Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Tamaa Kubwa ya Kusafiri Angani
    Amkeni!—1999 | Machi 8
    • Tamaa Kubwa ya Kusafiri Angani

      “NDEGE zote zimethibitisha haraka methali ya wakati wa ujana wetu isemayo, ‘Aliye juu mngojee chini.’”

      Ndivyo ilivyoanza tahariri yenye kutilia shaka kwa kiasi fulani katika gazeti la The New York Times la Mei 25, 1908—kipindi kinachopungua miaka mitano baada ya ndugu wawili walioitwa Wright kufunga safari yao ya angani iliyo mashuhuri huko Kitty Hawk, North Carolina, Marekani. Bado wakitilia shaka mafanikio ya “mashine [mpya] zinazoruka” zilizokuwa zimeanza kutokea angani, mwandishi alifikiri kwamba “kwa kulinganishwa ni wachache kati yetu walio na tamaa ya kuelea hewani wakiwa juu sana kutoka duniani.” Ingawa ilikubali kwamba vizazi vya wakati ujao vyaweza kuwa na mwelekeo wa kukubali kusafiri kwa ndege, makala hiyo ilisisitiza kwamba “tamaa kubwa sana ya kutengeneza ndege za abiria za kusafiri masafa marefu . . . huenda isitimizwe kamwe.”

      Utabiri huo ulikosea kama nini! Leo, abiria zaidi ya bilioni moja husafiri angani katika “ndege za kusafiri masafa marefu” kila mwaka. Ndiyo, katika karne moja, ndege zimebadilishwa kutoka kuwa vidude hafifu vya mbao na viunzi katika mwanzo wa karne ya 20 hadi kuwa ndege za kisasa zenye mitindo na zilizo na kompyuta, ambazo husafiri kilometa 10 juu ya dunia na kubeba mamia ya abiria hadi maeneo ya mbali sana zikiwa na hali nzuri zenye kustarehesha.

      Maendeleo ya haraka ya ufundi wa vyombo vya anga katika karne ya 20 kwa kweli yamekuwa ya kipekee na yamebadili kwa kasi ulimwengu wetu. Kwa hakika, tamaa ya binadamu ya kuvumbua mambo ya anga yaweza kufuatiliwa zaidi ya miongo michache—au hata kupita karne chache zilizopita. Safari za angani za binadamu ni tamaa kubwa sana ambayo wanadamu wamekuwa nayo tangu nyakati za kale.

  • “Hakika Anga Liko Wazi”!
    Amkeni!—1999 | Machi 8
    • “Hakika Anga Liko Wazi”!

      “TAMAA ya kusafiri angani ni ya kale kama mwanadamu,” akasema mwanahistoria Berthold Laufer katika The Prehistory of Aviation. Kumbukumbu za Wagiriki, Wamisri, na Waashuri wa kale pamoja na hekaya za Mashariki zina hadithi nyingi sana za wafalme, miungu, na mashujaa waliojaribu kupata nguvu za kuruka angani. Katika karibu visa vyote, hadithi hizo zinahusisha watu wakiiga ndege wanaopaa.

      Kwa kielelezo, Wachina husimulia hadithi juu ya Maliki Shun mwenye hekima na mjasiri, anayedhaniwa kuwa aliishi miaka zaidi ya 2,000 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kulingana na hekaya, Shun, alijikuta amenaswa juu ya ghala iliyokuwa ikiwaka moto, akajivika manyoya, na kutoroka kwa kupuruka. Simulizi lingine lasema kwamba aliruka kutoka kwenye mnara na kutumia vyepeo viwili vikubwa vya mafunjo kama miavuli naye akatua ardhini salama.

      Miongoni mwa Wagiriki, kuna hadithi ya miaka 3,000 ya Daedalus, msanii mkuu na mvumbuzi, aliyejenga mabawa yaliyotengenezwa kwa manyoya, kitani, na nta ambayo yangemwezesha yeye na mwana wake Icarus kutoroka Krete, mahali ambapo walizuiwa wakiwa uhamishoni. “Hakika anga liko wazi, na ndiyo njia tutakayofuata,” akatangaza Daedalus. Mara ya kwanza, mabawa yalifanya kazi kikamilifu. Lakini Icarus, akiwa amevutiwa na uwezo wake wa kupaa juu, alizidi kupuruka juu zaidi mpaka nta iliyounganisha mabawa yake ilipoyeyushwa na jua. Mvulana huyo alitumbukia kwenye bahari iliyokuwa chini akafa.

      Hadithi za namna hiyo zilichochea fikira za wavumbuzi na wanafalsafa waliotamani sana kupaa angani. Mapema kufikia karne ya tatu W.K., Wachina walikuwa wakijenga tiara na kuzijaribu, wakidhihirisha kwamba walielewa kanuni fulani za elimu ya anga muda mrefu kabla majaribio ya aina hii hayajaanza katika Ulaya. Katika karne ya 15, Giovanni da Fontana, tabibu wa Venice, alifanyia majaribio roketi sahili zilizotengenezwa kwa mbao na karatasi zilizorushwa kwa mlipuko wa baruti. Yapata mwaka wa 1420, da Fontana aliandika hivi: “Mimi, kwa kweli, sina shaka lolote kwamba inawezekana kumfungia mwanadamu mabawa yanayoweza kusogezwa, ambayo yatamwezesha kupaa hewani na kusafiri kutoka mahali pamoja hadi pengine na kupanda minara na kuvuka bahari.”

      Mapema katika karne ya 16, Leonardo da Vinci, aliyekuwa mchoraji, mchongaji, na mhandisi aliye stadi, alichora ramani zisizo stadi za helikopta na miavuli na vilevile za nyiririko zenye ncha za mabawa yanayopigapiga. Uthibitisho unadokeza kwamba angalau alijenga miundo ya mashine kadhaa za angani ambazo alikuwa amedokeza. Hata hivyo, hakuna muundo hata mmoja wa Vinci ulioweza kutumika.

      Katika karne mbili zilizofuata kuna masimulizi kadhaa ya jitihada za wanaume hodari waliojifunga mabawa waliyojitengenezea na kujaribu kuyapigapiga walipokuwa wakiruka kutoka kando za vilima na kwenye minara. Hawa ‘marubani wa majaribio’ walikuwa hodari na wajasiri—lakini jitihada zao hazikufua dafu.

      Puto za Moto na “Hewa Yenye Kuwaka Moto”

      Katika mwaka wa 1783 habari kuhusu mafanikio yenye kutazamisha ya usafiri wa angani zilienea Paris kote na katika mikoa ya Ufaransa. Ndugu wawili, Joseph-Michel na Jacques-Étienne Montgolfier, waligundua kwamba wangeweza kufanya puto ndogo za karatasi ziinuke haraka na kwa wepesi angani kwa kuzijaza hewa yenye moto. Puto yao ya kwanza kubwa ya moto, kama ilivyoitwa, ilitengenezwa kwa karatasi na kitani na ilijazwa moshi wenye harufu mbaya uliotoka kwenye moto mkubwa. Puto hiyo ambayo haikuwa na mtu iliruka na kufikia mwinuko wa zaidi ya meta 1,800 wakati wa safari yake ya kwanza ya angani. Mnamo Novemba 21, 1783, puto hiyo ilibeba abiria wawili—walioitwa na umma wanaanga—kwa safari ya dakika 25 juu ya Paris. Katika mwaka huohuo, mvumbuzi mwingine, Jacques Charles, alifunua puto ya kwanza iliyokuwa imejazwa gesi, iliyojazwa hidrojeni, au “hewa inayoshika moto,” kama ilivyojulikana wakati huo.

      Tekinolojia ya puto ilipozidi kuboreka, anga lilianza kufikiwa na wanaanga wajasiri. Kufikia mwaka wa 1784, puto zilikuwa zikipaa na kufikia mwinuko unaozidi meta 3,400. Mwaka mmoja tu baadaye, Jean-Pierre-François Blanchard alifanikiwa kuvuka Mlango-Bahari wa Uingereza akiwa ndani ya puto ya hidrojeni akibeba barua za kwanza ulimwenguni zilizosafirishwa angani. Kufikia mwaka wa 1862, wanaanga walikuwa wamefunga safari Ulaya na Marekani kote na walikuwa wamefaulu kufikia miinuko inayozidi kilometa nane!

      Lakini wanaanga wa mapema bado walikuwa wakipelekwa popote pale na pepo; hakukuwa na njia ya kudhibiti upande au mwendo wa safari za anga za puto. Kutokezwa kwa vyombo vya anga vinavyoendeshwa na petroli na umeme mwishoni mwa karne ya 19 kulifanya usafiri wa angani uwezekane kwa kiwango kikubwa, lakini vyombo hivyo vya anga vyenye umbo la soseji na vyepesi kuliko hewa vilisafiri polepole—kwa kawaida vikisafiri kati ya kilometa 10 hadi 30 kwa saa. Jambo jipya lilihitajiwa ikiwa mwanadamu ‘angepaa hewani na kusafiri kutoka mahali pamoja hadi pengine,’ kama alivyotabiri da Fontana.

  • Ndege Ziliwasilije?
    Amkeni!—1999 | Machi 8
    • Ndege Ziliwasilije?

      WABUNI walifanikiwaje mwishowe kutokeza mashine zinazoruka angani zilizo nzito kuliko hewa? Walielekeza uangalifu wao kwa wasanii stadi wa safari za angani—ndege wanaopuruka. Katika mwaka wa 1889 mhandisi Mjerumani aliyeitwa Otto Lilienthal, akichochewa na mazoea ya koikoi ya kusafiri angani, alichapisha kitabu “Bird Flight as the Basis of Aviation.” Miaka miwili baadaye alijenga nyiririko yake ya kwanza iliyo sahili. Katika mwaka wa 1896, baada ya safari za angani 2,000 za nyiririko, Lilienthal alikufa alipokuwa akifanyia majaribio ndege ya bawa moja. Octave Chanute, mhandisi Mmarekani aliyezaliwa Ufaransa, alifanyia marekebisho muundo wa Lilienthal na kutokeza nyiririko ya injini mbili ambayo nayo ilipiga hatua kubwa katika kuunda mashine inayoruka angani iliyo nzito kuliko hewa.

      Kisha akina Wright wakajitokeza. Orville na Wilbur Wright walikuwa na duka la baiskeli katika Dayton, Ohio, Marekani, nao walianza majaribio yao ya kwanza ya kunyiririka mwaka wa 1900, wakitegemea msingi uliowekwa na Lilienthal na Chanute. Akina Wright walifanya kazi polepole na kwa utaratibu kwa miaka mitatu iliyofuata, wakifunga safari za angani za majaribio mara kadhaa katika Kitty Hawk, North Carolina. Walitokeza miundo mipya inayotumia mashimo ya kupitishia upepo, na kwanza walitengeneza kwa kutumia sanduku la wanga. Katika safari yao ya kwanza ya angani kwa kutumia injini, walitengeneza injini yao wenyewe yenye silinda nne na nguvu-farasi 12 na kuipandisha kwenye bawa la chini la ndege mpya. Injini hiyo iliendesha rafadha mbili za mbao, moja katika kila upande wa usukani wa nyuma wa ndege.

      Mnamo Desemba 14, 1903, ndege mpya iliyovumbuliwa na akina Wright ilipaa kutoka kwenye ubao wa kuipeperushia kwa mara ya kwanza—na kubaki hewani kwa sekunde tatu u nusu! Siku tatu baadaye ndugu hao walipaa wakitumia mashine hiyo tena. Hatimaye ilibaki hewani kwa karibu dakika moja na kusafiri umbali wa meta 260. Ndege hiyo ikafanikiwa.a

      Kwa kushangaza, utimizo huo mkubwa haukuvutia uangalifu wowote wa ulimwengu. Hatimaye wakati The New York Times lilipochapisha habari kuhusu akina Wright katika Januari 1906, lilisema kwamba “mashine ya kuruka angani” ilikuwa imebuniwa kwa siri kubwa na kwamba ndugu hao walikuwa wamepata “mafanikio kidogo tu ya kusafiri angani” mwaka wa 1903. Kwa kweli, Orville alikuwa amempelekea baba yake telegramu usiku huohuo wa safari hiyo ya kihistoria, akimsihi aeleze vyombo vya habari. Hata hivyo, ni magazeti ya habari matatu tu huko Marekani yaliyojishughulisha kuchapisha habari hiyo wakati huo.

      Je, Hakutakuwa na Ndege za Biashara?

      Kwa ujumla ulimwengu ulikuwa na shaka kuhusu vyombo vya anga wakati vilipokuwa vikianza. Hata Chanute, mmojawapo wa waanzilishi wa vyombo vya anga alitabiri hivi mwaka wa 1910: “Kwa maoni ya wataalamu stadi ni kazi bure kutarajia kuwa na mashine zinazoruka angani za biashara. Sikuzote kutakuwako kipimo ambacho kitazuia kubeba abiria au shehena kupita kadiri fulani.”

      Hata hivyo, ufundi wa vyombo vya anga ulisonga mbele upesi baada ya safari za kwanza za angani za akina Wright. Katika miaka mitano ndugu hao walikuwa wamejenga ndege yenye mabawa mawili kila upande inayobeba watu wawili ambayo ingeweza kufikia mwendo wa kilometa 71 kwa saa na kupaa kufikia mwinuko wa meta 43. Katika mwaka wa 1911 safari ya kwanza kuvuka bara la Marekani kwa ndege ilifanywa; safari hiyo kutoka New York hadi California ilichukua karibu siku 49! Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, mwendo wa ndege uliongezwa kutoka kilometa 100 kwa saa hadi kufikia kilometa 230 kwa saa. Pia upesi rekodi za mwinuko zilifikia meta 9,000.

      Rekodi za vyombo vya anga ziliendelea kutangazwa katika vyombo vya habari katika miaka ya 1920. Maofisa wawili wa kijeshi Wamarekani walifunga safari ya kwanza bila kutua wakivuka Marekani mwaka wa 1923, nao walisafiri kutoka pwani moja hadi nyingine kwa muda unaopungua saa 27. Miaka minne baadaye Charles A. Lindbergh akawa maarufu mara moja kwa kusafiri kwa ndege bila kutua kutoka New York hadi Paris kwa muda wa saa 33 na dakika 20.

      Wakati huohuo, mashirika machanga ya ndege yalikuwa yameanza kuvutia wateja. Kufikia mwisho wa mwaka wa 1939, safari za ndege zilikuwa zimefikia hatua ambapo mashirika ya ndege ya Marekani yalikuwa yakihudumia karibu abiria milioni tatu kila mwaka. Ndege ya kawaida ya miaka ya 1930, DC-3, ilibeba abiria 21 tu na kusafiri kwa mwendo wa kilometa 270 kwa saa; lakini baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, ndege za biashara zikawa kubwa zaidi na zenye nguvu zaidi, zikisafiri kwa mwendo wa zaidi ya kilometa 480 kwa saa. Uingereza ilianzisha huduma za ndege yenye injini aina ya turbojet mwaka wa 1952. Na ndege kubwa-kubwa, kama vile Boeing 747 zinazoweza kubeba watu 400, ziliibuka mwaka wa 1970.

      Mafanikio mengine yalipatikana mwaka wa 1976 wakati kikundi cha wahandisi Waingereza na Wafaransa walipotokeza ndege aina ya Concorde, yenye mabawa yanayoelekea nyuma iwezayo kubeba abiria 100 na kusafiri mwendo maradufu wa sauti—zaidi ya kilometa 2,300 kwa saa. Lakini gharama za juu za kudumisha ndege hiyo zimesababisha ndege hizo zisitumiwe sana kibiashara.

      Kuuelekeza Ulimwengu

      Hata ikiwa hujawahi kusafiri kwa ndege, yawezekana kwamba maisha yako yameelekezwa na mabadiliko haya ya haraka ya kitekinolojia. Ndege zinazobeba shehena husafiri na kuvuka tufe lote; mara nyingi chakula tunachokula, mavazi tunayovalia, na mashine tunazotumia kazini vimesafirishwa kwa ndege kutoka ng’ambo ya bahari au ng’ambo ya bara. Barua na vifurushi hupelekwa kutoka nchi moja hadi nyingine kwa njia ya ndege. Biashara hutegemea sana huduma za usafirishaji zinazofanywa na ndege ili kuendesha shughuli za kila siku. Bidhaa na huduma tunazopata na gharama tunazozilipia zote zimeathiriwa na uwezo wa mwanadamu wa kusafiri kwa ndege.

      Pia vyombo vya anga vimechangia sana mabadiliko makubwa ya kijamii. Bila shaka, kwa sababu ya vyombo vya anga ulimwengu umekuwa mdogo sana. Kwa muda wa saa chache, unaweza kuwa karibu mahali popote ulimwenguni—ikiwa una uwezo wa kifedha. Habari husafiri haraka, ndivyo na watu.

      Gharama ya Maendeleo

      Lakini maendeleo hayo yametokeza gharama fulani. Ndege zinapozidi kuongezeka, wengine wanahofia anga inazidi kuwa hatari. Kila mwaka ndege za kibinafsi na za kibiashara zinazoanguka hupoteza uhai wa watu wengi. “Kukiwa na mkazo wa kushindana, mashirika mengi ya ndege yanapuuza hatua za ziada za usalama ambazo yalidumisha kwa ukawaida wakati ambapo abiria wangelipia gharama hizo za ziada,” lasema gazeti Fortune. Gazeti hilo laripoti kwamba Shirika la Serikali Linalosimamia Vyombo vya Anga, lenye daraka la kuhakikisha usalama wa ndege huko Marekani, “halina pesa za kutosha, halina wafanyakazi wa kutosha, na linasimamiwa vibaya.”

      Wakati huohuo, idadi inayozidi kuongezeka ya wanamazingira wanashtushwa na ongezeko la uchafuzi wa hewa na wa kelele unaotokana na ndege nyingi sana. Kushughulika na mahangaiko kuhusu matatizo ya kelele ni “mojawapo ya masuala yanayosababisha mgawanyiko zaidi katika kusafirisha raia ulimwenguni,” likasema gazeti Aviation Week & Space Technology.

      Matatizo haya yanaongezewa na uhakika wa kwamba ndege nyingi zinazidi kuchakaa: Katika mwaka wa 1990, ndege 1 kati ya 4 za Marekani zilipatikana kuwa zimedumu kwa zaidi ya miaka 20, na thuluthi moja zilikuwa zimetumiwa sana kupita “muda uliokusudiwa” kama ulivyopangwa hapo mwanzoni na mtengenezaji.

      Hivyo, wahandisi wa usafiri wa anga sasa wanakabiliwa na magumu makubwa sana. Wanahitaji kubuni njia zilizo salama zaidi na zisizo ghali za kubebea abiria zaidi, kama vile gharama zinavyopanda na mahangaiko kuhusu mazingira yanavyoongezeka.

      Tayari masuluhisho fulani ya kupunguza gharama yameanza kutokea. Jim Erickson, akiandika katika Asiaweek, asema kwamba kikundi cha wanasayansi wa anga wa Ufaransa na Uingereza kinapanga kutokeza ndege iwezayo kubeba kufikia abiria 300 na kusafiri mwendo maradufu wa sauti. Gharama na matumizi ya fueli kwa kila abiria zitakuwa chini. Na kufuatia hali ya msongamano wa ndege kwenye viwanja vingi vya ndege, watu fulani wamependekeza kutokezwa kwa helikopta kubwa za kubebea watu—kila moja ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 100. Wanaamini kwamba siku moja ndege hizi, zitaweza kushughulikia usafirishaji wa mwendo mfupi ambao sasa hufanywa na ndege za kawaida zenye mabawa.

      Je, kweli helikopta kubwa sana na ndege zenye mwendo wa kasi sana zitatimiza mahitaji muhimu ya usafiri wa ndege katika miaka ijayo? Itajulikana baada ya muda kupita huku mwanadamu akijisukuma kufuatia ‘kufungua anga’ kwa safari zake.

      [Maelezo ya Chini]

      a Watu fulani wanadai kwamba mnamo mwaka wa 1901, Gustave Whitehead (Weisskopf), mhamiaji Mjerumani aliyeishi Connecticut, Marekani, pia aliendesha ndege aliyoibuni. Hata hivyo, hakuna picha za kuthibitisha dai hilo.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki