Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Wameipata Safina ya Noa?
    Mnara wa Mlinzi—2009 | Julai 1
    • Biblia inafunua kwamba safina ya Noa ‘ilitua kwenye milima ya Ararati.’ (Mwanzo 8:4) Eneo la Ararati linatia ndani kilele maarufu kinachoitwa sasa Mlima Ararati mashariki mwa Uturuki, karibu na mipaka ya Armenia na Iran.

      Safari nyingi ambazo zimefanywa katika eneo hilo za kutafuta safina ya Noa zimetokeza madai mengi yenye kusisimua, lakini si uthibitisho wenye kusadikisha. Picha zenye kuvutia zilizopigwa kutoka angani, kupatikana kwa vipande vya mbao vilivyopakwa lami, na ripoti za watu wanaodai kwamba waliona safina hiyo zimewachochea watu wajitahidi kutafuta uthibitisho wenye kusadikisha. Hata hivyo, kazi ya kutafuta hiyo safina imekuwa ngumu sana. Eneo moja ambalo linatajwa mara kwa mara linapatikana futi 15,000 hivi juu ya miteremko ya Mlima Ararati. Zaidi ya hayo, kwa sababu ya misukosuko ya kisiasa katika eneo hilo, mara nyingi wasafiri kutoka nchi za kigeni hawapewi kibali cha kupanda mlima huo.

      Hata hivyo, watafiti wengi wenye bidii ya kutafuta safina hiyo wana hamu ya kuona safari nyingi zaidi zikifanywa katika eneo hilo. Wanaamini kwamba vipande vya safina hiyo ambavyo havijaharibika viko kwenye kilele kilichofunikwa na theluji cha Mlima Ararati, vikiwa chini ya theluji na barafu kwa muda mwingi katika mwaka. Lakini wanadai kwamba kuna tumaini la kuiona na kuifikia safina katika miaka yenye joto la kiangazi tu.

      Matumaini hayo yamechochewa na ripoti nyingi. Josephus, mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza W.K., anataja wanahistoria wengi wa mapema ambao walisema kwamba bado safina inaonekana kwa mbali juu ya milima ya Ararati. Hata ilisemekana kwamba watu walichukua sehemu za mbao zilizopakwa lami kuwa kumbukumbu. Kati ya watu waliotajwa na Josephus ni Berossus, Mbabiloni aliyekuwa mwandikaji wa matukio katika karne ya tatu K.W.K.

      Katika karne iliyopita, mojawapo ya ripoti zenye kusisimua ilitoka kwa mwanamume fulani Mwarmenia, George Hagopian. Alisema kwamba alipokuwa kijana mdogo yeye na mjomba wake walienda kuona safina mwanzoni mwa miaka ya 1900 na kwamba hata walipanda ndani ya chombo hicho. Hagopian alikufa mwaka wa 1972, lakini ushahidi wake bado unawasisimua na kuwashangaza watu wengi.

      Je, Ni Msingi wa Kweli wa Imani?

      Je, kuna msingi wa kweli wa kuamini kwamba wachunguzi wameipata safina au huenda wataipata wakati ujao? Labda wataipata, lakini inaonekana kuna mashaka mengi zaidi kuhusu kupatikana kwa safina hiyo. Kwanza kabisa, kumbuka kwamba Biblia haisemi ni wapi hasa safina ilipotua wakati maji ya gharika yalipopungua. Inataja tu “milima ya Ararati.”

      Ni jambo la asili tu kwa wachunguzi na wenye kukisia kuchagua mlima ulio mrefu zaidi katika eneo hilo. Hata hivyo, Maandiko hayasemi moja kwa moja kwamba Mungu alipanga ili safina ije kutua juu ya Mlima Ararati, ambao leo ni mlima mrefu zaidi na wenye barafu ambao kilele chake ni karibu maili tatu juu ya usawa wa bahari.a Kumbuka kwamba Noa na familia yake waliishi ndani ya safina kwa miezi mingi baada ya safina hiyo kutua. (Mwanzo 8:4, 5) Inaelekea pia kuwa ni jambo lisilopatana na akili kufikiri kwamba baada ya kutoka ndani ya safina, wao pamoja na wanyama wengi waliokuwa ndani ya safina walilazimika kuteremka chini kama wapanda-milima wanaotoka kwenye kilele cha juu cha mlima. Labda wakati huo eneo ambako safina ilitua lilikuwa lenye kufikika zaidi kuliko vile wachunguzi fulani wa leo wanavyofikiri, hata hivyo bado ni mrefu vya kutosha kupatana na maelezo ya Mwanzo 8:4, 5. Na haidhuru safina ilitua wapi katika eneo la Ararati, je, si kweli kwamba huenda ilitoweka karne nyingi zilizopita kwa sababu ya kuharibika na kuoza?

  • Je, Wameipata Safina ya Noa?
    Mnara wa Mlinzi—2009 | Julai 1
    • a Mlima ambao unaitwa leo Mlima Ararati ni volkano ambayo haijalipuka tangu mwaka wa 1840. Kilele chake kinafikia mita 5,165 na kinafunikwa na theluji mwaka mzima.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki