-
Matatizo Yanayoleta TumainiMnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Matatizo Yanayoleta Tumaini
“Katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.”—2 TIMOTHEO 3:1.
JE, UMEWAHI kusikia au kuona mojawapo ya mambo yenye kuhuzunisha yanayofuata?
● Ugonjwa mbaya waua watu wengi.
● Njaa yaua mamia ya watu.
● Tetemeko la nchi laua maelfu ya watu na kuwaacha wengine wengi bila makao.
Katika kurasa zinazofuata, utasoma mambo yatakayofanya ufikirie kwa uzito hali katika ulimwengu leo. Pia utaona kuwa Biblia ilitabiri kwamba hali hizo zingetokea katika kipindi cha wakati kinachoitwa “siku za mwisho.”a
Hata hivyo, kusudi la makala hizi si kukusadikisha kwamba tunaishi katika ulimwengu wenye matatizo mengi. Yaelekea wewe mwenyewe umeyaona. Badala yake, zimekusudiwa kukupa tumaini. Zitaonyesha kwamba kutimia kwa unabii huo unaohusu mambo sita kunaonyesha kuwa “siku za mwisho” zitafikia kikomo hivi karibuni. Makala hizi pia zitazungumzia vipingamizi fulani ambavyo watu hutoa mara nyingi kuhusu siku za mwisho, na zitatoa sababu nzuri za kuthibitisha kwamba hali zitakuwa bora hivi karibuni.
[Maelezo ya Chini]
a Ili kujua ni kwa nini Mungu anaruhusu hali hizi mbaya ziwepo, ona makala “Kwa Nini Mungu Anaruhusu Uovu na Kuteseka?” kwenye ukurasa wa 16 na 17 wa toleo hili.
-
-
Unabii wa 1. Matetemeko ya NchiMnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Unabii wa 1. Matetemeko ya Nchi
“Kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi.”—LUKA 21:11.
● Winnie, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu hivi, anaokolewa kwenye mabaki ya nyumba iliyobomoka nchini Haiti. Wapiga picha wa kituo fulani cha televisheni, wanaoripoti kuhusu msiba huo, walimsikia akilia kwa sauti hafifu chini ya mabomoko hayo. Anaokoka tetemeko hilo, lakini wazazi wake wanakufa.
MAMBO ya HAKIKA YANAONYESHA NINI? Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 300,000 walikufa wakati tetemeko la nchi lenye kipimo cha 7.0 lilipotokea nchini Haiti mnamo Januari (Mwezi wa 1) 2010. Wengine milioni 1.3 waliachwa bila makao kwa ghafula. Ingawa tetemeko hilo lilikuwa kubwa sana, halikuwa ndilo tetemeko pekee duniani. Matetemeko makubwa ya nchi yapatayo 18 yalitokea kote duniani kati ya Aprili (Mwezi wa 4) 2009 na Aprili 2010.
NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Matetemeko ya nchi si mengi kuliko zamani; yanaonekana kuwa mengi kwa sababu tekinolojia ya kisasa inatuwezesha kupata habari nyingi zaidi kuyahusu kuliko hapo zamani.
JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Fikiria jambo hili: Biblia haikazii idadi ya matetemeko ya nchi yanayotokea katika siku za mwisho. Hata hivyo, inasema kuwa “matetemeko makubwa ya nchi” yatatokea “katika mahali pamoja baada ya pengine,” na hivyo kuyafanya kuwa sehemu ya maana ya kipindi hiki muhimu katika historia.—Marko 13:8; Luka 21:11.
UNA MAONI GANI? Je, tunaona matetemeko makubwa ya nchi, kama Biblia ilivyotabiri?
Huenda matetemeko ya nchi pekee yasiwe uthibitisho wa kutosha kuwa tunaishi katika siku za mwisho. Hata hivyo, matetemeko hayo ni sehemu moja tu ya unabii unaotimia. Fikiria unabii wa pili.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Sisi [wanajiofizikia] tunayaita matetemeko makubwa ya nchi. Wengine wanayaita misiba mikubwa.”—KEN HUDNUT, SHIRIKA LA MAREKANI LA UCHUNGUZI WA KIJIOLOJIA.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
© William Daniels/Panos Pictures
-
-
Unabii wa 2. NjaaMnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Unabii wa 2. Njaa
“Kutakuwa na upungufu wa chakula.”—MARKO 13:8.
● Mtu fulani amekimbilia kijiji cha Quaratadji, nchini Niger. Binamu zake na pia ndugu na dada zake, wamekimbilia kijiji hichohicho kutoka sehemu za ndani za nchi hiyo ili kuepuka njaa. Lakini, mtu huyo amelala chini kwenye mkeka akiwa peke yake. Kwa nini? “Hawezi kuilisha [familia yake], hivyo hawezi kuvumilia kutazama hali yao,” anaeleza Sidi, chifu wa kijiji hicho.
MAMBO ya HAKIKA YANAONYESHA NINI? Mtu 1 hivi kati ya kila watu 7 duniani hapati chakula cha kutosha kila siku. Hali ni mbaya hata zaidi katika nchi za Afrika zilizo kusini ya jangwa la Sahara, ambako mtu 1 kati ya kila watu 3 hapati chakula cha kutosha kwa kipindi kirefu. Ili upate kuelewa jambo hilo, fikiria familia yenye baba, mama, na mtoto. Ikiwa chakula kinachopatikana kinatosha tu watu wawili kati yao, ni nani hatakula? Baba, mama, au mtoto? Huo ndio uamuzi ambao familia kama hizo zinalazimika kufanya kila siku.
NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Dunia inatokeza chakula cha kutosha kwa ajili ya kila mtu. Kinachohitajiwa tu ni kusimamia vizuri maliasili za dunia.
JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Ni kweli kwamba wakulima wanaweza kuzalisha na kusafirisha chakula kingi zaidi kuliko zamani. Nazo serikali za wanadamu zinaweza kutatua tatizo la njaa kwa kusimamia vizuri chakula kinachozalishwa duniani. Hata hivyo, kwa miaka mingi zimejaribu kufanya hivyo, lakini zimeshindwa.
UNA MAONI GANI? Je, andiko la Marko 13:8 linatimia? Ingawa hatua kubwa zimepigwa kuhusiana na mambo ya kiteknolojia, je, upungufu wa chakula bado unawaathiri watu duniani kote?
Mara nyingi, matetemeko ya nchi na njaa ni mambo yanayotangulia matatizo ambayo yanatokana na sehemu nyingine ya ishara ya siku za mwisho.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
“Zaidi ya asilimia 33 ya watoto wanaokufa kutokana na nimonia, kuhara, na magonjwa mengine hawangekufa ikiwa wangepata lishe bora.”—ANN M. VENEMAN, ALIYEKUWA MKURUGENZI MKUU WA HAZINA YA WATOTO YA UMOJA WA MATAIFA.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 5]
© Paul Lowe/Panos Pictures
-
-
Unabii wa 3. MagonjwaMnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Unabii wa 3. Magonjwa
“Kutakuwa . . . na magonjwa ya kuambukiza.”—LUKA 21:11, Habari Njema kwa Watu Wote.
● Bonzali, ofisa wa afya katika nchi moja ya Afrika ambayo imekumbwa na vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe, anajitahidi anavyoweza kuwatibu wafanyakazi kwenye mgodi fulani katika mji wa kwao ambao wanakufa kwa ugonjwa wa Marburg.a Maombi yake ya kupata msaada kutoka kwa maofisa walioko jijini yanakosa kujibiwa. Miezi minne baadaye, msaada unafika, lakini Bonzali tayari amekufa. Aliambukizwa ugonjwa wa Marburg na wale wafanyakazi wa migodi aliokuwa anajaribu kuwaokoa.
MAMBO ya HAKIKA YANAONYESHA NINI? Magonjwa yanayoathiri mapafu (kama vile nimonia), magonjwa ya kuharisha, UKIMWI, kifua kikuu, na malaria ni kati ya magonjwa mabaya zaidi yanayomwathiri mwanadamu. Katika mwaka wa 2004 pekee, magonjwa hayo matano yalisababisha vifo vya watu wapatao milioni 10.7. Hilo linamaanisha kwamba magonjwa hayo yalisababisha kifo cha mtu mmoja baada ya kila sekunde tatu, katika mwaka wote mzima.
NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Idadi ya watu duniani inaendelea kuongezeka, hivyo lazima kuwe na visa vingi zaidi vya magonjwa. Kuna watu wengi zaidi wanaoweza kuambukizwa.
JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Idadi ya watu duniani imeongezeka sana. Vivyo hivyo, uwezo wa mwanadamu wa kupima, kudhibiti, na kutibu magonjwa umeongezeka. Hivyo basi, magonjwa na madhara yake kwa mwanadamu yanapaswa kuwa yamepungua. Lakini, mambo ni kinyume cha hayo.
UNA MAONI GANI? Je, watu wanapatwa na magonjwa mabaya kama Biblia ilivyotabiri?
Matetemeko ya nchi, njaa, na magonjwa yanaathiri mamilioni ya watu. Lakini, mamilioni ya wengine huteswa na wanadamu wenzao—wengi wakitendewa vibaya na wale ambao wanapaswa kuwalinda. Ona yale ambayo unabii wa Biblia unasema yangetokea.
[Maelezo ya Chini]
a Homa ya Kuvuja Damu ya Marburg inasababishwa na kirusi kinachohusianishwa na Ebola.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Ni jambo baya sana kuliwa na simba au mnyama mwingine, lakini ni jambo baya vilevile kuliwa kutoka ndani na ugonjwa fulani na kuona wengine pia wakiathiriwa.”—MTAALAMU WA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA, MICHAEL OSTERHOLM.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 6]
© William Daniels/Panos Pictures
-
-
Unabii wa 4. Watu Hawatakuwa na Upendo wa AsiliMnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Unabii wa 4. Watu Hawatakuwa na Upendo wa Asili
“Watu watakuwa . . . wasiowapenda wa kwao.”—2 TIMOTHEO 3:1-3, Union Version.
● Chris anafanya kazi na kikundi cha kuwasaidia watu wanaokabili jeuri nyumbani, huko Wales Kaskazini. “Ninakumbuka mwanamke mmoja ambaye alikuwa amepigwa vibaya sana hivi kwamba nisingeweza kumtambua ingawa nilikuwa nimemwona hapo awali,” anasema Chris. “Wanawake wengine huathiriwa sana kihisia kiasi kwamba hawawezi kuinua macho yao kukutazama.”
MAMBO YA HAKIKA YANAONYESHA NINI? Katika nchi moja barani Afrika, inakadiriwa kwamba mwanamke 1 kati ya kila wanawake 3 alilalwa kinguvu akiwa mtoto. Uchunguzi uliofanywa katika nchi hiyo ulionyesha kwamba zaidi ya asilimia 33 ya wanaume wanaona kwamba ni sawa kuwapiga wake zao. Hata hivyo, si wanawake tu wanaokabili jeuri nyumbani. Kwa mfano, nchini Kanada, karibu wanaume 3 kati ya kila wanaume 10 wamepigwa au kutendewa vibaya na wanawake wanaoishi nao.
NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Jeuri inayotokea nyumbani si jambo jipya, imekuwako sikuzote. Lakini wakati huu inatangazwa zaidi kuliko hapo zamani.
JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Katika miaka ya hivi karibuni, jeuri inayotokea nyumbani imetangazwa sana. Lakini je, jambo hilo limefanya visa vya jeuri inayotokea nyumbani vipungue? Hapana. Watu wasio na upendo wa asili wanazidi kuongezeka.
UNA MAONI GANI? Je, andiko la 2 Timotheo 3:1-3 linatimia? Je, watu wengi wanakosa upendo kwa familia zao, sifa ambayo kiasili wanapaswa kuwa nayo?
Unabii wa tano unaotimia sasa unahusu dunia, makao yetu. Ona yale ambayo Biblia inasema kuhusu jambo hilo.
[Blabu katika ukurasa wa 7]
“Jeuri inayotokea nyumbani ni mojawapo ya mambo yanaripotiwa mara chache sana katika jamii. Mwanamke atashambuliwa mara 35 hivi na mwanamume anayeishi naye kabla ya kuripoti jambo hilo kwa polisi.”—MSEMAJI WA KITUO CHA KUWASAIDIA WATU WANAOTENDEWA JEURI NYUMBANI NCHINI WALES.
-
-
Unabii wa 5. Kuharibiwa kwa DuniaMnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Unabii wa 5. Kuharibiwa kwa Dunia
‘Mungu atawaharibu wale wanaoiharibu dunia.’—UFUNUO 11:18.
● Bw. Pirri ni mgemaji wa pombe ya mnazi huko Kpor, Nigeria. Biashara yake imeharibiwa na mafuta mengi yaliyomwagika kwenye delta ya Mto Niger. “Mafuta hayo yanaua samaki wetu, yanaharibu ngozi yetu, na kuchafua mito yetu,” Pirri anasema. “Sina njia nyingine ya kupata riziki.”
MAMBO ya HAKIKA YANAONYESHA NINI? Wataalamu fulani wanasema kwamba tani milioni 6.5 za takataka huingia baharini kila mwaka. Asilimia 50 hivi ya takataka hizo ni vifaa vya plastiki ambavyo vitaelea baharini kwa mamia ya miaka kabla ya kuoza. Kando na kuchafua dunia, wanadamu wanamaliza maliasili za dunia kwa kiwango kikubwa sana. Uchunguzi unaonyesha kwamba dunia huhitaji mwaka mmoja na miezi mitano ili kutokeza tena maliasili ambayo wanadamu hutumia kwa mwaka mmoja. “Ikiwa idadi ya watu na matumizi ya maliasili yatazidi kuongezeka, basi tutahitaji kuwa na Dunia mbili kufikia mwaka wa 2035,” linaripoti gazeti Sydney Morning Herald la Australia.
NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Wanadamu wana akili na wanaweza kutatua matatizo yao kwa njia nzuri.
JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Vikundi mbalimbali na pia watu mmoja-mmoja wamejitahidi sana kuwaeleza watu umuhimu wa mazingira. Hata hivyo, dunia inaendelea kuchafuliwa kwa kiwango kikubwa sana.
UNA MAONI GANI? Je, kuna uhitaji wa Mungu kuingilia kati na kuiokoa dunia isiharibiwe—kama ambavyo ameahidi kufanya?
Kwa kuongezea mambo hayo matano ambayo yamezungumziwa kuhusu unabii, Biblia pia ilitabiri mambo mazuri ambayo yangetokea siku za mwisho. Ona mfano mmoja katika unabii wa sita.
[Blabu katika ukurasa wa 8]
“Ninahisi kana kwamba nimepoteza paradiso na badala yake kumiliki rundo la takataka zenye sumu.”—MANENO YA ERIN TAMBER, MKAAJI WA PWANI YA MAREKANI, KUHUSU MADHARA YA MAFUTA YALIYOMWAGIKA KWENYE GHUBA YA MEXICO, 2010.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Je, Tumlaumu Mungu?
Kwa kuwa Biblia ilitabiri hali mbaya tunazoona leo, je, hilo linamaanisha kuwa tunaweza kumlaumu Mungu kwa sababu ya hali hizo? Je, yeye ndiye anayesababisha mateso yanayotupata? Unaweza kupata majibu yenye kuridhisha ya maswali hayo katika sura ya 11 ya kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
U.S. Coast Guard photo
-
-
Unabii wa 6. Kazi ya Kuhubiri Katika Dunia YoteMnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Unabii wa 6. Kazi ya Kuhubiri Katika Dunia Yote
“Hii habari njema ya ufalme itahubiriwa katika dunia yote.”—MATHAYO 24:14.
● Vaiatea anaishi kwenye kisiwa kimoja kati ya visiwa vya mbali vya Tuamotu, katika bahari ya Pasifiki. Ingawa visiwa vya Tuamotu ambavyo ni 80 hivi, vimesambaa katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 802,900 za mraba, vina watu wapatao 16,000 tu. Hata hivyo, Vaiatea na jirani zake wametembelewa na Mashahidi wa Yehova. Kwa nini? Kwa sababu Mashahidi wangependa kuwahubiria watu wote habari njema kuhusu Ufalme wa Mungu—hata wawe wanaishi wapi.
MAMBO ya HAKIKA YANAONYESHA NINI? Ujumbe wa Ufalme unaenezwa katika pembe zote za dunia. Katika mwaka wa 2010 pekee, Mashahidi wa Yehova walitumia muda wa saa bilioni 1.6 wakitangaza habari njema katika nchi 236. Kwa hiyo, kila Shahidi alihubiri muda wa dakika 30 hivi kila siku. Katika miaka kumi iliyopita, wametayarisha na kugawa vifaa zaidi ya bilioni 20 vya kuwasaidia watu kuielewa Biblia.
NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Ujumbe wa Biblia umehubiriwa kwa maelfu ya miaka.
JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Ni kweli kwamba watu wengi wamehubiri ujumbe fulani wa Biblia. Hata hivyo, wengi wamefanya hivyo kwa muda mfupi na kwa kiwango kidogo. Kinyume cha hilo, Mashahidi wa Yehova wanashiriki katika kazi iliyopangwa vizuri ya kuhubiri duniani kote, na wameweza kuwafikia mamilioni ya watu. Mashahidi wameendelea na kazi yao ya kuhubiri ingawa wamekabili upinzani kutoka kwa mashirika yenye nguvu na yenye ukatili zaidi katika historia ya wanadamu.a (Marko 13:13) Zaidi ya hayo, Mashahidi wa Yehova hawalipwi ili kuhubiri. Badala yake, wanatumia wakati wao kuhubiri, na wanatoa machapisho yao bila malipo. Kazi yao yote inategemezwa kwa michango ya hiari.
UNA MAONI GANI? Je, “habari njema ya ufalme” inahubiriwa katika dunia yote? Je, kutimia kwa unabii huo kunaweza kumaanisha kwamba kuna mambo mazuri yatakayotokea hivi karibuni?
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi, tazama video hizi tatu: “Faithful Under Trials,” “Purple Triangles,” na “Jehovah’s Witnesses Stand Firm Against Nazi Assault,” ambazo zimetolewa na Mashahidi wa Yehova.
[Blabu katika ukurasa wa 9]
“Maadamu Yehova hajaleta mwisho huo, tutaendelea kuhubiri habari njema ya Ufalme kwa bidii, tukifanya yote tuwezayo ili kuwafikia watu katika maeneo yetu.”—2010 KITABU CHA MWAKA CHA MASHAHIDI WA YEHOVA.
-
-
Hali Zitakuwa Nzuri Hivi Karibuni!Mnara wa Mlinzi—2011 | Mei 1
-
-
Hali Zitakuwa Nzuri Hivi Karibuni!
“Bado muda kidogo tu, na mtu mwovu hatakuwako tena . . . Bali wapole wataimiliki dunia, nao watapata furaha yao tele katika wingi wa amani.”—ZABURI 37:10, 11.
JE, UNGEPENDA kuona unabii ambao umetajwa ukitimia? Bila shaka. Kuna sababu nzuri za kuamini kwamba utatimia hivi karibuni.
Makala zilizotangulia zilizungumzia baadhi ya unabii wa Biblia ambao unaonyesha waziwazi kwamba tunaishi katika “siku za mwisho.” (2 Timotheo 3:1-5) Kupitia roho yake, Mungu aliwaongoza waandikaji wa Biblia watabiri matukio hayo ili tuwe na tumaini. (Waroma 15:4) Kutimia kwa unabii huo kunaonyesha kwamba matatizo tunayokabili sasa yataisha hivi karibuni.
Ni nini kitakachofuata baada ya siku za mwisho? Ufalme wa Mungu utatawala wanadamu wote. (Mathayo 6:9, 10) Ona maelezo ya Biblia kuhusu jinsi hali zitakavyokuwa duniani wakati huo:
● Njaa itaisha. “Kutakuwa na wingi wa nafaka duniani; juu ya milima kutakuwa na mafuriko.”—Zaburi 72:16.
● Magonjwa yataondolewa. “Hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”—Isaya 33:24.
● Dunia itafanywa kuwa mpya. “Nyika na nchi isiyo na maji itafurahi; na nchi tambarare ya jangwani itakuwa na shangwe na kuchanua maua kama zafarani.”—Isaya 35:1.
Hayo ni mambo machache tu ya unabii mwingi wa Biblia ambao utatimia hivi karibuni. Tunakutia moyo uwaombe Mashahidi wa Yehova wakueleze sababu inayofanya wawe na hakika kwamba hali zitakuwa nzuri hivi karibuni.
-