhisi vema zaidi,” basi fanya hivyo. Wengine huonya kwamba mifoko ya kawaida ya hasira ni “dalili ya kufa mapema ambayo ina nguvu kuliko mambo mengine hatari kama kuvuta sigareti, msongo wa damu, na kiwango kikubwa cha kolesteroli.” Neno la Mungu lasema hivi waziwazi: “Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya.” (Zaburi 37:8) Kwa nini Biblia hutoa shauri hilo mahususi?

Hisia zisizodhibitiwa husababisha vitendo visivyodhibitiwa. Hilo lilidhihirika mapema sana katika historia ya mwanadamu. Twasoma hivi: “Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.” Hilo lilimwongoza kufanya nini? Alishikwa na hasira, ikamdhibiti sana hivi kwamba moyo wake ukawa mgumu asikubali shauri la Yehova kuhusu kufanya mema. Hasira ya Kaini isiyodhibitiwa ilimfanya atende dhambi nzito—kuua ndugu yake kimakusudi.—Mwanzo 4:3-8.

Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli, alidhibitiwa na hasira vivyo hivyo aliposikia Daudi akipokea sifa kuu. “Wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza.” Hasira ilidhibiti kufikiri kwa Sauli sana hivi kwamba ikamfanya ajaribu mara kadhaa kumwua Daudi. Hata ingawa Daudi alichukua hatua ya kuanzisha urafiki, Sauli hakuwa tayari kufuata amani na upatano. Hatimaye, alipoteza kabisa upendeleo wa Yehova.—1 Samweli 18:6-11; 19:9, 10; 24:1-21; Mithali 6:34, 35.

Mtu anapojiruhusu apatwe na hasira isiyodhibitiwa, haikosi atasema na kufanya mambo yatakayoumiza wote wanaohusika. (Mithali 29:22) Kaini na Sauli walikasirika kwa sababu kila mmoja, kwa njia yake mwenyewe, alikuwa mwenye wivu na husuda. Hata hivyo, milipuko ya hasira yaweza kusababishwa na mambo mengi. Uchambuzi usio halali, tusi, kutoelewana, au kutendewa isivyofaa vyaweza kuwa visababishi vya mfoko.

Mifano ya Kaini na Sauli yadokeza kasoro kubwa ambayo wote wawili walikuwa nayo. Yaonekana dhabihu ya Kaini haikutolewa kwa imani. (Waebrania 11:4) Kushindwa kwa Sauli kutii amri mahususi za Yehova na majaribio yake ya baadaye ya kujitetea yalifanya apoteze upendeleo na roho ya Mungu. Ni dhahiri kwamba wanaume hao wawili walivunja uhusiano wao na Yehova.

Tofautisha mielekeo hiyo na ule wa Daudi, ambaye alikuwa na sababu ya kukasirikia jinsi alivyotendewa na Sauli. Daudi alijizuia. Kwa nini? Alisema: “Hasha! nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili.” Daudi alikumbuka vizuri uhusiano wake na Yehova, nao uliathiri jinsi alivyomtendea Sauli. Yeye kwa unyenyekevu aliacha mambo mikononi mwa Yehova.—1 Samweli 24:6, 15.

Kwa kweli, hasira isiyodhibitiwa hutokeza mambo mazito sana. Mtume Paulo alitoa tahadhari hii: “Iweni na hasira ya kisasi, na bado msifanye dhambi.” (Waefeso 4:26) Ingawa kuna wakati ufaao wa kuonyesha hasira ya uadilifu, daima kunakuwa na hatari kwamba hasira yaweza kutukwaza. Basi, haishangazi kwamba twakabili ugumu wa kudhibiti hasira yetu. Tunawezaje kufanya hivyo?

Njia kuu ni kusitawisha uhusiano wenye nguvu na Yehova. Yeye hukutia moyo umweleze hisia zako za moyoni na akilini. Mweleze mashaka na mahangaiko yako, nawe umwombe akupe moyo mtulivu wa kudhibiti hasira. (Mithali 14:30) Uwe na uhakika kwamba “macho ya Yehova yako juu ya waadilifu, na masikio yake yaelekea dua zao.”—1 Petro 3:12.

Sala inaweza kukuongoza na kukuelekeza. Kwa njia gani? Inaweza kuathiri sana jinsi unavyowatendea wengine. Kumbuka jinsi ambavyo Yehova amekutendea. Kama Maandiko yasemavyo, Yehova “hakututenda sawasawa na hatia zetu, wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.” (Zaburi 103:10) Roho ya kusamehe ni muhimu ili “[u]sipate kushindwa akili na Shetani.” (2 Wakorintho 2:10, 11) Isitoshe, sala hufunua moyo wako ili uongozwe na roho takatifu, inayoweza kushinda mambo ambayo umezoea sana maishani. Yehova hutoa kwa furaha ‘amani izidiyo fikira yote,’ inayoweza kukuondolea nguvu yenye kudhibiti ya hasira.—Wafilipi 4:7.

Hata hivyo, sala yapaswa iambatane na uchunguzi wa kawaida wa Maandiko ili ‘tuendelee kufahamu mapenzi ya Yehova ni nini.’ (Waefeso 5:17; Yakobo 3:17) Ikiwa wewe binafsi unaona ni vigumu kudhibiti hasira yako, jitahidi kujua maoni ya Yehova kuhusu jambo hilo. Tafakari maandiko yanayohusiana kihususa na kudhibiti hasira.

Mtume Paulo atoa kikumbusha hiki muhimu: “Acheni sisi tufanye lililo jema kuelekea wote, lakini hasa kuelekea wale ambao katika imani ni jamaa zetu.” (Wagalatia 6:10) Kaza fikira na utendaji wako juu ya kufanyia wengine mema. Utendaji huo wenye kujenga na ufaao utachochea hisia-mwenzi na kutumaini, nao utapunguza kutoelewana kunakoweza kutokeza hasira kwa urahisi.

Mtunga-zaburi alisema: “Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, uovu usije ukanimiliki. Wana amani nyingi waipendao sheria yako, wala hawana la kuwakwaza.” (Zaburi 119:133, 165) Hali yaweza kuwa hivyo kwako.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

HATUA ZA KUDHIBITI HASIRA

□ Sali kwa Yehova.—Zaburi 145:18.

□ Chunguza Maandiko kila siku.—Zaburi 119:133, 165.

□ Jishughulishe na utendaji unaofaa.—Wagalatia 6:9, 10.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki