Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Yehova Amenipa “Nguvu Ipitayo Iliyo ya Kawaida”
    Mnara wa Mlinzi—2002 | Januari 1
    • Mwaka huohuo, nilijuana na John Marks (Markopoulos), mwanamume wa kiroho kutoka Marekani aliyeheshimiwa sana. John alizaliwa kusini mwa Albania, na baada ya kuhamia Marekani, akawa Shahidi wa Yehova. Katika mwaka wa 1950 alikuwa nchini Ugiriki akitafuta kibali cha kuingia Albania—ambayo wakati huo haikuwa inaruhusu watu kuingia humo kwa kuwa ilifuata Ukomunisti kwa dhati. Ingawa John hakuwa ameiona familia yake tangu mwaka wa 1936, hakuruhusiwa kuingia Albania.

  • Yehova Amenipa “Nguvu Ipitayo Iliyo ya Kawaida”
    Mnara wa Mlinzi—2002 | Januari 1
    • Kwa mfano, ujumbe mmoja kutoka Albania uliokuwa umetumwa kwa maandishi ya siri ulisema: “Tuombeeni kwa Bwana. Wanaenda nyumba hadi nyumba na kuchukua vichapo. Hawaturuhusu tujifunze. Watu watatu wamekamatwa.”

      Hivyo, mnamo Novemba 1960 tulifunga safari ya miezi sita kutembelea baadhi ya nchi hizo. Ilikuwa wazi kwamba tungehitaji “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida,” ujasiri kutoka kwa Mungu, na busara ili kutimiza kazi yetu. (2 Wakorintho 4:7) Tulitaka kutembelea nchi ya Albania kwanza. Tulinunua gari jijini Paris na kuanza safari. Baada ya kufika Roma, John peke yake ndiye aliyekubaliwa kuingia Albania. Ilinibidi niende kumngojea huko Athens, Ugiriki.

      John aliingia Albania mwishoni mwa Februari 1961 na kukaa humo hadi mwisho wa mwezi wa Machi. Huko Tiranë alikutana na ndugu 30. Walifurahi kama nini kupata vichapo na kitia moyo walichohitaji sana! Hawakuwa wametembelewa na mtu yeyote kutoka nje ya nchi kwa muda wa miaka 24.

      John alichochewa na uaminifu na uvumilivu wa ndugu hao. Alifahamishwa kwamba wengi walikuwa wamepoteza kazi zao na kufungwa kwa sababu walikataa kushiriki shughuli za kisiasa za nchi hiyo ya Kikomunisti. Aliguswa moyo sana wakati ndugu wawili waliokuwa na umri wa miaka 80 na kitu walipompa mchango wa dola 100 hivi (za Marekani) kwa ajili ya kazi ya kuhubiri. Kwa miaka mingi, walikuwa wakiweka akiba kiasi fulani cha pesa kidogo za uzeeni walizokuwa wakilipwa na serikali.

      John alitakiwa kuondoka Albania Machi 30, 1961—tarehe ya Ukumbusho wa kifo cha Yesu. John alitoa hotuba ya Ukumbusho kwa wasikilizaji 37. Baada ya hotuba kuisha, ndugu walimwongoza John haraka-haraka kupitia mlango wa nyuma na kumsafirisha kwa gari hadi bandari ya Durrës, ambako alipanda meli ya biashara ya Uturuki iliyokuwa inasafiri kwenda Piraiévs (Piraeus), Ugiriki.

  • Yehova Amenipa “Nguvu Ipitayo Iliyo ya Kawaida”
    Mnara wa Mlinzi—2002 | Januari 1
    • Hatimaye ilibidi jitihada mpya zifanywe ili kuwasiliana na ndugu zetu huko Albania. Kwa kuwa jamaa za mume wangu waliishi huko, niliulizwa kama ningependa kwenda huko. Bila shaka singekataa kwenda!

      Baada ya kujitahidi kwa miezi mingi, nilipata kibali cha kuingia Albania kutoka ofisi ya ubalozi wa nchi hiyo huko Athens Mei 1986. Wafanyakazi wa Ubalozi huo walinionya vikali kwamba mambo yakienda mrama, nisitarajie kupata msaada kutoka nje ya nchi hiyo. Msimamizi wa ofisi za kuuzia tikiti za ndege alishangaa sana nilipomwendea ili kulipa nauli ya kwenda Albania. Sikuruhusu woga unizuie, hivyo baada ya muda mfupi nilikuwa kwenye ndege pekee iliyosafiri kutoka Athens kwenda Tiranë mara moja kwa juma. Ndani ya ndege hiyo mlikuwemo Waalbania watatu wazee sana ambao walikuwa wameenda Ugiriki kutibiwa.

      Mara tu ndege ilipotua, nilipelekwa kwenye kibanda kisichokuwa na kitu kilichotumiwa kama ofisi ya forodha. Ndugu na dada ya mume wangu, ambao hawakuwa Mashahidi wa Yehova, walikuwa tayari kunisaidia kuwasiliana na ndugu wachache huko Albania. Sheria iliwataka wajulishe mkuu wa jumuiya kuhusu kuwasili kwangu. Kwa hiyo, nilikuwa chini ya upelelezi mkali wa polisi. Hivyo, jamaa zangu wakapendekeza nikae nyumbani kwao nao wakaenda wakitafuta ndugu wawili walioishi Tiranë na kuwaleta nyumbani.

      Wakati huo, kulikuwa na ndugu tisa tu waliojiweka wakfu nchini Albania. Kwa sababu ya marufuku ya miaka mingi, kunyanyaswa, na upelelezi mkali, ndugu hao walikuwa wenye tahadhari sana. Nyuso zao zilikuwa zimekunjamana. Baada ya kuwahakikishia ndugu hao wawili kwamba sikuwa mpelelezi, swali lao la kwanza lilikuwa: “Wapi magazeti ya Mnara wa Mlinzi?” Kwa miaka mingi walikuwa na nakala mbili tu za vitabu fulani vya zamani—hawakuwa hata na Biblia.

      Walinieleza kwa kirefu jinsi serikali ilivyokuwa inawatendea kikatili. Walitaja kisa cha ndugu mmoja mpendwa ambaye aliazimia kutounga mkono upande wowote kisiasa katika uchaguzi fulani uliokuwa unakaribia. Kwa kuwa Serikali ndiyo iliyosimamia kila kitu, hiyo ilimaanisha kwamba familia yake haingepata chakula. Watoto wake na familia zao wangefungwa gerezani, japo hawakuwa Mashahidi. Ilisemekana kwamba kwa sababu ya kuogopa, watu wa familia ya ndugu yake walimwua usiku uliotangulia uchaguzi huo, wakatupa mwili wake ndani ya kisima, kisha wakadai kwamba alijiua kwa sababu ya woga.

      Hali ya umaskini ya hao Wakristo wenzetu ilikuwa ya kusikitisha. Hata hivyo, nilipojaribu kuwapa kila mmoja wao dola 20 za Marekani, walikataa na kusema, “Tunataka tu chakula cha kiroho.” Ndugu hao wapendwa walikuwa wameishi kwa miaka mingi chini ya serikali ya kimabavu ambayo ilikuwa imefanikiwa kusadikisha raia wengi waamini kwamba hakuna Mungu. Lakini walikuwa na imani na azimio lenye nguvu sawa na Mashahidi wengine katika nchi nyingine. Wakati nilipoondoka Albania majuma mawili baadaye, nilikuwa nimeamini kabisa kwamba Yehova anaweza kutoa “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida,” hata chini ya hali ngumu sana.

      Nilikuwa na pendeleo la kutembelea Albania tena mwaka wa 1989 na mwaka wa 1991. Watu walipopata uhuru zaidi wa kusema na kuabudu nchini humo, waabudu wa Yehova waliongezeka haraka. Wakristo wachache waliojiweka wakfu ambao walikuwa humo mwaka wa 1986 sasa wameongezeka na kuwa wahubiri 2,200 wenye bidii. Melpo, dada ya mume wangu, alikuwa mmoja wao. Hatuna shaka kwamba Yehova alibariki kikundi hicho cha ndugu waaminifu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki