Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kutoa Hotuba kwa Njia ya Maongezi
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
    • SOMO LA 28

      Kutoa Hotuba kwa Njia ya Maongezi

      Unahitaji kufanya nini?

      Unahitaji kutoa hotuba kama unavyozungumza kwa kawaida lakini kwa namna inayofaa wasikilizaji.

      Kwa Nini Ni Muhimu?

      Hotuba inayotolewa kwa njia inayofaa ya maongezi hustarehesha wasikilizaji na hufanya waweze kukubali mambo unayosema.

      KWA kawaida watu hustarehe wanapozungumza na marafiki. Maneno yao yanatiririka tu. Watu wengine ni wachangamfu sana ilhali wengine huwa kimya. Hata hivyo, maongezi ya kawaida kama hayo huvutia.

      Lakini unapokutana na mtu ambaye humjui si vizuri kuzungumza naye kana kwamba unamjua sana wala kuzungumza naye kwa njia inayokosa adabu. Katika jamii nyingi mazungumzo yote kati ya watu ambao hawajuani huanza kwa njia rasmi sana. Lakini baada ya salamu za heshima, kwa busara unaweza kuanza kuzungumza kwa njia ya kawaida ya maongezi.

      Tahadhari pia unapotoa hotuba jukwaani. Kutoa hotuba kwa njia ya kizembe kutafanya mkutano wa Kikristo ukose heshima na watu wakose kuthamini mambo unayosema. Katika jamii fulani unapaswa kusema maneno fulani unapozungumza na mtu anayekuzidi umri, mwalimu, ofisa fulani, au mzazi. (Ebu ona maneno yanayotumiwa katika Matendo 7:2 na 13:16.) Maneno tofauti-tofauti hutumiwa kumwita mume au mke au rafiki unayempenda. Ingawa hatupaswi kuongea kwa njia rasmi sana jukwaani, tunapaswa kuongea kwa heshima.

      Hata hivyo, kuna mambo ambayo yanaweza kumfanya mtu atoe hotuba bila kubadilikana. Mojawapo ya sababu hizo ni muundo wa sentensi. Tatizo huzuka msemaji anapojaribu kurudia maneno yaleyale kama yalivyoandikwa katika vichapo. Kwa kawaida watu huzungumza kwa njia tofauti na jinsi maneno yanavyoandikwa. Ni kweli kwamba kwa kawaida tunatayarisha hotuba kupitia habari iliyochapwa. Labda muhtasari uliochapwa ndio msingi wa hotuba. Lakini ikiwa unazungumza kana kwamba unasoma kichapo au ikiwa unasoma moja kwa moja muhtasari wa hotuba, inaelekea hutatoa hotuba kwa njia ya maongezi. Ili utoe hotuba kwa njia ya maongezi, tumia maneno yako mwenyewe na kuepuka sentensi ngumu-ngumu.

      Jambo jingine ni kubadili-kubadili mwendo wako wa kuzungumza. Usemi baridi-baridi na ulio rasmi kupita kiasi husababishwa na maneno yanayofuatana kwa mwendo uleule mmoja usiobadilika. Katika mazungumzo ya kawaida, watu hubadili-badili mwendo na kutua-tua kwa njia tofauti-tofauti.

      Bila shaka, unapohutubia watu wengi unapaswa kuhutubu kwa njia ya maongezi na kwa sauti ya juu, kwa mkazo, na kwa shauku ili waendelee kukusikiliza kwa makini.

      Ili uzungumze kwa njia ya maongezi inayofaa utumishi, unahitaji kuwa na mazoea ya kuzungumza vizuri kila siku. Haimaanishi kwamba ni lazima uwe na elimu ya juu. Lakini ni vizuri uwe na mazoea mazuri ya usemi ambayo yatafanya wengine wakusikilize kwa heshima. Basi, ukiwa na mambo hayo akilini, ebu ona kama unahitaji kufanyia kazi sifa zifuatazo katika mazungumzo ya kawaida:

      1. Epuka lugha chafu au matusi kwa kupatana na shauri la Wakolosai 3:8. Kwa upande mwingine, si vibaya kutumia lugha inayotumiwa kwa kawaida inayopatana na lugha sanifu ingawa si rasmi.

      2. Jifunze kutumia maneno yanayoonyesha wazi jambo unalomaanisha.

      3. Uwe na mazoea ya kusema jambo unalotaka watu wakumbuke kwa njia inayoeleweka wazi na kwa maneno rahisi.

      JINSI YA KUKUZA SIFA HII

      • Uwe na maoni mazuri juu ya wasikilizaji. Waone kama marafiki, lakini usiwazoee kupita kiasi. Waheshimu.

      • Zungumza bila kutazama sana maandishi. Usitumie miundo ileile ya maneno yaliyo katika kichapo. Jieleze kwa maneno yako mwenyewe. Tumia sentensi fupi-fupi, na ubadili-badili mwendo wako.

      • Kazia akili hamu yako ya kufundisha. Zungumza kwa hisia. Jambo muhimu ni ujumbe, wala si jinsi watu wanavyokuona.

      • Boresha mazungumzo yako ya kawaida. Tumia hatua kwa hatua madokezo yanayoonyeshwa katika ukurasa huu.

      MAZOEZI: Chunguza mazoea yako ya kuzungumza. Fanyia kazi mambo matano ambayo yameorodheshwa hapo juu, ukishughulikia jambo moja kwa wakati mmoja siku kutwa. Ukifanya kosa lolote, angalau rudia tena wazo hilo akilini mwako kwa njia sahihi.

  • Ubora wa Sauti
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
    • SOMO LA 29

      Ubora wa Sauti

      Unahitaji kufanya nini?

      Unahitaji kuboresha sauti yako kwa kupumua vizuri na kutuliza misuli yako badala ya kuiga mtu mwingine.

      Kwa Nini Ni Muhimu?

      Sauti nzuri hufanya wengine watulie na kufurahia kusikiliza. Sauti mbaya huharibu mawasiliano, na inaweza kumfadhaisha msemaji na wasikilizaji.

      KWA KAWAIDA watu hawavutiwi tu na mambo yanayosemwa, bali wanavutiwa pia na jinsi yanavyosemwa. Ikiwa mtu anayezungumza nawe ana sauti nzuri, changamfu, ya kirafiki, na yenye fadhili, utafurahia kumsikiliza kuliko kama ana sauti kali isiyo ya kirafiki, sivyo?

      Kukuza sifa hizo nzuri hakutegemei tu kuboresha sauti. Kunaweza kuhusu utu wa mtu pia. Mtu anapoendelea kujifunza kweli ya Biblia na kuifuata, kwa wazi njia yake ya kuzungumza inabadilika. Sauti yake huonyesha sifa kama vile upendo, shangwe, na fadhili. (Gal. 5:22, 23) Anapojali wengine sana, sauti yake inaonyesha. Anapokuwa mwenye shukrani badala ya kulalamika daima, maneno anayosema na sauti yake inaonyesha hivyo. (Wim. 3:39-42; 1 Tim. 1:12; Yuda 16) Hata kama huelewi lugha fulani, ni rahisi kujua ikiwa mtu anazungumza kwa njia ya ufidhuli, hana uvumilivu, anachambua, ni mkali, na pia ni rahisi kujua kama mwingine anazungumza kwa unyenyekevu, subira, fadhili, na upendo.

      Nyakati nyingine sauti isiyofaa inaweza kusababishwa na kasoro fulani ambayo mtu amezaliwa nayo au ugonjwa uliodhuru zoloto. Huenda kasoro hizo zisiweze kurekebishwa katika mfumo huu wa mambo. Lakini, unaweza kuboresha sauti yako ukijifunza kutumia vizuri viungo vya usemi.

      Kwanza, tufahamu kwamba sauti za watu hutofautiana. Kwa hiyo, usijaribu kuiga sauti ya mtu mwingine. Badala yake, boresha sauti yako mwenyewe pamoja na hali zake. Unawezaje kufaulu? Kuna mambo mawili makuu.

      Pumua Vizuri. Ili sauti yako iwe nzuri, unahitaji hewa ya kutosha na unahitaji kupumua vizuri. Bila kufanya hivyo, sauti yako inaweza kuwa dhaifu mno na unaweza kukata-kata maneno katika hotuba yako.

      Sehemu kubwa za mapafu haziko juu kifuani; sehemu hizo huonekana kubwa kwa sababu tu ya mifupa ya mabega. Lakini, sehemu za mapafu zilizo pana zaidi ziko chini, juu tu ya kiwambo. Kiwambo kinashikana na mbavu za chini na kinatenganisha kifua na tumbo.

      Ukivuta pumzi na kujaza tu sehemu za juu za mapafu, utakosa pumzi haraka. Sauti yako itakosa nguvu na utachoka haraka. Ili uvute pumzi vizuri, unahitaji kuketi au kusimama vizuri na kurejesha mabega nyuma. Jaribu sana usipanue sehemu ya juu pekee ya kifua unapovuta pumzi. Kwanza vuta pumzi kabisa. Sehemu za chini za mapafu zikijaa hewa, mbavu zako za chini zitapanuka. Kwa wakati huohuo, kiwambo kitasonga chini, kikisukuma chini kwa utaratibu sehemu za tumbo hivi kwamba utasikia mkazo kwenye mshipi wako au kwenye vazi katika eneo la tumbo. Lakini mapafu hayako kwenye eneo la tumbo; yamefunikwa na mbavu. Unaweza kuthibitisha jambo hilo kwa kuweka mkono mmoja kila upande wa mbavu za chini. Kisha vuta pumzi kabisa. Kama unavuta pumzi vizuri, utaona kwamba huingizi hewa tumboni na kuinua mabega. La, badala yake, utasikia mbavu zikisonga juu kidogo na kupanuka.

      Kisha, jaribu kushusha pumzi. Usishushe pumzi kwa ghafula. Ishushe polepole. Usijaribu kuzuia pumzi kwa kukaza koo kwa sababu sauti itajikaza au itakuwa nyembamba sana. Mkazo wa misuli ya tumbo na mkazo wa misuli iliyo kati ya mbavu huondosha pumzi, lakini kiwambo hudhibiti mwendo wa pumzi hiyo.

      [Michoro katika ukurasa wa 183]

      Msemaji anaweza kudhibiti jinsi anavyopumua kwa kujizoeza kama vile tu mwanariadha anavyofanya mazoezi ya mbio. Simama vizuri kama umerejesha nyuma mabega, vuta pumzi kabisa ili sehemu za chini za mapafu zijae hewa, kisha shusha pumzi polepole na kwa utaratibu ukihesabu kwa kadiri uwezavyo kabla ya kuvuta tena pumzi. Kisha jizoeze kusoma kwa sauti ukipumua kwa njia hiyo.

      Tuliza Mkazo wa Misuli. Jambo jingine muhimu linalotokeza sauti nzuri ni utulivu! Unaweza kuboresha sana sauti yako ukijifunza kutulia unapozungumza. Ni lazima akili na mwili zitulie, kwa kuwa mkazo wa akili husababisha mkazo wa misuli.

      Ondoa mkazo wa akili kwa kuwa na maoni mazuri juu ya watu unaozungumza nao. Ikiwa unakutana nao katika huduma ya shambani, kumbuka kwamba hata kama umejifunza Biblia kwa miezi michache tu, unajua mambo mazuri sana kuhusu kusudi la Yehova ambayo unaweza kuwaeleza. Na unawatembelea kwa sababu wanahitaji msaada, iwe wanatambua jambo hilo au la. Na kama unatoa hotuba katika Jumba la Ufalme, wengi wa wasikilizaji ni watu wa Yehova. Wao ni rafiki zako na wanataka ufaulu. Hakuna wasemaji wengine duniani ambao huhutubia wasikilizaji wenye urafiki na wenye upendo kama sisi.

      Ifikirie misuli ya koo na kujaribu kuituliza. Kumbuka kwamba nyuzi zako za sauti hutikisika zinapopitisha hewa. Sauti hubadilika misuli hiyo ikikazika au ikitulia kama tu vile uzi wa gitaa hubadili sauti ukikazwa au ukilegezwa. Sauti hurudi chini nyuzi za sauti zinapotulia. Kutuliza misuli ya koo pia hufanya mianzi ya pua ibaki wazi, na hiyo huboresha sauti.

      Tuliza mwili wako mzima—magoti, mikono, mabega, na shingo. Ukifanya hivyo, utaweza kuvumisha sauti vizuri ili isikike wazi. Sauti huvumishwa wakati mwili wote unapohusika kuitokeza, lakini mkazo huizuia. Sauti hutokezwa kwenye zoloto nayo huvumishwa katika mianzi ya pua, kwenye mifupa ya kifua, meno, na kaakaa ya mdomo na mianya iliyo katika mifupa ya pua. Sehemu hizo zote zinaweza kuchangia ubora wa sauti. Ukiweka kitu kwenye kibao cha gitaa cha kupaazia sauti, sauti itafifia; ni lazima kibao hicho kisiwe na kitu ili kitikisike na kutoa sauti vizuri. Ndivyo ilivyo pia na mifupa ya mwili wetu ambayo imeshikiliwa na misuli. Uvumishaji mzuri wa sauti unakuwezesha kuwa na ubadilifu wa sauti na kuweza kuonyesha hisia mbalimbali unapozungumza. Pia utaweza kuhutubia watu wengi zaidi bila kukaza sauti.

      SAUTI HUTOKEZWAJE?

      Sauti zote hutokezwa na hewa inayotoka mapafuni. Mapafu hupiga hewa kama pampu kupitia koo na kuingia ndani ya zoloto ambayo iko katikati ya koo. Ndani ya zoloto mna misuli miwili midogo inayoitwa nyuzi za sauti, msuli mmoja uko upande mmoja na msuli mwingine upande mwingine. Nyuzi hizo za sauti ndizo vitokezaji vikuu vya sauti. Misuli hiyo hufungua na kufunga njia ya hewa katika zoloto ili kuingiza hewa na kuitoa na vilevile kuzuia vitu visivyotakikana visiingie kwenye mapafu. Tunapopumua kwa njia ya kawaida nyuzi za sauti hazitokezi sauti wakati hewa inapopita. Lakini mtu akitaka kuzungumza, misuli hufinya nyuzi za sauti, na nyuzi hizo hutikisika wakati hewa inayotoka mapafuni inaposukumwa kuzipitia. Utaratibu huo hutokeza sauti.

      Kadiri nyuzi za sauti zinavyokazika, ndivyo zinavyotikisika kwa kasi zaidi na ndivyo sauti inavyoinuka. Na kadiri nyuzi hizo zinavyolegea, ndivyo sauti inavyopungua. Mawimbi ya sauti yanayotoka kwenye zoloto huingia sehemu ya juu ya koo inayoitwa koromeo. Kisha mawimbi hayo hupitia mdomo na pua. Hapo sauti nyinginezo huongezwa ili kurekebisha, kukuza, na kuimarisha sauti ya awali. Kaakaa la mdomo, ulimi, meno, utaya, na midomo huungana pamoja ili kutawanya mawimbi ya sauti, na kutokeza usemi unaoeleweka.

      Sauti ya mwanadamu ni ajabu sana, na haina kifani ikilinganishwa na chombo chochote kile ambacho binadamu ametengeneza. Ina uwezo wa kuonyesha hisia mbalimbali kama vile upendo na chuki kali. Sauti ikikuzwa na kuzoezwa vizuri, inaweza kubadilikana sana na kutokeza nyimbo tamutamu na semi zinazogusa mioyo.

      KUSHINDA MATATIZO FULANI HUSUSA

      Sauti dhaifu. Sauti ndogo huenda isiwe dhaifu. Ikiwa nzuri na yenye kuvutia, wengine wanaweza kufurahi kuisikiliza. Lakini ni lazima sauti iwe yenye kiasi kinachofaa ili iweze kufaidi wengine.

      Ili uboreshe ukubwa wa sauti yako, unahitaji kuivumisha zaidi. Unahitaji kutuliza mwili wote mzima, kama ilivyoonyeshwa katika somo hili. Pamoja na kutuliza mwili, fanya mazoezi ya kuimba hali umefunga midomo. Midomo inapaswa kugusana kidogo, isishikane sana. Unapoimba kwa njia hiyo, sikia mitikisiko ya wimbo huo akilini na kifuani.

      Nyakati nyingine sauti husikika kuwa dhaifu au kukazika kwa sababu ya ugonjwa au kukosa usingizi. Bila shaka, hali hiyo ikiboreka, sauti itaboreka.

      Sauti inayoinuka juu sana. Mkazo kwenye nyuzi za sauti hufanya sauti iinuke. Sauti yenye mkazo hufanya wasikilizaji wawe na mkazo. Unaweza kupunguza sauti nyembamba kwa kutuliza misuli ya koo ili kupunguza mkazo kwenye nyuzi za sauti. Jaribu kufanya hivyo, ukifanya mazoezi kila siku unapozungumza. Pia ni vizuri kuvuta pumzi kabisa.

      Sauti ya kubana pua. Nyakati nyingine pua iliyofungika hutokeza tatizo hilo, lakini mara nyingi hali hiyo husababishwa na jambo jingine. Nyakati nyingine kwa kukaza misuli ya koo na mdomo, mtu hufunga mianya ya pua na kuzuia hewa isipite vizuri. Jambo hilo hutokeza sauti inayobana pua. Unahitaji kutulia ili kuepuka jambo hilo.

      Sauti nzito na kali. Sauti kama hiyo haitokezi mazungumzo ya kirafiki. Inaweza kutisha wengine.

      Katika hali fulani, jambo muhimu ni kuendelea kujitahidi kubadili utu wako. (Kol. 3:8, 12) Ikiwa tayari umefanya hivyo, kujaribu kutumia kanuni za kurekebisha sauti kunaweza kusaidia. Tuliza koo na taya. Kufanya hivyo kutafanya sauti yako ipendeze zaidi na kufanya maneno mengine yasitokee vibaya kwa kuyalazimisha kupitia meno.

      JINSI YA KUFAULU

      • Kuza sifa za utu wa Kikristo.

      • Fanya mazoezi ya kuvuta pumzi, ukijaza sehemu za chini za mapafu kwa hewa.

      • Unapozungumza, tuliza misuli yako ya koo, shingo, mabega, na mwili wote mzima.

      MAZOEZI: (1) Kwa dakika chache kila siku katika juma, fanya mazoezi ya kuvuta pumzi kabisa mpaka uzijaze sehemu za chini za mapafu yako. (2) Jaribu kutuliza misuli ya koo unapoongea, angalau mara moja kwa siku.

  • Kupendezwa na Wengine
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
    • SOMO LA 30

      Kupendezwa na Wengine

      Unahitaji kufanya nini?

      Unahitaji kuonyesha kwamba unajali maoni na hali za watu wengine.

      Kwa Nini Ni Muhimu?

      Hiyo ni mojawapo ya njia za kuiga upendo wa Yehova, na inaweza kutusaidia kugusa moyo wa mtu.

      MBALI na kuwafundisha watu kweli za Biblia, kuna mambo tunayohitaji kufanya. Ni lazima tuvutie mioyo yao. Mojawapo ya njia za kuvutia mioyo ya watu ni kupendezwa sana nao. Tunaweza kuonyesha upendezi huo kwa njia kadhaa.

      Fikiria Maoni ya Wasikilizaji. Mtume Paulo alifikiria malezi na maoni ya wasikilizaji. Alieleza hivi: “Kwa Wayahudi nilipata kuwa kama Myahudi, ili niweze kuwapata Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria nilipata kuwa kama aliye chini ya sheria, ingawa mimi mwenyewe siko chini ya sheria, ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nilipata kuwa kama aliye bila sheria, ijapokuwa mimi siko bila sheria kuelekea Mungu bali niko chini ya sheria kuelekea Kristo, ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. Kwa walio dhaifu nilipata kuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mambo yote kwa watu wa namna zote, ili nipate kwa vyovyote kuokoa wengine. Lakini nafanya mambo yote kwa ajili ya habari njema, ili nipate kuwa mshiriki wayo pamoja na wengine.” (1 Kor. 9:20-23) Tunawezaje ‘kuwa mambo yote kwa watu wa namna zote’ leo?

      Ukiwatazama wengine hata kwa muda mfupi tu kabla ya kuongea nao, unaweza kuona dalili za mapendezi yao na hali zao. Je, unaweza kutambua kazi zao? dini zao? na hali za familia yao? Kulingana na hali unazoona, je, unaweza kufanya mahubiri yako yawavutie zaidi?

      Ili mahubiri yako yavutie, unahitaji kufikiria mapema jinsi utakavyowafikia watu katika eneo lenu. Katika maeneo mengine, unahitaji kuwafikiria pia watu ambao wametoka nchi za kigeni. Ikiwa watu kama hao wanaishi katika eneo lenu, je, umepata njia bora ya kuwahubiria? Kwa kuwa mapenzi ya Mungu ni kwamba “watu wa namna zote waokolewe na kuja kwenye ujuzi sahihi wa kweli,” basi kusudi lako liwe kutangaza ujumbe wa Ufalme kwa njia inayowavutia watu wote unaokutana nao.—1 Tim. 2:4.

      Sikiliza kwa Makini. Ingawa Yehova ana uwezo wa kujua mambo yote anayotaka kujua, yeye huwasikiliza wengine. Nabii Mikaya alipokea njozi fulani, na katika njozi hiyo Yehova aliwaomba malaika watoe maoni juu ya njia ya kushughulikia jambo fulani. Kisha Mungu akaruhusu mmojawapo wa hao malaika afuate maoni aliyotoa. (1 Fal. 22:19-22) Abrahamu alipohangaika kuhusu hukumu ya Sodoma, Yehova alimsikiliza kwa fadhili. (Mwa. 18:23-33) Tunawezaje kuiga mfano wa Yehova wa kusikiliza tunapokuwa katika huduma?

      Waruhusu wengine watoe maoni. Uliza swali linalofaa, kisha utue kwa muda unaowatosha kujibu. Sikiliza vizuri. Kuwafikiria kwa njia hiyo kutawafanya wazungumze kwa uhuru zaidi. Kama majibu yao yanadokeza jambo fulani linalowapendeza, basi endelea kuuliza maswali kwa njia ya busara. Jaribu kuwafahamu zaidi bila kufanya mazungumzo yawe kama mahoji. Wapongeze sana kwa sababu ya maoni yao. Hata kama hukubaliani nao, uwe mwenye fadhili unapozungumzia maoni yao.—Kol. 4:6.

      Lakini tujihadhari ili kupendezwa kwetu na watu wengine kusivuke mpaka. Kuwajali watu wengine si kuingilia mambo yao ya kibinafsi. (1 Pet. 4:15) Tunahitaji kutahadhari ili mtu wa jinsia tofauti asielewe vibaya upendezi wenye fadhili tunaomwonyesha. Tunahitaji kutumia utambuzi kwa sababu kile kinachoonwa kuwa upendezi unaofaa hutofautiana katika kila nchi, na hata kwa kila mtu.—Luka 6:31.

      Kufanya matayarisho kunaweza kukusaidia kuwa msikilizaji mzuri. Ujumbe wetu ukiwa wazi akilini mwetu, tunakuwa watulivu na tunaweza kuwasikiliza wengine kwa njia ya kawaida. Hiyo inafanya wastarehe na kuwa huru zaidi kuzungumza nasi.

      Ni tendo la heshima kuwasikiliza wengine. (Rom. 12:10) Inathibitisha kwamba tunathamini maoni yao na hisia zao. Wanaweza kutusikiliza kwa makini zaidi tukiwaonyesha heshima. Ndiyo sababu Neno la Mungu linatushauri tuwe ‘wepesi sana juu ya kusikia, wa polepole juu ya kusema.’—Yak. 1:19.

      Wasaidie Wengine Wafanye Maendeleo. Ikiwa tunawajali wengine, tutaendelea kuwafikiria wale wanaopendezwa na kuwatembelea tena ili kuwafundisha kweli za Biblia zinazotimiza mahitaji yao. Unapofikiria ziara inayofuata, kumbuka mambo uliyopata kujua juu yao katika ziara za awali. Tayarisha habari zinazohusu hali zao. Kazia jinsi wanavyoweza kutumia habari hiyo maishani, ukiwasaidia kuona jinsi wanavyoweza kufaidika na mambo wanayojifunza.—Isa. 48:17.

      Ikiwa yule unayezungumza naye anakuambia jambo fulani au tatizo fulani ambalo linamtatiza, hiyo ni nafasi nzuri ya kumhubiria habari njema. Iga mfano wa Yesu ambaye nyakati zote alikuwa tayari kufariji wale waliosononeka. (Mk. 6:31-34) Usitoe suluhisho la haraka-haraka wala usitoe mashauri ya kijuu-juu tu. Mtu huyo anaweza kufikiri hupendezwi naye. Badala yake mwonyeshe huruma. (1 Pet. 3:8) Kisha fanya utafiti katika vichapo vyetu vinavyotegemea Biblia, na umpe habari zenye kumjenga za kumsaidia kukabili hali hiyo. Bila shaka, hutafunua siri zake ikiwa unamjali kwa upendo, ila tu kuwe na sababu nzuri za kuzifunua.—Mit. 25:9.

      Tupendezwe hasa na wanafunzi wetu wa Biblia. Fikiria kupitia sala mahitaji ya kila mwanafunzi, na utayarishe funzo ukikumbuka mahitaji hayo. Jiulize, ‘Yeye anahitaji kufanya nini ili aendelee kufanya maendeleo ya kiroho?’ Kwa upendo, msaidie mwanafunzi kufahamu mambo ambayo Biblia na vichapo vya “mtumwa mwaminifu na mwenye busara” vinasema juu ya jambo hilo. (Mt. 24:45) Nyakati nyingine haitoshi tu kumweleza jambo. Inaweza kufaa kumwonyesha mwanafunzi jinsi ya kutumia kanuni fulani ya Biblia, hata kufanya jambo fulani pamoja naye linaloonyesha jinsi ya kutumia kanuni hiyo.—Yn. 13:1-15.

      Unahitaji usawaziko na busara unapowasaidia wengine wafuate kanuni za Yehova maishani mwao. Watu wana malezi tofauti-tofauti na uwezo mbalimbali, na maendeleo yao hutofautiana. Basi, uwe na usawaziko kuhusu maendeleo yao. (Flp. 4:5) Usiwalazimishe kubadili maisha zao. Acha Neno la Mungu na roho yake iwachochee. Yehova anapenda watu wamtumikie kwa hiari, si kwa kulazimishwa. (Zab. 110:3) Epuka kuwapa maoni yako mwenyewe kuhusu maamuzi ambayo wanapaswa kujifanyia, na hata kama wanakuuliza, uwe mwangalifu usiwafanyie maamuzi.—Gal. 6:5.

      Toa Msaada Unaofaa. Ingawa Yesu alijali sana hali ya kiroho ya wasikilizaji wake, pia alitambua mahitaji yao mengine. (Mt. 15:32) Hata kama sisi si matajiri, tunaweza kuwasaidia kwa njia nyinginezo nyingi.

      Kupendezwa na wengine kunafanya tuwajali. Kwa mfano, kama hali ya hewa inamsumbua mtu unayezungumza naye, nendeni mahali panapofaa zaidi, au panga uendeleze mazungumzo wakati mwingine. Ukimtembelea mtu wakati usiofaa, mwambie utarudi baadaye. Kama jirani au mtu mwingine anayependezwa ni mgonjwa au amelazwa hospitalini, onyesha unamjali kwa kumpelekea kadi au barua fupi au umtembelee. Ikifaa, unaweza pia kumpelekea chakula chepesi au kumtendea fadhili nyinginezo.

      Wanafunzi wa Biblia wanapozidi kufanya maendeleo, wanaweza kuwa na upweke fulani kwa sababu sasa hawatumii wakati mwingi na rafiki zao wa zamani kama walivyozoea kufanya. Uwe rafiki yao. Zungumza nao baada ya funzo la Biblia na nyakati nyinginezo. Watie moyo kuwa na mashirika mazuri. (Mit. 13:20) Wasaidie kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Keti nao mikutanoni, na uwasaidie kushughulikia watoto wao ili wote waweze kufaidika kabisa na mikutano.

      Pendezwa na Watu Kutoka Moyoni. Kupendezwa na watu ni sifa ya moyoni wala si ustadi ambao mtu anajifunza. Kadiri tunavyopendezwa na wengine huonekana katika njia nyingi. Jinsi tunavyosikiliza na pia jambo tunalosema huonyesha kwamba tunapendezwa na wengine. Upendezi huo huonyeshwa na fadhili na jinsi tunavyowajali wengine. Hata wakati hatusemi au kutenda jambo fulani, mtazamo wetu na ishara za uso huonyesha kama tunapendezwa. Ikiwa kwa kweli tunawajali wengine, kwa wazi watatambua tunawajali.

      Sababu muhimu zaidi ya kupendezwa sana na wengine ni kwamba tunaiga upendo na rehema ya Baba yetu wa mbinguni. Hiyo inawasaidia wale wanaotusikiliza wawe na uhusiano wa karibu na Yehova na kufanya wapendezwe na ujumbe ambao ametupa tutangaze. Basi, unapohubiri habari njema, jaribu kufikiria ‘si masilahi ya kibinafsi ya mambo yako mwenyewe tu, bali pia masilahi ya kibinafsi yale ya wengine.’—Flp. 2:4.

      JINSI YA KUPENDEZWA KIKWELI NA WENGINE

      • Sikiliza mtu mwingine anapozungumza. Mshukuru kwa kueleza maoni yake na hisia zake. Uliza maswali ili umwelewe vizuri.

      • Baada ya kuzungumza na mtu huyo, mfikirie. Mtembelee upesi baadaye.

      • Mfundishe kweli za Biblia ambazo zinatimiza mahitaji yake.

      • Msaidie kwa njia mbalimbali. Fikiria mahitaji yake ya wakati huu na ya baadaye.

      MAZOEZI: (1) Kabla ya mkutano wa kutaniko, pendezwa na mtu fulani ambaye amehudhuria. Usimsalimu tu. Jaribu kumfahamu vizuri. Onyesha unamjali. Uwe na mazoea ya kufanya hivyo. (2) Ukiwa katika utumishi wa shambani, pendezwa na mtu unayekutana naye. Usimhubirie tu. Jaribu kumjua vizuri. Jaribu kufanya mambo unayosema na kutenda yafaane na hali unazojua kumhusu. Endelea kutafuta nafasi za kufanya hivyo.

  • Kuwaheshimu Wengine
    Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
    • SOMO LA 31

      Kuwaheshimu Wengine

      Unahitaji kufanya nini?

      Unahitaji kuwajali wengine na kuwaonyesha staha.

      Kwa nini ni muhimu?

      Mkristo ana wajibu wa kuonyesha heshima, na sifa hii inaweza kuwafanya wengine wakubali kwa urahisi ujumbe wako wa Biblia.

      MAANDIKO yanatuambia ‘tuheshimu watu wa namna zote’ na ‘tusiseme kwa ubaya juu ya yeyote.’ (1 Pet. 2:17; Tit. 3:2) Kwa kweli, kila mtu tunayekutana naye ‘amekuja kuwako “katika ufanani wa Mungu.”’ (Yak. 3:9) Kristo alikufa kwa ajili ya kila mtu. (Yn. 3:16) Na watu wote wanahitaji kusikia habari njema na kuzifuata ili waokolewe. (2 Pet. 3:9) Watu wengine wana sifa au mamlaka zinazostahili heshima ya kipekee.

      Kwa nini watu wengine hujaribu kukataa kuonyesha heshima ambayo Biblia inatuhimiza tuonyeshe? Desturi za mahali zinaweza kudai uonyeshe wengine heshima kulingana na jamii yao, rangi, jinsia, afya, umri, utajiri, au cheo chao. Kuenea kwa ufisadi miongoni mwa maafisa wa umma kumefanya wengi wasiheshimu wenye mamlaka. Katika nchi fulani watu hawaridhiki kamwe na hali yao maishani, kwa sababu labda wanafanya kazi kwa saa nyingi sana ili wapate angalau riziki, na wamezingirwa na watu ambao hawana heshima. Vijana hukazwa na rafiki zao kujiunga na maasi dhidi ya walimu wasiopendwa na watu wengine wenye mamlaka. Watu wengi huathiriwa na vipindi vya televisheni vinavyoonyesha jinsi watoto wanavyowazidi akili na kuwaongoza wazazi wao. Tunahitaji kujitahidi sana ili kuzuia mawazo kama hayo ya kilimwengu yasiathiri maoni yetu juu ya wengine. Lakini tunapowaheshimu wengine, inakuwa rahisi kuzungumza nao.

      Kuwafikia Wengine kwa Njia ya Heshima. Mtu anayefanya kazi ya kidini anapaswa kuonyesha heshima kwa kuvaa vizuri na kutenda inavyotakikana. Adabu hutofautiana kulingana na mahali. Wengine huona ni kukosa adabu kuzungumza na mtu ukiwa umevaa kofia au mkono ukiwa mfukoni. Lakini mahali pengine si vibaya kufanya hivyo. Fikiria hali za mahali ili usije ukawaudhi watu. Ukifanya hivyo, unaweza kuepuka mambo yanayoweza kukuzuia usitangaze habari njema kwa njia bora.

      Ndivyo ilivyo na salamu, hasa tunaposalimu watu wenye umri mkubwa. Kwa ujumla, ni kukosa adabu kwa vijana kuwaita watu wazima kwa majina yao ya kwanza ila tu kama wameruhusiwa. Kuna sehemu nyingine ambazo watu wazima pia hawapaswi kuwaita wageni kwa majina ya kwanza. Pia lugha fulani hutumia neno la wingi “nyinyi” au maneno mengine kuonyesha heshima kwa mtu mwenye umri mkubwa au mwenye mamlaka.

      Salamu Zenye Heshima. Katika vijiji fulani unapaswa kumsalimu mtu unayekutana naye, ama njiani au uingiapo katika nyumba. Salamu hizo zinaweza kuwa kuamkiana kidogo, tabasamu, kutikisa kichwa, au kuinua macho. Kutomsalimu mtu huonwa kuwa kukosa heshima.

      Hata hivyo, wengine wanaweza kufikiri unawapuuza hata ingawa umewasalimu. Kwa nini? Kwa sababu wanaona huwajali. Ni kawaida kwa watu kutambulishwa kwa kasoro fulani za mwili. Mara nyingi watu wenye ulemavu fulani na magonjwa hupuuzwa. Lakini, Neno la Mungu linatuonyesha jinsi tunavyopaswa kuwapenda na kuwaheshimu watu kama hao. (Mt. 8:2, 3) Kwa kadiri fulani sisi sote tumeathiriwa na dhambi ya Adamu tuliyorithi. Je, unaweza kuona unaheshimiwa ikiwa nyakati zote wengine wanakutambulisha kwa kasoro zako? Ungefurahi kutambuliwa kwa sifa zako nyingi nzuri, sivyo?

      Heshima inahusu pia kutambua ukichwa. Kuna sehemu ambazo ni lazima uzungumze kwanza na kichwa cha familia kabla ya kuzungumza na wengine katika nyumba hiyo. Ingawa tumeagizwa na Yehova tuhubiri na kufundisha, tunatambua kwamba wazazi ndio wamepewa mamlaka na Mungu ya kuwazoeza watoto wao, kuwatia nidhamu, na kuwaongoza. (Efe. 6:1-4) Basi, tunapozuru nyumba fulani, kwa kawaida ni vizuri kuomba kuzungumza na wazazi kabla ya kuzungumza zaidi na watoto.

      Ni lazima tuwaheshimu wazee kwa sababu kuishi kwingi ni kuona mengi. (Ayu. 32:6, 7) Nchini Sri Lanka, dada mmoja kijana aliye painia alitambua jambo hilo na likamsaidia alipomtembelea mzee fulani. Kwanza yule mzee alikataa kumsikiliza, akisema: “Wewe mtoto unawezaje kunifundisha Biblia?” Lakini akajibu: “Kwa kweli, sikuja kukufundisha bali kukueleza jambo fulani ambalo nilijifunza. Jambo hilo limenifurahisha sana hivi kwamba niliona niwaeleze wengine.” Majibu yenye heshima ya painia huyo yaliamsha upendezi wa mzee. “Basi, niambie, ulijifunza nini?” yule mzee akauliza. “Nimejifunza jinsi ya kuishi milele,” painia akajibu. Mzee huyo akaanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Si wazee wote watadai waheshimiwe, lakini wengi watafurahi wakiheshimiwa.

      Lakini, wengine wanaweza kuonyesha heshima kupita kiasi. Katika visiwa vya Pasifiki na kwingineko, Mashahidi wakitumia salamu za kidesturi zenye heshima wanapomfikia mkuu wa kijiji au mkuu wa kabila fulani, wanaweza kusikilizwa na kuruhusiwa kuzungumza na wakuu hao na raia. Lakini haifai wala si lazima kumsifu mtu kupita kiasi. (Mit. 29:5) Vilevile, lugha fulani inaweza kutumia majina ya heshima, lakini kuonyesha staha ya Kikristo si kutumia kupita kiasi majina hayo ya heshima.

      Kutoa Hotuba kwa Njia ya Heshima. Biblia inatuhimiza tufafanue tumaini letu “kwa tabia-pole na staha yenye kina kirefu.” (1 Pet. 3:15) Kwa hiyo, ingawa ni rahisi kumkosoa mtu mwingine, je, kweli inafaa kumkosoa kwa njia inayomkosesha heshima? Ingefaa kusikiliza kwa subira, na labda kuuliza sababu inayomfanya ahisi hivyo, kisha tufikirie maoni yake tunaposababu naye katika Maandiko, sivyo?

      Tunapokuwa jukwaani tuwaonyeshe wasikilizaji heshima kama ile tunayomwonyesha mtu tunayezungumza naye ana kwa ana. Msemaji mwenye heshima hawachambui wasikilizaji vikali wala hasemi mambo kama: “Mnaweza kufuata shauri hili kama mnataka.” Kuzungumza kwa njia hiyo huvunja wengine moyo. Ni afadhali kuwaona wasikilizaji kuwa watu wanaompenda Yehova na wanaotaka kumtumikia. Tumwige Yesu na kuonyesha fadhili tunaposhughulika na wale ambao wanaweza kuwa dhaifu kiroho, wasio na uzoefu, au ambao hawafuati shauri la Biblia haraka.

      Wasikilizaji hutambua kwamba msemaji anawaheshimu akizungumza kana kwamba yeye mwenyewe anahitaji kufuata Neno la Mungu zaidi. Kwa hiyo, inafaa kuepuka kutumia sana neno “wewe” unapotumia maandiko. Kwa mfano, ebu ona tofauti iliyoko kati ya swali hili, “Je, unajitahidi kadiri uwezavyo?” na sentensi hii “Ni vizuri kila mmoja wetu ajiulize: ‘Je, ninajitahidi kadiri niwezavyo?’” Jambo linalokaziwa na kila mojawapo ya maswali hayo ni lilelile, lakini swali la kwanza linadokeza kwamba msemaji hahusishwi na mazungumzo. Swali la pili linamtia moyo kila mtu, pamoja na msemaji, kuchunguza hali zake mwenyewe na makusudio yake.

      Epuka kujaribu kuchekesha watu eti ili tu wapasue kicheko. Hiyo inafanya ujumbe wa Biblia usiheshimiwe. Ni kweli kwamba tunafurahia utumishi wetu kwa Mungu. Na kunaweza kuwa na sehemu fulani za hotuba zetu ambazo zinaweza kuchekesha. Lakini kufanya mambo mazito kuwa vichekesho hakumheshimu Mungu wala wasikilizaji.

      Salamu zetu, adabu zetu, na usemi wetu nyakati zote na zionyeshe kwamba tunawaona wengine kwa njia ambayo Yehova ametufundisha.

      JINSI YA KUFAULU

      • Tambua jinsi Yehova anavyowaona watu.

      • Tambua ukichwa, umri, na wenye mamlaka.

      • Waruhusu watu wakueleze maoni yao.

      • Elewa wasikilizaji.

      MAZOEZI: Mfikirie mtu ambaye anakuzidi sana kwa umri au unayemzidi sana kwa umri. Fikiria jinsi unavyoweza kumfikia, jambo unaloweza kusema ili kuanzisha mazungumzo, na jambo la kufanya ili kumheshimu na kuheshimu maoni yake. Fanya vile umepanga.

      Jinsi ninavyoweza kuonyesha heshima zaidi

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

      ․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․․

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki