Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI
    Amkeni!—2004 | Novemba 22
    • Kutumia Dawa

      Gazeti Time la Septemba 29, 1986, lilikuwa na kichwa hiki, “Kuna Tumaini Katika Pambano Dhidi ya Ukimwi.” “Tumaini” hilo lilitokea wakati dawa ya azidothymidine (AZT) ilipojaribiwa. Hiyo ni dawa ya kudhibiti virusi na inatumiwa kutibu watu wenye virusi vya UKIMWI. Inapendeza kwamba watu wenye virusi vya UKIMWI waliotumia AZT waliishi kwa muda mrefu zaidi. Tangu wakati huo, dawa za kudhibiti virusi zimerefusha maisha ya mamia ya maelfu ya watu. (Ona sanduku “Dawa za Kudhibiti Virusi,” kwenye ukurasa wa 7.) Je, dawa hizo zimefaulu kuwatibu watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI?

      Licha ya msisimko uliotokea baada ya dawa ya AZT kugunduliwa, gazeti Time liliripoti kwamba watafiti wa UKIMWI “walikuwa na uhakika kuwa dawa ya AZT haiwezi kuponya UKIMWI.” Walisema kweli. Wagonjwa fulani waliathiriwa na dawa ya AZT, hivyo dawa nyingine za kudhibiti virusi zikabuniwa. Baadaye, Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani liliidhinisha dawa mbalimbali za kudhibiti virusi zitumiwe pamoja ili kuwatibu wagonjwa walioathiriwa sana na virusi vya UKIMWI. Wafanyakazi wanaowahudumia wagonjwa wa UKIMWI waliyasisimukia matibabu hayo ambayo baadaye yalihusisha kutumia pamoja dawa tatu au zaidi ili kudhibiti virusi. Kwenye mkutano mmoja wa kimataifa kuhusu UKIMWI uliofanywa mwaka wa 1996, daktari mmoja alitangaza kwamba huenda dawa hizo zikaangamiza kabisa virusi vya UKIMWI mwilini!

      Kwa kusikitisha, katika kipindi cha mwaka mmoja, ilionekana wazi kwamba virusi vya UKIMWI haviwezi kukomeshwa hata dawa hizo tatu zinapotumiwa pamoja. Hata hivyo, ripoti moja ya UNAIDS inasema kwamba “kutumia pamoja dawa mbalimbali za kudhibiti virusi kumewawezesha watu walio na virusi vya UKIMWI kuishi maisha marefu zaidi, wajihisi nafuu, na kuendelea na shughuli zao maishani.” Kwa mfano, huko Marekani na Ulaya, matibabu hayo yamepunguza vifo vinavyosababishwa na UKIMWI kwa zaidi ya asilimia 70. Isitoshe, uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba matibabu ya pekee yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi yanaweza kupunguza sana uwezekano wa mama mjamzito kumwambukiza mtoto wake virusi vya UKIMWI.

      Hata hivyo, mamilioni ya watu walio na virusi vya UKIMWI hawapati dawa hizo. Kwa nini?

      “Ugonjwa Unaowakumba Hasa Maskini”

      Dawa za kudhibiti virusi hutumiwa sana katika nchi tajiri. Hata hivyo, Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba katika nchi fulani zinazoendelea, ni asilimia 5 tu ya wagonjwa wanaopata dawa hizo. Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wamefafanua hali hiyo kuwa “ukosefu mkubwa wa haki” na “ukosefu mkubwa wa maadili katika ulimwengu wa leo.”

      Katika nchi fulani, wagonjwa wengine hupata dawa hizo na wengine hawazipati. Gazeti The Globe and Mail linaripoti kwamba Mkanada 1 kati ya Wakanada 3 anayekufa kutokana na UKIMWI, hajawahi kutibiwa kwa dawa za kudhibiti virusi. Hata ingawa dawa hizo hutolewa bila malipo nchini Kanada, watu fulani wamepuuzwa. Gazeti Globe linasema kwamba “wale wasiopata matibabu yanayofaa ndio hasa wanaoyahitaji zaidi, yaani, wenyeji wa asili, wanawake na maskini.” Gazeti The Guardian lilimnukuu mama mmoja Mwafrika ambaye ana virusi vya UKIMWI akisema hivi: “Sielewi kwa nini wanaume wazungu ambao hufanya ngono na wanaume wenzao wanaendelea kuishi nami naelekea kufa!” Tatizo ambalo mama huyo alitaja linahusiana na biashara ya kutengeneza na kugawanya dawa.

      Huko Marekani na Ulaya, matibabu yanayohusisha dawa tatu za kudhibiti virusi hugharimu kwa wastani kati ya dola 10,000 na dola 15,000 kwa mwaka. Ingawa katika nchi fulani zinazoendelea dawa zilizoigwa za matibabu hayo hugharimu dola 300 au chini kwa mwaka, bado watu wengi walio na virusi vya UKIMWI na wanaoishi katika maeneo ambako dawa hizo zinahitajiwa sana hawawezi kuzipata. Dakt. Stine anasema hivi kuhusu hali hiyo: “UKIMWI ni ugonjwa unaowakumba hasa maskini.”

      Biashara ya Kutengeneza Dawa

      Haijawa rahisi kutengeneza dawa zilizoigwa na kuziuza kwa bei ya chini. Katika nchi nyingi kuna sheria kali zinazowakataza watu kutengeneza dawa hizo bila idhini. Msimamizi wa kampuni moja kubwa ya kutengeneza dawa anasema kwamba “hilo ni pambano la kibiashara.” Anasema kwamba kutengeneza dawa zilizoigwa na kuziuza katika nchi zinazoendelea ili kupata faida “ni kuwadhulumu watu waliovumbua dawa hizo.” Pia, makampuni yaliyo na haki ya kutengeneza dawa fulani yanasema kwamba kupungua kwa faida kunaweza kusababisha ukosefu wa pesa za kutosha kugharimia miradi ya utafiti na maendeleo ya kitiba. Wengine wanahofia kwamba dawa za bei ya chini za kudhibiti virusi ambazo zimekusudiwa kupelekwa katika nchi zinazoendelea zinaweza kuuzwa kimagendo katika nchi zilizoendelea.

      Watetezi wa dawa hizo za bei ya chini wanadai kwamba utengenezaji wa dawa mpya unaweza kugharimu kati ya asilimia 5 na asilimia 10 ya gharama zinazopendekezwa na makampuni ya kutengeneza dawa. Pia wanasema kwamba miradi ya utafiti na ya maendeleo inayosimamiwa na makampuni ya kibinafsi ya kutengeneza dawa hupuuza magonjwa yanayokumba nchi maskini. Hivyo, Daniel Berman, msimamizi wa Mradi wa Kuwawezesha Watu Kupata Dawa za Msingi, anasema: “Kunahitajika kuwa na mfumo wa kimataifa wa kupunguza bei za dawa mpya ili watu katika nchi zinazoendelea wazipate.”

      Kutokana na uhitaji huo wa dawa za kudhibiti virusi ulimwenguni pote, Shirika la Afya Ulimwenguni limeanzisha mradi wa kutoa dawa hizo kwa watu milioni tatu walio na virusi vya UKIMWI kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2005. Nathan Ford wa Shirika la Médecins Sans Frontières anasema: “Tunatarajia kwamba mradi huo hautakosa kufaulu kama miradi mingine ya Umoja wa Mataifa. Idadi hiyo ya watu milioni tatu ni nusu tu ya watu waliokadiriwa kuwa wanahitaji matibabu ya UKIMWI leo, nayo itaongezeka sana [kufikia mwaka wa 2005].”

      Vizuizi Vingine

      Hata nchi zinazoendelea zikipata dawa za kutosha za kudhibiti virusi, bado kuna vizuizi vingine. Dawa fulani zinahitaji kumezwa pamoja na maji safi na chakula, lakini mamia ya maelfu ya watu katika nchi kadhaa hula baada ya kila siku mbili. Dawa hizo (mara nyingi tembe 20 au zaidi kwa siku) zinapaswa kumezwa kwa wakati hususa kila siku, lakini wagonjwa wengi hawana saa. Wagonjwa wanapaswa kupewa dawa mbalimbali kulingana na hali zao. Lakini katika nchi nyingi hakuna madaktari wa kutosha. Bila shaka, ni vigumu sana kuwatibu watu kwa dawa za kudhibiti virusi katika nchi zinazoendelea.

      Hata wagonjwa katika nchi zinazoendelea wanakabili matatizo ya kutumia dawa mbalimbali pamoja. Utafiti unaonyesha kwamba watu wengi sana hawamezi dawa zote kwa wakati unaofaa. Hilo linaweza kufanya virusi vianze kukinza dawa. Halafu watu wengine wataambukizwa virusi sugu vya UKIMWI.

      Dakt. Stine anataja tatizo lingine linalowakumba watu walio na virusi vya UKIMWI. Anasema hivi: “Jambo la kushangaza kuhusu matibabu ya virusi vya UKIMWI ni kwamba nyakati nyingine matibabu hayo husababisha maumivu mengi kuliko ugonjwa wenyewe, hasa ugonjwa huo unapoanza kutibiwa kabla ya dalili kuonekana.” Watu walio na virusi vya UKIMWI ambao wanatumia dawa za kudhibiti virusi huathiriwa na matatizo kama vile ugonjwa wa kisukari, kuenea kwa mafuta katika sehemu mbalimbali za mwili tofauti na ilivyokuwa awali, kuongezeka kwa kolesteroli mwilini, na kupungua kwa uzito wa mifupa. Baadhi ya athari hizo zinaweza kusababisha kifo.

  • Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI
    Amkeni!—2004 | Novemba 22
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Dawa za Kudhibiti Virusia

      Katika mwili wa mtu mwenye afya, chembe zinazoitwa helper T huchochea mfumo wa kinga ili upigane na maambukizo. Virusi vya UKIMWI hushambulia chembe hizo hasa. Virusi hivyo hutumia chembe za helper T kutokeza virusi vingine vya UKIMWI, kisha hudhoofisha na kuharibu chembe hizo mpaka mfumo wa kinga unapodhoofika kabisa. Dawa za kudhibiti virusi huzuia virusi hivyo visiongezeke.

      Kwa sasa, dawa nne za kudhibiti virusi zinatumiwa katika matibabu. Dawa zinazoitwa nucleoside analogues na non-nucleoside analogues huzuia virusi vya UKIMWI visiathiri DNA ya mtu. Dawa zinazoitwa protease inhibitors huzuia kimeng’enya fulani kilicho ndani ya chembe zilizoambukizwa kisitokeze virusi vipya vya UKIMWI. Dawa zinazoitwa fusion inhibitors huzuia virusi vya UKIMWI visiingie ndani ya chembe. Kwa kuzuia virusi vya UKIMWI visiongezeke, dawa za kudhibiti virusi zinaweza kumzuia mtu aliye na virusi hivyo asipate UKIMWI haraka, kwani ugonjwa huo hutokea mtu anapokuwa amedhoofishwa kabisa na virusi hivyo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Matibabu yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi hayatolewi kwa watu wote walio na virusi vya UKIMWI. Wale walio na virusi vya UKIMWI au wale wanaodhania kwamba wanavyo wanapaswa kupata ushauri wa wataalamu wa tiba kabla ya kupata matibabu yoyote. Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa.

      [Picha]

      KENYA Daktari anamshauri mgonjwa wa UKIMWI kuhusu dawa za kudhibiti virusi

      [Hisani]

      © Sven Torfinn/Panos Pictures

      [Picha]

      KENYA Mgonjwa wa UKIMWI katika hospitali akipokea dawa za kudhibiti virusi

      [Hisani]

      © Sven Torfinn/Panos Pictures

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki