-
Ni Nani Atakayeutawala Ulimwengu?Sikiliza Unabii wa Danieli!
-
-
MTAWALA MCHANGA AUSHINDA ULIMWENGU
MIAKA 2,300 hivi iliyopita, jenerali wa kijeshi mwenye nywele za manjano, mwenye umri wa miaka 20 na kitu alisimama ukingoni mwa Bahari ya Mediterania. Alikaza macho yake kwenye jiji lililokuwa kisiwa umbali wa karibu kilometa moja. Akiwa amekatazwa kuingia, jenerali huyo mwenye hasira aliazimu kulishinda jiji hilo. Alipanga kushambuliaje? Alipanga kujenga barabara iliyoinuka juu kwenye maji hadi kisiwani na kuyapanga majeshi yake yakapige vita dhidi ya jiji hilo. Ujenzi wa barabara hiyo tayari ulikuwa umeanza.
Lakini ujumbe kutoka kwa mfalme mkuu wa Milki ya Uajemi ulimkatiza jenerali huyo kijana. Akitaka sana kufanya amani, mtawala wa Uajemi aliahidi jambo lisilo la kawaida: Talanta 10,000 za dhahabu (zaidi ya dola bilioni mbili za Marekani kwa thamani ya kisasa), aoe mmoja wa binti za mfalme, na sehemu yote ya magharibi ya Milki ya Uajemi. Mfalme aliahidi yote hayo ili kuipata familia yake, ambayo jenerali huyo alikuwa ameiteka.
Kamanda aliyepaswa kuamua kukubali au kukataa toleo hilo alikuwa Aleksanda wa Tatu wa Makedonia. Je, akubali toleo hilo? “Ilikuwa pindi muhimu kwa ulimwengu wa kale,” asema mwanahistoria Ulrich Wilcken. “Matokeo ya uamuzi wake, kwa kweli, yameenea katika Enzi za Kati hadi siku zetu wenyewe, Mashariki na vilevile Magharibi.” Kabla ya kufikiria jibu la Aleksanda, acheni tuone ni matukio gani yaliyotangulia pindi hiyo muhimu.
MALEZI YA ALEKSANDA
Aleksanda alizaliwa Pella, Makedonia, mwaka wa 356 K.W.K. Baba yake alikuwa Mfalme Philip wa Pili, na mama yake alikuwa Olympias. Aleksanda alifundishwa na mama yake kwamba wafalme wa Makedonia walitokana na Hercules, mwana wa mungu wa Wagiriki, Zeus. Kulingana na Olympias, Achilles—yule mhusika mkuu wa shairi la Homer liitwalo Iliad—alikuwa babu wa zamani wa Aleksanda. Baada ya kufundishwa hivyo na wazazi wake kwa ajili ya ushindi na utukufu wa kifalme, Aleksanda mchanga hakupendezwa sana na mambo mengine. Alipoulizwa ikiwa angekimbia mbio fulani kwenye Michezo ya Olimpiki, Aleksanda alidokeza kwamba angekimbia iwapo tu angekimbia na wafalme. Alikuwa na tamaa ya kufanya mambo makuu kuliko baba yake na kupata utukufu kupitia mambo aliyotimiza.
Akiwa na umri wa miaka 13, Aleksanda alifundishwa na Aristotle, mwanafalsafa Mgiriki, ambaye alimsaidia kukuza upendezi katika falsafa, tiba, na sayansi. Watu wana maoni tofauti juu ya kiwango ambacho mafundisho ya Aristotle ya falsafa yaliathiri njia ya kufikiri ya Aleksanda. “Yaelekea kuwa sahihi kusema kwamba kuna mambo mengi ambayo watu hao wawili hawakukubaliana,” akaonelea Bertrand Russell, mwanafalsafa wa karne ya 20. “Maoni ya kisiasa ya Aristotle yalitegemea serikali za jiji za Ugiriki zilizokuwa zikielekea kutoweka.” Ile dhana ya serikali ndogo ya jiji haingemvumtia mwana-mfalme mwenye kutaka makuu aliyetaka kujenga milki kubwa yenye utawala mmoja. Lazima Aleksanda alitilia shaka sera ya Aristotle ya kuwatumikisha wasio Wagiriki kwa kuwa alitarajia milki yenye ushirikiano mzuri kati ya washindi na washinde.
Hata hivyo, hakuna shaka kwamba Aristotle alikuza kupendezwa kwa Aleksanda katika kusoma na kujifunza. Aleksanda aliendelea kuwa msomaji mwenye bidii katika maisha yake yote, akipendezwa hasa na maandishi ya Homer. Yadaiwa kwamba alikariri mistari yote 15,693 ya shairi liitwalo Iliad.
Kuelimishwa na Aristotle kulikoma ghafula mwaka wa 340 K.W.K. wakati ambapo mwana-mfalme huyo mwenye umri wa miaka 16 alirudi Pella akatawale Makedonia kwa kuwa baba yake hakuwako. Upesi, mrithi huyo wa kiti cha ufalme akaonyesha uhodari wake kivita. Alilikomesha haraka Maedi, kabila la Thrasi lililoasi, akateka jiji lao kuu mara moja, na kupaita mahali hapo Alexandroúpolis, kutokana na jina lake mwenyewe, jambo lililomfurahisha sana Philip.
KUENDELEA NA USHINDI
Aleksanda alirithi kiti cha ufalme cha Makedonia mwaka wa 336 K.W.K., akiwa na umri wa miaka 20 Philip alipouawa. Akiingia Asia kupitia Hellespont (paitwapo Dardanelles leo) mapema Mei mwaka wa 334 K.W.K., Aleksanda alianzisha kampeni ya ushindi akiwa na jeshi dogo lakini hodari la askari-jeshi 30,000 wa miguu na askari wapanda-farasi 5,000. Wahandisi, mabwana-pima, wasanifuujenzi, wanasayansi, na wanahistoria waliandamana na jeshi lake.
Kwenye Mto Granicus upande wa kaskazini magharibi mwa Asia Ndogo (leo inaitwa Uturuki), Aleksanda alishinda vita yake ya kwanza dhidi ya Uajemi. Katika kipindi cha majira ya baridi kali cha wakati huo alishinda sehemu ya magharibi ya Asia Ndogo. Katika masika ya mwaka wa 333 K.W.K. vita vingine vya kukata maneno dhidi ya Uajemi vilipiganwa Issus, upande wa kusini-mashariki mwa Asia Ndogo. Akiwa na jeshi la watu wapatao nusu milioni, Mfalme mkuu wa Uajemi, Dario wa Tatu, akaja kupigana na Aleksanda. Akiwa na uhakika kupita kiasi, Dario akaja pia na mama yake, mke wake, na washiriki wengine wa familia yake ili washuhudie kile ambacho kilipaswa kuwa ushindi mkubwa ajabu. Lakini Waajemi hawakuwa tayari kukabili shambulio la Wamakedonia la ghafula na lenye nguvu. Majeshi ya Aleksanda yalilishinda kabisa jeshi la Uajemi, na Dario akakimbia, akaiacha familia yake mikononi mwa Aleksanda.
Badala ya kuwafuata Waajemi waliokuwa wakikimbia, Aleksanda alielekea kusini kandokando ya Pwani ya Mediterania, akishinda vituo vilivyotumiwa na meli zenye nguvu za Uajemi. Lakini Tiro, kisiwa kilichokuwa jiji, kilikinza uvamizi. Akiwa ameazimia kulishinda, Aleksanda alianza mazingiwa yaliyodumu miezi saba. Wakati wa mazingiwa hayo ndipo Dario alipotoa ahadi iliyotajwa awali. Mambo yaliyoahidiwa yalikuwa yenye kuvutia sana hivi kwamba Parmenio, mshauri ambaye Aleksanda alimtumaini, aripotiwa kuwa alisema: ‘Ningalikuwa Aleksanda, ningalikubali.’ Lakini jenerali huyo mchanga akajibu hivi: ‘Hata mimi ningefanya hivyo, ikiwa ningekuwa Parmenio.’ Akikataa kufanya mapatano, Aleksanda aliendelea na mazingiwa na kuharibu Tiro mwezi wa Julai mwaka wa 332 K.W.K.
Akiliacha Yerusalemu, lililosalimu amri mbele zake, Aleksanda alisonga mbele kuelekea kusini, na kushinda Gaza. Wakiwa wamechoshwa na utawala wa Uajemi, Misri ilimkaribisha kama mwokozi. Huko Memphis, aliwapendeza makuhani wa Misri kwa kumtolea dhabihu mungu Apis mwenye sura ya fahali. Alianzisha pia jiji la Aleksandria, ambalo baadaye lilishindana na Athene likiwa kituo cha kujifunza nalo bado laitwa hivyo.
Kisha, Aleksanda akageuka kuelekea kaskazini-mashariki, akipitia Palestina na kuelekea Mto Tigris. Mwaka wa 331 K.W.K., alipigana vita kubwa ya tatu dhidi ya Uajemi, huko Gaugamela, karibu na magofu ya Ninewi. Huko, askari-jeshi 47,000 wa Aleksanda walilishinda nguvu jeshi la Uajemi lililopangwa upya la angalau askari-jeshi 250,000! Dario alikimbia na baadaye akauawa na watu wake mwenyewe.
Akiwa amesisimuka kwa sababu ya ushindi, Aleksanda aligeuka na kuelekea kusini na kulitwaa Babiloni, jiji kuu la Uajemi la wakati wa majira ya baridi kali. Pia alimiliki majiji makuu huko Susa na Persepolisi, akanyakua hazina kubwa ya Uajemi na kuyachoma makao makuu ya mfalme Shasta. Hatimaye, jiji kuu la Ecbatana likaanguka mikononi mwake. Mshindi huyo wa haraka akatiisha sehemu iliyosalia ya milki ya Uajemi, akienda mbali upande wa mashariki hadi Mto Indus, ulio katika Pakistan ya leo.
Alipovuka Indus, mpakani mwa mkoa wa Uajemi uitwao Taxila, Aleksanda alikutana na mpinzani mgumu sana, Porus, mtawala wa India. Aleksanda alipigana vita yake kubwa ya nne na ya mwisho dhidi yake mwezi wa Juni mwaka wa 326 K.W.K. Jeshi la Porus lilitia ndani askari-jeshi 35,000 na tembo 200, ambao waliwaogofya farasi wa Wamakedonia. Vita hivyo vilikuwa vikali na watu wengi walikufa, lakini majeshi ya Aleksanda yakashinda. Porus alisalimu amri na kujiunga nao.
Zaidi ya miaka minane ilikuwa imepita tangu jeshi la Makedonia livuke na kuingia Asia, nao askari-jeshi walikuwa wachovu na walitamani kurudi nyumbani. Wakiwa wamechoshwa na vile vita vikali dhidi ya Porus, walitaka kurudi nyumbani. Ingawa alisitasita mwanzoni, Aleksanda alikubali waliyotaka. Kwa kweli, Ugiriki ilikuwa imekuwa serikali ya ulimwengu. Koloni za Ugiriki zikiwa zimeanzishwa katika nchi zilizoshindwa, lugha na utamaduni wa Kigiriki zikaenea kotekote katika milki hiyo.
KIONGOZI WA JESHI HILO
Utu wa Aleksanda uliliunganisha jeshi la Makedonia kwa miaka yote hiyo. Baada ya vita, Aleksanda alikuwa na desturi ya kuwatembelea waliojeruhiwa, kuchunguza majeraha yao, kuwasifu askari-jeshi kwa sababu ya matendo yao ya kishujaa, na kuwapa zawadi za fedha kwa sababu ya mambo waliyotimiza. Aleksanda alipanga wale waliokufa vitani wazikwe kwa fahari. Wazazi na watoto wa watu waliokufa hawakutakiwa kulipa kodi wala kufanya aina fulani za utumishi. Ili kugeuza fikira baada ya vita, Aleksanda alipanga michezo na mashindano. Pindi moja, hata aliwapa wanaume waliokuwa wameoa karibuni likizo, ikiwawezesha kuwa na wake zao wakati wa majira ya baridi kali, huko Makedonia. Matendo hayo yalifanya watu wake wampende na kuvutiwa naye.
Kuhusu Aleksanda kumwoa Roxana, Binti-Mfalme wa Bactria, mwandika-wasifu Mgiriki Plutarch aandika hivi: “Kwa kweli, walipendana, na kwa wakati uleule ilionekana kama jambo hilo lilifaa kusudi lake. Kwa kuwa watu aliowashinda waliridhika kumwona akimchagua mke miongoni mwao, na kuwafanya wampende sana, kwa kuona kwamba hata katika upendo pekee ambao ulimshinda yeye, mtu asiyeonyesha hisia sana, alijidhibiti hadi alipoweza kumwoa kihalali kwa njia yenye kuheshimika.”
Aleksanda aliheshimu pia ndoa za wengine. Ingawa mke wa Mfalme Dario alikuwa mateka wake, alihakikisha kwamba alitendewa kwa njia ya heshima. Hali kadhalika, alipopata kujua kwamba askari-jeshi wawili wa Makedonia walikuwa wamewatenda vibaya wake za wageni fulani, aliagiza wauawe ikiwa wangepatikana na hatia.
Sawa na mama yake, Olympias, Aleksanda alikuwa mtu wa dini kwelikweli. Alitoa dhabihu kabla na baada ya vita naye aliwasiliana na wanajimu wake ili kujua maana ya ishara fulani za mambo ya wakati ujao. Pia aliwasiliana na mwaguzi wa Ammon, huko Libya. Na akiwa Babiloni alitekeleza maagizo ya Wakaldayo kuhusu kutoa dhabihu, hasa kwa mungu wa Babiloni, Bel (Marduki).
Ingawa Aleksanda alikuwa na kiasi katika mazoea yake ya kula, hatimaye alianza kunywa kupindukia. Kwa kadiri alivyokunywa, ndivyo alivyoongea sana na kujisifia mafanikio yake. Mojawapo ya matendo maovu zaidi aliyofanya Aleksanda lilikuwa kumwua rafiki yake Clitus, akiwa na hasira za ulevi. Lakini Aleksanda alijilaumu sana hivi kwamba alilala siku tatu kitandani, bila kula wala kunywa. Hatimaye, rafiki zake walifaulu kumshawishi ale.
Kadiri wakati ulivyopita, tamaa ya Aleksanda ya kupata utukufu ilimfanya atokeze vitabia vingine visivyopendeza. Alianza kusadiki kwa urahisi mashtaka yasiyo ya kweli na kuanza kutoa adhabu kali sana. Kwa mfano, baada ya kufanywa aamini kwamba Philotas alihusika katika jaribio la kumwua, Aleksanda aliagiza yeye na baba yake, Parmenio, ambaye alikuwa mshauri aliyemtumaini wakati mmoja, wauawe.
KUSHINDWA KWA ALEKSANDA
Punde baada ya kurudi Babiloni, Aleksanda akaugua malaria, naye hakupona. Juni 13, 323 K.W.K., baada ya kuishi miaka 32 na miezi 8 tu, Aleksanda akasalimu amri mikononi mwa adui mwenye kutisha zaidi, kifo.
Ni kama vile tu watu fulani wenye hekima wa India walivyosema: “Ee Mfalme Aleksanda, kila mtu humiliki kiasi kidogo tu cha dunia kama mahali hapa tunaposimama; na kwa kuwa u mwanadamu kama wanadamu wengine, isipokuwa tu kwamba una utendaji mwingi na bidii, wazurura kotekote katika dunia hii mbali na nyumbani kwako, ukisumbuka, na kuwasumbua wengine. Lakini punde si punde utakufa, nawe utamiliki kiasi cha dunia kinachotosha maziko yako.”
-
-
Ni Nani Atakayeutawala Ulimwengu?Sikiliza Unabii wa Danieli!
-
-
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
USHINDI MBALIMBALI WA ALEKSANDA
MAKEDONIA
MISRI
Babiloni
Mto Indus
[Picha]
Aleksanda
[Picha]
Aristotle na mwanafunzi wake Aleksanda
[Picha]
[Picha]
Medali isemwayo kwamba ina picha ya Aleksanda Mkuu
-