Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Imani Yajaribiwa Ulaya Wakati wa Wanazi
    Amkeni!—2003 | Februari 8
    • Ndugu Yangu, Willi

      Willi, aliyekuwa mkubwa wangu kwa miaka minne, hakuwa amewasiliana nasi kwa zaidi ya miaka tisa tangu tulipotoka Ufaransa. Ingawa Mama alikuwa amemfundisha Biblia tangu ujana, alikuwa amepumbazwa aamini kwamba sera ya kisiasa ya Hitler ingeleta mafanikio wakati ujao. Katika Mei 1940, mahakama moja ya Ufaransa ilimhukumia Willi kifungo cha miaka miwili kwa sababu ya makosa aliyofanya alipokuwa Mnazi. Muda mfupi baadaye, aliachiliwa wakati majeshi ya Ujerumani yalipovamia Ufaransa. Wakati huo, alitutumia kadi akiwa Paris. Tulifurahi kujua kwamba alikuwa hai, lakini tulishangaa kusikia mambo aliyokuwa ameshawishwa kuamini!

      Wakati wa vita, Willi alipata nafasi ya kututembelea mara nyingi kwa sababu alikuwa na uhusiano mzuri na kikosi cha SS (Schutzstaffel, walinzi wa Hitler). Alivutiwa sana na mafanikio ya kijeshi ya Hitler. Kila nilipojaribu kumkumbusha kuhusu tumaini letu linalotegemea Biblia alisema: “Huo ni upuuzi! Ona vile Hitler ameshambulia ghafula. Hivi karibuni Wajerumani watatawala ulimwengu mzima!”

      Mnamo Februari 1942, alipokuja nyumbani likizoni, nilimpatia kitabu Enemies, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Nilishangazwa sana alipokisoma chote mara hiyo. Alianza kutambua kwamba utawala wa Hitler haungeweza kufanikiwa na alikuwa anaunga mkono mfumo mkatili. Aliazimia kurekebisha makosa yake.

      Msimamo wa Willi Katika Kweli ya Biblia

      Willi alipotutembelea mwezi uliofuata, alikuwa amebadilika sana. Alisema: “Anton, nilikuwa nimepotea!”

      Nilimwambia, “Willi, laiti ungalijua hivyo mapema.”

      “La,” akajibu, “sijachelewa sana! Biblia inasema ‘ufanye unalopaswa kufanya maadamu u hai,’ ninamshukuru Mungu kwa sababu ningali hai!”—Mhubiri 9:10.

      “Na sasa utafanya nini?” nilimwuliza.

      “Sitaendelea kutumika jeshini,” alinijibu. “Nitavunja uhusiano wangu na Wanazi ili nione jinsi itakavyokuwa.”

      Mara moja akaenda Zagreb, Yugoslavia, kumtembelea tena dada yangu, Pepi. Baada ya kuhudhuria kwa muda mikutano iliyokuwa imepigwa marufuku ya Mashahidi, alibatizwa kisiri. Hatimaye, mwana mpotevu alirejea!—Luka 15:11-24.

      Ili aepuke Wanazi huko Ufaransa, Willi alijaribu kuingia Uswisi. Lakini akakamatwa na polisi wa jeshi la Ujerumani. Alipelekwa mahakamani huko Berlin, na mnamo Julai 27, 1942, alihukumiwa kifo kwa sababu ya kutoroka. Niliruhusiwa kumtembelea katika Gereza la Kijeshi la Berlin-Tegel. Nilielekezwa kwenye chumba kidogo, na baada ya muda mfupi Willi aliingia akiwa amefunganishwa na mlinzi kwa mnyororo. Machozi yalinitoka nilipomwona katika hali hiyo. Hatukuruhusiwa kukumbatiana na tulipewa dakika 20 tu za kuagana.

      Willi aliponiona nikitoa machozi aliniuliza: “Anton, kwa nini unalia? Unapaswa kufurahi! Ninamshukuru Yehova sana kwa kunisaidia niipate kweli tena! Iwapo ningekufa nikipigana kwa ajili ya Hitler, singekuwa na tumaini. Lakini nikifa kwa ajili ya Yehova, nina hakika nitafufuliwa na tutaonana tena!”

      Katika barua aliyoandika ili kutuaga, Willi alisema: “Mungu wetu mpendwa, ninayemtumikia, hunipa kila kitu ninachohitaji na atanitegemeza hadi mwisho, ili niweze kuvumilia na kushinda. Ninasema tena, mwe na hakika kwamba sijutii jambo lolote na nimedumu nikiwa imara katika Bwana!”

      Willi aliuawa katika Gereza la Brandenburg, karibu na Berlin, siku iliyofuata, Septemba 2, 1942. Alikuwa na umri wa miaka 27. Maisha yake yalionyesha ukweli wa maneno ya Wafilipi 4:13: “Kwa mambo yote ninayo nguvu kwa njia ya yeye anipaye nguvu.”

  • Imani Yajaribiwa Ulaya Wakati wa Wanazi
    Amkeni!—2003 | Februari 8
    • [Picha katika ukurasa wa 18]

      Ndugu yangu, Willi, muda mfupi kabla hajauawa

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki