-
Afrika Kusini2007 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Wakati uliopita, kulikuwa na mizozo baina ya jamii mbalimbali. Sera ya ubaguzi wa rangi ilifanya taifa hilo lishutumiwe na mataifa mengine. Katika miaka ya karibuni, nchi hiyo imesifiwa kwa kuondolea mbali ubaguzi wa rangi na kuanzisha serikali iliyoteuliwa kidemokrasia.
Sasa, watu wa jamii zote wanaweza kuchangamana kwa uhuru, wanaweza kwenda sehemu zozote za umma, kama kwenye majumba ya sinema au mikahawa. Mtu wa jamii yoyote anaweza kuishi popote apendapo, maadamu ana uwezo wa kifedha.
Hata hivyo, baada ya msisimuko wa awali kutulia, maswali fulani ya msingi yalizuka. Serikali hiyo mpya ingetatua dhuluma zilizoletwa na ubaguzi wa rangi kwa kadiri gani? Ingechukua muda gani?
-
-
Afrika Kusini2007 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 68, 69]
Sera ya Ubaguzi wa Rangi
Neno apartheid linalotafsiriwa ubaguzi wa rangi linamaanisha “kutenga” nalo lilitumiwa kwa mara ya kwanza na chama cha National Party wakati wa uchaguzi wa kisiasa uliofanywa mwaka wa 1948. Chama hicho kilishinda uchaguzi mwaka huo, nao ubaguzi wa kijamii ukawa sera rasmi ya serikali ya Afrika Kusini, iliyoungwa mkono kabisa na Kanisa la Dutch Reformed. Sera hiyo iliyoanzishwa ili kuimarisha mamlaka ya wazungu, ilichangia kuanzishwa kwa sheria zilizoweka mipaka kuhusu mambo ya msingi maishani, kama vile makao, kazi, elimu, rasilimali za umma, na siasa.
Watu waligawanywa katika vikundi vifuatavyo: wazungu, Wabantu (Waafrika weusi), machotara (mchanganyiko wa rangi), na Waasia (Wahindi). Watetezi wa ubaguzi wa rangi walitangaza kwamba jamii mbalimbali ziwe na maeneo yao wenyewe ambako wangeweza kuishi na kuendeleza utamaduni na mila zao. Ingawa jambo hilo lilionekana kuwa rahisi, halikufaulu. Kwa sababu ya kuogopa bunduki, gesi za kutoa machozi, na mbwa wakali, weusi wengi walifukuzwa kutoka makwao na kuhamishiwa kwingineko wakiwa na vitu vichache tu. Sehemu nyingi za umma kama vile benki na posta, zilikuwa na vitengo vya wazungu na vya jamii nyingine. Mikahawa na majumba ya sinema yalikuwa ya wazungu peke yao.
Weusi waliwafanyia wazungu kazi katika biashara zao na nyumbani, nao walilipwa mishahara midogo. Hilo lilitenganisha familia. Kwa mfano, wanaume weusi waliruhusiwa kwenda majijini kufanya kazi katika migodi au viwandani nao walikaa katika mabweni ya wanaume huku wake zao wakiwa nyumbani. Hilo lilivuruga maisha ya familia na kusababisha uasherati. Kwa kawaida watumishi weusi waliokuwa wakifanya kazi katika nyumba za wazungu waliishi katika chumba kwenye boma la mkubwa wao. Familia zao hazingeweza kuishi katika ujirani huo wa wazungu, kwa hiyo wazazi hawakuona familia zao kwa muda mrefu. Weusi walipaswa kubeba vitambulisho nyakati zote.
Kulikuwa na ubaguzi katika sehemu nyingi za maisha, kutia ndani elimu, ndoa, kazi, na kumiliki mali. Ingawa Mashahidi wa Yehova walijulikana kuwa watu wasio na ubaguzi, walitii sheria za serikali maadamu hazikuwazuia kutoa utumishi mtakatifu kwa Mungu. (Rom. 13:1, 2) Walijitahidi kushirikiana na waabudu wenzao wa jamii mbalimbali kadiri ambavyo wangeweza.
Kuanzia miaka ya katikati ya 1970, serikali ilifanya mabadiliko kadhaa, na hivyo sera zake za ubaguzi wa rangi zikalegezwa. Mnamo Februari 2, 1990, Rais F. W. de Klerk, alitangaza mikakati mbalimbali ya kukomesha ubaguzi wa rangi, kama vile kuidhinisha vyama vya kisiasa vya weusi, na kuachiliwa kutoka gerezani kwa Nelson Mandela. Kufuatia ushindi wa serikali ambayo walio wengi walikuwa weusi katika uchaguzi wa kidemokrasia uliofanywa 1994, ubaguzi wa rangi ulikoma rasmi.
-