-
Je, Unaweza “Kutofautisha Lililo Sahihi na Lililo Kosa Pia”?Mnara wa Mlinzi—2001 | Agosti 1
-
-
Wale Wasemao Kwamba “Uovu Ni Wema na Wema Ni Uovu”
8. (a) Watu hutafuta mashauri wapi? (b) Ni mashauri ya aina gani yanayotolewa?
8 Mambo si tofauti sana leo. Karibu katika nyanja zote ambazo wanadamu wanajitahidi kutimiza mambo fulani, kuna wataalamu wengi. Washauri wa masuala ya ndoa na familia, waandishi wa habari, watu wanaojiita wanatiba, wanajimu, watu wanaowasiliana na roho, na wengineo wako tayari kutoa mashauri kwa kulipwa. Lakini wao hutoa mashauri ya aina gani? Mara nyingi, viwango vya Biblia vya maadili hupuuzwa, na badala yake maadili mapya kukaziwa zaidi. Kwa mfano, ikizungumzia jinsi serikali ilivyokataa kusajili “ndoa za watu wa jinsia moja,” tahariri ya gazeti moja linalozungumzia mambo kwa ujumla nchini Kanada, The Globe and Mail lasema: ‘Katika mwaka wa 2000, ni jambo la upumbavu kukataza wenzi wanaopendana na wanaowajibika kwa mmoja na mwenzake kufunga ndoa kwa sababu tu ni wa jinsia moja.’ Watu wana mwelekeo wa kuvumilia mambo, si kuyachambua. Hakuna sheria dhahiri kuhusu lililo sahihi na lililo kosa; kila jambo linaamuliwa kwa kutegemea matokeo yake.—Zaburi 10:3, 4.
9. Mara nyingi watu wanaoonekana kuwa wenye kuheshimika katika jamii hufanya nini?
9 Wengine huwaona watu ambao wamefanikiwa kijamii na kiuchumi—matajiri na watu mashuhuri—kuwa mifano ya kuigwa wanapofanya maamuzi yao. Ijapokuwa matajiri na watu mashuhuri huonwa kuwa watu wenye kuheshimika katika jamii ya leo, mara nyingi wao hutaja tu unyofu na kutumainika lakini hawadhihirishi sifa hizo. Wengi huvunja au kukwepa kanuni za maadili bila kujali, kusudi wapate mamlaka na faida za kifedha. Ili wapate sifa na wawe mashuhuri, watu fulani hupuuza kanuni na viwango vinavyokubaliwa na hupendelea tabia isiyo ya kawaida na yenye kutisha. Kwa sababu hiyo, kumekuwa na jamii ambayo hutaka kujifaidi na yenye uendekevu, ambayo wito wake ni, “Jambo lolote linaruhusiwa.” Je, inashangaza kwamba watu wametatanika na hawana uhakika kuhusu lililo sahihi na lililo kosa?—Luka 6:39.
10. Maneno ya Isaya kuhusu uovu na wema yamethibitikaje kuwa ya kweli?
10 Tunaona matokeo yenye kuhuzunisha ya maamuzi mabaya yanayofanywa kwa kutegemea mwongozo wenye makosa—ndoa na familia zilizovunjika, matumizi mabaya ya vileo na dawa za kulevya, vikundi vya vijana wenye jeuri, ngono za ovyoovyo, maradhi yanayoambukizwa kingono, kwa kutoa mifano michache tu. Kwa kweli, tunawezaje kutarajia matokeo tofauti na hayo iwapo watu wanapuuza mambo ya msingi yanayokubaliwa kuhusu lililo sahihi na lililo kosa? (Waroma 1:28-32) Ni kama alivyosema nabii Isaya: “Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!
-