Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w09 12/1 kur. 13-15
  • “Siku za Mfalme Herode”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Siku za Mfalme Herode”
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupigania Mamlaka Huko Yudea
  • Kuibuka kwa Herode
  • Afanywa Kuwa Mfalme wa Yudea
  • Herode Aimarisha Mamlaka Yake
  • Mauaji Yaliyochochewa na Wivu
  • Fungu la Herode Mkuu Katika Historia
  • Mauaji Kwenye Sherehe ya Sikukuu ya Kuzaliwa
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Herode Mkuu—Mjenzi Stadi
    Amkeni!—2009
  • Pilato na Herode Wakosa Kumpata na Hatia
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Wanaume Walioongozwa na Nyota
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
w09 12/1 kur. 13-15

“Siku za Mfalme Herode”

AKIJARIBU kumwua Yesu mchanga, Herode Mkuu, mfalme wa Yudea, aliwatuma watu wakawaue wavulana wote waliokuwa chini ya umri wa miaka miwili huko Bethlehemu. Historia inaonyesha mambo mengi yaliyotukia “siku za Mfalme Herode,” mambo yanayotusaidia tuelewe vizuri zaidi matukio na hali zilizokuwapo wakati wa maisha na huduma ya Yesu.—Mathayo 2:1-16.

Ni nini kilichomfanya Herode atake kumwua Yesu? Na kwa nini Wayahudi walikuwa na mfalme wakati Yesu alipozaliwa, lakini Yesu alipokufa, Pontio Pilato, Mroma, ndiye aliyekuwa gavana juu yao? Ili tupate picha kamili ya fungu ambalo Herode alitimiza katika historia na pia ili tuelewe kwa nini yeye ni mtu muhimu kwa wasomaji wa Biblia, tunahitaji kurudi nyuma makumi ya miaka kabla ya Yesu kuzaliwa.

Kupigania Mamlaka Huko Yudea

Katika miaka 50 ya kwanza ya karne ya pili K.W.K., Yudea ilitawaliwa na ukoo wa Seleuko Msiria. Hiyo ilikuwa moja kati ya falme nne zilizotokea baada ya kuvunjika kwa milki ya Aleksanda Mkuu. Hata hivyo, karibu mwaka wa 168 K.W.K., mfalme wa ukoo wa Seleuko alipojaribu kubadili ibada ya Yehova na madhehebu ya Zeu katika hekalu la Yerusalemu, Wayahudi waliasi, wakiongozwa na familia ya Wamakabayo. Wamakabayo walitawala Yudea kuanzia 142-63 K.W.K.

Katika mwaka wa 66 K.W.K., wana wa mfalme wa ukoo wa Makabayo, Hirakano wa 2 na ndugu yake Aristobulo, walipigania kiti cha ufalme. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vikafyatuka na wote wawili wakaomba msaada kutoka kwa Pompey, jenerali Mroma, ambaye wakati huo alikuwa huko Siria. Pompey alichukua hatua mara moja.

Kwa kweli, Waroma walikuwa wakipanua milki yao upande wa mashariki na kufikia wakati huo walitawala sehemu kubwa ya Asia Ndogo. Hata hivyo, watawala dhaifu wa Siria waliruhusu kuwe na vurugu katika eneo hilo na hivyo kutishia amani ambayo Waroma walitaka kudumisha katika maeneo ya Mashariki. Kwa hiyo, Pompey alifika ili kuidhibiti Siria.

Ili kutatua mzozo huo wa Wamakabayo, Pompey aliamua kumuunga mkono Hirakano, na katika mwaka wa 63 K.W.K., Waroma walivamia Yerusalemu na kumtawaza kuwa mfalme. Hata hivyo, hawakumruhusu Hirakano awe mtawala huru. Waroma walikuwa wamejiingiza katika mambo ya eneo hilo nao hawakuwa tayari kuachilia udhibiti wao juu ya eneo hilo. Hirakano akawa gavana ambaye alitawala chini ya mamlaka ya Roma na utawala wake ulitegemea tu utegemezo wao. Angeweza kushughulikia mambo ya ndani kwa njia yoyote aliyotaka, lakini alihitaji kufuata sera ya Roma aliposhughulikia mambo ya nje.

Kuibuka kwa Herode

Hirakano alikuwa mtawala dhaifu. Hata hivyo, aliungwa mkono na Antipater, wa eneo la Idumea ambaye alikuwa baba ya Herode Mkuu. Antipater ndiye aliyeufanya utawala wa Hirakano uwe na nguvu. Alizuia vikundi vya upinzani vya Wayahudi visiwe na udhibiti wowote juu ya watu na baada ya muda mfupi akawa na udhibiti mkubwa juu ya Yudea. Alimsaidia Yulio Kaisari kupigana na maadui huko Misri, nao Waroma wakamthawabisha Antipater kwa kumpa cheo chenye mamlaka juu ya eneo lote la Yudea. Kwa upande wake, Antipater aliwaweka rasmi wana wake Phasael na Herode kuwa magavana wa Yerusalemu na Galilaya.

Antipater aliwafundisha wana wake kwamba hakuna kitu ambacho kingetimizwa bila idhini ya Roma. Herode alikumbuka jambo hilo vizuri sana. Muda wote wa utawala wake, alilazimika kusawazisha matakwa ya Waroma waliompa mamlaka na yale ya raia wake Wayahudi. Ustadi wake akiwa jenerali na uwezo wake wa kupanga mambo ulimsaidia sana. Alipowekwa kuwa gavana, Herode mwenye umri wa miaka 25 alijishindia sifa kutoka kwa Wayahudi na Waroma kwa kuangamiza vikundi vya wavamizi kutoka katika eneo lake.

Katika mwaka wa 43 K.W.K. wapinzani walipomwua Antipater kwa sumu, Herode akawa mtu mwenye nguvu zaidi huko Yudea. Lakini alikuwa na maadui. Wayahudi wa tabaka la juu huko Yerusalemu walimwona kuwa mnyakuzi na walijitahidi kuwasadikisha Waroma wamwondoe mamlakani. Lakini walishindwa. Waroma walikumbuka matendo ya Antipater na walithamini sana uwezo wa mwana wake.

Afanywa Kuwa Mfalme wa Yudea

Miaka 20 hivi mapema, mbinu ambayo Pompey alitumia kutatua mzozo kati ya Wamakabayo ilikuwa imewachukiza watu wengi. Wale walioshindwa wakati huo walijaribu mara nyingi kunyakua mamlaka, na katika mwaka wa 40 K.W.K., walifaulu wakisaidiwa na Waparthi waliokuwa maadui wa Roma. Wakitumia vurugu zilizotokezwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Roma, walivamia Siria, wakamwondoa Hirakano mamlakani, na kumtawaza mtawala wa ukoo wa Makabayo ambaye aliwapinga Waroma.

Herode alikimbilia Roma, ambako alipokewa kwa uchangamfu. Waroma walitaka Waparthi waondolewe huko Yudea na eneo hilo lirudi chini ya udhibiti wao likisimamiwa na mtawala waliyemchagua. Walihitaji mtu ambaye angetegemeka na waliona kwamba Herode ndiye angefaa. Kwa hiyo, Baraza la Roma lilimtawaza Herode kuwa mfalme wa Yudea. Ili kuonyesha mambo mengi ambayo alikuwa tayari kufanya ili kudumisha mamlaka yake, Herode aliongoza msafara kutoka kwenye Baraza hilo hadi kwenye hekalu la Sumbula, ambako alitoa dhabihu kwa miungu ya kipagani.

Akisaidiwa na vikosi vya Roma, Herode aliwashinda maadui wake huko Yudea na akachukua mamlaka yake. Alitekeleza kisasi dhidi ya wapinzani wake kwa ukatili. Aliwaua Wamakabayo na Wayahudi wa tabaka la juu waliowaunga mkono, kutia ndani watu wowote ambao hawakutaka kutawaliwa na mtu aliyekuwa rafiki ya Waroma.

Herode Aimarisha Mamlaka Yake

Mnamo 31 K.W.K. Octavius alipoibuka akiwa mtawala asiyepingwa wa Waroma kwa kumshinda Mark Antony huko Actium, Herode alitambua kwamba urafiki wake wa muda mrefu na Mark Antony ungetokeza mashaka. Kwa hiyo, Herode alimhakikishia upesi Octavius kwamba angekuwa mshikamanifu kwake. Mtawala huyo mpya wa Roma alimkubali Herode kuwa mfalme wa Yudea na kupanua eneo lake.

Katika miaka iliyofuata, Herode aliimarisha na kutajirisha ufalme wake, akigeuza Yerusalemu kuwa kituo cha utamaduni wa Kigiriki. Alianzisha miradi mingi ya ujenzi, kama vile kujenga makasri, jiji la bandarini la Kaisaria, na majengo mapya makubwa katika hekalu la Yerusalemu. Muda huo wote, sera zake na nguvu zake zilitokana na urafiki wake na Roma.

Herode alidhibiti kabisa eneo lote la Yudea; mamlaka yake ilikuwa kamili. Pia, Herode alikuwa na uvutano juu ya kuhani mkuu, kwani alimpa mtu yeyote aliyemtaka cheo hicho.

Mauaji Yaliyochochewa na Wivu

Maisha ya kibinafsi ya Herode yalikuwa na msukosuko. Wengi kati ya wake zake kumi walitaka wana wao warithi utawala wa baba yao. Msukosuko katika nyumba yake ulimfanya Herode awashuku watu na kuwa mkatili. Kwa sababu ya wivu, aliamuru kwamba Mariamne, mke wake ambaye alimpenda zaidi auawe, na baadaye akawanyonga wana wawili wa Mariamne eti kwa sababu walikuwa wakipanga njama dhidi yake. Basi simulizi la Mathayo kuhusu mauaji ya watoto huko Bethlehemu yanapatana na mambo yanayojulikana kuhusu hasira ya Herode na azimio lake la kuwaangamiza wapinzani wake.

Watu fulani wanasema kwamba kwa kuwa Herode alijua hapendwi na watu, aliazimia kwamba badala ya kushangilia wakati wa kifo chake, watu waomboleze. Ili afaulu katika jambo hilo, aliwakamata raia maarufu wa Yudea na akaamuru kwamba wote wauawe wakati wa kifo chake. Amri yake haikutekelezwa.

Fungu la Herode Mkuu Katika Historia

Herode alipokufa, Waroma waliamuru Arkelao arithi utawala wa baba yake huko Yudea na wakawafanya wana wake wawili kuwa maliwali—Antipa akisimamia Galilaya na Perea, Filipo akisimamia Iturea na Trakonitisi. Arkelao hakupendwa na Waroma na pia na raia zake. Waroma walimwondoa baada ya miaka kumi ya utawala wake usio na uvutano na wakamweka gavana wao wenyewe, aliyetawala kabla ya Pontio Pilato. Lakini bado Antipa—ambaye Luka anamwita tu Herode—na Filipo waliendelea kusimamia maeneo yao. Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa Yesu alipoanza huduma yake.—Luka 3:1.

Herode Mkuu alikuwa mwanasiasa mwerevu na mwuaji mkatili, labda tendo lake baya zaidi la ukatili likiwa lile jaribio la kumwua Yesu akiwa mtoto. Kuchunguza fungu la Herode katika historia ni muhimu kwa wasomaji wa Biblia—kunasaidia kufafanua matukio muhimu ya wakati huo, kunaeleza jinsi Waroma walikuja kuwatawala Wayahudi, na kunatoa muktadha wa maisha na huduma ya Yesu duniani.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Palestina na maeneo yaliyoizunguka wakati wa Herode

SIRIA

ITUREA

GALILAYA

TRAKONITISI

Bahari ya Galilaya

Mto Yordani

Kaisaria

SAMARIA

PEREA

Yerusalemu

Bethlehemu

YUDEA

Bahari ya Chumvi

IDUMEA

[Picha katika ukurasa wa 13]

Herode alikuwa mmoja tu kati ya watu waliotawala Yudea katika karne mbili kabla ya huduma ya Yesu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki