Mnyanyasaji Aona Nuru Kubwa
SAULI alikuwa akiwaka hasira kali kwa sababu ya wafuasi wa Yesu. Akiwa hajatosheka na mnyanyaso ambao tayari walikuwa wamepata huko Yerusalemu, kutia ndani kupigwa mawe kwa Stefano, sasa alitafuta kuendeleza ukandamizaji huo. “Sauli, bado akipumua tisho na uuaji-kimakusudi dhidi ya wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani wa cheo cha juu na kumwomba barua za kwenda kwenye masinagogi katika Damasko, ili apate kuwaleta hadi Yerusalemu wakiwa wamefungwa wowote ambao angewapata walio wa Ile Njia, wanaume na pia wanawake.”—Matendo 9:1, 2.
Sauli alipokuwa akipiga mwendo kuelekea Damasko, hapana budi alitafakari jinsi ya kutekeleza utume wake kwa njia bora zaidi. Mamlaka ambayo kuhani wa cheo cha juu alimpa bila shaka ingefanya aungwe mkono na viongozi wa jumuiya kubwa ya Wayahudi jijini humo. Sauli angeomba msaada wao.
Hapana shaka msisimko wa Sauli ulizidi kupanda alipokaribia Damasko. Safari ya kutoka Yerusalemu kwenda Damasko—safari ya miguu ya siku saba hadi nane ya kilometa 220—ilikuwa imemchosha sana. Kwa ghafula mwendo wa adhuhuri, nuru nyangavu kuliko jua ilimweka kumzunguka Sauli, naye akaanguka chini. Alisikia sauti ikimwambia hivi katika Kiebrania: “Sauli, Sauli, kwa nini unaninyanyasa mimi? Kufuliza kupiga teke dhidi ya michokoo hufanya iwe vigumu kwako.” “Wewe ni nani, Bwana?,” Sauli akauliza. “Mimi ni Yesu, ambaye wewe unanyanyasa,” akajibiwa. “Hata hivyo, inuka usimame kwa miguu yako. Kwa maana kwa madhumuni haya nimejifanya mwenyewe nionekane kwako, ili nikuchague wewe uwe hadimu na shahidi wa mambo ambayo umeona na pia mambo nitakayokufanya uyaone kwa habari yangu; huku mimi nikikukomboa kutoka watu hawa na kutoka katika mataifa, ambao kwao ninakutuma wewe.” “Nitafanya nini, Bwana?,” Sauli akauliza. “Inuka, shika njia yako uende kuingia katika Damasko, na huko utaambiwa juu ya kila kitu ambacho umewekewa kufanya.”—Matendo 9:3-6; 22:6-10; 26:13-17.
Watu waliokuwa wakisafiri na Sauli walisikia sauti, lakini hawakumwona msemaji wala kuelewa alichosema. Kwa sababu ya wangavu wa nuru hiyo, Sauli alipoinuka hakuweza kuona na ilibidi aongozwe kwa kushikwa mkono. “Kwa siku tatu hakuona kitu chochote, naye hakula wala kunywa.”—Matendo 9:7-9; 22:11.
Atafakari kwa Siku Tatu
Sauli alikaribishwa na Yudasi, aliyeishi kwenye barabara iitwayo Nyoofu.a (Matendo 9:11) Barabara hiyo—iitwayo Darb al-Mustaqim katika Kiarabu—ingali barabara kuu jijini Damasko. Fikiri tu mambo aliyowazia Sauli alipokuwa nyumbani kwa Yudasi. Mambo yaliyompata Sauli yalimwacha katika hali ya upofu na mshtuko. Sasa alikuwa na wakati wa kutafakari maana ya mambo hayo.
Mnyanyasaji huyo alikabiliwa na jambo alilolipuuza kuwa ni upumbavu. Bwana Yesu Kristo aliyetundikwa mtini—aliyehukumiwa na mamlaka kuu ya Wayahudi na ‘kudharauliwa na kukataliwa na watu’—alikuwa hai. Kwani, hata alipata kibali cha kukaa mkono wa kuume wa Mungu kwenye “nuru isiyokaribika”! Yesu alikuwa ndiye Mesiya. Stefano na wengine walikuwa sahihi. (Isaya 53:3; Matendo 7:56; 1 Timotheo 6:16) Sauli alikuwa amekosea kabisa, kwa kuwa Yesu aliwaunga mkono watu ambao Sauli alikuwa akinyanyasa! Kukiwa na uthibitisho huo, Sauli angefulizaje “kupiga teke dhidi ya michokoo”? Hata fahali mkaidi hatimaye hushawishiwa kwenda kule atakako mmilikaji wake. Kwa kukataa kutii sihi za Yesu, basi Sauli angekuwa akijiumiza mwenyewe.
Yesu hangeweza kuhukumiwa na Mungu, kwa maana alikuwa ndiye Mesiya. Ingawa hivyo, Yehova alimruhusu afe kifo cha aibu zaidi na kupata hukumu hii ya Sheria: “Aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu.” (Kumbukumbu la Torati 21:23) Yesu alikufa akiwa ametundikwa juu ya mti wa mateso. Alilaaniwa, si kwa sababu ya dhambi zake mwenyewe, kwa maana hakuwa na dhambi yoyote, bali kwa sababu ya dhambi za wanadamu. Baadaye Sauli alieleza hivi: “Wote wale wategemeao kazi za sheria wako chini ya laana; kwa maana imeandikwa: ‘Mwenye kulaaniwa ni kila mtu asiyeendelea katika mambo yote yaliyoandikwa katika hati-kunjo ya Sheria kusudi ayafanye.’ Zaidi ya hayo, kwamba kwa sheria hakuna yeyote ambaye hutangazwa kuwa mwadilifu kwa Mungu ni dhahiri . . . Kristo kwa kununua alituachilia kutokana na laana ya Sheria kwa kuwa laana badala yetu, kwa sababu imeandikwa: ‘Mwenye kulaaniwa ni kila mtu aliyeangikwa juu ya mti.’”—Wagalatia 3:10-13.
Dhabihu ya Yesu ilikuwa na thamani ya ukombozi. Kwa kukubali dhabihu hiyo, ni kana kwamba Yehova aliipigilia misumari Sheria na laana yake mtini. Baada ya kufahamu jambo hilo, Sauli angeweza kuuona mti wa mateso kama “hekima ya Mungu,” ambao “kwa Wayahudi ni sababu ya kukwaza.” (1 Wakorintho 1:18-25; Wakolosai 2:14) Hivyo, ikiwa wokovu haungepatikana kwa kazi za sheria bali kwa fadhili isiyostahiliwa ya Mungu kwa watenda-dhambi kama Sauli mwenyewe, basi kulikuwa na uwezekano wokovu huo uwafikie wale walio nje ya Sheria. Kwa hiyo Yesu alikuwa akimtuma Sauli kwa wasio Wayahudi.—Waefeso 3:3-7.
Hatujui Sauli alielewa mambo hayo kadiri gani alipogeuzwa imani. Baadaye Yesu alisema naye tena, labda zaidi ya mara moja, kuhusu utume wake kwa mataifa. Isitoshe, miaka kadhaa ilipita kabla Sauli hajaandika mambo hayo yote chini ya upulizio wa Mungu. (Matendo 22:17-21; Wagalatia 1:15-18; 2:1, 2) Hata hivyo, baada ya siku chache, Sauli akapata mwelekezo zaidi kutoka kwa Bwana wake mpya.
Anania Amtembelea
Baada ya kumtokea Sauli, Yesu alimtokea pia Anania, akimwambia: “Nenda kwenye barabara iitwayo Nyoofu, na kwenye nyumba ya Yudasi tafuta mtu aitwaye jina Sauli, kutoka Tarso. Kwa maana, tazama! yeye anasali, na katika ono ameona mwanamume aitwaye jina Anania akiingia na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”—Matendo 9:11, 12.
Kwa kuwa Anania alimjua Sauli, basi waweza kuelewa sababu alishtuka kusikia maneno ya Yesu. Alisema hivi: “Bwana, nimesikia kutoka kwa wengi juu ya mtu huyu, mambo mengi mabaya aliyowafanya watakatifu wako katika Yerusalemu. Naye hapa ana mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwaweka vifungoni wote wale wanaoita jina lako.” Hata hivyo, Yesu akamwambia Anania: “Shika njia yako uende, kwa sababu mtu huyu ni chombo-kichaguliwa kwangu ili kupeleka jina langu kwa mataifa vilevile kwa wafalme na wana wa Israeli.”—Matendo 9:13-15.
Huku akiwa ametiwa moyo, Anania alienda mahali ambapo Yesu alimweleza. Alipomkuta na kumsalimu Sauli, Anania akaweka mikono yake juu yake. “Na mara,” masimulizi hayo yasema, “kukaanguka kutoka kwenye macho yake kile kilichoonekana kama magamba, naye akapata kuona tena.” Sauli sasa alikuwa tayari kusikiliza. Maneno ya Anania yalithibitisha mambo ambayo labda Sauli alifahamu kutokana na maneno ya Yesu: “Mungu wa baba zetu wa zamani amekuchagua uje kujua mapenzi yake na kuona yule Aliye mwadilifu na kuisikia sauti ya kinywa chake, kwa sababu wewe wapaswa kuwa shahidi kwa ajili yake kwa watu wote juu ya mambo ambayo umeona na kusikia. Na sasa kwa nini unakawia? Inuka, ubatizwe na uoshe dhambi zako kwa kuitia jina lake.” Halafu ikawaje? Sauli “akainuka na kubatizwa, naye akala chakula na kupata nguvu.”—Matendo 9:17-19; 22:12-16.
Baada ya kutimiza utume wake, Anania mwaminifu alitoweka ghafula, kama alivyoingia, katika masimulizi hayo, nasi hatuelezwi tena lolote kumhusu. Lakini Sauli aliwashangaza wote waliomsikia! Mnyanyasaji huyo wa awali, aliyekuja Damasko kuwakamata wanafunzi, alianza kuhubiri katika masinagogi na kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Kristo.—Matendo 9:20-22.
“Mtume kwa Mataifa”
Mambo yaliyomkumba Sauli barabarani kuelekea Damasko yalikomesha unyanyasaji wake. Baada ya kufahamu utambulisho wa Mesiya, Sauli angeweza kutumia mawazo na unabii mwingi wa Maandiko ya Kiebrania kumhusu Yesu. Ufahamu wa kwamba Yesu ameonekana kwake na ‘kumshika’ na kumpa utume wa kuwa “mtume kwa mataifa” uliyabadili kabisa maisha ya Sauli. (Wafilipi 3:12; Waroma 11:13) Sasa akiwa mtume Paulo, alikuwa na pendeleo na mamlaka ambazo zingeathiri sana siku zake za baadaye duniani na pia mwendo wa historia ya Ukristo.
Miaka kadhaa baadaye, wakati utume wa Paulo ulipopingwa, alitetea mamlaka yake kwa kurejezea mambo yaliyomkumba barabarani akielekea Damasko. “Je, mimi si mtume? Je, mimi sijamwona Yesu Bwana wetu?,” akauliza. Na baada ya kutaja vile Yesu aliyefufuliwa alivyoonekana kwa wengine, Sauli (Paulo) alitaarifu: “Mwisho wa wote alionekana pia kwangu kama kwamba kwa mmoja aliyezaliwa kabla ya wakati wake.” (1 Wakorintho 9:1; 15:8) Ilikuwa kana kwamba Sauli, kupitia ono lake la utukufu wa Yesu wa mbinguni, alikuwa amepewa heshima ya kuzaliwa, au kufufuliwa, kwenye uhai wa roho kabla ya wakati wake.
Sauli alikubali pendeleo lake naye akajitahidi kulitimiza. “Mimi ni mdogo zaidi sana kati ya wale mitume, nami sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililinyanyasa kutaniko la Mungu,” akaandika. “Lakini . . . fadhili [ya Mungu] isiyostahiliwa iliyonielekea mimi haikuthibitika kuwa bure, bali nilifanya kazi ya jasho kwa kuwazidi [wale mitume wengine wote].”—1 Wakorintho 15:9, 10.
Labda wewe, sawa na Sauli, hukumbuka wakati ulitambua kwamba ili kupata upendeleo wa Mungu, inakubidi kubadili mawazo ya kidini uliyoshikilia kwa muda mrefu. Hapana shaka ulishukuru sana kwa sababu Yehova alikusaidia kuielewa kweli. Sauli alipoona nuru na kutambua mambo yaliyohitajika kutoka kwake, hakusita kuyatimiza. Naye aliendelea kuyatimiza kwa bidii na uthabiti kwa muda wote uliobaki wa maisha yake duniani. Hicho ni kielelezo bora kama nini kwa wote wanaotamani kupata upendeleo wa Yehova leo!
[Maelezo ya Chini]
a Msomi mmoja aonelea kwamba huenda Yudasi alikuwa kiongozi wa jumuiya ya Wayahudi wa hapo au mmiliki wa hoteli ndogo ya Wayahudi.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]
Barabara iitwayo Nyoofu katika Damasko ya leo
[Hisani]
Photo by ROLOC Color Slides