Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ufalme wa Mungu Wazaliwa!
    Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!
    • Drakoni Mkubwa wa Rangi-Moto

      7. Ni ishara gani nyingine ambayo Yohana aona katika mbingu?

      7 Baada ya hapo Yohana aona nini? “Na ishara nyingine ikaonekana katika mbingu, na, tazama! drakoni mkubwa wa rangi-moto, mwenye vichwa saba na pembe kumi na juu ya vichwa vyake mataji saba; na mkia wake huburuta theluthi ya nyota za mbingu, na ukazivurumisha chini kwenye dunia. Na drakoni akafuliza kusimama mbele ya mwanamke ambaye alikuwa karibu kuzaa, kwamba, wakati ambapo yeye angezaa, apate kumeza mtoto wake.”—Ufunuo 12:3, 4, NW.

      8. (a) Ni nini ulio utambulisho wa huyo drakoni mkubwa wa rangi-moto? (b) Ni nini kinachoonyeshwa na drakoni huyo kuwa na vichwa saba, pembe kumi, na taji juu ya kila kichwa?

      8 Drakoni huyu ni Shetani, “nyoka wa awali kabisa.” (Ufunuo 12:9; Mwanzo 3:15, NW) Yeye ni mharabu mwenye ukali—drakoni mwenye vichwa saba, au mmezaji, ambaye anaweza kumeza kabisa windo lake. Anaonekana kigeni kama nini! Hivyo vichwa saba na pembe kumi huonyesha kwamba yeye ndiye mbuni wa hayawani-mwitu wa kisiasa ambaye karibuni ataelezwa habari zake katika Ufunuo sura ya 13. Pia hayawani huyu ana vichwa saba na pembe kumi. Kwa kuwa Shetani ana taji juu ya kila kichwa—vyote saba—sisi tunaweza kuwa na hakika kwamba zile serikali kubwa za ulimwengu zinazowakilishwa katika hayawani-mwitu huyo zimekuwa chini ya utawala wake. (Yohana 16:11) Pembe kumi ni ufananisho wenye kufaa wa ukamili wa mamlaka ambayo yeye ametumia katika ulimwengu huu.

      9. Ni nini kinachoonyeshwa na uhakika wa kwamba mkia wa huyo drakoni “huburuta theluthi ya nyota za mbingu” kuziangusha chini kwenye dunia?

      9 Pia drakoni ana mamlaka katika milki ya kiroho. Kwa mkia wake, yeye “huburuta theluthi ya nyota za mbingu.” Nyota zaweza kuwakilisha malaika. (Ayubu 38:7) Mtajo “theluthi” ungekazia kwamba idadi kubwa sana ya malaika wameongozwa vibaya na Shetani. Mara hawa walipokuja chini ya udhibiti wake, hawakuwa na njia ya kuponyoka. Hawangeweza kurudi kwenye tengenezo takatifu la Mungu. Wakaja kuwa roho waovu, wakawa kana kwamba wameburutwa na Shetani, mfalme, au mtawala wao. (Mathayo 12:24) Shetani pia aliwatupa duniani. Hii bila shaka inarejezea siku ya Noa kabla ya Furiko, wakati Shetani alipowashawishi hawa wana waasi wa Mungu waende chini duniani wakaishi pamoja na binti za wanadamu. Ikiwa adhabu, hawa “malaika ambao walifanya dhambi” wametupwa na Mungu katika hali iliyo kama gereza inayoitwa Tartaro.—Mwanzo 6:4; 2 Petro 2:4; Yuda 6, NW.

      10. Ni matengenezo gani yenye kupingana yanayoonekana, na ni kwa nini drakoni hutafuta kumeza mtoto wakati mwanamke anapozaa?

      10 Hivyo, matengenezo mawili yenye kupingana yamekuja kuonekana waziwazi—tengenezo la Yehova la kimbingu kama linavyotolewa picha na mwanamke na tengenezo la Shetani la roho waovu ambalo hupinga enzi kuu ya Mungu. Lile suala kubwa la enzi kuu lazima limalizwe. Jinsi gani? Shetani, akiwa angali anaburuta roho waovu pamoja naye, ni kama hayawani mkali wa mawindo mwenye kutupia jicho windo liwezekanalo. Yeye anangojea mwanamke azae. Yeye anataka kumeza hiki kitoto kichanga kinachotarajiwa kwa sababu yeye anajua kwamba kinatokeza tisho baya sana katika kuendelea kuwako kwake na kule kwa ulimwengu ambao juu yao yeye anatumia utawala.—Yohana 14:30.

      Mwana, wa Kiume

      11. Yohana anaelezaje habari za uzawa wa huyo mtoto wa mwanamke, na ni kwa nini mtoto huitwa “mwana, wa kiume”?

      11 Wakati uliowekewa mataifa kutawala bila kukatizwa na Mungu ulikuja kwenye kikomo katika 1914. (Luka 21:24) Ndipo, kwa wakati barabara, mwanamke anajifungua mtoto wake: “Na yeye akazaa mwana, wa kiume, ambaye anapaswa kuchunga mataifa yote kwa ufito wa chuma. Na mtoto wake akadakwa mbali hadi kwa Mungu na kwenye kiti cha ufalme chake. Na yule mwanamke akakimbia kwenda katika jangwa, ambako yeye ana mahali palipotayarishwa na Mungu, ili wao wapaswe kulisha yeye huko siku elfu moja mia mbili na sitini.” (Ufunuo 12:5, 6, NW) Mtoto ni “mwana, wa kiume.” Ni kwa nini Yohana anatumia usemi huu wa maradufu? Yeye anafanya hivyo kuonyesha kufaa kwa mtoto, uwezo wake wa kutawala mataifa kwa uweza wa kutosha. Unakazia pia jinsi uzawa huu ulivyo pindi ya tukio lenye maana sana, la shangwe! Una daraka la maana sana katika kuleta siri takatifu ya Mungu kwenye tamati. Kwani, mtoto huyu wa kiume hata ‘atachunga mataifa yote kwa ufito wa chuma’!

      12. (a) Katika Zaburi, Yehova aliahidi nini kiunabii kwa habari za Yesu? (b) Ni nini kinachofananishwa na huyo mwanamke kuzaa mwana “ambaye anapaswa kuchunga mataifa yote kwa ufito wa chuma”?

      12 Sasa, je! usemi huo unasikika kuwa wenye kuzoeleka? Ndiyo, Yehova aliahidi kiunabii kwa mintarafu ya Yesu: “Wewe utavunja wao kwa fimbo ya kifalme ya chuma, kana kwamba ni chombo cha mfinyanzi wewe utaponda wao vipande vipande.” (Zaburi 2:9, NW) Pia unabii ulitolewa kwa habari yake hivi: “Ufito wa imara yako Yehova atapeleka kutoka Sayuni, akisema: ‘Enda ukishinda katikati ya maadui wako.’” (Zaburi 110:2, NW) Kwa hiyo, uzawa ulioonwa na Yohana unahusu sana Yesu Kristo. La, si kuzaliwa kwa Yesu na bikira huko nyuma kabla ya karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida wetu; wala haungeweza kuwa ukirejezea kuinuliwa kwa Yesu tena kwenye uhai wa roho katika 33 W.K. Zaidi ya hilo, si uhamaji. Badala ya hivyo, ni uzawa wa Ufalme wa Mungu katika 1914 ukiwa uhalisi, Yesu akiwa—sasa katika mbingu kwa karibu karne 20—ameketishwa katika kiti cha ufalme akiwa Mfalme.—Ufunuo 12:10.

      13. Ni nini kinachofananishwa na huyo mtoto wa kiume ‘kudakwa mbali hadi kwa Mungu na kwenye kiti cha ufalme chake’?

      13 Yehova hangeweza kamwe kuruhusu Shetani ameze mke Wake au mwana Wake aliyezaliwa hivi sasa! Wakati wa uzawa, mtoto huyo wa kiume ‘anadakwa mbali kwa Mungu na hadi kwenye kiti cha ufalme chake.’ Yeye anakuja hivyo chini ya himaya ya Yehova, ambaye ataangalia kikamili huu Ufalme uliozaliwa hivi sasa, chombo Chake cha kutakasia jina Lake takatifu. Wakati ule ule, huyo mwanamke anakimbilia mahali alipotayarishiwa na Mungu jangwani. Tutapata habari zaidi juu ya hilo baadaye! Kwa habari ya Shetani, sasa jukwaa limetayarishwa kwa ajili ya tukio lenye maana kubwa ambalo litafanya isiwezekane kabisa kwake kutisha tena hata kidogo Ufalme ulio katika mbingu. Ni tukio gani hilo?

      Vita Katika Mbingu

      14. (a) Kama Yohana anavyolieleza, ni tukio gani linalofanya Shetani asiweze tena kutisha Ufalme? (b) Shetani na roho waovu wake wamezuiliwa mahali gani?

      14 Yohana anatuambia: “Na vita ikafyatuka katika mbingu: Mikaeli na malaika zake wakapigana na drakoni, na drakoni na malaika zake akapigana lakini hakushinda, wala mahali hapakupatikana kwa ajili yao tena katika mbingu. Hivyo chini yule drakoni mkubwa akavurumishwa, nyoka wa awali kabisa, mmoja ambaye huitwa Ibilisi na Shetani, ambaye anaongoza vibaya dunia nzima yote inayokaliwa; yeye akavurumishwa chini kwenye dunia, na malaika zake wakavurumishwa chini pamoja na yeye.” (Ufunuo 12:7-9, NW) Kwa hiyo likiwa tukio la kidrama katika kuleta siri takatifu ya Mungu kwenye tamati, Shetani anatolewa, anaondoshwa nje ya mbingu, na roho waovu wake wanatupwa chini kwenye dunia pamoja naye. Mmoja ambaye ameongoza vibaya dunia nzima yote inayokaliwa kwa kadiri ya kuwa mungu wayo mwishowe anazuiwa kwenye ujirani wa sayari hii, ambako uasi wake ulianzia awali.—2 Wakorintho 4:3, 4.

      15, 16. (a) Mikaeli ni nani, na sisi tunajuaje? (b) Ni kwa nini inafaa kwamba Mikaeli ndiye anayepaswa kuvurumisha Shetani kutoka katika mbingu?

      15 Ni nani wanaotimiza ushindi huu mkubwa katika jina la Yehova? Biblia inasema ni Mikaeli na malaika zake. Lakini Mikaeli ni nani? Jina “Mikaeli” lamaanisha “Ni Nani Aliye Kama Mungu?” Kwa hiyo lazima Mikaeli awe anapendezwa na kutetea enzi kuu ya Yehova kwa kuthibitisha kwamba hakuna wa kulinganishwa na Yeye. Katika Yuda 9 yeye anaitwa “Mikaeli, malaika mkuu.” Kwa kupendeza, jina la cheo “malaika mkuu” limetumiwa mahali pengine katika Biblia kuhusiana na mtu mmoja tu: Yesu Kristo.b Paulo husema kwa habari yake hivi: “Bwana mwenyewe atashuka kutoka katika mbingu akiwa na mwito wenye kuamuru pamoja, na sauti ya malaika mkuu na pamoja na tarumbeta ya Mungu.” (1 Wathesalonike 4:16, NW) Jina la cheo “malaika mkuu” lamaanisha “mkuu wa malaika.” Kwa hiyo haishangazi kwamba Ufunuo husema juu ya “Mikaeli na malaika zake.” Mahali pengine ambapo Biblia hutaja malaika wakitii mtumishi mwadilifu wa Mungu hurejezea Yesu. Hivyo, Paulo husema juu ya “ufunuo wa Bwana Yesu Kristo kutoka katika mbingu pamoja na malaika zake wenye nguvu.”—2 Wathesalonike 1:7, NW; ona pia Mathayo 24:30, 31; 25:31.

      16 Haya na maandiko mengine yanatuongoza kwenye mkataa usioepukika kwamba Mikaeli si mwingine ila Bwana Yesu Kristo katika cheo chake cha kimbingu. Sasa, katika siku ya Bwana, yeye hasemi tu kwa Shetani tena: “Yehova na akemee wewe.” Kwa kuwa huu ni wakati wa kuhukumu, Yesu, akiwa Mikaeli, huvurumisha chini mwovu huyu Shetani na malaika zake waovu kutoka katika mbingu. (Yuda 9, NW; Ufunuo 1:10) Inafaa kabisa kabisa kwamba yampasa Yeye awe ndiye Mmoja wa kufanya hivyo, kwa kuwa yeye ndiye Mfalme aliyetawazwa hivi sasa. Pia Yesu ndiye ile Mbegu, iliyoahidiwa huko nyuma katika Edeni, ambaye mwishowe kabisa atapondaponda kichwa cha huyo nyoka, hivyo amwondolee mbali kabisa asiwepo kwa wakati wote. (Mwanzo 3:15) Kwa kuondosha Shetani nje ya mbingu, Yesu amechukua hatua kuelekea kupondwapondwa huko kwa mwisho kabisa.

      “Mwe na Nderemo, Nyinyi Mbingu”

      17, 18. (a) Yohana anaripoti tendo-mwitikio gani kwa habari ya anguko la Shetani kutoka katika mbingu? (b) Ni jipi linaloelekea kuwa chimbuko la sauti kubwa anayosikia Yohana?

      17 Yohana anaripoti tendo-mwitikio kwa anguko hili kubwa mno la Shetani: “Na mimi nikasikia sauti kubwa katika mbingu ikisema: ‘Sasa kumetukia wokovu na nguvu na ufalme wa Mungu wetu na mamlaka ya Kristo wake, kwa sababu mshtaki wa ndugu zetu amevurumishwa chini, ambaye huwashtaki mchana na usiku mbele za Mungu wetu! Na wao walishinda yeye kwa sababu ya damu ya Mwana-Kondoo na kwa sababu ya neno la kushuhudu kwao, na wao hawakupenda nafsi zao hata usoni mwa kifo. Kwa minajili hii mwe na nderemo, nyinyi mbingu na nyinyi ambao hukaa ndani yazo!’”—Ufunuo 12:10-12a, NW.

      18 Ni ya nani sauti kubwa hiyo ambayo Yohana anasikia? Biblia haisemi. Lakini kilio kama hicho kinachoripotiwa kwenye Ufunuo 11:17 kilikuja kutoka kwa wazee 24 waliofufuliwa wakiwa katika vyeo vyao vya kimbingu, ambako sasa wao wanaweza kuwakilisha watakatifu 144,000. (Ufunuo 11:18) Na kwa kuwa watumishi wapakwa-mafuta wa Mungu wanaonyanyaswa ambao wangali duniani wanasemwa hapa kuwa “ndugu zetu,” taarifa hiyo ingeweza kwa uzuri kutoka kwa chimbuko lile lile. Hapana shaka kwamba hawa waaminifu wanaweza kuunga sauti zao, kwa kuwa ufufuo wao ungefuata upesi baada ya Shetani na magenge yake ya roho waovu kuwa wametupwa nje ya mbingu.

      19. (a) Kumalizwa kwa siri takatifu ya Mungu kunafungulia Yesu njia afanye nini? (b) Ni nini kinachoonyeshwa na Shetani kuitwa “mshtaki wa ndugu zetu”?

      19 Kumalizwa kwa siri takatifu ya Mungu kunahitaji Yesu achukue mamlaka katika Ufalme wa Yehova. Hivyo njia inafunguliwa kwa ajili ya Mungu kutimiza kusudi lake kubwa la kukomboa aina ya binadamu jaminifu. Yesu analeta wokovu si kwa wanafunzi wake pekee wenye kuhofu Mungu walio duniani sasa bali pia kwa yale mamilioni yasiyohesabika ya wafu ambao wako katika kumbumbu la Mungu. (Luka 21:27, 28) Kumwita Shetani “mshtaki wa ndugu zetu” kunaonyesha kwamba, hata ingawa mashtaka yake dhidi ya Ayubu yalithibitishwa kuwa bandia, yeye alifuliza moja kwa moja kutilia shaka ukamilifu wa watumishi wa kidunia wa Mungu. Kwa wazi, yeye alirudia kwa pindi nyingi lile shtaka la kwamba mtu atatoa vyote alivyo navyo kwa kubadilishana na nafsi yake. Lo! jinsi Shetani ameshindwa kwa kusikitisha!—Ayubu 1:9-11; 2:4, 5.

      20. Wakristo waaminifu wamemshindaje Shetani?

      20 Wakristo wapakwa-mafuta, wanaohesabiwa kuwa waadilifu “kwa sababu ya damu ya Mwana-Kondoo,” wanaendelea kutoa ushuhuda kwa Mungu na kwa Yesu Kristo ijapokuwa minyanyaso. Kwa zaidi ya miaka 120, hii jamii ya Yohana imekuwa ikielekeza kwenye lile suala kubwa linalohusiana na kukoma kwa majira ya Mataifa katika 1914. (Luka 21:24) Na sasa umati mkubwa unatumikia kishikamanifu kando yao. Hakuna wowote wa hawa ‘wanahofu wale wanaoua mwili lakini hawawezi kuua nafsi,’ kama vile maono ya maisha halisi ya Mashahidi wa Yehova katika wakati wetu yameonyesha tena na tena. Kwa neno la kinywa na kwa mwenendo unaofaa wa Kikristo, wao wameshinda Shetani, wakithibitisha bila ugeugeu kwamba yeye ni mwongo. (Mathayo 10:28; Mithali 27:11; Ufunuo 7:9, NW) Wanapofufuliwa kwenda katika mbingu, ni lazima Wakristo wapakwa-mafuta wawe na furaha kama nini, kwa kuwa Shetani hayuko juu kule ili kushtaki ndugu zao! Kweli kweli, ni wakati wa wingi wote wa malaika, kuitikia kwa shangwe mwito: “Mwe na nderemo, nyinyi mbingu na nyinyi ambao hukaa ndani yazo!”

      Ole wa Ushindani!

      21. Shetani ameleteaje dunia na bahari ole?

      21 Akiudhika kwa sababu ya ole wa tatu, sasa Shetani ananuia kusumbua aina ya binadamu kwa namna yake mwenyewe ya ole. Ni: “Ole kwa ajili ya dunia na kwa ajili ya bahari, kwa sababu Ibilisi amekuja chini kwa nyinyi, akiwa na kasirani kubwa, akijua yeye ana kipindi kifupi cha wakati.” (Ufunuo 12:12b, NW) Kutupwa kwa Shetani nje ya mbingu bila shaka kunamaanisha ole kwa dunia halisi, ambayo inaangamizwa na binadamu wenye ubinafsi walio chini ya udhibiti wake. (Kumbukumbu 32:5) Hata zaidi hivyo, sera ya Shetani ‘tawala au angamiza’ huleta ole kwa dunia ya ufananisho, muundo wa jamii ya kibinadamu, pamoja na bahari ya ufananisho, lile tungamo lenye msukosuko la aina ya binadamu yenyewe. Wakati wa vita viwili vya ulimwengu, hasira-kisasi ya Shetani ilionyeshwa kwa hasira-kisasi ya mataifa yaliyotiishwa chini yake, na milipuko ya hasira kali ya roho waovu kama hiyo inaendelea hadi leo hii—ingawa si kwa muda mrefu zaidi! (Marko 13:7, 8) Lakini hata mbinu za Ibilisi ziwe zenye kuogofya namna gani, hazitaweza kamwe kukaribia tokeo lenye ole ambalo ole wa tatu—tendo kupitia Ufalme wa Mungu—litafanyiza juu ya tengenezo lionekalo la Shetani!

      22, 23. (a) Yohana husema ni nini kinachokuwa baada ya drakoni kuwa amevurumishwa chini kwenye dunia? (b) Inawezekanaje kwa drakoni kunyanyasa “mwanamke ambaye alizaa mtoto wa kiume”?

      22 Tangu kutupwa nje kwa Shetani kwenye msiba mkubwa, ndugu za Kristo ambao wangali duniani wamevumilia ukatili wa hasira-kisasi yake. Yohana huripoti hivi: “Sasa wakati drakoni alipoona kwamba amevurumishwa chini kwenye dunia, alinyanyasa mwanamke ambaye alizaa mtoto wa kiume. Lakini mabawa mawili ya tai akapewa mwanamke, ili yeye apate kuruka kwenda katika jangwa kwenye mahali pake; huko ndiko yeye analishwa kwa wakati na nyakati na nusu wakati mbali na uso wa nyoka.”—Ufunuo 12:13, 14, NW.

      23 Hapa njozi inachukua wazo lililotolewa katika mstari wa 6, ambao unatuambia kwamba baada ya uzawa wa mtoto wake, mwanamke akimbia kwenda katika jangwa, mbali na drakoni. Huenda sisi tukataka kujua jinsi huyo drakoni anavyoweza kunyanyasa mwanamke, kwa kuwa yeye yuko katika mbingu na drakoni huyo sasa ametupwa chini kwenye dunia. Basi, kumbuka kwamba huyo mwanamke ana watoto hapa duniani, mbegu yake. Baadaye katika njozi hii, sisi tunaarifiwa kwamba Shetani anaonyesha hasira-kali yake kuelekea huyo mwanamke kwa kunyanyasa mbegu yake. (Ufunuo 12:17) Yale yanayoipata mbegu ya mwanamke hapa duniani yaweza kuonwa kuwa yakipata huyo mwanamke mwenyewe. (Linga Mathayo 25:40.) Na hesabu yenye kukua ya waandamani wa hiyo mbegu duniani ingepatwa pia na minyanyaso hiyo.

      Taifa Jipya

      24. Ni nini kilichopata Wanafunzi wa Biblia kilichofanana na kukombolewa kwa Waisraeli kutoka Misri?

      24 Vita ya ulimwengu ya kwanza ilipokuwa ikipiganwa, ndugu waaminifu wa Yesu waliendelea na kushuhudu kwao kadiri walivyoweza. Hiyo ilifanywa usoni mwa upinzani ulioongezewa mkazo kutoka Shetani na vibaraka wake wakali. Mwishowe, kushuhudu peupe kwa Wanafunzi wa Biblia karibu kulisimamishwa. (Ufunuo 11:7-10) Hiyo ilikuwa wakati walipopatwa na kituko kama kile cha Waisraeli katika Misri ambao pia walivumilia chini ya uonevu mkubwa. Ikawa ndipo Yehova alipowaleta upesi, kama kwa mabawa ya tai, kwenye usalama katika jangwa la Sinai. (Kutoka 19:1-4) Hali kadhalika, baada ya mnyanyaso mkali wa 1918-19, Yehova alikomboa mashahidi wake, wenye kuwakilisha mwanamke wake, akawaingiza ndani ya hali ya kiroho iliyokuwa salama kwao kama jangwa lilivyokuwa kwa Waisraeli. Hiyo ilikuja ikiwa jibu la sala zao.—Linga Zaburi 55:6-9.

      25. (a) Ni nini alichotokeza Yehova katika 1919, kama alivyotokeza Waisraeli wakiwa taifa jangwani? (b) Ni nani wanaojumlika kuwa taifa hili, nao wameletwa ndani ya nini?

      25 Huko jangwani, Yehova aliwatokeza Waisraeli wakiwa taifa, akiwaandalia kiroho na kimwili. Hali moja na hiyo, kuanzia 1919, Yehova aliitokeza mbegu ya mwanamke ikiwa taifa la kiroho. Hili lisifikiriwe kuwa ule Ufalme wa Kimesiya ambao umekuwa ukitawala kutoka katika mbingu tangu 1914. Badala ya hivyo, washiriki wa hili taifa jipya ni baki la mashahidi wapakwa-mafuta walio duniani, walioletwa ndani ya hali ya kiroho tukufu katika 1919. Wakiwa sasa wanaandaliwa “kipimo cha ugavi wa chakula chao kwa wakati unaofaa,” hao waliimarishwa kwa ajili ya kazi iliyokuwa mbele.—Luka 12:42, NW; Isaya 66:8.

      26. (a) Kile kipindi cha wakati kinachotajwa kwenye Ufunuo 12:6, 14 ni cha urefu gani? (b) Ni nini lililokuwa kusudi la kipindi hicho cha nyakati tatu na nusu, kilianza lini na kilikwisha lini?

      26 Pumziko la muda hili la mbegu ya mwanamke wa Mungu lilidumu kwa muda gani? Ufunuo 12:6 husema siku 1,260. Ufunuo 12:14 hukiita kipindi hicho wakati, nyakati, na nusu wakati; kwa maneno mengine, nyakati tatu na nusu. Kwa kweli, semi zote mbili husimamia miaka mitatu na nusu, ikiendelea katika Kizio cha Kaskazini kutoka masika ya 1919 kufika vuli ya 1922. Hiki kilikuwa kipindi cha ponyo lenye kuburudisha na kujipanga tena kitengenezo kwa jamii ya Yohana iliyorudishwa.

      27. (a) Kulingana na ripoti ya Yohana, yule drakoni alifanya nini baada ya 1922? (b) Ni nini lililokuwa kusudi la Shetani kutapika nje furiko la mnyanyaso dhidi ya Mashahidi?

      27 Yule drakoni hakuchoka! “Na drakoni akatapika maji kama mto kutoka kinywa chake baada ya mwanamke, ili kufanya yeye azamishwe na mto.” (Ufunuo 12:15, NW) Ni nini kinachomaanishwa na “maji kama mto,” au “furiko la maji”? (The New English Bible) Mfalme Daudi wa kale alisema juu ya waovu ambao walimpinga kuwa “mafuriko-bubujiko ya watu wasiofaa kitu [“vijito vya wasio na thamani,” Young]. (Zaburi 18:4, 5, 16, 17, NW) Hali kadhalika, anachofungulia Shetani ni kunyanyaswa na wasio na thamani au “watu wasiofaa kitu.” Baada ya 1922 Shetani alitapika furiko la mnyanyaso dhidi ya Mashahidi. (Mathayo 24:9-13) Hilo lilikuja kutia ndani jeuri ya kimwili, “kutunga matata kwa amri,” vifungo, na hata kunyongwa kwa kutundikwa, kupigwa risasi, na kukatwa kichwa. (Zaburi 94:20, NW) Shetani aliyetwezwa, akiwa amenyimwa ruhusa ya kumfikia moja kwa moja mwanamke wa Mungu, alianza kushambulia kwa hasira-kisasi ile mbegu yake inayobaki duniani na kuwaangamiza, ama moja kwa moja ama kwa kusababisha wapoteze kibali cha Mungu kwa kuvunja ukamilifu wao. Lakini azimio lao lilithibitika kuwa kama lile la Ayubu: “Mpaka mimi niishe mimi sitaondolea mbali ukamilifu wangu kutoka kwangu mwenyewe!”—Ayubu 27:5, NW.

      28. Furiko la mnyanyaso lilifikiaje kilele wakati wa Vita ya Ulimwengu 2?

      28 Furiko hili la ukatili la mnyanyaso lilifikia kilele wakati wa Vita ya Ulimwengu 2. Katika Ulaya Mashahidi wapatao 12,000 walitiwa katika kambi za mateso za Nazi, na 2,000 hivi wakafa. Chini ya mabwana wa vita waliotawala Italia, Japani, Korea, na Taiwani, Mashahidi waaminifu walipata kutendewa kikatili vivyo hivyo. Hata katika yale mabara yanayoitwa eti ya kidemokrasi, Mashahidi walishambuliwa na vikundi vya Aksio Katoliki, wakapakwa lami na kuvikwa manyoya, na wakafukuzwa kutoka mji. Makusanyiko ya Wakristo yalivunjwa na watoto wa Mashahidi wakafukuzwa shuleni.

      29. (a) Yohana anaelezaje habari ya muawana ukiwasili kutoka chimbuko lisilotazamiwa? (b) “Dunia ikaja kusaidia mwanamke” jinsi gani? (c) Yule drakoni alieendelea kufanya nini?

      29 Muawana uliwasili kutoka chimbuko lisilotazamiwa: “Lakini dunia ikaja kusaidia mwanamke, na dunia ikafungua kinywa chayo na ikameza kabisa mto ambao yule drakoni alitapika kutoka kinywa chake. Na drakoni akajaa hasira-kisasi kuelekea mwanamke, na akatoka kwenda kufanya vita na wabakio wa mbegu yake, ambao hushika amri za Mungu na wana kazi ya kutoa ushahidi kwa Yesu.” (Ufunuo 12:16, 17, NW) “Dunia”—elementi zilizo ndani ya mfumo wa mambo wa Shetani mwenyewe—ikaanza kumeza ule “mto,” au “furiko.” Wakati wa miaka ya 1940 Mashahidi walianza kupata mfululizo wa maamuzi yenye kupendeleka katika Mahakama Kuu Zaidi Sana ya United States, na kutoka mamlaka zenye kutawala katika mabara fulani, ambayo yalitetea uhuru wa ibada. Mwishowe, Mataifa-Mafungamani yakameza kabisa hiyo kani kubwa gandamizi ya Kinazi-Fashisti, kwa kuauni Mashahidi ambao walikuwa wameteseka chini ya tawala katili za kidikteta. Minyanyaso haikukoma kabisa, kwa kuwa yule drakoni ameendelea mpaka leo hii, naye huendeleza vita dhidi ya wale ambao “wana kazi ya kutoa ushahidi kwa Yesu.” Katika mabara mengi, Mashahidi washikamanifu wangali wamo gerezani, na baadhi yao wangali wanakufa kwa sababu ya ukamilifu wao. Lakini katika mengine ya mabara haya, wakati kwa wakati wenye mamlaka hulegeza mbano wao, na Mashahidi hufurahia kipimo kikubwa zaidi cha uhuru.c Hivyo, katika utimizo wa unabii, dunia huendelea kumeza mto wa mnyanyaso.

      30. (a) Dunia imeandaa muawana wa kutosha kwa ajili ya kitu gani kitukie? (b) Ukamilifu wa watu wa Mungu hutokeza nini?

      30 Katika njia hii, dunia imeandaa muawana wa kutosha kuruhusu kazi ya Mungu iendelee kwenye mabara 235 hivi na kuzaa wahubiri wa habari njema waaminifu zaidi ya milioni sita. Pamoja na wabakio wa mbegu ya mwanamke, umati mkubwa wa kimataifa wa waumini wapya unashika amri za Mungu kwa habari ya kujitenga na ulimwengu, adili safi, na upendo kwa akina ndugu, na wao wanashuhudia Ufalme wa Kimesiya. Ukamilifu wao unajibu shtaka lenye suto la Shetani, hivi kwamba onyo la kifo linavumishwa kwa ajili ya Shetani na mfumo wake wa mambo.—Mithali 27:11.

  • Kupambana na Hayawani Wawili Wakali Sana
    Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!
    • 1, 2. (a) Yohana anasema nini juu ya drakoni? (b) Yohana kwa lugha ya ufananisho, huelezaje habari ya tengenezo lionekanalo linalotumiwa na drakoni?

      YULE drakoni mkubwa ametupwa chini kwenye dunia! Funzo letu juu ya Ufunuo limedhihirisha kwamba Nyoka au wafuasi wake roho waovu hawataruhusiwa tena kamwe warudi ndani ya mbingu. Lakini hatujamaliza habari ya “mmoja ambaye huitwa Ibilisi na Shetani, ambaye anaongoza vibaya dunia nzima yote inayokaliwa.” Simulizi linafuata kutambulisha kirefu njia anayotumia Shetani kupiga vita dhidi ya ‘mwanamke na mbegu yake.’ (Ufunuo 12:9, 17, NW) Yohana anasema hivi juu ya drakoni huyo wa kinyoka: “Na huyo akasimama tuli juu ya mchanga wa bahari.” (Ufunuo 13:1a, NW) Kwa hiyo acheni sisi tutue na kuchunguza njia ya utendaji ya huyo drakoni.

      2 Mbingu takatifu hazisumbuliwi tena na kuwapo kwa Shetani na roho waovu wake. Hao roho waovu wamekwisha fukuzwa nje ya mbingu na kufungiwa kwenye ujirani wa dunia. Hapana shaka hii ndiyo sababu ya ukuzi mkubwa mno wa mazoea ya uwasiliano na roho nyakati hizi. Nyoka mwenye hila angali anadumisha tengenezo la roho lenye ufisadi. Lakini je! yeye pia anatumia tengenezo linaloonekana ili kuongoza vibaya aina ya binadamu? Yohana hutuambia hivi: “Na mimi nikaona hayawani-mwitu akipanda kutoka bahari, mwenye pembe kumi na vichwa saba, na juu ya pembe zake mataji kumi, lakini juu ya vichwa vyake majina yenye kufuru. Sasa hayawani-mwitu ambaye mimi niliona alikuwa kama chui, lakini nyayo zake zilikuwa kama zile za dubu, na kinywa chake kilikuwa kama kinywa cha simba. Na drakoni akampa hayawani nguvu zake na kiti cha ufalme chake na mamlaka kubwa.”—Ufunuo 13:1b, 2, NW.

      3. (a) Ni hayawani gani wakali sana alioona nabii Danieli katika njozi? (b) Hayawani wakubwa mno wa Danieli 7 waliwakilisha nini?

      3 Huyu hayawani wa kiajabu ni nini? Biblia yenyewe hutoa jibu. Kabla ya anguko la Babuloni katika 539 K.W.K., Danieli nabii Myahudi aliona njozi zilizohusu hayawani wakali sana. Kwenye Danieli 7:2-8, NW yeye anaeleza habari za hayawani wanne wakitoka baharini, wa kwanza akishabihi simba, wa pili dubu, wa tatu chui, na “ona kule! hayawani wa nne, mwenye kuhofisha na mwenye kutisha na mwenye nguvu isivyo kawaida . . . na alikuwa na pembe kumi.” Huyu ni sawa kabisa na hayawani aliyeonwa na Yohana wapata mwaka 96 W.K. Pia hayawani huyo ana hulka za simba, dubu, na chui, na ana pembe kumi. Ni nini ulio utambulisho wa wale hayawani wakubwa mno walioonwa na Danieli? Yeye anatuarifu: “Hayawani hawa wakubwa mno . . . ni wafalme wanne ambao watasimama katika dunia.” (Danieli 7:17, NW) Ndiyo, hayawani hao wanawakilisha “wafalme,” au serikali kubwa za kisiasa za dunia.

      4. (a) Katika Danieli 8, kondoo-dume na mbuzi-dume ni taswira ya nini? (b) Ni nini kilichoonyeshwa wakati upembe mkubwa wa mbuzi-dume ulipovunjwa na nyingine nne zikachukua mahali pao?

      4 Katika njozi nyingine, Danieli anaona kondoo-dume mwenye pembe mbili ambaye anapigwa mpaka chini na mbuzi mwenye upembe mkubwa. Malaika Gabrieli anamweleza maana yayo: “Kondoo-dume . . . husimama kwa ajili ya wafalme wa Umedi na Uajemi. Na mbuzi-dume mwenye manyoya anasimama kwa ajili ya mfalme wa Ugiriki.” Gabrieli anaendelea kutoa unabii kwamba upembe mkubwa wa mbuzi-dume ungevunjwa na kufuatwa na pembe nne. Kwa kweli hilo lilitukia miaka zaidi ya 200 baadaye Aleksanda Mkuu alipokufa na ufalme wake ukagawanywa kuwa falme nne zilizotawalwa na wanne wa majenerali wake.—Danieli 8:3-8, 20-25, NW.a

      5. (a) Neno la Kigiriki kwa hayawani linawasilisha maana gani? (b) Hayawani-mwitu wa Ufunuo 13:1, 2, pamoja na vichwa vyake saba anasimamia nini?

      5 Kwa hiyo, ni wazi kwamba Mtungaji Biblia iliyovuviwa huziona serikali za kisiasa za dunia kuwa hayawani. Ni hayawani wa aina gani? Mfasili mmoja anaita hayawani-mwitu wa Ufunuo 13:1, 2 “mshenzi,” na kuongeza: “Sisi tunakubali maana zote ambazo θηρίον [the·riʹon, neno la Kigiriki kwa “hayawani”] huwasilisha, kama dubwana mkatili, mharibifu, mwenye kutia kikuli, mlafuaji, n.k.”b Lo! jinsi hiyo inavyoeleza vizuri mfumo wa kisiasa wenye madoa ya damu ambao kwa huo Shetani ametawala aina ya binadamu! Vichwa saba vya huyu hayawani-mwitu husimama kwa ajili ya serikali sita kubwa za ulimwengu ambazo zimeelezwa katika historia ya Biblia kufikia siku ya Yohana—Misri, Ashuru, Babuloni, Umedi-Uajemi, Ugiriki, na Roma—na serikali kubwa ya ulimwengu ya saba iliyotolewa unabii kutokea baadaye.—Linga Ufunuo 17:9, 10.

      6. (a) Vichwa saba vya hayawani-mwitu vilichukua uongozi katika nini? (b) Roma ilitumiwaje na Yehova katika kufikiliza hukumu zake mwenyewe juu ya mfumo wa mambo wa Kiyahudi, na Wakristo katika Yerusalemu walikuwa katika hali gani?

      6 Ni kweli, kumekuwako serikali nyinginezo kubwa za ulimwengu katika historia mbali na zile saba—kama vile hayawani-mwitu ambaye Yohana aliona alivyokuwa na mwili pamoja na vichwa saba na pembe kumi. Lakini vichwa saba huwakilisha zile serikali kubwa ambazo, kila mojapo katika zamu yayo, imechukua uongozi katika kuonea watu wa Mungu. Katika 33 W.K., wakati Roma ilipokuwa mamlaka kuu yenye kutawala, Shetani alitumia hicho kichwa cha hayawani-mwitu kuua Mwana wa Mungu. Wakati huo, Mungu aliuacha mfumo wa mambo wa Kiyahudi usioaminika na baadaye, katika 70 W.K., akaruhusu Roma itekeleze hukumu yake juu ya taifa hilo. Kwa furaha, Israeli wa kweli wa Mungu, kundi lililopakwa mafuta la Wakristo, alikuwa ameonywa kimbele, na wale ambao walikuwa katika Yerusalemu na Yudea walikuwa wamekimbilia usalama ng’ambo ya Mto Yordani.—Wagalatia 6:16; Mathayo 24:15, 16.

      7. (a) Kungetukia nini wakati umalizio wa mfumo wa mambo ungewasili na siku ya Bwana kuanza? (b) Ni nini kilichothibitika kuwa ndicho kichwa cha saba cha hayawani-mwitu wa Ufunuo 13:1, 2?

      7 Hata hivyo, kufikia mwisho wa karne ya kwanza W.K., wengi katika hili kundi la mapema walikuwa wameanguka kutoka ukweli, na ngano ya kweli ya Kikristo, “wale wana wa ufalme,” ilikuwa imesongwa sana na magugu, “wale wana wa yule mwovu.” Lakini wakati umalizio wa mfumo wa mambo ulipowasili, Wakristo wapakwa-mafuta walitokea tena wakiwa kikundi kilichopangwa kitengenezo. Wakati wa siku ya Bwana, ulikuwa umefika wakati wa waadilifu ‘waangaze kwa uangavu kama jua.’ Kwa sababu hiyo, kundi la Kikristo lilipangwa kitengenezo kwa ajili ya kazi. (Mathayo 13:24-30, 36-43, NW) Kufikia wakati huo, Milki ya Roma haikuwapo tena. Milki kubwa ya Uingereza, pamoja na United States ya Amerika yenye nguvu nyingi, zilishikilia kitovu cha jukwaa la ulimwengu. Hii serikali ya ulimwengu ya uwili ilithibitika kuwa ndiyo kichwa cha saba cha hayawani-mwitu.

      8. Ni kwa nini haipasi kushtusha kwa vile Uingereza-Amerika serikali kubwa ya uwili, inafananishwa na hayawani?

      8 Lakini je! haishtushi kutambulisha serikali za kisiasa na hayawani-mwitu? Ndivyo baadhi ya wapinzani walivyodai wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, hadhi ya Mashahidi wa Yehova, wakiwa tengenezo na wakiwa watu mmoja mmoja, ilipokuwa ikitiliwa shaka katika mahakama za sheria kotekote duniani. Lakini tua ufikirie! Je! mataifa yenyewe hayatumii hayawani au viumbe-mwitu kuwa ishara za kitaifa zao? Mathalani, kuna simba wa Uingereza, tai wa Amerika, na drakoni wa Uchina. Basi sababu gani yeyote apinge ikiwa Mtungaji wa kimungu wa Biblia Takatifu anatumia pia hayawani kufananisha serikali za ulimwengu?

      9. (a) Ni kwa nini mmoja hapaswi kupinga Biblia inaposema kwamba Shetani humpa hayawani-mwitu mamlaka yake kubwa? (b) Shetani anaelezwaje katika Biblia, naye anatumiaje uvutano juu ya serikali?

      9 Zaidi ya hilo, sababu gani yeyote apinge Biblia inaposema kwamba Shetani ndiye anayewapa hawa hayawani-mwitu mamlaka yao kubwa? Mungu ndiye Chimbuko la taarifa hiyo, na mbele zake ‘mataifa ni kama tone kutoka ndoo na kama filamu tu ya vumbi.’ Mataifa hayo yangefanya vizuri kutafuta kibali cha Mungu kuliko kuudhikia njia ambayo Neno lake hueleza habari zayo. (Isaya 40:15, 17; Zaburi 2:10-12, NW) Shetani si mtu wa hadithi ya uwongo mwenye mgawo wa kuzitesa nafsi zilizoondoka katika moto. Hakuna mahali kama hapo. Badala ya hivyo, Shetani anaelezwa habari zake katika Maandiko kuwa “malaika wa nuru”—stadi wa udanganyi anayetumia uvutano wenye nguvu katika mambo ya kisiasa kwa ujumla.—2 Wakorintho 11:3, 14, 15; Waefeso 6:11-18.

      10. (a) Ni nini inayoonyeshwa na uhakika wa kwamba juu ya kila mojapo pembe kumi palikuwa na taji? (b) Pembe kumi na mataji kumi huwakilisha nini?

      10 Hayawani-mwitu ana pembe kumi juu ya vichwa vyake saba. Labda kila kimoja cha vichwa vinne kilikuwa na upembe mmoja na kila kimoja cha vichwa vitatu kilikuwa na pembe mbili. Zaidi ya hilo, alikuwa na mataji kumi juu ya pembe zake. Katika kitabu cha Danieli, hayawani wenye kuhofisha wanaelezwa, na hesabu ya pembe yapasa ifasiriwe kihalisi. Mathalani, pembe mbili za kondoo-dume huwakilisha milki ya ulimwengu yenye washirika wawili, Umedi na Uajemi, hali pembe nne zilizo juu ya mbuzi huwakilisha milki nne zilizokuwako wakati ule ule ambazo zilikua kutokana na milki ya Ugiriki ya Aleksanda Mkuu. (Danieli 8:3, 8, 20-22) Hata hivyo, juu ya hayawani ambaye Yohana aliona hesabu ya pembe kumi yaonekana kuwa ya ufananisho. (Linga Danieli 7:24; Ufunuo 17:12.) Zinawakilisha ukamili wa serikali zenye enzi ambazo hujumlika kuwa tengenezo la kisiasa la Shetani. Pembe hizi zote ni zenye jeuri na zenye kutaka vita, lakini kama inavyoonyeshwa na vichwa saba, ukichwa hukaa katika serikali kubwa moja ya ulimwengu, wakati mmoja. Hali kadhalika, yale mataji kumi huonyesha kwamba serikali zote zenye enzi zingetumia mamlaka yenye kutawala wakati ule ule mmoja na dola kuu au serikali kubwa ya ulimwengu, ya wakati huo.

      11. Ni nini kinachoonyeshwa na uhakika wa kwamba hayawani-mwitu ana “juu ya vichwa vyake majina ya kufuru”?

      11 Huyo hayawani-mwitu ana “juu ya vichwa vyake majina yenye kufuru,” akijifanyia madai yanayoonyesha utovu mkubwa wa kustahi Yehova Mungu na Kristo Yesu. Ametumia majina ya Mungu na Kristo kuwa kisingizio cha kutimizia makusudi yake ya kisiasa; naye amecheza pamoja na dini bandia, hata kukubali viongozi wa kidini washiriki sehemu katika mambo ya siasa. Mathalani, Nyumba ya Mabwana ya Uingereza hutia ndani maaskofu. Makardinali wa Kikatoliki wamekuwa na vyeo vya umashuhuri katika Ufaransa na Italia, na hivi majuzi mapadri wametwaa vyeo vya kisiasa katika Amerika ya Kilatini. Serikali huchapa shime za kidini, kama “IN GOD WE TRUST” (Sisi Twaitibari Mungu), kwenye noti zao za benki, na juu ya sarafu zao zinadai kwamba watawala wazo wana kibali cha kimungu, wakitaarifu, mathalani, kwamba hao wanawekwa rasmi “kwa neema ya Mungu.” Kwa kweli yote haya ni makufuru, kwa kuwa hujaribu kumhusisha Mungu katika uwanja wa kisiasa wa kitaifa wenye kutiwa uchafu.

      12. (a) Ni nini kinachoashiriwa na kutoka kwa hayawani-mwitu katika “bahari,” naye alianza kutokea wakati gani? (b) Ni nini kinachoonyeshwa na uhakika wa kwamba drakoni anampa hayawani wa ufananisho mamlaka yake kubwa?

      12 Hayawani-mwitu hutoka katika “bahari,” ambayo ni ufananisho wenye kufaa wa yale matungamo yenye msukosuko ambayo kwayo serikali za kibinadamu huchipuka. (Isaya 17:12, 13) Hayawani-mwitu huyu alianza kuibuka katika bahari yenye msukosuko huko nyuma katika siku za Nimrodi (yapata karne ya 21 K.W.K.), wakati mfumo wa mambo wa baada ya Furiko, wenye kupinga Yehova, ulipojidhihirisha kwa mara ya kwanza. (Mwanzo 10:8-12; 11:1-9) Lakini ni katika pindi ya ile siku ya Bwana tu ndipo kichwa chake cha saba kimejidhihirisha kabisa. Vilevile angalia, drakoni ndiye “akampa hayawani nguvu zake na kiti cha ufalme chake na mamlaka kubwa.” (Linga Luka 4:6.) Hayawani huyo ni ubuni wa Shetani miongoni mwa matungamo ya aina ya binadamu. Kwa kweli Shetani ndiye “mtawala wa ulimwengu huu.”—Yohana 12:31, NW.

      Dharuba ya Kifo

      13. (a) Ni baa gani linalompata hayawani-mwitu mapema katika siku ya Bwana? (b) Ni jinsi gani hayawani-mwitu mzima wote aliumia wakati kichwa kimoja kilipopokea dharuba-kifo?

      13 Mapema katika siku ya Bwana, baa linampiga hayawani-mwitu. Yohana huripoti: “Na mimi nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimechinjwa hadi kifo, lakini dharuba-kifo yake ikaponeshwa, na dunia nzima yote ikafuata hayawani-mwitu kwa kusifu mno.” (Ufunuo 13:3, NW) Mstari huu husema kwamba kichwa kimoja cha huyu hayawani-mwitu kilipokea dharuba ya kifo, lakini mstari wa 12 husema kana kwamba hayawani mzima wote aliumia. Ni kwa nini hivyo? Basi, si vichwa vyote vya huyo hayawani vinavyodhibiti pamoja mamlaka kuu. Kila kimoja katika zamu yacho kimepiga ubwana juu ya aina ya binadamu, hasa juu ya watu wa Mungu. (Ufunuo 17:10) Hivyo, siku ya Bwana inapoanza, kuna kichwa kimoja tu, kile cha saba, kikitenda kuwa ndicho serikali kubwa ya ulimwengu yenye kutawala. Dharuba ya kifo kwenye kichwa hicho humletea hayawani-mwitu mzima wote taabu kubwa.

      14. Ni lini dharuba-kifo ilipopigwa, na ofisa mmoja wa kijeshi alielezaje tokeo layo juu ya hayawani-mwitu wa Shetani?

      14 Ni nini iliyokuwa dharuba-kifo? Baadaye, huitwa dharuba-upanga, na upanga ni ufananisho wa vita. Dharuba-kifo hii, iliyopigwa mapema katika siku ya Bwana, lazima ihusiane na vita ya ulimwengu ya kwanza, iliyokumba na ikamkausha hayawani-mwitu wa kisiasa wa Shetani. (Ufunuo 6:4, 8;13:14) Mtunga vitabu Maurice Genevoix, aliyekuwa ofisa wa kijeshi katika vita hiyo, alisema kuihusu hivi: “Kila mmoja anakubali katika kutambua kwamba katika historia ya aina ya binadamu kwa ujumla, tarehe chache zimekuwa na umaana wa Agosti 2, 1914. Kwanza Ulaya na upesi baadaye karibu binadamu wote walijikuta wametumbukia ndani ya tukio lenye kuhofisha. Kawaida, miafaka, sheria za kiadili, misingi yote ilitikisika; kutoka siku moja hadi inayofuata, kila kitu kilitiliwa shaka. Tukio hilo lilipasa kuzidi mabashiri ya kisilika na mataraja ya kiasi pia. Likiwa kubwa mno, lenye machafuko, lenye kutia hofu, lingali laburuta sisi katika njia yalo.”—Maurice Genevoix, mshiriki wa Acadeʹmie Française, aliyenukuliwa katika kitabu Promise of Greatness (1968).

      15. Ni jinsi gani kichwa cha saba cha hayawani mwitu kilipokea dharuba-kifo?

      15 Vita hiyo ilikuwa msiba mkubwa wa kichwa kikuu cha saba cha hayawani-mwitu. Pamoja na mataifa mengine ya Ulaya, Uingereza ilipoteza vijana wayo kwa hesabu yenye kuumiza sana. Katika pigano moja pekee, lile Pigano la Mto Somme katika 1916, kulikuwa na askari-jeshi 420,000 wa Uingereza waliokufa au kupotea vitani, pamoja na 194,000 wa Ufaransa na 440,000 wa Ujeremani—jumla ya watu zaidi ya 1,000,000 waliokufa au kupotea vitani! Kiuchumi, vilevile, Uingereza—pamoja na sehemu nyingine ya Ulaya—ilivunjwavunjwa. Milki kubwa mno ya Uingereza ilitetereka chini ya hilo pigo na haikupona kikamili kamwe. Kweli kweli, vita hiyo, ikiwa na mataifa mashuhuri 28 ilifanya ulimwengu mzima wote uyumbeyumbe kana kwamba kwa pigo la kifo. Katika Agosti 4, 1979, miaka 65 tu baada ya kufyatuka Vita ya Ulimwengu 1, The Economist, la London, Uingereza lilieleza: “Katika 1914 ulimwengu ulipoteza ushikamano ambao haujaweza kuupata tena tangu hapo.”

      16. Wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, United States ilionyeshaje kwamba ilikuwa sehemu ya serikali kubwa ya ulimwengu ya uwili?

      16 Wakati ule ule, ile Vita Kubwa, kama ilivyoitwa wakati huo, ilifungulia njia United States kuibuka waziwazi ikiwa sehemu ya Serikali Kubwa ya Ulimwengu ya Uingereza-Amerika. Katika miaka ya kwanza ya vita hiyo, maoni ya umma yaliondoa United States katika pambano hilo. Lakini kama alivyoandika mwanahistoria Esmé Wingfield-Stratford, hayo “yote yalikuwa swali la kama, katika saa hii ya hatari kubwa mno, Uingereza na United States zingezamisha tofauti zao katika kupata umoja [wao] wenye ushindi na udhamini wa pamoja.” Kama vile matukio yalivyopata kuwa, zilifanya hivyo. Katika 1917 United States ilichanga rasilimali na askari-jeshi ili kusaidia jitihada za Mataifa-Mafungamani yaliyokuwa yakiyumbayumba. Hivyo, kichwa cha saba, kikiunganisha Uingereza na United States, kikatokea kikiwa upande wenye kushinda.

      17. Kukawa nini kwa mfumo wa kidunia wa Shetani baada ya vita?

      17 Ulimwengu baada ya vita hiyo ulikuwa tofauti sana. Mfumo wa kidunia wa Shetani, ujapokuwa ulikumbwa na pigo la kifo, ulipona na ukawa wenye nguvu zaidi kuliko wakati wowote na hivyo ukasifiwa sana na wanadamu kwa sababu ya nguvu zao za kupona.

      18. Inaweza kusemwaje kwamba aina ya binadamu kwa ujumla ‘imefuata hayawani-mwitu kwa kusifu mno’?

      18 Mwanahistoria Charles L. Mee, Jr., anaandika: “Anguko la utaratibu wa kale [lililosababishwa na vita ya ulimwengu ya kwanza] lilikuwa utangulizi uliohitajiwa kabisa kwa mtandazo wa kujitawala, ule ukombozi wa mataifa mapya na matabaka, kuachiliwa kwa uhuru na kujitegemea kupya.” Chenye kuongoza katika mwendeleo wa kipindi hiki cha baada ya vita kilikuwa kichwa cha saba cha hayawani-mwitu, kikiwa sasa kimepona, na United States ya Amerika ikichukua daraka kuu. Hiyo serikali kubwa ya ulimwengu ya uwili ilichukua uongozi katika kutetea Ushirika wa Mataifa na Umoja wa Mataifa. Kufikia mwaka wa 2005, nguvu za kisiasa za U.S. zilikuwa zimeongoza mataifa yenye mapendeleo zaidi katika kubuni kiwango cha juu zaidi cha maisha, katika kupigana na magonjwa, na katika kuendeleza tekinolojia. Hata ilikuwa imepeleka watu 12 kwenye mwezi. Basi, si ajabu, kwamba aina ya binadamu kwa ujumla ‘imefuata hayawani-mwitu kwa kusifu mno.’

      19. (a) Ni jinsi gani aina ya binadamu imepita kiasi katika kusifu mno hayawani-mwitu? (b) Ni nani aliye na mamlaka isiyopingwa juu ya falme zote za dunia, na sisi tunajuaje? (c) Shetani huwakilishaje mamlaka hiyo kwa hayawani-mwitu, na kukiwa na tokeo gani juu ya halaiki ya watu?

      19 Aina ya binadamu imepita kiasi cha kusifu mno huyo hayawani-mwitu, kama Yohana anavyofuata kutaarifu: “Na wao wakaabudu drakoni kwa sababu alimpa mamlaka hayawani-mwitu, na wao wakaabudu hayawani-mwitu kwa maneno haya: ‘Ni nani aliye kama hayawani-mwitu, na ni nani anayeweza kufanya pigano na yeye?’” (Ufunuo 13:4, NW) Yesu alipokuwa hapa duniani, Shetani alidai kuwa na mamlaka juu ya falme zote za dunia. Yesu hakupinga hilo; kwa kweli, yeye alirejeza kwa Shetani kuwa mtawala wa ulimwengu na akakataa kushiriki katika siasa za siku hiyo. Baadaye Yohana aliandikia Wakristo wa kweli hivi: “Sisi twajua kwamba sisi tunatokana na Mungu, lakini ulimwengu kwa ujumla unalala katika nguvu za mwovu.” (1 Yohana 5:19; Luka 4:5-8; Yohana 6:15; 14:30, NW) Shetani huwakilisha mamlaka kwa hayawani-mwitu, naye hufanya hivyo kwa msingi wa utukuzo wa taifa. Hivyo, badala ya kuunganishwa na vifungo vya upendo wa kimungu, aina ya binadamu imegawanywa na kiburi cha kabila, jamii, na taifa. Halaiki kubwa ya watu, kwa kweli, huabudu sehemu ya hayawani-mwitu iliyo na mamlaka katika bara wanamojikuta wakiishi. Hivyo hayawani kwa ujumla hupata kusifiwa na kuabudiwa mno.

      20. (a) Ni katika maana gani watu huabudu hayawani-mwitu? (b) Ni kwa nini Wakristo ambao huabudu Yehova Mungu hawashiriki ibada hiyo ya hayawani-mwitu, nao wanafuata kielelezo cha nani?

      20 Ibada katika maana gani? Katika maana ya kuweka upendo wa nchi mbele ya upendo wa Mungu. Watu walio wengi wanapenda bara la uzawa wao. Wakiwa wananchi wema, Wakristo wa kweli wanaheshimu pia watawala na mifano ya nchi ambako wao wanakaa, wanatii sheria, na kuchangia kihakika masilahi ya jumuiya yao na majirani wao. (Warumi 13:1-7; 1 Petro 2:13-17) Hata hivyo, wao hawawezi kujitoa kipumbavu kwa ajili ya nchi moja dhidi ya zile nyingine zote. “Nchi yetu, ikosee isikosee” si fundisho la Kikristo. Kwa hiyo Wakristo wanaomwabudu Yehova Mungu hawawezi kushiriki kutoa ibada ya kizalendo yenye kiburi kwa sehemu yoyote ya hayawani-mwitu, kwa kuwa hiyo ingekuwa ni kuabudu drakoni—chimbuko la mamlaka ya huyo hayawani.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki