-
Kufungua Kufuli ya Siri TakatifuUfunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!
-
-
Ule Uasi-Imani Mkubwa
10. Ni jambo gani lililoupata mfumo wa Kiyahudi na wategemezaji wao wasiotubu katika 70 W.K.?
10 Wakati Yohana alipoandika Ufunuo, Ukristo ulikuwa na umri wa zaidi ya miaka 60. Mwanzoni, ulikuwa umeokoka miaka 40 ya upinzani wa daima kutoka dini ya Kiyahudi. Kisha mfumo wa Kiyahudi ukapokea pigo la kifo katika 70 W.K. wakati Wayahudi wasiotubu walipopoteza utambulishi wao wa kuwa taifa pamoja na kile ambacho kwao kilikaribia sana kuwa sanamu ya kuabudiwa—lile hekalu katika Yerusalemu.
11. Kwa nini ilifaa sana yule Mchungaji Mkuu ayaonye makundi juu ya miendo iliyokuwa ikisitawi?
11 Hata hivyo, mtume Paulo alikuwa ametabiri kwamba kungekuwako uasi-imani miongoni mwa Wakristo wapakwa-mafuta, na jumbe za Yesu huonyesha kwamba katika umri wa uzee wa Yohana uasi-imani huu ulikuwa tayari ukisitawi. Yohana alikuwa wa mwisho wa wale waliokuwa wakitenda wakiwa kizuizi katika jaribio hili la kupindukia la Shetani la kufisidi ile mbegu ya mwanamke. (2 Wathesalonike 2:3-12; 2 Petro 2:1-3; 2 Yohana 7-11) Kwa hiyo ulikuwa wakati unaofaa kwa Mchungaji Mkuu wa Yehova kuandikia wazee katika makundi, akiwaonya juu ya miendo iliyokuwa ikisitawi na kuwatia moyo wale wenye mioyo iliyo sawa wasimame imara kwa ajili ya uadilifu.
12. (a) Ule uasi-imani ulisitawije katika karne za baada ya siku ya Yohana? (b) Jumuiya ya Wakristo ilipataje kuwako?
12 Sisi hatujui jinsi makundi yalivyoitikia jumbe za Yesu katika 96 W.K. Lakini tunalojua ni kwamba ule uasi-imani ulisitawi kwa haraka sana baada ya kifo cha Yohana. “Wakristo” waliacha kutumia jina Yehova na badala yalo wakaweka “Bwana” au “Mungu” katika hati za Biblia. Kufikia karne ya nne, lile fundisho bandia la Utatu lilikuwa limepenya kisirisiri katika makundi. Katika pindi ii hii ya wakati, lile wazo la kutokufa kwa nafsi lilikuwa likikubaliwa. Hatimaye, Konstantino Maliki Mroma aliipa dini ya “Kikristo” idhini rasmi ya Serikali, nayo hatua hiyo ikatokeza Jumuiya ya Wakristo, ambamo Kanisa na Serikali ziliunganisha kani zao katika kutawala kwa miaka elfu moja. Lilikuwa jambo rahisi kuwa “Mkristo” wa mtindo mpya. Makabila kwa ujumla yalirekebisha zile itikadi za mapema za kipagani zikawa namna za dini hii. Walio wengi wa viongozi katika Jumuiya ya Wakristo wakawa watawala wa kisiasa wenye kuonea, wakishurutisha watu wakubali maoni yao ya uasi-imani kwa kutumia upanga.
13. Ijapokuwa onyo la Yesu juu ya kufanyiza mafarakano, Wakristo waliokuwa wakiasi imani walichukua mwendo gani?
13 Maneno ya Yesu kwa yale makundi saba yalipuuzwa kabisa na Wakristo hao waliokuwa wakiasi imani. Yesu alikuwa amewaonya Waefeso waupate tena ule upendo waliokuwa nao hapo kwanza. (Ufunuo 2:4) Hata hivyo, washiriki wa Jumuiya ya Wakristo, bila kuwa wameungana tena katika upendo kwa ajili ya Yehova, walipiga vita vikali sana na wakanyanyasana vibaya sana. (1 Yohana 4:20) Yesu alikuwa amelionya kundi katika Pargamamu juu ya kufanyiza mafarakano. Hata hivyo, mafarakano yalitokea hata katika karne ya pili, na leo Jumuiya ya Wakristo ina maelfu ya mafarakano na dini zenye kuzozana.—Ufunuo 2:15.
14. (a) Ingawa Yesu alionya dhidi ya kuwa mfu kiroho, ni mwendo gani uliochukuliwa na wale waliojidai kuwa Wakristo? (b) Ni katika njia zipi wale waliodai kuwa Wakristo walishindwa kutii onyo la Yesu dhidi ya ibada ya sanamu na ukosefu wa adili?
14 Yesu alikuwa amelionya kundi katika Sardisi dhidi ya kuwa mfu kiroho. (Ufunuo 3:1) Kama hao katika Sardisi, waliodai kuwa Wakristo walisahau upesi juu ya kazi za Kikristo na bila kukawia wakakabidhi kazi ya maana zaidi ya kuhubiri kwa kikundi kidogo, cha jamii ya viongozi wa kidini wenye kulipwa mshahara. Yesu alikuwa amelionya kundi katika Thiatira dhidi ya ibada ya sanamu na uasherati. (Ufunuo 2:20) Hata hivyo, Jumuiya ya Wakristo ilikubali waziwazi utumizi wa sanamu, pamoja na kuendeleza ibada ya sanamu yenye werevu zaidi ya utukuzo wa taifa na upendo wa vitu vya kimwili. Na ukosefu wa adili, ingawa nyakati fulani mahubiri ya kuupinga yalitolewa, sikuzote umekuwa ukivumiliwa kotekote.
15. Maneno ya Yesu kwa yale makundi saba yanafichua nini kuhusu dini za Jumuiya ya Wakristo, nao makasisi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wamethibitika kuwa nini?
15 Kwa sababu hiyo, maneno ya Yesu kwa yale makundi saba yanafichua kule kushindwa kabisa kwa dini za Jumuiya ya Wakristo kuwa watu wa pekee wa Yehova. Kweli kweli, viongozi wa dini za Jumuiya ya Wakristo wamekuwa ndio washiriki wenye kutokeza zaidi wa ile mbegu ya Shetani. Akisema juu ya hao kuwa ‘yule mtu wa uasi-sheria,’ mtume Paulo alitabiri kwamba ‘kuwapo kwao ni kulingana na utendaji wa Shetani pamoja na kila kazi yenye nguvu na ishara za kusema uwongo na maajabu na pamoja na kila danganyo lisilo la uadilifu.’—2 Wathesalonike 2:9, 10, NW.
16. (a) Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo walionyesha uchukivu wa pekee kwa nani? (b) Ni jambo gani lililotukia katika Jumuiya ya Wakristo katika kile kipindi cha zile Enzi za Katikati? (c) Je! ule uasi au Mapinduzi Makuu ya Kiprotestanti, yalibadili njia za uasi-imani za Jumuiya ya Wakristo?
16 Huku wakidai kuwa wachungaji wa kundi la Mungu, viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, wa kidini na wa kiserikali, walionyesha uchukivu wa pekee kwa yeyote aliyejaribu kutia moyo usomaji wa Biblia au yeyote aliyefichua mazoea yao yasiyo ya kimaandiko. John Hus na mtafsiri Biblia William Tyndale, walinyanyaswa na wakauawa kwa sababu ya imani yao. Katika kile kipindi chenye kutiwa giza cha Enzi za Katikati, utawala wa wenye kuasi imani ulifikia upeo wao kwa lile Baraza la Kuhukumia Wazushi wa Kidini lenye ukatili mwingi la Kikatoliki. Watu wowote waliopinga mafundisho au mamlaka ya kanisa walikandamizwa bila rehema, na maelfu yasiyohesabika ya wale walioitwa eti wazushi wa kidini waliteswa-teswa mpaka kifo au wakachomwa penye nguzo. Hivyo Shetani alijitahidi kuhakikisha kwamba mbegu yoyote ya kweli ya tengenezo la Yehova lililo mfano wa mwanamke ingepondwa-pondwa kwa haraka sana. Wakati ule uasi au Mapinduzi Makuu ya Kiprotestanti yalipotukia (kuanzia 1517 na kuendelea), makanisa mengi ya Kiprotestanti yalidhihirisha roho ile ile ya kutovumilia. Hayo vilevile yakawa yenye hatia ya damu kwa kuwaua kwa sababu ya imani yao wale wote waliojaribu kuwa washikamanifu kwa Mungu na Kristo. Kweli kweli, “damu ya watakatifu” ilimwagwa kwa wingi sana!—Ufunuo 16:6; linga Mathayo 23:33-36.
-
-
Kufungua Kufuli ya Siri TakatifuUfunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!
-
-
[Picha katika ukurasa wa 31]
Dini ya Jumuiya ya Wakristo ilijiletea hatia ya damu kubwa kwa kunyanyasa na kuua wale waliotafsiri, wakasoma, au hata wakawa na Biblia
-