-
Babiloni MkubwaKutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
-
-
Babiloni la kale lilijulikana sana kwa dini zake na ukaidi wake kwa Yehova
Mwa. 10:8-10: “Nimrodi . . . akajionyesha kuwa mwindaji mwenye nguvu kwa kumpinga Yehova. . . . Nao mwanzo wa ufalme wake ukawa Babeli [baadaye ukaitwa Babiloni].”
Dan. 5:22, 23: “Na wewe, [Belshaza mfalme wa Babiloni] . . . ulijiinua juu ya Bwana wa mbingu, . . . nawe umeisifu miungu minyonge ya fedha na ya dhahabu, shaba, chuma, miti na mawe, ambayo haioni chochote, wala kusikia chochote, wala kujua chochote; lakini hukumtukuza Mungu ambaye pumzi yako imo mkononi mwake na ambaye njia zako zote ni zake.”
Maandishi fulani ya kale yanasema hivi: “Kwa ujumla katika Babiloni kuna mahekalu 53 ya miungu mikuu, mahekalu madogo 55 ya Marduku, mahekalu madogo 300 kwa ajili ya miungu ya kidunia, mahekalu madogo 600 kwa ajili ya miungu ya kimbingu, madhabahu 180 kwa ajili ya mungu wa kike Ishtar, 180 kwa ajili ya miungu Nergali na Adadi na madhabahu mengine 12 kwa ajili ya miungu mbalimbali.”—Yamenukuliwa katika The Bible as History (New York, 1964), W. Keller, uku. 301.
The Encyclopedia Americana inaeleza hivi: “Ustaarabu wa Kisumeri [uliokuwa sehemu ya Babilonia] ulitawaliwa na makuhani; na mkuu wa serikali alikuwa lugal (kihalisi ‘mtu mkuu’), mwakilishi wa miungu.”—(1977), Buku la 3, uku. 9.
Kwa hiyo, Babiloni Mkubwa kama linavyotajwa katika Ufunuo ni la kidini. Kwa kuwa liko kama jiji na milki, si kikundi kimoja tu cha kidini bali hutia ndani dini zote zinazompinga Yehova, Mungu wa kweli.
Mafundisho na matendo ya kale ya kidini ya Babiloni yanapatikana katika dini ulimwenguni pote
“Misri, Uajemi, na Ugiriki ziliathiriwa na dini ya Kibabiloni . . . Mchanganyiko mkubwa wa mambo ya Kisemiti katika hadithi za kwanza za Kigiriki na pia katika madhehebu ya kwanza ya Kigiriki sasa unakubaliwa kwa ujumla na wasomi hivi kwamba hauhitaji maelezo zaidi. Mambo hayo ya Kisemiti kwa kadiri kubwa ni ya Kibabiloni hasa.”—The Religion of Babylonia and Assyria (Boston, 1898), M. Jastrow, Jr., uku. 699 na 700.
Miungu yao: Kulikuwako miungu mitatu-mitatu, na kati ya miungu yao kulikuwako miungu iliyowakilisha nguvu mbalimbali za asili na miungu iliyotumia uvutano wa pekee katika utendaji fulani wa wanadamu. (Babylonian and Assyrian Religion, Norman, Okla.; 1963, S. H. Hooke, uku. 14-40) “Utatu wa Plato, ukiwa tu mpangilio mpya wa miungu mitatu-mitatu ya watu wa kale, waonekana kuwa ndio utatu wenye kupatana na akili na falsafa wa sifa tatu-tatu, uliotokeza sehemu tatu za maana sana za utatu au miungu mitatu inayofundishwa na makanisa ya Kikristo. . . . Fundisho hilo la mwanafalsafa Mgiriki [Plato] la miungu mitatu . . . linapatikana katika dini zote za kale [za kipagani].”—Nouveau Dictionnaire Universel (Paris, 1865-1870), kilichohaririwa na M. Lachâtre, Buku la 2, uku. 1467.
Matumizi ya sanamu: “[Katika dini ya Mesopotamia] sanamu zilitimiza sehemu kubwa katika madhehebu na pia katika ibada ya watu binafsi, kama vile kuenea kwa mifano ya sanamu hizo kunavyoonyesha. Kwa msingi, iliaminiwa kwamba mungu alikuwa katika sanamu yake ikiwa sanamu hiyo ilikuwa na maumbo fulani pamoja na vifaa hususa, nayo ilitunzwa inavyofaa.”—Ancient Mesopotamia—Portrait of a Dead Civilization (Chicago, 1964), A. L. Oppenheim, uku. 184.
Imani kuhusu kifo: “Watu wala viongozi wa imani za kidini [katika Babiloni] hawakukubali kamwe uwezekano wa kuangamizwa kabisa kwa kiumbe kilichoumbwa. Kifo kilikuwa njia ya kuingia kwenye maisha ya aina nyingine.”—The Religion of Babylonia and Assyria, uku. 556.
Cheo cha makasisi: “Dini [ya Kibabiloni] huwatenganisha makasisi na watu wa kawaida.”—Encyclopædia Britannica (1948), Buku la 2, uku. 861.
Mazoea ya unajimu, uaguzi, uchawi, na ulozi: Mwanahistoria A. H. Sayce anaandika hivi: “[Katika] dini ya Babilonia ya kale . . . kila kitu na kila nguvu ya asili ilidhaniwa kuwa ina zi au roho, ambayo ingeweza kudhibitiwa na uchawi wa Shaman, au kasisi wa ulozi.” (The History of Nations, New York, 1928, Buku la 1, uku. 96) “Wakaldayo [Wababiloni] walifanya maendeleo makubwa katika uchunguzi wa nyota wakijitahidi kuvumbua wakati ujao kupitia nyota. Ufundi huo tunauita ‘unajimu.’”—The Dawn of Civilization and Life in the Ancient East (Chicago, 1938), R. M. Engberg, uku. 230.
-
-
Babiloni MkubwaKutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
-
-
Baada ya Gharika ya siku za Noa, dini ya uwongo ilianzia Babeli (ambapo baadaye paliitwa Babiloni). (Mwa. 10:8-10; 11:4-9) Kisha, imani za kidini za Kibabiloni na matendo yalienea kwenye nchi nyingi.
-