-
Dhahabu Ingali InavutiaAmkeni!—2005 | Septemba 22
-
-
Karibu wakati huohuo, dhahabu iligunduliwa upande mwingine wa dunia, katika koloni mpya ya Australia. Edward Hargraves, ambaye alijifunza kuchimba dhahabu katika migodi ya California, alielekea Australia na kupata dhahabu katika kijito karibu na mji mdogo wa Bathurst, huko New South Wales. Mnamo 1851, maeneo yenye dhahabu nyingi yalipatikana huko Ballarat na Bendigo, katika jimbo la Victoria. Habari za ugunduzi huo zilipoenea, harakati nyingine ikaanza. Baadhi ya watu waliokuja walikuwa wachimbaji stadi. Hata hivyo, wengi walikuwa wafanyakazi wa shambani au wa ofisini ambao hawakuwa wamewahi kutumia sururu ya wachimba migodi. Likieleza jinsi hali ilivyokuwa katika mji mmoja ambako wanaharakati walikuwa wakiishi, gazeti moja la eneo hilo lilisema hivi wakati huo: “Mji wa Bathurst umepatwa na kichaa tena. Kichaa cha kutafuta dhahabu kimerudi kwa kishindo. Wanaume hukutana, hutazamana kijinga, huzungumza upuuzi usioeleweka, na kushangaa ni nini kitakachotokea.”
Ni nini kilichotokea? Idadi ya watu iliongezeka haraka. Miaka kumi baada ya 1851, idadi ya watu nchini Australia iliongezeka maradufu, huku watu kutoka pembe zote za ulimwengu waliokuwa wakitafuta madini wakikutana katika nchi hiyo. Dhahabu iligunduliwa katika viwango mbalimbali barani humo. Harakati moja ilipopungua, nyingine ilianza. Mnamo 1856 pekee, Waaustralia ambao hutafuta madini walichimba tani 95 za dhahabu. Kisha, mnamo 1893, wachimbaji walianza kuchimba dhahabu karibu na Kalgoorlie-Boulder, Australia Magharibi. Tangu wakati huo, zaidi ya tani 1,300 zimechimbwa katika eneo ambalo limetajwa kuwa “sehemu yenye ukubwa wa kilometa 2.5 za mraba yenye dhahabu nyingi zaidi ulimwenguni.” Bado eneo hilo hutokeza dhahabu na sasa mgodi huo ni mojawapo ya migodi ya dhahabu yenye kina kirefu zaidi ulimwenguni, kwani umekuwa bonde lenye upana wa kilometa mbili hivi, urefu wa kilometa tatu hivi, na kina kinachofikia meta 400!
Leo, Australia ndiyo nchi ya tatu inayotokeza dhahabu kwa wingi ulimwenguni. Watu 60,000 wameajiriwa katika kazi hiyo, nayo hutokeza tani 300 hivi za dhahabu, au dhahabu yenye thamani ya dola bilioni tano (za Australia) kila mwaka.
-
-
Dhahabu Ingali InavutiaAmkeni!—2005 | Septemba 22
-
-
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mgodi wa dhahabu wenye kina kirefu zaidi ulimwenguni, huko Kalgoorlie—Boulder, Australia Magharibi
[Hisani]
Courtesy Newmont Mining Corporation
-