Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Dawa ya UKIMWI Yahitajiwa Upesi!
    Amkeni!—2004 | Novemba 22
    • Dawa ya UKIMWI Yahitajiwa Upesi!

      Grace huuza viatu vya bei ghali katika Soko Kuu la Lilongwe, huko Malawi. Anaonekana kuwa mwenye furaha na mwenye afya. Hata hivyo, ijapokuwa anatabasamu, ana matatizo makubwa.

      Katika mwaka wa 1993, Grace na mume wake walifurahi sana binti yao Tiyajane alipozaliwa. Mwanzoni, Tiyajane alionekana kuwa mwenye afya. Hata hivyo, muda si muda akaacha kuongeza uzito na kuambukizwa ugonjwa mmoja baada ya mwingine. Tiyajane alikufa kutokana na UKIMWI (ukosefu wa kinga mwilini) akiwa na umri wa miaka mitatu.

      Miaka michache baadaye, mume wa Grace akaanza kuwa mgonjwa pia. Siku moja alizimia na kupelekwa hospitalini. Madaktari walishindwa kumwokoa. Mume wa Grace akafa kutokana na athari za UKIMWI baada ya ndoa yao ya miaka minane.

      Sasa Grace anaishi peke yake katika chumba kimoja kwenye vitongoji vya Lilongwe. Kwa kuwa ana miaka 30, huenda ukamtazamia aanze upya maisha yake. Hata hivyo, Grace anaeleza hivi: “Kwa kuwa nina virusi vya UKIMWI, siwezi kuolewa wala kuzaa.”a

      KWA kusikitisha, kuna visa vingi vya aina hiyo nchini Malawi, ambako inakadiriwa kwamba asilimia 15 ya watu wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Gazeti Globe and Mail linasema kwamba katika hospitali moja ya mashambani “idadi ya wagonjwa wanaolazwa imezidi kiwango cha kawaida kwa asilimia 50, na hospitali hiyo imepoteza zaidi ya nusu ya wafanyakazi” kwa sababu ya UKIMWI. Watu wengi hata zaidi wameambukizwa virusi vya UKIMWI katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Katika mwaka wa 2002, ripoti moja ya Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI (UNAIDS) ilisema hivi: “Kwa sasa, watu katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara wanatarajiwa kuishi miaka 47. Ikiwa UKIMWI haungekuwepo, wangetarajiwa kuishi miaka 62.”

      Hata hivyo, si bara la Afrika tu linalokumbwa na janga la UKIMWI. Mradi wa UNAIDS unakadiria kwamba watu wazima wapatao milioni nne nchini India wana virusi vya UKIMWI. Isitoshe, UNAIDS inasema hivi: “Kwa kuzingatia idadi ya watu walio na virusi vya UKIMWI, inaonekana watu wazima wengi watakufa hasa kutokana na ugonjwa huo katika kipindi hiki cha miaka kumi.” Ugonjwa huo unaenea upesi sana katika mataifa mengi yaliyokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti. Ripoti moja inasema kwamba huko Uzbekistan “idadi ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI mwaka wa 2002 pekee ilizidi ile ya wale walioambukizwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.” Huko Marekani, virusi vya UKIMWI vingali kisababishi kikuu cha vifo vya Wamarekani walio na umri wa kati ya miaka 25 na 44.

      Mfululizo wa kwanza wa makala kuhusu UKIMWI katika gazeti la Amkeni! ulichapishwa mwaka wa 1986. Mwaka huohuo, Dakt. H. Mahler, aliyekuwa msimamizi wa Shirika la Afya Ulimwenguni, alionya kwamba huenda watu milioni kumi hivi tayari wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Miaka 20 hivi baadaye, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI ulimwenguni imeongezeka kufikia milioni 42 hivi. Idadi hiyo inaongezeka mara kumi zaidi ya ongezeko la idadi ya watu! Wataalamu wanasema kwamba hali itazidi kuwa mbaya. UNAIDS inaripoti hivi: “Katika nchi 45 zilizoathiriwa zaidi, inakadiriwa kwamba watu milioni 68 watakufa mapema kutokana na UKIMWI kati ya mwaka wa 2000 na 2020.”

      Kwa kuwa idadi ya watu wanaoambukizwa inaongezeka haraka sana, ni wazi kwamba dawa ya UKIMWI inahitajiwa upesi kuliko wakati mwingine wowote. Hivyo, watafiti wa tiba wamejitahidi juu chini kupambana na virusi vya UKIMWI. Wamepata mafanikio gani? Je, kweli UKIMWI utakwisha?

      [Maelezo ya Chini]

      a Virusi vya UKIMWI huitwa HIV.

      [Blabu katika ukurasa wa 4]

      Ulimwenguni pote, inakadiriwa kwamba watu milioni 42 wana virusi vya UKIMWI; milioni 2.5 ni watoto

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      ◼ INDIA Wahudumu wa afya wa kujitolea wanaelimishwa kuhusu UKIMWI

      [Hisani]

      © Peter Barker/Panos Pictures

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      ◼ BRAZILI Mfanyakazi wa huduma za jamii anamfariji mwanamke anayeugua UKIMWI

      [Hisani]

      © Sean Sprague/Panos Pictures

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      ◼ THAILAND Mfanyakazi wa kujitolea akimtunza mtoto aliyezaliwa akiwa na virusi vya UKIMWI

      [Hisani]

      © Ian Teh/Panos Pictures

  • Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI
    Amkeni!—2004 | Novemba 22
    • Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI

      Katika kitabu chake AIDS Update 2003, Dakt. Gerald J. Stine anasema kwamba utafiti kuhusu UKIMWI ni hatua kubwa sana ya kisayansi. Kwa kipindi kifupi, watafiti wamejifunza mambo mengi sana kuhusu ugonjwa huo wenye kutatanisha sana. Wamepata mafanikio gani?

      UJUZI na utaalamu wa kitiba umewawezesha watafiti kugundua dawa ambazo zikitumiwa pamoja zinaweza kuwasaidia watu walio na virusi vya UKIMWI. Isitoshe, miradi ya kuelimisha watu kuhusu UKIMWI imefanikiwa katika nchi kadhaa. Lakini je, mafanikio hayo yanaonyesha kwamba ugonjwa huo umeanza kukomeshwa? Je, jitihada za kisayansi na za kuwaelimisha watu zinaweza kuzuia kuenea kwa UKIMWI? Fikiria mambo yafuatayo.

      Kutumia Dawa

      Gazeti Time la Septemba 29, 1986, lilikuwa na kichwa hiki, “Kuna Tumaini Katika Pambano Dhidi ya Ukimwi.” “Tumaini” hilo lilitokea wakati dawa ya azidothymidine (AZT) ilipojaribiwa. Hiyo ni dawa ya kudhibiti virusi na inatumiwa kutibu watu wenye virusi vya UKIMWI. Inapendeza kwamba watu wenye virusi vya UKIMWI waliotumia AZT waliishi kwa muda mrefu zaidi. Tangu wakati huo, dawa za kudhibiti virusi zimerefusha maisha ya mamia ya maelfu ya watu. (Ona sanduku “Dawa za Kudhibiti Virusi,” kwenye ukurasa wa 7.) Je, dawa hizo zimefaulu kuwatibu watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI?

      Licha ya msisimko uliotokea baada ya dawa ya AZT kugunduliwa, gazeti Time liliripoti kwamba watafiti wa UKIMWI “walikuwa na uhakika kuwa dawa ya AZT haiwezi kuponya UKIMWI.” Walisema kweli. Wagonjwa fulani waliathiriwa na dawa ya AZT, hivyo dawa nyingine za kudhibiti virusi zikabuniwa. Baadaye, Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani liliidhinisha dawa mbalimbali za kudhibiti virusi zitumiwe pamoja ili kuwatibu wagonjwa walioathiriwa sana na virusi vya UKIMWI. Wafanyakazi wanaowahudumia wagonjwa wa UKIMWI waliyasisimukia matibabu hayo ambayo baadaye yalihusisha kutumia pamoja dawa tatu au zaidi ili kudhibiti virusi. Kwenye mkutano mmoja wa kimataifa kuhusu UKIMWI uliofanywa mwaka wa 1996, daktari mmoja alitangaza kwamba huenda dawa hizo zikaangamiza kabisa virusi vya UKIMWI mwilini!

      Kwa kusikitisha, katika kipindi cha mwaka mmoja, ilionekana wazi kwamba virusi vya UKIMWI haviwezi kukomeshwa hata dawa hizo tatu zinapotumiwa pamoja. Hata hivyo, ripoti moja ya UNAIDS inasema kwamba “kutumia pamoja dawa mbalimbali za kudhibiti virusi kumewawezesha watu walio na virusi vya UKIMWI kuishi maisha marefu zaidi, wajihisi nafuu, na kuendelea na shughuli zao maishani.” Kwa mfano, huko Marekani na Ulaya, matibabu hayo yamepunguza vifo vinavyosababishwa na UKIMWI kwa zaidi ya asilimia 70. Isitoshe, uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba matibabu ya pekee yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi yanaweza kupunguza sana uwezekano wa mama mjamzito kumwambukiza mtoto wake virusi vya UKIMWI.

      Hata hivyo, mamilioni ya watu walio na virusi vya UKIMWI hawapati dawa hizo. Kwa nini?

      “Ugonjwa Unaowakumba Hasa Maskini”

      Dawa za kudhibiti virusi hutumiwa sana katika nchi tajiri. Hata hivyo, Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba katika nchi fulani zinazoendelea, ni asilimia 5 tu ya wagonjwa wanaopata dawa hizo. Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wamefafanua hali hiyo kuwa “ukosefu mkubwa wa haki” na “ukosefu mkubwa wa maadili katika ulimwengu wa leo.”

      Katika nchi fulani, wagonjwa wengine hupata dawa hizo na wengine hawazipati. Gazeti The Globe and Mail linaripoti kwamba Mkanada 1 kati ya Wakanada 3 anayekufa kutokana na UKIMWI, hajawahi kutibiwa kwa dawa za kudhibiti virusi. Hata ingawa dawa hizo hutolewa bila malipo nchini Kanada, watu fulani wamepuuzwa. Gazeti Globe linasema kwamba “wale wasiopata matibabu yanayofaa ndio hasa wanaoyahitaji zaidi, yaani, wenyeji wa asili, wanawake na maskini.” Gazeti The Guardian lilimnukuu mama mmoja Mwafrika ambaye ana virusi vya UKIMWI akisema hivi: “Sielewi kwa nini wanaume wazungu ambao hufanya ngono na wanaume wenzao wanaendelea kuishi nami naelekea kufa!” Tatizo ambalo mama huyo alitaja linahusiana na biashara ya kutengeneza na kugawanya dawa.

      Huko Marekani na Ulaya, matibabu yanayohusisha dawa tatu za kudhibiti virusi hugharimu kwa wastani kati ya dola 10,000 na dola 15,000 kwa mwaka. Ingawa katika nchi fulani zinazoendelea dawa zilizoigwa za matibabu hayo hugharimu dola 300 au chini kwa mwaka, bado watu wengi walio na virusi vya UKIMWI na wanaoishi katika maeneo ambako dawa hizo zinahitajiwa sana hawawezi kuzipata. Dakt. Stine anasema hivi kuhusu hali hiyo: “UKIMWI ni ugonjwa unaowakumba hasa maskini.”

      Biashara ya Kutengeneza Dawa

      Haijawa rahisi kutengeneza dawa zilizoigwa na kuziuza kwa bei ya chini. Katika nchi nyingi kuna sheria kali zinazowakataza watu kutengeneza dawa hizo bila idhini. Msimamizi wa kampuni moja kubwa ya kutengeneza dawa anasema kwamba “hilo ni pambano la kibiashara.” Anasema kwamba kutengeneza dawa zilizoigwa na kuziuza katika nchi zinazoendelea ili kupata faida “ni kuwadhulumu watu waliovumbua dawa hizo.” Pia, makampuni yaliyo na haki ya kutengeneza dawa fulani yanasema kwamba kupungua kwa faida kunaweza kusababisha ukosefu wa pesa za kutosha kugharimia miradi ya utafiti na maendeleo ya kitiba. Wengine wanahofia kwamba dawa za bei ya chini za kudhibiti virusi ambazo zimekusudiwa kupelekwa katika nchi zinazoendelea zinaweza kuuzwa kimagendo katika nchi zilizoendelea.

      Watetezi wa dawa hizo za bei ya chini wanadai kwamba utengenezaji wa dawa mpya unaweza kugharimu kati ya asilimia 5 na asilimia 10 ya gharama zinazopendekezwa na makampuni ya kutengeneza dawa. Pia wanasema kwamba miradi ya utafiti na ya maendeleo inayosimamiwa na makampuni ya kibinafsi ya kutengeneza dawa hupuuza magonjwa yanayokumba nchi maskini. Hivyo, Daniel Berman, msimamizi wa Mradi wa Kuwawezesha Watu Kupata Dawa za Msingi, anasema: “Kunahitajika kuwa na mfumo wa kimataifa wa kupunguza bei za dawa mpya ili watu katika nchi zinazoendelea wazipate.”

      Kutokana na uhitaji huo wa dawa za kudhibiti virusi ulimwenguni pote, Shirika la Afya Ulimwenguni limeanzisha mradi wa kutoa dawa hizo kwa watu milioni tatu walio na virusi vya UKIMWI kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2005. Nathan Ford wa Shirika la Médecins Sans Frontières anasema: “Tunatarajia kwamba mradi huo hautakosa kufaulu kama miradi mingine ya Umoja wa Mataifa. Idadi hiyo ya watu milioni tatu ni nusu tu ya watu waliokadiriwa kuwa wanahitaji matibabu ya UKIMWI leo, nayo itaongezeka sana [kufikia mwaka wa 2005].”

      Vizuizi Vingine

      Hata nchi zinazoendelea zikipata dawa za kutosha za kudhibiti virusi, bado kuna vizuizi vingine. Dawa fulani zinahitaji kumezwa pamoja na maji safi na chakula, lakini mamia ya maelfu ya watu katika nchi kadhaa hula baada ya kila siku mbili. Dawa hizo (mara nyingi tembe 20 au zaidi kwa siku) zinapaswa kumezwa kwa wakati hususa kila siku, lakini wagonjwa wengi hawana saa. Wagonjwa wanapaswa kupewa dawa mbalimbali kulingana na hali zao. Lakini katika nchi nyingi hakuna madaktari wa kutosha. Bila shaka, ni vigumu sana kuwatibu watu kwa dawa za kudhibiti virusi katika nchi zinazoendelea.

      Hata wagonjwa katika nchi zinazoendelea wanakabili matatizo ya kutumia dawa mbalimbali pamoja. Utafiti unaonyesha kwamba watu wengi sana hawamezi dawa zote kwa wakati unaofaa. Hilo linaweza kufanya virusi vianze kukinza dawa. Halafu watu wengine wataambukizwa virusi sugu vya UKIMWI.

      Dakt. Stine anataja tatizo lingine linalowakumba watu walio na virusi vya UKIMWI. Anasema hivi: “Jambo la kushangaza kuhusu matibabu ya virusi vya UKIMWI ni kwamba nyakati nyingine matibabu hayo husababisha maumivu mengi kuliko ugonjwa wenyewe, hasa ugonjwa huo unapoanza kutibiwa kabla ya dalili kuonekana.” Watu walio na virusi vya UKIMWI ambao wanatumia dawa za kudhibiti virusi huathiriwa na matatizo kama vile ugonjwa wa kisukari, kuenea kwa mafuta katika sehemu mbalimbali za mwili tofauti na ilivyokuwa awali, kuongezeka kwa kolesteroli mwilini, na kupungua kwa uzito wa mifupa. Baadhi ya athari hizo zinaweza kusababisha kifo.

      Jitihada za Kuzuia UKIMWI Usienee

      Kumekuwa na mafanikio gani katika jitihada za kuzuia UKIMWI usienee na katika jitihada za kubadili mazoea hatari yanayofanya watu waambukizwe? Imekadiriwa kwamba miradi ya kuwaelimisha watu kuhusu UKIMWI nchini Uganda katika miaka ya 1990, ilipunguza kuenea kwa virusi vya UKIMWI nchini humo kutoka asilimia 14 hadi asilimia 8 katika mwaka wa 2000. Vivyo hivyo, jitihada za Senegal za kuwaelimisha raia zake kuhusu hatari za kuambukizwa virusi vya UKIMWI zimewezesha viwango vya kuenea kwa virusi hivyo visizidi asilimia 1 miongoni mwa watu wazima. Mafanikio hayo yanafurahisha sana.

      Kwa upande mwingine, jitihada za kuwaelimisha watu kuhusu UKIMWI hazijaleta mafanikio makubwa katika nchi nyingine. Uchunguzi uliofanywa mwaka wa 2002 kuhusu vijana 11,000 nchini Kanada ulionyesha kwamba nusu ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule za sekondari waliamini kuna tiba ya UKIMWI. Kulingana na uchunguzi uliofanywa mwaka huohuo nchini Uingereza, asilimia 42 ya wavulana walio kati ya miaka 10 na 11 hawakuwa wamesikia kuhusu UKIMWI. Kwa upande mwingine, vijana wanaojua kwamba kuna UKIMWI na kwamba hauna tiba, hawajali. Daktari mmoja anasema hivi: “Vijana wengi huona UKIMWI kuwa sawa na matatizo ya kawaida yanayowahangaisha kama vile wataishi na nani, ikiwa watapata chakula kizuri, na ikiwa wataenda shule.”

      Basi, si ajabu kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kuwa “huenda kuwalenga vijana kukawa njia bora zaidi ya kupambana na ugonjwa huo, hasa katika nchi zenye watu wengi walioambukizwa.” Vijana wanaweza kusaidiwaje kutii maonyo ambayo wamepewa kuhusu UKIMWI? Je, tunaweza kutarajia kupata dawa ya UKIMWI?

      [Blabu katika ukurasa wa 6]

      Mwaka uliopita, asilimia 2 ya watu wanaohitaji dawa za kudhibiti virusi barani Afrika walizipata, ikilinganishwa na asilimia 84 katika mabara ya Amerika

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

      Dawa za Kudhibiti Virusia

      Katika mwili wa mtu mwenye afya, chembe zinazoitwa helper T huchochea mfumo wa kinga ili upigane na maambukizo. Virusi vya UKIMWI hushambulia chembe hizo hasa. Virusi hivyo hutumia chembe za helper T kutokeza virusi vingine vya UKIMWI, kisha hudhoofisha na kuharibu chembe hizo mpaka mfumo wa kinga unapodhoofika kabisa. Dawa za kudhibiti virusi huzuia virusi hivyo visiongezeke.

      Kwa sasa, dawa nne za kudhibiti virusi zinatumiwa katika matibabu. Dawa zinazoitwa nucleoside analogues na non-nucleoside analogues huzuia virusi vya UKIMWI visiathiri DNA ya mtu. Dawa zinazoitwa protease inhibitors huzuia kimeng’enya fulani kilicho ndani ya chembe zilizoambukizwa kisitokeze virusi vipya vya UKIMWI. Dawa zinazoitwa fusion inhibitors huzuia virusi vya UKIMWI visiingie ndani ya chembe. Kwa kuzuia virusi vya UKIMWI visiongezeke, dawa za kudhibiti virusi zinaweza kumzuia mtu aliye na virusi hivyo asipate UKIMWI haraka, kwani ugonjwa huo hutokea mtu anapokuwa amedhoofishwa kabisa na virusi hivyo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Matibabu yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi hayatolewi kwa watu wote walio na virusi vya UKIMWI. Wale walio na virusi vya UKIMWI au wale wanaodhania kwamba wanavyo wanapaswa kupata ushauri wa wataalamu wa tiba kabla ya kupata matibabu yoyote. Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa.

      [Picha]

      KENYA Daktari anamshauri mgonjwa wa UKIMWI kuhusu dawa za kudhibiti virusi

      [Hisani]

      © Sven Torfinn/Panos Pictures

      [Picha]

      KENYA Mgonjwa wa UKIMWI katika hospitali akipokea dawa za kudhibiti virusi

      [Hisani]

      © Sven Torfinn/Panos Pictures

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

      Wanawake na UKIMWI

      Nusu ya watu wazima walio na virusi vya UKIMWI ni wanawake

      Ilipogunduliwa kwamba wanawake fulani wana ugonjwa wa UKIMWI katika mwaka wa 1982, ilidhaniwa walikuwa wameambukizwa kupitia sindano za dawa za kulevya. Punde baadaye, iligunduliwa kwamba wanawake wanaweza kuambukizwa virusi vya UKIMWI kwa kufanya ngono kama kawaida na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa virusi hivyo. Ulimwenguni pote, nusu ya watu wazima walio na virusi vya UKIMWI ni wanawake. UNAIDS inaripoti hivi: “Ugonjwa huo huwapata hasa wanawake na wasichana waliobalehe ambao huathiriwa kwa urahisi kwa sababu ya hali za kijamii, kitamaduni, kimwili, na kiuchumi, na ambao huwatunza wagonjwa na wale wanaoelekea kufa.”

      Kwa nini watu wanaowahudumia wagonjwa wa UKIMWI wanahangaikia sana jinsi ugonjwa huo ulivyoenea miongoni mwa wanawake? Mara nyingi, wanawake walio na virusi vya UKIMWI hubaguliwa zaidi ya wanaume, hasa katika nchi zinazoendelea. Ikiwa mwanamke ni mjamzito, afya ya mtoto wake imo hatarini; ikiwa ana watoto, inakuwa vigumu kuwatunza, hasa ikiwa hana mume. Isitoshe, kwa kulinganisha, ni mambo machache tu yanayojulikana kuhusu hali za kipekee na matibabu ya wanawake walioambukizwa virusi vya UKIMWI.

      Hali fulani za kitamaduni huwafanya wanawake wakabili hatari kubwa zaidi. Katika nchi nyingi, wanawake hawaruhusiwi kuzungumza kuhusu ngono, nao hukabili hatari ya kubakwa wanapokataa kufanya ngono. Kwa kawaida, wanaume hufanya ngono na wanawake wengi na kuwaambukiza virusi vya UKIMWI bila kujua. Wanaume fulani Waafrika hufanya ngono na wasichana ili kuepuka kuambukizwa virusi hivyo au kwa kuamini kwamba kufanya ngono na mabikira kunaweza kuponya UKIMWI. Si ajabu kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni linasema hivi: “Jitihada zinapaswa kuelekezwa kwa wanaume (na vilevile kwa wanawake) ili kuwalinda wanawake.”

      [Picha]

      PERU Mama aliye na virusi vya UKIMWI akiwa na binti yake ambaye hana virusi hivyo

      [Hisani]

      © Annie Bungeroth/Panos Pictures

      [Picha]

      THAILAND Wanafunzi wanamtembelea mgonjwa wa UKIMWI ili kujifunza kuhusu ugonjwa huo

      [Hisani]

      © Ian Teh/Panos Pictures

      [Picha]

      KENYA Mkutano pamoja na wanachama wa shirika la Wanawake Walio na UKIMWI

      [Hisani]

      © Sven Torfinn/Panos Pictures

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

      Uwongo Kuhusu UKIMWI

      ◼ Watu walio na virusi vya UKIMWI huonekana wagonjwa. Dakt. Gerald J. Stine anasema hivi: “Kwa wastani, inachukua miaka 10 hadi 12 hivi kabla ya mtu aliye na virusi vya UKIMWI kuanza kuugua UKIMWI. Katika kipindi hicho, mtu aliye na virusi hivyo hataonyesha dalili zozote za ugonjwa huo, ingawa anaweza kuwaambukiza watu wengine.”

      ◼ UKIMWI ni ugonjwa wa wanaume wanaofanya ngono na wanaume. Mapema katika miaka ya 1980, UKIMWI ulionwa kuwa ugonjwa wa wanaume wanaofanya ngono na wanaume. Hata hivyo, leo katika sehemu nyingi ulimwenguni, watu huambukizwa virusi vya UKIMWI hasa wanapofanya ngono na watu wa jinsia tofauti.

      ◼ Ngono ya kinywa ni “ngono salama.” Kulingana na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, “uchunguzi mwingi umeonyesha kwamba mtu anaweza kuambukizwa virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa kupitia ngono ya kinywa.” Kuna hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo kupitia aina nyingine za ngono kuliko ilivyo kupitia ngono ya kinywa. Hata hivyo, zoea la kufanya ngono ya kinywa limeenea sana hivi kwamba madaktari fulani wanasema kwamba itakuwa njia moja kuu ya kueneza virusi vya UKIMWI.

      ◼ Kuna dawa ya UKIMWI. Ingawa matibabu yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi yanaweza kuzuia virusi vya UKIMWI visienee haraka katika miili ya wagonjwa fulani na kusababisha UKIMWI, bado hakuna chanjo wala dawa ya ugonjwa huo.

      [Picha]

      CHEKI Kupima damu ili kugundua UKIMWI, unaoweza kutibiwa lakini hauwezi kuponywa

      [Hisani]

      © Liba Taylor/Panos Pictures

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      ZAMBIA Wasichana wawili walio na virusi vya UKIMWI wanasubiri kupewa dawa

      [Hisani]

      © Pep Bonet/Panos Pictures

  • UKIMWI Utakwisha Lini?
    Amkeni!—2004 | Novemba 22
    • UKIMWI Utakwisha Lini?

      Tangu wakiwa wachanga, vijana huathiriwa na habari nyingi kuhusu ngono ambazo huwashawishi kuishi maisha mapotovu. Watu wengi hujidunga sindano za dawa za kulevya ambazo pia hueneza sana virusi vya UKIMWI. Kwa kuwa kuna upotovu mwingi ulimwenguni na maoni ya kutojali, huenda ukajiuliza ikiwa UKIMWI utakwisha.

      KWA kufaa, wataalamu wa afya wanasema kwamba mabadiliko katika tabia za watu ni njia muhimu ya kupambana na UKIMWI. Ripoti moja iliyochapishwa na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa ilisema kwamba “kila kizazi cha vijana kinahitaji kuendelea kuelimishwa sana kuhusu afya na kusaidiwa kujua jinsi ya kuepuka tabia zinazoweza kusababisha waambukizwe virusi vya UKIMWI. Wazazi na walimu wanapaswa kuhusishwa katika miradi hiyo ya kuwaelimisha vijana.”

      Kwa wazi, wazazi wanahitaji kuwaelimisha watoto wao kuhusu hatari hizo kabla hawajapotoshwa na marafiki zao. Hilo si jambo rahisi, lakini linaweza kuokoa uhai wa mtoto wako. Huwezi kuwaharibu watoto wako kwa kuwafahamisha kuhusu ngono na matumizi ya dawa za kulevya. Kuwafahamisha mambo hayo kunaweza kuwazuia wasiharibike.

      Ni Muhimu Wazazi Wawazoeze Watoto Wao

      Wazazi waliomwabudu Mungu nyakati za kale walipaswa kuwafundisha watoto wao kuhusu ngono na jinsi wanavyoweza kutunza afya yao. Kwa kupendeza, sheria ambazo Waisraeli wa kale walipewa zilitia ndani miongozo hususa ya kiadili na vilevile mazoea ambayo walipaswa kuepuka ili wasipatwe na maambukizo. (Mambo ya Walawi 18:22, 23; 19:29; Kumbukumbu la Torati 23:12, 13) Watu wangefundishwaje sheria hizo? Yehova Mungu aliwaambia Waisraeli hivi: “Maneno haya ninayokuamuru leo lazima yawe moyoni mwako.” Kwanza, wazazi walipaswa kuelewa faida za kufuata sheria hizo na madhara ya kutozifuata. Kisha wakaagizwa hivi: “Uyakazie kwa mwana wako na kuyasema unapoketi katika nyumba yako na unapotembea barabarani na unapolala na unapoamka.”—Kumbukumbu la Torati 6:6, 7.

      Neno la Kiebrania linalotafsiriwa ‘kazia’ linamaanisha “kurudia,” “kusema tena na tena,” au “kuingiza.” Bila shaka, wakati unahitajiwa ili kufanya hivyo. Wazazi wanaotenga wakati ili kuwafundisha wana na binti zao kuhusu hatari za matumizi ya dawa za kulevya na ngono haramu, wanaweza kufurahia kuwaona watoto wao wakiepuka tabia zinazoweza kuwafanya waambukizwe virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine.a

      Faraja kwa Wagonjwa wa UKIMWI

      Jitihada za kuzuia UKIMWI haziwafariji sana mamilioni ya watu wenye virusi vya UKIMWI. Zaidi ya athari za kimwili wanazopata, mara nyingi wao hudharauliwa na kuepukwa. Jinsi gani? Watu wengi hufikiri kimakosa kwamba mtu anaweza kuambukizwa virusi vya UKIMWI kwa kumgusa mgonjwa. Tunaweza kuelewa sababu za watu kuogopa kupata UKIMWI, kwani huo ni ugonjwa wa kuambukiza na wa kufisha. Kwa sababu ya kuhofia kupata ugonjwa huo, watu fulani huwaogopa sana wale walio na virusi vya UKIMWI. Wagonjwa wa UKIMWI wamenyimwa matibabu, wamefukuzwa makanisani, na hata kushambuliwa kijeuri.

      Watu fulani wamedai kwamba UKIMWI ni laana ya Mungu kwa waovu. Ni kweli kwamba kufuata viwango vya Biblia kuhusu ngono, dawa za kulevya, na damu kungewazuia watu wengi wasiambukizwe ugonjwa huo. (Matendo 15:28, 29; 2 Wakorintho 7:1) Hata hivyo, Biblia inaonyesha kwamba Mungu hawaletei watu magonjwa ili kuwaadhibu kwa sababu ya dhambi fulani. Badala yake, Biblia husema hivi: “Mungu hawezi kujaribiwa na mambo maovu wala yeye mwenyewe hamjaribu yeyote.” (Yakobo 1:13; Yohana 9:1-3) Mtu aliyeambukizwa UKIMWI kwa sababu ya kutotii viwango vya Biblia kisha akabadili mwenendo wake, anaweza kuwa na hakika kwamba Mungu hajamwacha.

      Mwana wa Mungu, Yesu, alipokuja duniani, alionyesha wazi huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya wagonjwa mahututi. Wakati mmoja Yesu alipokutana na mtu mwenye ukoma, ‘alimsikitikia, naye akanyoosha mkono wake akamgusa.’ Yesu alitumia nguvu zake za kufanya miujiza kumponya mtu huyo mwenye ukoma. (Marko 1:40-42) Yesu hakuwadharau wagonjwa. Upendo wake kwao ulionyesha kikamili upendo wa Baba yake wa mbinguni.—Luka 10:22.

      UKIMWI Utakomeshwa Karibuni!

      Mbali na kutuhakikishia kwamba Mungu anatupenda, maponyo ya kimuujiza ya Yesu hutuhakikishia mengi zaidi. Biblia inatueleza kwamba sasa Yesu Kristo anatawala akiwa Mfalme mbinguni. (Ufunuo 11:15) Huduma yake alipokuwa duniani ilionyesha kwamba ana uwezo na nia ya kuponya magonjwa yote yanayowakumba wanadamu. Atafanya vivyo hivyo.

      Unabii wa Biblia unatuhakikishia kwamba hivi karibuni “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’” (Isaya 33:24) Ijapokuwa wanadamu wameshindwa kuzuia UKIMWI usienee na kushindwa kuwawezesha wagonjwa wote kupata matibabu yanayofaa, tunaweza kuwa na hakika kwamba UKIMWI utakomeshwa. Mfalme Daudi alisema hivi: “Mbariki Yehova, Ee nafsi yangu, wala usiyasahau matendo yake yote, Yeye anayesamehe makosa yako yote, anayeponya magonjwa yako yote.”—Zaburi 103:2, 3.

      Hayo yatatukia lini? Mungu anataka watu wafanye nini ili wapate baraka hizo? Tunakuomba uwasiliane na Mashahidi wa Yehova ili ujifunze mengi zaidi kuhusu ahadi hizo za ajabu za Biblia.

      [Maelezo ya Chini]

      a Wazazi wengi wameona kwamba kitabu Jifunze Kutoka kwa Mwalimu Mkuu, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova, ni kifaa muhimu cha kuwafundisha watoto wachanga hatua kwa hatua kuhusu ngono na kanuni za msingi za maadili.

      [Blabu katika ukurasa wa 11]

      Unabii wa Biblia unatuhakikishia kwamba hivi karibuni “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa’”

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Watoto wako wanaweza kuepuka matatizo ukiwafundisha kuhusu ngono na dawa za kulevya

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Uwezo na nia ya Yesu ya kuwaponya wagonjwa ilionyesha yale atakayofanya wakati ujao

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki