-
Ulimwengu Usio na Magari?Amkeni!—1996 | Juni 8
-
-
Ulimwengu Usio na Magari?
JE, WAWEZA kuwazia ulimwengu usio na magari? Au waweza kutaja uvumbuzi ambao kwa karne iliyopita umebadili mitindo-maisha na mwenendo wa watu kwa njia kuu kama ambavyo magari yamefanya? Bila magari, hakungekuwa na moteli, hakungekuwa mikahawa ambapo watu hushughulikiwa wakiwa magarini mwao, hakungekuwa mahali pa maonyesho ambapo watu huketi magarini mwao. La maana zaidi, bila basi, teksi, magari, au magari ya kubeba mizigo, ungefikaje kazini? shuleni? Wakulima na watengenezaji-vitu wangefikishaje bidhaa zao sokoni?
“Biashara moja kati ya kila biashara sita za Marekani hutegemea kutengenezwa, kusambazwa, kurekebishwa, au kutumiwa kwa magari,” yataja The New Encyclopædia Britannica, ikiongeza hivi: “Mauzo na risiti za makampuni ya magari huwakilisha zaidi humusi ya biashara ya mauzo-jumla ya Marekani na zaidi ya robo ya biashara ya rejareja. Kwa nchi nyinginezo milinganisho hii ni midogo kidogo, lakini Japani na nchi za Ulaya magharibi zimekaribia kwa haraka sana kiwango cha Marekani.”
Hata hivyo, watu fulani husema kwamba ulimwengu usio na magari ungekuwa mahali bora zaidi. Wanasema hilo kwa sababu mbili hasa.
Msongamano wa Magari wa Ulimwenguni Pote
Ikiwa umepata kuendesha gari kuzunguka barabara kwa kipindi kirefu ukitafuta nafasi ya kuegesha, unatambua vema sana kwamba hata ingawa magari yana faida, kuwa na magari mengi katika eneo lililosongamana hakuna faida. Au ikiwa umepata kunaswa katika msongamano mkubwa wa magari, unajua jinsi inavyofedhehesha kuzuiwa katika gari ambalo liliundwa kusonga lakini limelazimishwa kusimama tuli.
Katika 1950, Marekani ndiyo ilikuwa nchi pekee iliyokuwa na gari 1 kwa kila watu 4. Kufikia 1974, Italia, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Ujerumani zilifikia kiwango hicho. Lakini kufikia wakati huo tarakimu ya Marekani ilikuwa imepanda hadi karibu gari 1 kwa kila watu 2. Sasa Ujerumani na Luxembourg zina gari 1 hivi kwa kila wakazi 2. Italia, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, na Uingereza hazijaachwa nyuma sana.
Majiji mengi makubwa—haidhuru yako wapi ulimwenguni—yamesongamana magari hivi kwamba yafanana na maegesho makubwa sana ya magari. Kwa kielelezo, katika India wakati wa uhuru katika 1947, New Delhi, jiji layo kuu, lilikuwa na magari ya kawaida na magari ya kubebea mizigo 11,000. Kufikia 1993 tarakimu hiyo ilipita 2,200,000! Ongezeko kubwa mno—lakini “idadi ambayo yatarajiwa kurudufika kufikia mwishoni mwa karne hii,” kulingana na gazeti Time.
Wakati huohuo, katika Ulaya Mashariki, yenye robo tu ya idadi ya magari kwa kila mtu kwa kulinganisha na Ulaya Magharibi, kuna wale wawezao kuwa wateja milioni 400. Kwa miaka michache, hali katika China, inayojulikana hadi sasa kwa baiskeli zayo milioni 400, itakuwa imebadilika. Kama ilivyoripotiwa katika 1994, “serikali inapanga ongezeko la haraka katika utokezaji wa magari,” kuanzia kiwango cha kila mwaka cha magari milioni 1.3 hadi milioni 3 kufikia mwishoni mwa karne hii.
Lile Tisho la Uchafuzi
“Uingereza imeishiwa na hewa safi,” likasema gazeti The Daily Telegraph la Oktoba 28, 1994. Labda hilo limetiwa chumvi lakini hata hivyo ni la kweli vya kutosha kusababisha hangaiko. Profesa Stuart Penkett, wa Chuo Kikuu cha East Anglia, alionya hivi: “Magari yanabadili muundo wa hali ya kiasili ya angahewa.”
Kiwango cha juu cha uchafuzi wa kaboni monoksidi, chasema kitabu 5000 Days to Save the Planet, “huunyima mwili oksijeni, hulemaza ufahamu na kufikiri, hupunguza mwendo wa sihiari na kusababisha usinziaji.” Na Shirika la Afya Ulimwenguni lasema: “Yapata nusu ya wakazi wa jijini katika Ulaya na Amerika Kaskazini wanapatwa na viwango vya juu isivyokubalika vya kaboni monoksidi.”
Yakadiriwa kwamba katika sehemu fulani mitokezo ya magari huua watu wengi kila mwaka—kuongezea kusababisha uharibifu wa kimazingira wenye kugharimu mabilioni ya dola. Katika Julai 1995 ripoti ya habari ya televisheni ilisema kwamba Waingereza wapatao 11,000 hufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa wenye kusababishwa na magari.
Katika 1995 Kongamano la Umoja wa Mataifa la Tabia-Nchi lilikutana katika Berlin. Wawakilishi kutoka nchi 116 walikubali kwamba jambo fulani lapasa kufanywa. Lakini kwa fadhaiko la wengi, jukumu la kuweka miradi hususa na kuanzisha kanuni hususa au kuorodhesha programu mahususi liliahirishwa.
Kulingana na kile ambacho kitabu 5000 Days to Save the Planet kilisema katika 1990, ukosefu huu wa maendeleo labda ulitarajiwa. “Jinsi uwezo wa kisiasa na kiuchumi unavyoongoza jamii ya kisasa ya viwanda,” hicho kikataja, “huamua kwamba hatua za kukabiliana na uharibifu wa mazingira zakubalika tu ikiwa haziingilii uendeshaji wa kiuchumi.”
Hivyo, majuzi Time lilionya juu ya “uwezekano wa kwamba kuongezeka kwa kaboni dioksidi na gesi nyinginezo za kuongeza joto katika angahewa kutaongeza joto polepole tufeni. Tokeo, kulingana na wanasayansi wengi, laweza kuwa ukame, kuyeyuka kwa barafu duniani, kupanda kwa usawa wa bahari, mafuriko ya pwani, dhoruba mbaya zaidi na misiba mingine ya tabia-nchi.”
Uzito wa tatizo la uchafuzi wataka kwamba jambo fulani lifanywe. Lakini ni jambo gani?
-
-
Kutafuta Masuluhisho YanayokubalikaAmkeni!—1996 | Juni 8
-
-
Kutafuta Masuluhisho Yanayokubalika
SI MAGARI peke yayo yatokezayo uchafuzi. Makao ya kibinafsi, viwanda, na vituo vya nguvu za umeme lazima pia vishiriki lawama. Hata hivyo, fungu la magari katika uchafuzi wa duniani pote ni kubwa.
Kwa hakika, kitabu 5000 Days to Save the Planet huthubutu kusema hivi: “Ikiwa sababu ya hasara hizi zote ingeelezwa—hasa hasara kwa tabia-nchi yetu kwa kutokezwa kwa kaboni monoksidi—basi yaelekea magari hayangetengenezwa kamwe.” Hata hivyo, hicho chakubali hivi: “Lakini hilo ni chaguo ambalo wala watengeneza-magari, wala wajenzi wa barabara, wala mashirika ya serikali, wala watu wote kwa ujumla, ambao maisha yao huzidi kutegemea usafiri wa kibinafsi, hawako tayari kulitafakari.”
Je, tekinolojia iliyompeleka mwanadamu mwezini haiwezi kutokeza gari lisiloleta uchafuzi? Kufanya si rahisi kamwe kama kusema, hivyo hadi vizuizi vya kufanyiza gari lisilotokeza uchafuzi viwezapo kushindwa, utafutaji wa masuluhisho mengineyo yanayokubalika waendelea.
Kupunguza Vichafuzi
Katika miaka ya 1960 Marekani ilipitisha sheria iliyoamrisha kuwekwa kwa vithibiti kwenye magari ili kuzuia mitokezo ya vichafuzi. Nchi na serikali nyinginezo zimefanya vivyohivyo.
Vifaa vigeuzavyo michemuo ya magari ili isidhuru, ambavyo huhitaji kutumia petroli isiyo na madini ya risasi, sasa vyatumiwa sana ili kuchuja vichafuzi vyenye kudhuru. Kati ya 1976 na 1980, baada ya idadi kubwa ya waendesha-magari kuanza kutumia petroli isiyo na madini ya risasi, kiwango cha madini ya risasi katika damu ya Wamarekani kilipungua kwa thuluthi. Na kilifanya vyema kupungua, kwa kuwa madini ya risasi yenye kupita kiasi yaweza kuathiri mfumo wa neva na kuzuia uwezo wa kujifunza. Hata hivyo, kwa kuhuzunisha, ingawa viwango vya madini ya risasi vimepungua katika nchi nyingi za ulimwengu uliositawi, hilo halijatukia katika nchi ambazo hazijasitawi sana.
Mafanikio ya vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru yanatosheleza, lakini utumizi wavyo bado wabishaniwa. Kwa sababu ya kupungua kwa uwezo wakati ambapo risasi haikuongezwa tena, mfanyizo wa hidrokaboni wa petroli ulibadilishwa. Hilo limetokeza ongezeko katika mitoko ya vichochezi vinginevyo vya kansa, kama vile benzeni na tolini, ambavyo mitokezo yavyo haiwezi kupunguzwa na vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru.
Isitoshe, vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru huhitaji utumizi wa platini. Kulingana na Profesa Iain Thornton, wa Chuo cha Imperial katika Uingereza, moja ya athari zayo mbaya imekuwa ongezeko la platini iliyotanda katika vumbi lililo kando ya barabara. Yeye alionya juu ya uwezekano kwamba “namna ziwezazo kuyeyuka za platini zaweza kuingia katika mtungo wa chakula.”
Licha ya mafanikio yoyote ya “vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru katika Amerika Kaskazini, Japani, Korea Kusini na nchi kadhaa za Ulaya,” 5000 Days to Save the Planet chakiri hivi kihalisi, “ongezeko kubwa mno la idadi za magari ulimwenguni pote limeharibu manufaa kwa ubora wa hewa.”
Kupunguza Mwendo
Njia nyingine ya kupunguza mitoko ya magari ni kuendesha gari polepole. Lakini katika Marekani, majimbo fulani hivi majuzi yameongeza kiwango cha mwendo. Katika Ujerumani kuweka vizuizi hakupendwi na wengi. Watengenezaji magari wanaokazia uwezo wao wa kutengeneza magari yenye nguvu ambayo huruhusu kwa urahisi mwendo wa kasi upitao kilometa 150 kwa saa kwa wazi wanapinga kupunguzwa kwa viwango vya mwendo, sawa na idadi kubwa ya madereva. Hata hivyo, yaonekana sasa kwamba Wajerumani zaidi na zaidi wako tayari kukubali vizuizi vya mwendo si kwa sababu za kimazingira tu bali pia kwa sababu ya usalama.
Katika nchi fulani madereva wanatakwa kupunguza mwendo wakati uchafuzi ufikapo viwango visivyokubalika—au labda kuacha kuendesha kabisa. Uchunguzi wa 1995 ulifunua kwamba asilimia 80 ya Wajerumani ingekubali kuanzishwa kwa viwango vya mwendo ikiwa viwango vya ozoni vyawa juu sana. Majiji kadhaa kotekote ulimwenguni, kutia ndani Athens na Rome, tayari yamechukua hatua za kupunguza uendeshaji chini ya hali fulani. Mengineyo yanafikiria kufanya vivyo hivyo.
Kutumia Baiskeli
Ili kupunguza msongamano wa magari, majiji fulani yameanzisha bei zilizopunguzwa kwa usafiri wa basi. Mengine huandaa usafiri usio na malipo kwa madereva ambao hulipa ada ndogo kuegesha magari yao katika maegesho yapatikanayo. Majiji mengine yana barabara zilizotengwa kwa ajili ya mabasi na teksi tu ili kuharakisha aina hizi za usafiri.
Njia mpya ya kukabiliana na tatizo hilo ilitajwa hivi majuzi katika gazeti The European: “Wakichochewa na kampeni katika Uholanzi katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1960, watu wa Denmark wenye maarifa wamefanya mpango wa kupunguza uchafuzi wa hewa na msongamano wa magari kwa kushurutisha watu watumie magurudumu mawili badala ya manne.” Baiskeli huwekwa katika mahali kadhaa kotekote katika barabara za Copenhagen. Kutumbukiza kisarafu ndani ya kifaa fulani hutoa baiskeli ya kutumiwa. Arbuni yaweza kudaiwa baiskeli irudishwapo baadaye katika mahali pafaapo. Kupita kwa wakati kutaonyesha ikiwa mradi huu utathibitika kuwa wenye kutumika na kupendwa na wengi.
Ili kutia moyo utumizi wa baiskeli badala ya magari, majiji fulani ya Ujerumani huruhusu waendesha-baiskeli kupitia barabara iendayo upande mmoja tu iliyo kinyume cha magari! Kwa kuwa thuluthi hivi ya safari zote jijini na zaidi ya thuluthi ya zile za mashambani ni fupi zaidi kuliko kilometa tatu, wananchi wengi wanaweza kwa urahisi kuenda safari hizo kwa kutembea au kwa kuendesha baiskeli. Hilo laweza kusaidia kupunguza uchafuzi; kwa wakati huohuo, waendesha-baiskeli watakuwa wakipata mazoezi ya mwili yahitajikayo.
Kufanyiza Muundo Mpya
Kazi inaendelea ya kuunda magari yasiyotoa uchafuzi. Magari ya umeme yawezayo kuenda kwa betri yametokezwa, lakini yana mapungukio kuhusiana na mwendo na muda wa uendeshaji. Na ndivyo ilivyo na magari yatumiayo nguvu za jua.
Uwezekano mwingine unaochunguzwa ni kutumia hidrojeni kuwa fueli. Hidrojeni huungua karibu bila mitokezo yoyote ya vichafuzi, lakini ni ghali sana.
Akitambua uhitaji wa kuvumbua upya magari rais Clinton wa Marekani alitangaza katika 1993 kwamba serikali na viwanda vya magari vya Marekani zingeshirikiana katika kuunda gari la wakati ujao. Alisema hivi: “Tutajaribu kuanzisha jambo la ujasiri la kitekinolojia la kiwango kikubwa sawa na lolote ambalo taifa letu limepata kujaribu.” Ikiwa itawezekana “kufanyiza gari lenye matokeo mno na lifaalo kimazingira kwa ajili ya karne ya 21,” ambalo alilizungumzia, ni jambo linalobaki kuonwa. Mipango ina lengo la kutokeza kiolezo cha kwanza mnamo mwongo mmoja—hata hivyo, kwa gharama kubwa mno.
Watengeneza-magari fulani wanafanyia kazi violezo ambavyo hutumia mchanganyiko wa petroli na umeme. Linalopatikana tayari katika Ujerumani—kwa gharama kubwa mno—ni gari la michezo linalotumia umeme liwezalo kuchapua mwendo mnamo sekunde tisa kuanzia kikao cha kusimama hadi kilometa 100 kwa saa, likizidi hadi mwendo wa kilometa 180 kwa saa. Lakini baada ya kilometa 200, betri hupungua nguvu na husimama hadi betri zichajiwe tena kwa angalau muda wa saa tatu. Utafiti unaendela, na maendeleo zaidi yatarajiwa.
Sehemu Tu ya Tatizo
Jinsi ya kuondosha mitoko yenye sumu ni sehemu tu ya tatizo. Magari pia husababisha uchafuzi wa kelele, jambo ajualo yeyote anayeishi karibu na barabara yenye magari mengi. Kwa kuwa kelele ya magari isiyokwisha yaweza kuathiri afya vibaya, hiyo pia ni sehemu ya msingi ya tatizo linalohitaji kutatuliwa.
Wapendao maumbile ya asili watataja pia kwamba mandhari nyingi za mashambani za urembo wa asili huharibiwa na kilometa nyingi za barabara kuu zenye sura mbaya, pamoja na mahali pa biashara penye sura isiyofurahisha na mabango ya matangazo ambayo huenda yakapakana na barabara hizo. Lakini huku idadi ya magari iongezekapo, ndivyo na uhitaji wa barabara zaidi.
Magari fulani, baada ya miaka mingi ya kuchafua hewa katika kutumikia wenyewe, huendelea na uchafuzi wayo hata “baada ya kifo.” Magari yaliyotupwa, yakiwa tu yenye kuudhi macho, yamekuwa tatizo sana hivi kwamba imebidi sheria ipitishwe katika mahali fulani kuepuka kurundikana kwayo ovyoovyo sehemu za mashambani. Je, gari lifaalo, ambalo limetengenezwa kwa maunzi yaliyo rahisi kutengenezwa upya, litapata kuundwa? Gari kama hilo halitapatikana karibuni.
“Wajerumani wengi wanahangaikia sana mazingira,” lataja gazeti la habari la majuzi, likiongeza, “lakini ni wachache tu wanaochukua hatua ifaayo.” Ofisa wa serikali alinukuliwa kusema hivi: “Hakuna anayejifikiria kuwa mkosaji, wala hakuna aliye tayari kulaumiwa.” Ndiyo, matatizo ni magumu kutatua katika ulimwengu uliojaa watu ambao ni “wenye kujipenda wenyewe,” na “wasiotaka kufanya suluhu.”—2 Timotheo 3:1-3.
Hata hivyo, utafutaji wa suluhisho linalokubalika waendelea. Je, suluhisho lifaalo kwa uchafuzi na magari laweza kupatikana?
-
-
Kupata Suluhisho LifaaloAmkeni!—1996 | Juni 8
-
-
Kupata Suluhisho Lifaalo
NENO LA MUNGU, Biblia, husema juu ya wakati ambapo serikali ya kimbingu ya Mungu itakapokuwa imesuluhisha matatizo yote ya wanadamu, ambayo sasa hutia ndani tatizo la uchafuzi usababishwao na magari. Je, Ufalme huu wa Kimesiya, ambao wengi wamefunzwa kuuomba, utaandaa suluhisho lifaalo kwa kutokeza magari yasiyotokeza uchafuzi kabisa? Au suluhisho lifaalo litapatikana kwa kuondoa magari yote duniani? Kwa kuwa Biblia haitupatii jibu hususa, hatuwezi kufanya lolote ila kungojea na kuona tu.—Mathayo 6:9, 10.
Lakini twaweza kuwa na uhakika juu ya hili: Serikali ya Mungu haitaruhusu uchafuzi uharibu urembo wa uumbaji katika Paradiso iliyorudishwa itakayoletwa na huo Ufalme.—Isaya 35:1, 2, 7; 65:17-25.
Kwa kuwa wale wanaotii Neno la Mungu tayari wanazoezwa kwa ajili ya maisha katika ulimwengu mpya usio na uchafuzi, wanapaswa kuhisije juu ya utumizi wa magari leo? Amkeni! la Juni 22, 1987 (la Kiingereza), lilishughulikia habari “Ni Nini Kinachoipata Misitu Yetu?” Hilo liliripoti kwamba wanasayansi fulani hufikiri kwamba kuna uhusiano kati ya vichafuzi vya hewa vilivyo katika michemuo ya magari na kufa kwa misitu. Hilo lilifanya msomaji mmoja aliyehangaishwa kuandikia Watchtower Society akiuliza ikiwa kwa sababu ya jambo hilo ingefaa Wakristo kuendesha magari. Aliuliza ikiwa kufanya hivyo kungeonyesha ukosefu wa staha kwa uumbaji wa Yehova.
Barua yake ilijibiwa hivi, kwa sehemu: “Mashahidi wa Yehova hutii kwa ushikamanifu sheria za kimazingira zilizowekwa na mamlaka za serikali ili kupunguza uchafuzi. (Warumi 13:1, 7; Tito 3:1) Kuchukua hatua zaidi ya kile ambacho serikali huamuru ni uamuzi wa mtu mmoja-mmoja. Ikiwa mtu aamua kutotumia tena gari, hilo ni jambo lake la kibinafsi. Hata hivyo, makala hiyo ya Amkeni! ilionyesha kile ambacho watu fulani huhisi, kwa kusema hivi kwenye ukurasa 8: ‘Wengi wanachukua hatua zifaazo za kupunguza uchafuzi wa hewa kwa kadiri wawezavyo. Wanaendesha polepole zaidi, hawasafiri sana, wanajiunga na mipango ya kusafiri kwa kikundi cha wenye magari katika gari moja, wanatumia petroli zisizo na madini ya risasi, na kutii maagizo yaliyo dhidi ya uchafuzi yaliyowekwa na serikali.’”
Usawaziko wa Kikristo
Jibu hilo lilidhihirisha usawaziko wa Kikristo. Ni lazima ikumbukwe kwamba si magari pekee yanayoleta uchafuzi. Ndege na magari-moshi—kwa hakika, aina nyingi za kisasa za usafiri—hufanya hivyo. Lakini namna hizi za usafiri hazikutokezwa kwa kusudi la moja kwa moja la kusababisha uchafuzi. Kwa kusikitisha, uchafuzi unaotokea ni athari mbaya inayosababishwa na ujuzi haba na mitazamo isiyokamilika.
Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 1993, ukurasa 31, lilizungumzia jambo hili, likisema hivi: “Tukiwa Mashahidi wa Yehova, tunahangaikia sana yale matatizo mengi ya kiekolojia (mazingira) yanayoathiri makao yetu ya kidunia. Zaidi ya watu wengi, sisi tunathamini kwamba dunia iliumbwa iwe makao safi, yenye afya kwa ajili ya familia kamilifu ya kibinadamu. (Mwanzo 1:31; 2:15-17; Isaya 45:18) . . . Kwa hiyo inafaa kufanya jitihada zenye usawaziko, zinazofaa ili kuepuka kuongezea ule uharibifu wa mwanadamu wa dunia yetu unaoendelea sasa. Lakini, angalia lile neno ‘zinazofaa.’ . . . Watu wa Mungu hawapaswi wawe wasahaulifu kuhusu mambo ya kiekolojia. Yehova aliwataka watu wake wa kale wachukue hatua za kuondolea mbali takataka, hatua zilizokuwa za muhimu kwa kiekolojia na kwa kiafya pia. (Kumbukumbu la Torati 23:9-14) Na kwa kuwa tunajua maoni yake juu ya wale wanaoiharibu dunia, kwa hakika hatupaswi kupuuza mambo tunayoweza kufanya ili kudumisha mazingira yakiwa safi. . . . Hata hivyo, kadiri ambayo Mkristo angejitahidi katika hayo ni jambo la kibinafsi isipokuwa ikiwa inahitajiwa na sheria. . . . Wanadamu wasiokamilika hutumbukia kwa urahisi katika mtego wa kuwa bila kiasi. . . . Jitihada za kibinadamu za kuiondolea dunia matatizo yayo makubwa ya kiekolojia, kutia na uchafuzi, hazitafanikiwa kikamili. Huenda yakawa maendeleo huko na huko, lakini suluhisho pekee la kudumu lataka mwingilio wa Mungu. Kwa sababu hiyo tunakaza jitihada na nyenzo zetu kwenye suluhisho la kimungu, kuliko kujaribu kusuluhisha dalili za kijuujuu tu.”
Wakristo ni wenye usawaziko wanapofuata kanuni za Biblia, wakikumbuka utume wa kimungu ambao wamepokea wa kuhubiri ujumbe wa Ufalme wa Mungu kotekote ulimwenguni. (Mathayo 24:14) Hakuna jambo lililo muhimu au lenye uharaka mkubwa kuliko hilo! Ikiwa namna ya kisasa ya usafiri na mawasiliano yaweza kuwasaidia Wakristo kutimiza wajibu huu, wana sababu nzuri ya kuitumia. Wakati huohuo, wao huepuka kutokeza uchafuzi bila sababu au kwa kusudi. Hivyo wanadumisha dhamiri njema mbele ya mwanadamu na Mungu.
Kwa hiyo ingawa sisi leo hatujui hasa jinsi tatizo la uchafuzi wa magari litakavyosuluhishwa hatimaye, twajua kwamba litatatuliwa. Kwa hakika, suluhisho lifaalo liko karibu sana.
[Sanduku katika ukurasa wa9]
Kupambana na Uchafuzi
• Kutembea au kuendesha baiskeli inapowezekana
• Kushiriki katika mipango ya kusafiri kwa kikundi cha wenye magari katika gari moja
• Kuhakikisha magari yanarekebishwa na kudumishwa kwa ukawaida
• Kuhakikisha natumia fueli isiyoleta uchafuzi sana
• Kuepuka usafiri usio wa lazima
• Kuendesha kwa mwendo wa kiasi lakini ufaao
• Kutumia usafiri wa umma iwezekanapo na ifaapo
• Kuzima injini badala ya kuiacha ikinguruma gari linaposimama kwa kipindi chochote cha wakati
-