-
Kuambatana na UpepoAmkeni!—2002 | Machi 8
-
-
Kuambatana na Upepo
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA
“NIPE KITAMBAA NA KAMBA, NAMI NITAWAONYESHA JAMBO LITAKALOSTAAJABISHA ULIMWENGU!” —JOSEPH-MICHEL MONTGOLFIER, 1782.
MIALI ya moto inayotokea ghafula hufanya puto la hewa ya joto lianze kupaa polepole. Kusafiri hewani kwa puto maridadi lenye rangi nyingi huwachangamsha na kuwapumzisha watu wenye shughuli nyingi. Mshabiki mmoja wa puto la hewa ya joto alisema kwamba kusafiri kwa puto “hutuliza na husisimua.”
Kusafiri kwa maputo kumewavutia watu tangu Joseph-Michel na Jacques-Étienne Montgolfier, wapange safari ya kwanza kwa puto la hewa ya joto, mapema katika miaka ya 1780. (Ona sanduku chini.) Hata hivyo, wengi walianza kupenda kusafiri kwa maputo tangu miaka ya 1960. Wakati huo ndipo vitambaa visivyoshika moto vilipoanza kutumiwa, na mbinu mpya za bei nafuu na zisizo hatari za kupasha hewa moto na kudhibiti joto ndani ya puto zilipobuniwa.
-
-
Kuambatana na UpepoAmkeni!—2002 | Machi 8
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14, 15]
SAFARI ZA KWANZA ZA PUTO
Inasemekana kwamba Joseph-Michel na Jacques-Étienne Montgolfier, wana wa tajiri mmoja aliyekuwa mtengenezaji wa karatasi huko Annonay, Ufaransa, ndio waliotengeneza puto la kwanza la hewa ya joto, na kupanga safari ya kwanza ya puto. Walifanya majaribio ya kwanzakwanza na maputo ya karatasi, mapema katika miaka ya 1780, nao walifikiri maputo hayo yalipaa kwa sababu ya moshi wa majani makavu na sufu zilizowaka moto. Punde si punde, wakagundua kwamba ilikuwa hewa yenye joto iliyofanya maputo yapae.
Baadaye, walipoanza kutengeneza maputo kwa kitambaa, waliona kwamba maputo makubwa zaidi yaliweza kupaa juu zaidi, kubeba mizigo mizito zaidi, na abiria wengi zaidi. Mnamo Juni 1783, walirusha puto kubwa kuliko yote ambayo walikuwa wamewahi kutengeneza kufikia wakati huo kutoka kwenye mtaa wa Annonay. Lilipaa kwa muda wa dakika kumi hivi, kisha likateremka.
Walipoona mafanikio hayo waliazimia kurusha puto lenye watu. Hata hivyo, kwanza walirusha puto lililobeba jogoo, bata, na kondoo. Maelfu ya watu walikusanyika kuangalia tukio hilo huko Versailles, mnamo Septemba 1783. Wanyama wote watatu hawakufa wala hawakuathiriwa hata kidogo na safari hiyo ya dakika nane. Punde baadaye, mnamo Novemba 21, 1783, puto lililobeba watu lilirushwa kwa mara ya kwanza. Mfalme Louis wa 16 alishawishiwa kuwaruhusu waungwana wawili kwenda safari hiyo. Walianza huko Château de la Muette, na kupeperuka kwa umbali wa kilometa nane hivi juu ya Paris. Baada ya dakika 25 hivi, wakalazimika kutua kwa kuwa puto lilikuwa linawaka moto.
Yapata wakati huo, wanasayansi wa Chuo cha Sayansi huko Paris walipendezwa na uvumbuzi huo. Profesa Jacques Charles, mmojawapo wa wanafizikia mashuhuri wa wakati huo, alishirikiana na mafundi wawili werevu, Charles na M. N. Robert, kutengeneza puto la kwanza lililojazwa gesi ya hidrojeni. Puto hilo lilijaribiwa Agosti 27, 1783. Puto hilo lilipeperuka kwa umbali wa kilometa 24 hivi, kwa muda wa dakika 45, nalo likapewa jina Charlière. Maputo ya aina hiyo hutumiwa hata leo hii.
[Sanduku katika ukurasa wa 17]
KUPAA HADI JUU
Mwingereza Henry Coxwell ni rubani mashuhuri aliyepaa hadi kimo cha juu. Mnamo Septemba 1862, alipewa kazi ya kumpeleka James Glaisher wa Shirika la Uingereza la Utabiri wa Hali ya Hewa hadi kimo cha juu ili Glaisher afanye uchunguzi wa kisayansi. Walipaa hadi kimo cha kilometa tisa hivi, bila vifaa vya kuongeza hewa ya kupumua!
Baada ya kufikia kimo cha meta 8,000 Coxwell alianza kufanya matayarisho ya kuteremka, huku akiwa na tatizo la kupumua kwa sababu ya upungufu wa hewa. Hata hivyo, kwa sababu ya kuzunguka-zunguka kwa puto, kamba ya kupunguza hewa ilikuwa imejipinda na Coxwell alilazimika kupanda juu ili kunyosha kamba hiyo. Glaisher tayari alikuwa amepoteza fahamu, na ilimbidi Coxwell kuivuta ile kamba kwa meno kwa kuwa mikono yake ilikuwa imepooza kwa sababu ya baridi. Hatimaye wakaanza kuteremka.
Wanaume wote wawili walipata nafuu kiasi cha kuweza kupunguza mwendo wa puto ili lisiteremke kwa kasi mno. Walikuwa wamefikia kimo cha meta 10,000 hivi. Rekodi hiyo haikuvunjwa kwa muda wa miaka 100. Safari yao ya puto, ni mojawapo ya safari maarufu za angani, kwa kuwa walisafiri katika kikapu kisichofunikwa, hawakuwa na akiba ya hewa, walivalia tu nguo za kawaida, na hawakujua mengi kuhusu anga la juu.
-