Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • “Ugonjwa Hatari Ambao Umeenea Zaidi Katika Historia Yote”
    Amkeni!—2002 | Novemba 8
    • “Ugonjwa Hatari Ambao Umeenea Zaidi Katika Historia Yote”

      NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

      “Ugonjwa hatari wa UKIMWI unaangamiza watu wengi zaidi kuliko vita yoyote ulimwenguni.” —COLIN POWELL, WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA MAREKANI.

      RIPOTI rasmi ya kwanza kuhusu UKIMWI (ukosefu wa kinga mwilini) ilitolewa mnamo Juni 1981. Peter Piot, mkurugenzi-mkuu wa Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI (UNAIDS) anasema hivi: “Sisi tulioshughulika na ugonjwa wa Ukimwi wakati ulipozuka hatungewazia kwamba ungeenea kwa kiwango kikubwa hivyo.” Katika kipindi cha miaka 20, UKIMWI umekuwa ugonjwa hatari zaidi wa kuambukiza kuwahi kutokea, na inaonekana kwamba utaendelea kuenea.

      Inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni 36 wana virusi vya UKIMWI (HIV), na watu milioni 22 tayari wamekufa kutokana na ugonjwa huo.a Mnamo mwaka wa 2000, watu milioni tatu ulimwenguni pote walikufa kutokana na UKIMWI. Hiyo ndiyo idadi kubwa ya vifo kuwahi kutokea katika mwaka mmoja tangu ugonjwa huo ulipozuka. Vifo hivyo vilitukia licha ya kwamba kuna dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI, hasa katika nchi tajiri.

      UKIMWI Waenea Afrika

      Eneo la Afrika lililoko kusini mwa jangwa la Sahara, ndilo limeathiriwa sana na ugonjwa huo. Inakadiriwa kwamba wakazi milioni 25.3 wa eneo hilo wameambukizwa. Katika eneo hilo peke yake, watu milioni 2.4 walikufa kutokana na UKIMWI katika mwaka wa 2000. Hiyo ni asilimia 80 ya idadi ya wale waliokufa ulimwenguni pote. Ugonjwa wa UKIMWI ndio kisababishi kikuu cha vifo katika eneo hilo.b

      Kati ya nchi zote ulimwenguni, nchi ya Afrika Kusini ndiyo ina idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa. Inakadiriwa kwamba watu milioni 4.7 wameambukizwa. Katika nchi hiyo, watoto 5,000 huzaliwa na virusi vya UKIMWI kila mwezi. Alipokuwa akihutubia Kongamano la 13 la Kimataifa Kuhusu UKIMWI lililofanywa huko Durban mwezi wa Julai 2000, Nelson Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini alisema hivi: “Tulishtuka kugundua kwamba nusu ya vijana wa Afrika Kusini watakufa kutokana na UKIMWI. Jambo lenye kutia hofu hata zaidi ni kwamba maambukizo yote hayo, na mateso yanayosababishwa nayo . . . yangeweza na yanaweza kuzuiwa.”

      UKIMWI Waenea Haraka Katika Nchi Nyingine

      Idadi ya watu wanaoambukizwa inaongezeka haraka katika Ulaya Mashariki, Asia, na Karibea. Mwishoni mwa mwaka wa 1999, watu 420,000 walikuwa wameambukizwa katika Ulaya Mashariki. Mwishoni mwa mwaka wa 2000, ilikadiriwa kwamba idadi hiyo ilikuwa imefikia 700,000.

      Uchunguzi uliofanywa katika majiji makubwa sita ya Marekani ulifunua kwamba asilimia 12.3 ya wanaume vijana wanaofanya ngono na wanaume wenzao wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Isitoshe, ni asilimia 29 tu waliojua kwamba wana virusi hivyo. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza aliyesimamia uchunguzi huo alisema hivi: “Tulisikitika sana kugundua kuwa ni wanaume wachache sana wenye virusi vya UKIMWI ambao walijua kwamba wameambukizwa. Hiyo inamaanisha kwamba watu walioambukizwa hivi majuzi wanaeneza virusi hivyo bila kujua.”

      Kwenye mkutano wa wataalamu wa UKIMWI uliofanywa Mei 2001 huko Switzerland, ugonjwa huo ulitajwa kuwa “ugonjwa hatari zaidi wa kuambukiza kuwahi kutokea.” Kama ilivyotajwa, UKIMWI umeenea zaidi katika eneo la Afrika lililoko kusini mwa jangwa la Sahara. Makala inayofuata inaonyesha sababu.

      [Maelezo ya Chini]

      a Takwimu zilizoonyeshwa ni makadirio yaliyochapishwa na UNAIDS.

      b Ona gazeti la Amkeni! la Februari 22, 2001, ukurasa wa 14-15.

      [Blabu katika ukurasa wa 3]

      “Jambo lenye kutia hofu hata zaidi ni kwamba maambukizo yote hayo, na mateso . . . yangeweza na yanaweza kuzuiwa.”—NELSON MANDELA

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      Watu wengi wenye virusi vya UKIMWI hawajui kwamba wameambukizwa

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      UN/DPI Photo 198594C/Greg Kinch

  • UKIMWI Waenea Katika Afrika
    Amkeni!—2002 | Novemba 8
    • UKIMWI Waenea Katika Afrika

      “Tunakabiliana na msiba mkubwa sana.”

      MANENO hayo ya Stephen Lewis, mwakilishi wa UM wa masuala ya UKIMWI katika Afrika, yanaonyesha jinsi watu wengi wanavyohangaikia janga la UKIMWI katika eneo la Afrika lililoko kusini mwa jangwa la Sahara.

      Mambo kadhaa yanachangia kuenea kwa virusi vya UKIMWI. Na UKIMWI umeongeza matatizo mengine. Mara nyingi, hali zilizo katika nchi fulani za Afrika na katika sehemu nyingine za ulimwengu ambako UKIMWI unaenea sana huhusiana na mambo yafuatayo.

      Maadili. Kwa kuwa virusi vya UKIMWI huenezwa hasa kupitia ngono, ni wazi kwamba ukosefu wa maadili unachangia sana kuenea kwa ugonjwa huo. Hata hivyo, wengi wanaonelea kwamba haiwezekani kuwazuia watu ambao hawajafunga ndoa kufanya ngono. Francois Dufour anaandika hivi katika gazeti la The Star la Johannesburg, Afrika Kusini: “Kuwaonya vijana wasifanye ngono hakuwezi kufua dafu. Kila siku kuna sinema zinazoonyesha mambo ya ngono na jinsi wanavyopaswa kuwa na jinsi wanavyopaswa kutenda.”

      Mwenendo wa vijana unaonyesha wazi jambo hilo. Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa katika nchi moja ulionyesha kwamba theluthi moja hivi ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17 wamewahi kufanya ngono.

      Ubakaji umetajwa kuwa tatizo kubwa nchini Afrika Kusini. Ripoti moja katika gazeti la Citizen la Johannesburg ilisema kwamba ubakaji “umeongezeka sana na kuwa kisababishi kikuu cha madhara ya afya kwa wanawake wa nchi hii na zaidi kwa watoto.” Makala hiyohiyo ilisema hivi: “Visa vya ubakaji wa watoto vimeongezeka maradufu hivi karibuni . . . Matendo hayo yanafanywa eti kwa sababu inaaminika kwamba mtu mwenye virusi vya UKIMWI hupona anapombaka bikira.”

      Magonjwa yanayoambukizwa kingono. Watu wengi wameambukizwa magonjwa hayo katika eneo hilo. Jarida la South African Medical Journal lilisema hivi: “Hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI vinavyoitwa HIV-1 huongezeka mara 2 au hata mara 5 kwa mtu aliye na ugonjwa unaoambukizwa kingono.”

      Umaskini. Nchi nyingi za Afrika zinakumbwa na umaskini, na hilo huchangia sana kuenea kwa UKIMWI. Vitu vinavyoonwa kuwa vya msingi katika nchi zilizoendelea havipatikani katika nchi nyingi zinazoendelea. Jamii nyingi kubwa hazina umeme wala maji safi. Barabara ni chache sana katika maeneo ya mashambani na sehemu nyingine hazina barabara. Wakazi wengi hawana chakula cha kutosha, na hospitali ni chache sana.

      UKIMWI huathiri sana biashara na viwanda. Mapato ya makampuni ya kuchimba migodi yanapungua kadiri wafanyakazi wengi wanavyoambukizwa virusi vya UKIMWI. Makampuni kadhaa yanafikiria njia za kuendesha shughuli fulani kwa mashine ili kulipia hasara hiyo. Katika kampuni moja ya kuchimbua platinamu, ilikadiriwa kwamba idadi ya wafanyakazi wenye ugonjwa wa UKIMWI iliongezeka karibu maradufu mnamo mwaka wa 2000, na asilimia 26 hivi ya wafanyakazi waliambukizwa virusi vya UKIMWI.

      Jambo moja la kusikitisha kuhusu UKIMWI ni kwamba watoto wengi sana huwa mayatima wazazi wao wanapokufa kutokana na ugonjwa huo. Mbali na kupoteza wazazi wao ambao wanawatunza, watoto hao hulazimika kukabiliana na aibu inayohusianishwa na UKIMWI. Mara nyingi watu wa ukoo au watu wa jumuiya huwa maskini sana hivi kwamba hawawezi kusaidia au hawataki kufanya hivyo. Mayatima wengi huacha shule. Wengine huanza ukahaba na hivyo kuchangia kuenea kwa UKIMWI. Nchi kadhaa zimeanzisha miradi ya serikali au ya kibinafsi kuwasaidia mayatima hao.

      Kutojua. Watu wengi hawajui kuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Wengi hawataki kupimwa kwa sababu wanahofu kuaibika na kutengwa wanapojulikana kuwa wana ugonjwa huo. Taarifa moja kwa waandishi wa habari iliyotolewa na Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI (UNAIDS) ilisema hivi: “Watu walio na virusi vya UKIMWI, au wale wanaoshukiwa kuwa navyo wanaweza kukataliwa hospitalini, kutoruhusiwa kukodisha nyumba, kutoajiriwa kazi, kuhepwa na marafiki na wafanyakazi wenzao, kutoruhusiwa kukata bima au kutokubaliwa katika nchi nyingine.” Wengine hata wameuawa ilipogunduliwa kuwa wana virusi vya UKIMWI.

      Utamaduni. Katika tamaduni nyingi za Kiafrika, mara nyingi wanawake hawaruhusiwi kuwauliza wenzi wao kuhusu mahusiano haramu ya ngono, kukataa ngono, au kuwaomba watumie vifaa vya kujikinga na magonjwa yanayoambukizwa kingono. Tamaduni nyingi hupinga kuwapo kwa UKIMWI. Kwa mfano, nyakati nyingine inadaiwa kwamba ugonjwa huo husababishwa na uchawi, na kwamba wachawi wanaweza kuutibu.

      Ukosefu wa hospitali za kutosha. Katika maeneo yenye hospitali chache, tayari hospitali zimejaa kupita kiasi kwa sababu ya UKIMWI. Hospitali mbili kubwa zinaripoti kwamba zaidi ya nusu ya wagonjwa waliolazwa humo wana virusi vya UKIMWI. Afisa mkuu wa tiba katika hospitali moja huko KwaZulu-Natal alisema kwamba idadi ya wagonjwa waliolazwa kwenye vyumba vya wagonjwa inazidi kwa asilimia 40 idadi inayotakikana. Nyakati nyingine, wagonjwa wawili hulazimika kulala kwenye kitanda kimoja, na mgonjwa mwingine hulala sakafuni chini ya kitanda!—South African Medical Journal.

      Tayari hali ni mbaya sana katika Afrika, na inaonekana itakuwa mbaya hata zaidi. Peter Piot wa UNAIDS alisema hivi: “Tungali katika hatua za mwanzo-mwanzo za ugonjwa huo.”

      Ni wazi kwamba katika nchi kadhaa jitihada zinafanywa ili kupambana na ugonjwa huo. Na kwa mara ya kwanza, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilifanya kongamano maalum la kuzungumzia ugonjwa wa UKIMWI mnamo Juni 2001. Je, jitihada za wanadamu zitafanikiwa? Ugonjwa hatari wa UKIMWI utakomeshwa lini?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

      DAWA YA UKIMWI YA NEVIRAPINE NA TATIZO LINALOKUMBA AFRIKA KUSINI

      Dawa ya Nevirapine ni nini? Kulingana na Nicole Itano, ambaye ni mwandishi wa habari, hiyo ni “dawa ya kuzuia utendaji wa virusi ambayo imejaribiwa na ikaonekana kwamba inaweza kupunguza kwa asilimia 50 uwezekano wa mama kumwambukiza mtoto wake UKIMWI.” Kampuni moja ya kutengeneza dawa huko Ujerumani ilijitolea kuipatia nchi ya Afrika Kusini dawa hiyo bila malipo kwa miaka mitano ijayo. Hata hivyo, kufikia Agosti 2001, serikali haikuwa imekubali msaada huo. Tatizo ni nini?

      Watu milioni 4.7 wana virusi vya UKIMWI nchini Afrika Kusini. Hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi ulimwenguni pote. Mnamo Februari 2002, gazeti la The Economist la London liliripoti kwamba Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini “anashuku yale maoni ya kawaida kwamba virusi vya HIV husababisha UKIMWI” na pia “ana shaka kuhusu gharama za dawa zinazozuia utendaji wa virusi vya UKIMWI, athari zake, na ikiwa zinafanya kazi. Hajazipiga marufuku, lakini madaktari wa Afrika Kusini wanavunjwa moyo wasizitumie.” Kwa nini jambo hilo linasababisha hangaiko kubwa? Kwa sababu kila mwaka maelfu ya watoto huzaliwa na virusi vya UKIMWI huko Afrika Kusini na asilimia 25 ya wanawake wajawazito wana virusi hivyo.

      Kwa sababu ya maoni hayo yanayotofautiana, kesi iliwasilishwa mahakamani ili kuilazimisha serikali igawe dawa ya nevirapine. Mahakama ya Sheria ya Afrika Kusini ilitoa uamuzi wake mnamo Aprili 2002. Kulingana na taarifa ambayo Ravi Nessman aliandika katika gazeti la The Washington Post, mahakama hiyo iliamua kwamba “serikali inapaswa kuruhusu dawa hiyo katika taasisi za matibabu ambazo zinaweza kuigawa kwa njia inayofaa.” Ijapokuwa serikali ya Afrika Kusini ilikuwa ikigawanya dawa hiyo katika vituo 18 vya majaribio nchini humo, inasemekana kwamba uamuzi huo umewapa tumaini wanawake wote wajawazito wenye virusi vya UKIMWI katika nchi hiyo.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

      VIRUSI INAYOVAMIA CHEMBE KWA UJANJA

      Hebu fikiria kidogo juu ya virusi ya UKIMWI (HIV) ambayo ni ndogo sana. Mwanasayansi mmoja alisema hivi: “Baada ya kuchunguza kwa miaka mingi chembechembe za virusi kwa hadubini, bado ninastaajabishwa na muundo tata na wenye usahihi kabisa wa kitu hicho kidogo sana.”

      Virusi ni ndogo kuliko bakteria, na bakteria ni ndogo sana kuliko chembe ya mwili wa mwanadamu. Kulingana na kitabu kimoja, virusi ya UKIMWI ni ndogo sana hivi kwamba “chembechembe milioni 230 [za virusi mbalimbali vya UKIMWI] zinaweza kutoshea kwenye alama ya kituo inayomalizia sentensi hii.” Virusi haiwezi kuongezeka bila kuingia katika chembe na kudhibiti utendaji humo.

      Virusi ya UKIMWI inapoingia katika mwili wa mwanadamu, inalazimika kupambana na silaha kali za mfumo wa kinga.a Kinga zinazotia ndani chembe nyeupe za damu hufanyizwa katika uboho wa mfupa. Chembe nyeupe za damu hutia ndani aina mbili kuu za chembe za limfu, zinazoitwa chembe za T na chembe za B. Chembe nyingine nyeupe huitwa fagositi, au “walaji wa chembe.”

      Aina tofauti-tofauti za chembe za T hufanya kazi mbalimbali. Chembe fulani za T (helper T cells) hutimiza daraka muhimu katika pambano hilo kwa kutambua virusi na kutoa habari ili chembe za kushambulia na kuangamiza virusi zifanyizwe. Virusi ya UKIMWI hulenga hasa chembe hizo za T. Chembe nyingine za T (killer T cells) husisimuliwa ili ziharibu chembe za mwili ambazo zimekwisha kushambuliwa. Chembe za B hufanyiza kinga za mwili ambazo hupambana na maambukizo.

      Shambulizi la Ujanja

      Virusi ya UKIMWI imefanyizwa kwa molekuli za RNA (ribonucleic acid) wala si za DNA (deoxyribonucleic acid). Virusi ya UKIMWI ni mojawapo ya virusi vinavyoweza kukaa kwa muda mrefu bila kutenda kabla ya dalili za ugonjwa kuonekana.

      Virusi ya UKIMWI ikiisha kuingia katika chembe ya kiumbe, inaweza kutumia chembe hiyo kutimiza lengo lake. Virusi hiyo “hubadili” DNA ya chembe ili kuzaa virusi vingi vya UKIMWI. Lakini kabla ya kufanya hivyo, ni lazima virusi hiyo itumie mbinu nyingine. Ni lazima ibadili RNA yake kuwa DNA ili iweze kukubaliwa na kueleweka na chembe hiyo. Ili kutimiza hilo, virusi ya UKIMWI hutumia kimeng’enya kinachoitwa reverse transcriptase. Muda si muda, chembe iliyovamiwa hufa, baada ya kufanyiza maelfu ya virusi vya UKIMWI. Virusi hivyo huambukiza chembe nyingine.

      Zile chembe za T zinazotambua virusi zikiisha pungua sana, viini vingine vinaweza kushambulia mwili bila kizuizi chochote. Mwili hushambuliwa na magonjwa na maambukizo ya kila aina. Kufikia hapo, mtu aliyeambukizwa huwa anadhoofishwa kabisa na UKIMWI. Virusi vya UKIMWI vimefaulu kuangamiza mfumo wote wa kinga.

      Hayo ni maelezo sahili. Tunapaswa kukumbuka kwamba bado watafiti hawafahamu mambo mengi kuhusu mfumo wa kinga na utendaji wa virusi vya UKIMWI.

      Kwa miaka 20 hivi, wataalamu hodari wa tiba ulimwenguni pote wametumia ujuzi wao na pesa nyingi kuchunguza virusi hiyo ndogo. Hivyo, wamejifunza mengi kuhusu virusi ya UKIMWI. Dakt. Sherwin B. Nuland, ambaye ni daktari-mpasuaji, alisema hivi miaka kadhaa iliyopita: “Habari ambazo . . . zimekusanywa kuhusu virusi ya UKIMWI na maendeleo yaliyofanywa kukinga mashambulizi yake yanastaajabisha sana.”

      Hata hivyo, ugonjwa hatari wa UKIMWI unazidi kuenea haraka sana.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona gazeti la Amkeni! la Februari 8, 2001, ukurasa wa 13-15.

      [Picha]

      Virusi ya UKIMWI hushambulia chembe za limfu za mfumo wa kinga na kuzibadili ili zifanyize virusi vingi zaidi

      [Hisani]

      CDC, Atlanta, Ga.

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Maelfu ya vijana hutii viwango vya Biblia

  • Je, UKIMWI Utakomeshwa? Ikiwa Ndivyo, Jinsi Gani?
    Amkeni!—2002 | Novemba 8
    • Je, UKIMWI Utakomeshwa? Ikiwa Ndivyo, Jinsi Gani?

      KWA miaka kadhaa watu katika nchi nyingi za Afrika wamepinga kuwepo kwa ugonjwa wa UKIMWI. Watu fulani hata hawataki kuzungumza juu yake. Hata hivyo, katika miaka ya hivi majuzi, jitihada zimefanywa kuwatia watu moyo kuzungumza waziwazi kuhusu ugonjwa huo na kuwaelimisha vijana hasa. Jitihada hizo hazijafaulu sana. Watu wamejikita katika maisha na desturi zao, na ni vigumu kuleta mabadiliko.

      Maendeleo ya Tiba

      Kwa habari ya tiba, wanasayansi wamejifunza mengi kuhusu virusi vya UKIMWI na kuvumbua dawa ambazo zimerefusha maisha ya watu wengi. Dawa tatu za kuzuia utendaji wa virusi zimetumiwa pamoja kwa mafanikio.

      Ijapokuwa dawa hizo haziponyi UKIMWI, zimepunguza idadi ya vifo vya watu wenye virusi vya UKIMWI, hasa katika nchi zilizoendelea. Watu wengi wanasisitiza kwamba ni muhimu dawa hizo zipelekwe katika nchi zinazoendelea. Hata hivyo, dawa hizo ni ghali, na watu wengi katika nchi hizo hawawezi kuzigharimia.

      Jambo hilo limezusha suala hili: Je, faida za kifedha ni muhimu kuliko uhai wa wanadamu? Dakt. Paulo Teixeira, mkurugenzi wa mradi wa Brazili wa kupambana na UKIMWI, aliunga mkono wazo hilo aliposema hivi: “Hatuwezi kuacha maelfu ya watu waumie kutokana na kukosa dawa eti kwa sababu ya faida za kifedha ambazo zinazidi zile zinazopatikana kwa ukawaida.” Aliongeza hivi: “Ninasisitiza sana kwamba faida za kifedha hazipasi kuonwa kuwa muhimu kuliko maadili na wanadamu.”

      Nchi kadhaa zimeamua kutengeneza dawa zisizokuwa na jina rasmi na kuziuza kwa bei ya chini katika nchi nyingine, hivyo zikipuuza sheria za kuzuia uigaji wa dawa zinazotengenezwa na makampuni fulani makubwa.a Uchunguzi mmoja ulioripotiwa katika jarida la South African Medical Journal unaonyesha kwamba “bei za chini kabisa [za dawa hizo zisizokuwa na jina rasmi] zilikuwa asilimia 82 chini ya bei za kawaida za Marekani.”

      Matatizo ya Matibabu

      Baada ya muda, yale makampuni makubwa yenye kibali cha kutengeneza dawa yalianza kuuzia nchi zinazoendelea dawa za UKIMWI kwa bei ya chini zaidi. Kwa kufanya hivyo, ilitumainiwa kwamba watu wengi zaidi wangefaidika kutokana na dawa hizo. Hata hivyo, kuna matatizo mengi makubwa yanayopasa kusuluhishwa ili dawa hizo zipatikane kwa urahisi katika nchi zinazoendelea. Tatizo moja ni gharama. Hata baada ya bei ya dawa hizo kupunguzwa sana, bado watu wengi wanaozihitaji hawawezi kuzigharimia.

      Tatizo jingine ni kwamba si rahisi kutoa dawa hizo kwa kiwango kinachofaa. Tembe nyingi zinapasa kumezwa kila siku kwa wakati maalum. Dawa hizo zisipotumiwa ipasavyo au zikiacha kutumiwa, hilo linaweza kufanyiza virusi sugu vya UKIMWI ambavyo hukinza dawa. Katika mazingira ya Afrika, ni vigumu kuhakikisha kwamba wagonjwa wanatumia kiwango kinachofaa cha dawa mahali ambako hakuna chakula cha kutosha, maji safi, na hospitali za kutosha.

      Isitoshe, wale wanaotumia dawa hizo wanapaswa kupewa uangalifu. Dawa hizo zapasa kubadilishwa zinapoacha kufanya kazi mwilini. Ili kufanya hivyo, wafanyakazi stadi wa huduma za afya wanahitajiwa, na kupimwa kunagharimu pesa nyingi sana. Vilevile, dawa hizo zina athari zake, na virusi fulani sugu vya UKIMWI vimeanza kukinza dawa.

      Kwenye kongamano maalum kuhusu UKIMWI lililofanywa Juni 2001 na Baraza Kuu la UM, ilipendekezwa kwamba kuwe na Hazina ya Afya ya Ulimwenguni Pote ya kusaidia nchi zinazoendelea. Ilikadiriwa kwamba kati ya dola bilioni 7 na bilioni 10 za Marekani zinahitajika. Kufikia sasa, jumla ya fedha ambazo wameazimia kuchanga hazijafikia kiasi kinachotakikana.

      Wanasayansi wana matumaini makubwa ya kupata chanjo, na chanjo tofauti-tofauti zinajaribiwa katika nchi mbalimbali. Hata jitihada hizo zikifua dafu, miaka kadhaa itapita kabla ya chanjo kupatikana, kujaribiwa, na kuthibitishwa kuwa salama kwa ajili ya matumizi ya umma.

      Nchi fulani kama vile Brazili, Thailand, na Uganda, zimefanikiwa sana katika miradi ya matibabu. Dawa zinazotengenezwa huko Brazili zimetumiwa nchini humo kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na UKIMWI kwa asilimia 50. Botswana, ambayo ni nchi ndogo yenye uwezo wa kifedha, inajitahidi kutoa dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI kwa wote wanaozihitaji na vilevile kuandaa huduma za afya.

      Kukomeshwa kwa UKIMWI

      UKIMWI unatofautiana na magonjwa mengine ya kuambukiza katika jambo hili muhimu: Unaweza kuzuiwa. Iwapo watu wako tayari kufuata kanuni za Biblia za msingi, wengi wao, au hata wote, wanaweza kuepuka kuambukizwa.

      Kanuni za Biblia kuhusu maadili ziko wazi. Wale ambao hawajafunga ndoa hawapaswi kufanya ngono. (1 Wakorintho 6:18) Wenzi wa ndoa wanapaswa kuwa waaminifu kwa wenzi wao na hawapaswi kufanya uzinzi. (Waebrania 13:4) Pia, kutii shauri la Biblia kuhusu kujiepusha na damu ni ulinzi.—Matendo 15:28, 29.

      Kwa kujifunza kuhusu ulimwengu usio na magonjwa ambao Mungu anaahidi utakuwepo hivi punde na kwa kutimiza matakwa ya Mungu, wale ambao wamekwisha kuambukizwa wanaweza kupata shangwe nyingi na faraja.

      Biblia inatuhakikishia kwamba hatimaye dhiki zote za wanadamu, kutia ndani magonjwa, zitakwisha. Ahadi hiyo inapatikana katika kitabu cha Ufunuo: “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha ufalme ikisema: ‘Tazama! Hema la Mungu liko pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao, nao watakuwa vikundi vya watu wake. Na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.’”—Ufunuo 21:3, 4.

      Ahadi hiyo hakika si kwa wale tu wanaoweza kugharimia matibabu ya pesa nyingi. Uhakika wa ahadi hiyo ya kiunabii ya Ufunuo sura ya 21 unaimarishwa na andiko la Isaya 33:24: “Hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” Kisha, wote wanaoishi duniani watafuata sheria za Mungu na kufurahia afya kamilifu. Hivyo, ugonjwa hatari wa UKIMWI na magonjwa mengine yote yatakomeshwa kabisa.

      [Maelezo ya Chini]

      a Dawa hizo hutengenezwa kwa kuiga zile zinazotengenezwa na makampuni yaliyo na kibali cha kuzitengeneza. Katika hali za dharura, nchi ambazo ni sehemu ya Shirika la Biashara Ulimwenguni zinaweza kupuuza sheria hizo kuhusu utengenezaji wa dawa.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9, 10]

      HIYO NDIYO DAWA NILIYOKUWA NIKITAFUTA

      Ninaishi kusini mwa Afrika, na nina umri wa miaka 23. Ninakumbuka siku niliyogundua kwamba nina virusi vya UKIMWI.

      Nilikuwa pamoja na mamangu katika chumba cha daktari wakati daktari alipotueleza habari hiyo. Sijawahi kamwe kupata habari mbaya kama hiyo. Nilivurugika. Sikuamini jambo hilo. Nilidhani kwamba huenda matokeo ya maabara yalikuwa na kasoro. Nilipumbaa. Nilitaka kulia, lakini machozi hayakutoka. Daktari alianza kumweleza mamangu kuhusu dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI na mambo mengine, lakini nilikuwa nimeduwaa sana kiasi cha kwamba sikuelewa jambo lolote.

      Nilitambua kuwa labda niliambukizwa na mtu fulani katika chuo kikuu. Nilitaka sana kuongea na mtu yeyote ambaye angeelewa hali yangu, lakini sikujua nizungumze na nani. Nilihisi kuwa sifai na kwamba maisha yangu yameharibika. Ingawa nilitegemezwa na familia yetu, nilikata tamaa na kuogopa sana. Kama ilivyo na vijana wote, nilikuwa na matumaini mengi mno maishani. Ningehitimu kwa digrii ya sayansi baada ya miaka miwili tu, lakini matumaini hayo yalididimia.

      Nilianza kutumia dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI na kwenda kupata ushauri kuhusu ugonjwa huo, lakini bado nilishuka moyo. Nilimwomba Mungu anionyeshe Ukristo wa kweli kabla sijafa. Nilikuwa mshiriki wa kanisa moja la Pentekoste, lakini hakuna hata mshiriki mmoja aliyenitembelea. Nilitaka kujua ukweli kuhusu mahali ambapo ningeenda baada ya kifo.

      Asubuhi moja mwanzoni mwa Agosti 1999, Mashahidi wa Yehova wawili walibisha mlango wangu. Nilikuwa mgonjwa sana siku hiyo, lakini niliweza kuketi sebuleni. Wanawake hao wawili waliniambia majina yao na kusema kwamba wanawasaidia watu kujifunza Biblia. Nilifarijiwa sana kuona sala zangu zikijibiwa hatimaye. Lakini kufikia wakati huo nilikuwa mnyonge sana hivi kwamba singeweza kusoma wala kukaza fikira kwa muda mrefu.

      Hata hivyo, niliwaeleza kwamba ningependa kujifunza Biblia, na wakaahidi kurudi. Lakini kwa kusikitisha, kabla ya wakati huo, nilipelekwa kwenye hospitali ya magonjwa ya akili kwa sababu ya kushuka moyo. Majuma matatu baadaye, niliondoka hospitalini na nilifarijiwa sana kuona kwamba bado Mashahidi hao walinikumbuka. Nakumbuka kwamba mmoja wao aliendelea kunijulia hali. Nilipata nafuu kwa kadiri fulani, na nikaanza kujifunza Biblia mwishoni-mwishoni mwa mwaka huo. Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi kwani nilikuwa mgonjwa mara kwa mara. Lakini yule aliyejifunza nami alielewa na alikuwa mwenye subira.

      Nilisisimuka sana nilipojifunza kuhusu Yehova na sifa zake katika Biblia, na pia maana ya kumjua na kutarajia uhai wa milele. Kwa mara ya kwanza, nilielewa pia kwa nini wanadamu huteseka. Nilipata shangwe nyingi nilipojifunza kuhusu Ufalme wa Mungu, ambao hivi punde utachukua mahali pa serikali zote za wanadamu. Hilo lilinichochea kubadili maisha yangu kabisa.

      Hiyo ndiyo dawa niliyokuwa nikitafuta. Nilifarijika sana kujua kwamba Yehova bado ananipenda na kunijali! Hapo awali, nilifikiri kwamba Mungu ananichukia na ndiyo sababu niliambukizwa ugonjwa huo. Lakini nilijifunza kwamba Yehova alifanya mpango kwa upendo ili tusamehewe dhambi kwa msingi wa dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo. Nikajua kwamba Mungu kweli anajali, kama vile 1 Petro 5:7 inavyosema: ‘Tupeni hangaiko lenu lote juu yake, kwa sababu yeye huwajali nyinyi.’

      Kwa kujifunza Biblia kila siku na kuhudhuria mikutano kwenye Jumba la Ufalme, ninajitahidi niwezavyo kumkaribia Yehova zaidi. Ijapokuwa si rahisi sikuzote, mimi humtupia Yehova mahangaiko yangu kupitia sala na kumwomba nguvu na faraja. Washiriki wa kutaniko hunitegemeza pia, kwa hiyo nina furaha.

      Mimi huhubiri kwa ukawaida pamoja na kutaniko letu. Ninataka kuwasaidia wengine kiroho, hasa wale wanaokabili hali sawa na yangu. Nilibatizwa mnamo Desemba 2001.

      [Picha]

      Nilipata shangwe nyingi nilipojifunza kuhusu Ufalme wa Mungu

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Kikundi cha watu wanaotoa mashauri kuhusu UKIMWI huko Botswana

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Katika dunia Paradiso, watu wote watafurahia afya kamilifu

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki