-
Ni Nani Atakayeutawala Ulimwengu?Sikiliza Unabii wa Danieli!
-
-
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
SERIKALI ZA ULIMWENGU ZA UNABII WA DANIELI
Ile sanamu kubwa (Danieli 2:31-45)
Wanyama wanne kutoka baharini (Danieli 7:3-8, 17, 25)
BABILONIA tangu 607 K.W.K.
UMEDI NA UAJEMI tangu 539 K.W.K.
UGIRIKI tangu 331 K.W.K.
ROMA tangu 30 K.W.K.
SERIKALI YA ULIMWENGU YA UINGEREZA NA MAREKANI tangu 1763 W.K.
ULIMWENGU ULIOGAWANYIKA KISIASA wakati wa mwisho
-
-
Ni Nani Atakayeutawala Ulimwengu?Sikiliza Unabii wa Danieli!
-
-
Sura Ya Tisa
Ni Nani Atakayeutawala Ulimwengu?
1-3. Fafanua ndoto na maono ambayo Danieli aliona mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza.
SASA unabii wa Danieli wenye kuvutia sana waturudisha nyuma hadi mwaka wa kwanza wa Mfalme Belshaza wa Babiloni. Danieli amekuwa uhamishoni Babiloni kwa muda mrefu, lakini uaminifu-maadili wake kwa Yehova haujayumbayumba kamwe. Sasa akiwa na umri wa miaka 70 na kitu, nabii huyo mwaminifu aona “ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake.” Nayo maono hayo yamwogofya wee!—Danieli 7:1, 15.
2 “Tazama,” Danieli asema kwa mshangao. “Hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali.” Wanyama wa ajabu kama nini! Wa kwanza ni simba mwenye mabawa, na wa pili ni kama dubu. Kisha chui mwenye mabawa manne na vichwa vinne atokea! Mnyama wa nne mwenye nguvu nyingi zisizo za kawaida ana meno ya chuma na pembe kumi. Pembe “ndogo” yatokea katikati ya pembe zake kumi ikiwa na “macho kama macho ya mwanadamu” na “kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu.”—Danieli 7:2-8.
3 Kisha maono ya Danieli yageukia mbingu. Mzee wa Siku aketi kwa utukufu akiwa Hakimu katika Mahakama ya kimbingu. ‘Maelfu elfu wanamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wamesimama mbele zake.’ Akiwahukumu wanyama hao vikali, awanyang’anya utawala na kumharibu mnyama wa nne. “Mmoja aliye mfano wa mwanadamu [“mwana wa binadamu,” NW]” apewa mamlaka atawale “watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote.”—Danieli 7:9-14.
4. (a) Danieli alimtegemea nani ili kupata maana ya kweli ya mambo hayo? (b) Kwa nini mambo ambayo Danieli aliona na kusikia usiku huo ni ya maana kwetu?
4 “Mimi,” Danieli asema, “roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha.” Kwa hiyo, amwuliza malaika “maana ya kweli ya hayo yote.” Kwa kweli malaika huyo amjulisha “tafsiri ya mambo hayo.” (Danieli 7:15-28) Kile ambacho Danieli aliona na kusikia usiku huo chatupendeza sana, kwa kuwa kilionyesha matukio ya ulimwengu ya wakati ujao yanayofikia nyakati zetu, wakati ambapo “mmoja aliye mfano wa mwanadamu [“mwana wa binadamu,” NW]” anapewa utawala juu ya “watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote.” Sisi pia twaweza kuelewa maana ya maono hayo ya kiunabii tukisaidiwa na Neno la Mungu na roho yake.a
WANYAMA WANNE WATOKA BAHARINI
5. Bahari iliyochafuliwa na upepo yafananisha nini?
5 “Wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini,” akasema Danieli. (Danieli 7:3) Ni nini kilichofananishwa na bahari iliyochafuliwa na upepo? Miaka mingi baadaye, mtume Yohana aliona hayawani-mwitu mwenye vichwa saba akitoka katika “bahari.” Bahari hiyo iliwakilisha “vikundi vya watu na umati na mataifa na lugha”—jamii kubwa ya wanadamu iliyotengana na Mungu. Basi, bahari ni ufananisho unaofaa wa umati wa watu waliojitenga na Mungu.—Ufunuo 13:1, 2; 17:15; Isaya 57:20.
6. Wale wanyama wanne wanafananisha nini?
6 Malaika wa Mungu akasema: “Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani.” (Danieli 7:17) Malaika aliwatambulisha waziwazi wanyama wanne ambao Danieli aliwaona kuwa “wafalme wanne.” Kwa hiyo, wanyama hao wanafananisha serikali za ulimwengu. Lakini serikali zipi?
7. (a) Wafafanuzi fulani wa Biblia husema nini juu ya ono ambalo Danieli aliona katika ndoto juu ya wanyama wanne na ile ndoto ya sanamu kubwa aliyoota Mfalme Nebukadreza? (b) Kila moja ya sehemu nne za metali za sanamu hiyo zawakilisha nini?
7 Kwa kawaida, wafafanuzi wa Biblia huhusianisha ono la Danieli kwenye ndoto juu ya wanyama wanne na ile ndoto ya Nebukadreza ya sanamu kubwa. Kwa kielelezo, kichapo The Expositor’s Bible Commentary chataarifu hivi: “Sura ya 7 [ya Danieli] yalingana na sura ya 2.” Kichapo The Wycliffe Bible Commentary chasema: “Kwa ujumla yakubalika kwamba mfuatano wa tawala nne za wasio Wayahudi . . . [katika Danieli sura ya 7] unafanana na ule unaotajwa katika [Danieli] sura ya 2.” Zile serikali nne za ulimwengu zilizowakilishwa na zile metali nne za ndoto ya Nebukadreza zilikuwa Milki ya Babiloni (kichwa cha dhahabu), Umedi na Uajemi (kifua na mikono ya fedha), Ugiriki (tumbo na viuno vya shaba), na Milki ya Roma (miguu ya chuma).b (Danieli 2:32, 33) Acheni tuone jinsi falme hizo zinavyolingana na wale wanyama wanne wakubwa ambao Danieli aliona.
MKALI KAMA SIMBA, MWEPESI KAMA TAI
8. (a) Danieli alimfafanuaje mnyama wa kwanza? (b) Mnyama wa kwanza alifananisha milki gani, nayo ilitendaje kama simba?
8 Danieli aliona wanyama wa ajabu kama nini! Akimfafanua mmoja wao, alisema hivi: “Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.” (Danieli 7:4) Mnyama huyo alifananisha utawala uleule uliowakilishwa na kichwa cha dhahabu cha ile sanamu kubwa, Serikali ya Ulimwengu ya Babiloni (607-539 K.W.K.). Kama ilivyo na “simba” mwindaji, Babiloni lilinyafua mataifa kwa ukali, kutia ndani watu wa Mungu. (Yeremia 4:5-7; 50:17) “Simba” huyo alisonga kasi katika ushindi wenye nguvu, kana kwamba alikuwa na mabawa ya tai.—Maombolezo 4:19; Habakuki 1:6-8.
9. Yule mnyama kama simba alibadilikaje, na mabadiliko hayo yalimwathirije?
9 Hatimaye, mabawa ya yule simba wa pekee “yakafutuka manyoya.” Mwishoni-mwishoni mwa utawala wa Mfalme Belshaza, Babiloni lilipoteza mwendo wake wa ushindi na ukuu wake kama simba juu ya mataifa. Halikwenda kasi kuliko binadamu akitembea kwa miguu miwili. Kwa kuwa lilipata “moyo wa kibinadamu,” likawa dhaifu. Babiloni halingeweza tena kutenda kama mfalme “kati ya wanyama wa msituni,” kwa kuwa halikuwa na “moyo wa simba.” (Linganisha 2 Samweli 17:10; Mika 5:8.) Mnyama mwingine mkubwa akamshinda.
MLAFI KAMA DUBU
10. “Dubu” alifananisha watawala gani?
10 “Tazama,” akasema Danieli, “mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele.” (Danieli 7:5) Mfalme aliyefananishwa na “dubu” huyo ndiye yuleyule aliyewakilishwa na kifua na mikono ya fedha ya ile sanamu kubwa—wale watawala mbalimbali wa Umedi na Uajemi (539-331 K.W.K.) kuanzia Dario Mmedi na Koreshi Mkuu hadi Dario wa Tatu.
11. Kuinuka upande mmoja kwa yule dubu wa mfano na kuwa na mifupa mitatu ya mbavu katika mdomo wake kulifananisha nini?
11 Yule dubu wa mfano “aliinuliwa upande mmoja,” huenda ili kuwa tayari kushambulia na kushinda mataifa na hivyo kudumu akiwa serikali ya ulimwengu. Au huenda kuinuka huko kulikusudiwa kuonyesha kwamba watawala wa Uajemi wangetawala kupita mfalme mmoja Mmedi, Dario. Ile mifupa mitatu ya mbavu katika meno ya dubu huyo ingeweza kufananisha pande tatu ambazo dubu huyo angeshinda. “Dubu” wa Umedi na Uajemi alienda kaskazini kuteka Babiloni mwaka wa 539 K.W.K. Kisha akaenda magharibi kupitia Asia Ndogo na kuingia Thrasi. Hatimaye, “dubu” huyo alienda kusini akashinde Misri. Kwa kuwa nambari tatu nyakati nyingine huonyesha mkazo, ile mifupa mitatu ya mbavu yaweza pia kukazia pupa ya ushindi, ya yule dubu wa mfano.
12. Kulitokea nini yule dubu wa mfano alipotii ile amri: “Inuka, ule nyama tele”?
12 “Dubu” huyo alishambulia mataifa kwa mujibu wa maneno haya: “Inuka, ule nyama tele.” Kwa kunyafua Babiloni kulingana na mapenzi ya Mungu, serikali ya Umedi na Uajemi ingeweza kutimiza utumishi wa maana kuelekea watu wa Yehova. Nayo ilifanya hivyo! (Ona “Mtawala Mvumilivu,” kwenye ukurasa wa 149.) Kupitia Koreshi Mkuu, Dario wa Kwanza (Dario Mkuu), na Artashasta wa Kwanza, serikali ya Umedi na Uajemi iliweka huru Wayahudi waliokuwa wametekwa na Babiloni na kuwasaidia kujenga upya hekalu la Yehova na kurekebisha kuta za Yerusalemu. Hatimaye, Umedi na Uajemi ikatawala wilaya 127, na mume wa Malkia Esta, Ahasuero (Shasta wa Kwanza), akamiliki “toka Bara Hindi mpaka Kushi.” (Esta 1:1) Hata hivyo, mnyama mwingine alikuwa akikaribia kuinuka.
MWEPESI KAMA CHUI MWENYE MABAWA!
13. (a) Mnyama wa tatu alifananisha nini? (b) Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya mwendo wa mnyama wa tatu na milki yake?
13 Mnyama wa tatu alikuwa “kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka.” (Danieli 7:6) Kama lile tumbo na viuno vya shaba vya sanamu ya ndoto ya Nebukadreza, chui huyo mwenye mabawa manne na vichwa vinne alifananisha watawala wa Makedonia, au Ugiriki, kuanzia Aleksanda Mkuu. Akiwa na wepesi na mwendo wa chui, Aleksanda alipitia Asia Ndogo, kusini kuingia Misri, na kusonga mbele kufikia mpaka wa magharibi wa India. (Linganisha Habakuki 1:8.) Milki yake ilikuwa kubwa kuliko ile ya “dubu,” kwa kuwa ilitia ndani Makedonia, Ugiriki, na Milki ya Uajemi.—Ona “Mtawala Mchanga Aushinda Ulimwengu,” kwenye ukurasa wa 153.
14. “Chui” alipataje kuwa na vichwa vinne?
14 “Chui” huyo alipata vichwa vinne baada ya Aleksanda kufa mwaka wa 323 K.W.K. Wanne kati ya majenerali wake walitawala baada yake katika sehemu tofauti-tofauti za milki yake. Seleuko alitawala Mesopotamia na Siria. Ptolemy akatawala Misri na Palestina. Lisimako akatawala Asia Ndogo na Thrasi, naye Kasanda akatawala Makedonia na Ugiriki. (Ona “Ufalme Mkubwa Wagawanyika,” kwenye ukurasa wa 162.) Kisha tisho jingine likazuka.
MNYAMA MKALI AWA TOFAUTI
15. (a) Mfafanue mnyama wa nne. (b) Mnyama wa nne alifananisha nini, naye alivunja vipande vipande na kula kila kitu kilichokuwa mbele yake jinsi gani?
15 Danieli alimfafanua mnyama wa nne kuwa “mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi.” Aliendelea kusema hivi: “Naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.” (Danieli 7:7) Mnyama huyo mkali alianza akiwa serikali ya kisiasa na ya kijeshi ya Roma. Ikatwaa hatua kwa hatua yale maeneo manne ya Kiyunani ya Milki ya Ugiriki, na kufikia mwaka wa 30 K.W.K., Roma ilikuwa imeinuka na kuwa serikali ya ulimwengu iliyofuata katika unabii wa Biblia. Ikishinda kwa nguvu za kijeshi kila kitu kilichokuwa mbele yake, hatimaye Milki ya Roma ikaenea toka Visiwa vya Uingereza hadi sehemu kubwa ya Ulaya, kotekote kuzunguka Mediterania, na ng’ambo ya Babiloni hadi Ghuba ya Uajemi.
16. Malaika alisema nini juu ya mnyama wa nne?
16 Akitaka kujua maana kamili ya mnyama huyu “mwenye kutisha,” Danieli alimsikiliza kwa makini malaika alipokuwa akimfafanua: “Na habari za zile pembe [zake] kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali [“tofauti,” BHN] na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.” (Danieli 7:19, 20, 24) “Pembe kumi,” au “wafalme kumi” walikuwa nani?
17. Zile “pembe kumi” za mnyama wa nne zafananisha nini?
17 Roma ilipozidi kutajirika na kuharibika kwa sababu ya maisha ya ufisadi miongoni mwa jamii ya watawala wake, nguvu yake ya kijeshi ilipungua. Hatimaye, kupungua kwa nguvu za kijeshi za Roma kukaonekana waziwazi. Mwishowe milki hiyo yenye nguvu ikavunjika na kuwa falme nyingi. Kwa kuwa Biblia mara nyingi hutumia nambari kumi kudokeza ukamili, zile “pembe kumi” za mnyama wa nne zawakilisha falme zote zilizotokana na kuvunjika kwa Roma.—Linganisha Kumbukumbu la Torati 4:13; Luka 15:8; 19:13, 16, 17.
18. Roma iliendeleaje kutawala Ulaya kwa karne nyingi baada ya kuondolewa kwa maliki wake wa mwisho?
18 Hata hivyo, Serikali ya Ulimwengu ya Roma haikuisha wakati maliki wake wa mwisho katika Roma alipopinduliwa mwaka wa 476 W.K. Kwa karne nyingi, Roma ya papa iliendelea kutawala Ulaya kisiasa na hasa kidini. Ilifanya hivyo kupitia mfumo wa kikabaila, ambamo wakazi wengi wa Ulaya walikuwa chini ya bwana, kisha chini ya mfalme. Na wafalme wote walikuwa chini ya mamlaka ya papa. Kwa hiyo, Milki ya Roma Takatifu, Roma ya papa ikiwa kituo chake kikuu, ilitawala mambo ya dunia kwa kipindi chote hicho kirefu cha historia kilichoitwa Enzi za Giza.
19. Kulingana na mwanahistoria mmoja, Roma ilitofautianaje na milki zilizoitangulia?
19 Ni nani awezaye kupinga kwamba mnyama wa nne hakuwa ‘tofauti na zile falme za kwanza’? (Danieli 7:7, 19, 23) Kuhusu hilo, mwanahistoria H. G. Wells aliandika hivi: “Serikali hiyo mpya ya Roma . . . ilitofautiana kwa njia kadhaa na milki nyingine kuu ambazo zilikuwa zimeutawala ulimwengu mstaarabu awali. . . . [Hiyo] ilitia ndani karibu Wagiriki wote ulimwenguni, na haikuwa na watu wengi wa jamii ya Hamu na jamii ya Shemu kama milki zilizotangulia . . . Lilikuwa jambo jipya katika historia kufikia wakati huo . . . Milki ya Roma ilikuwa ukuzi, ukuzi mpya ambao haukupangiwa; Waroma walijikuta bila kujua katika mradi mkubwa wa kutawala.” Hata hivyo, yule mnyama wa nne angekua hata zaidi.
PEMBE NDOGO YAPATA UTAWALA
20. Malaika alisema nini juu ya kumea kwa pembe ndogo kwenye kichwa cha mnyama wa nne?
20 “Nikaziangalia sana pembe zake,” akasema Danieli, “na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang’olewa kabisa.” (Danieli 7:8) Kuhusu ukuzi huo, malaika alimwambia Danieli hivi: “Mwingine ataondoka baada ya hao [wale wafalme kumi]; naye atakuwa mbali [“tofauti,” BHN] na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.” (Danieli 7:24) Mfalme huyo ni nani, aliinuka lini, naye alishusha wafalme gani watatu?
21. Uingereza ilipataje kuwa ile pembe ndogo ya mfano ya mnyama wa nne?
21 Fikiria mambo yafuatayo. Mwaka wa 55 K.W.K., Jenerali Mroma Juliasi Kaisari alivamia Uingereza lakini akashindwa kuidhibiti daima. Mwaka wa 43 W.K., Maliki Klaudio alianza ushindi wa kudumu zaidi dhidi ya Uingereza kusini. Kisha, mwaka wa 122 W.K., Maliki Hadriani akaanza kujenga ukuta kutoka Mto Tyne hadi Ghuba ya Solway, akiweka mpaka wa kaskazini wa Milki ya Roma. Mapema katika karne ya tano, majeshi ya Roma yaliondoka kisiwa hicho. “Katika karne ya kumi na sita,” akaeleza mwanahistoria mmoja, “Uingereza haikuwa serikali yenye nguvu sana. Haikuwa na utajiri mwingi kama Uholanzi. Ilikuwa na watu wachache kuliko Ufaransa. Majeshi yake (kutia ndani jeshi la wanamaji) hayakuwa na nguvu kama majeshi ya Hispania.” Yaonekana kwamba Uingereza ulikuwa ufalme mdogo wakati huo, uliokuwa pembe ndogo ya mfano ya mnyama wa nne. Lakini hali hiyo ingebadilika.
22. (a) Ile pembe “ndogo” ilishinda pembe zipi nyingine tatu za yule mnyama wa nne? (b) Kisha Uingereza ikawa nini?
22 Mwaka wa 1588, Philip wa Pili wa Hispania alituma Manowari za Hispania zikashambulie Uingereza. Kundi hilo la meli 130, zilizobeba watu zaidi ya 24,000, lilisafiri kupitia Mlango-Bahari wa Uingereza, nalo lilishindwa na jeshi la wanamaji la Uingereza na kuhasiriwa na pepo zilizovuma dhidi yao na dhoruba kali za Atlantiki. Tukio hilo “lilionyesha kwamba sasa Uingereza ndiyo iliyokuwa na jeshi kuu la wanamaji na wala si Hispania,” akasema mwanahistoria mmoja. Katika karne ya 17, Waholanzi walikuwa na meli nyingi zaidi ulimwenguni za kufanyia biashara. Hata hivyo, kwa sababu ya koloni zenye kuongezeka ng’ambo, Uingereza iliushinda ufalme huo pia. Katika karne ya 18, Waingereza na Wafaransa walipigana huko Amerika Kaskazini na India, hilo likiongoza kwenye Mkataba wa Paris mwaka wa 1763. Mwandishi William B. Willcox alisema kwamba mkataba huo “ulitambua wadhifa mpya wa Uingereza ikiwa serikali kuu ya Ulaya katika ulimwengu nje ya Ulaya.” Ukuu wa Uingereza ulithibitishwa ilipomshinda vibaya Napoléon wa Ufaransa mwaka wa 1815 W.K. Kwa hiyo, wale “wafalme watatu” ambao Uingereza ‘ilishusha’ ni Hispania, Uholanzi, na Ufaransa. (Danieli 7:24) Kwa hiyo, Uingereza ikawa serikali kubwa zaidi ulimwenguni ya kikoloni na ya kibiashara. Naam, ile pembe “ndogo” ikakua na kuwa serikali ya ulimwengu!
23. Ile pembe ndogo ya mfano ‘ilikulaje dunia yote’?
23 Malaika alimwambia Danieli kwamba mnyama wa nne, au ufalme wa nne, ‘ungekula dunia yote.’ (Danieli 7:23) Ndivyo ilivyokuwa kuhusu mkoa wa Roma ambao wakati mmoja uliitwa Uingereza. Hatimaye ukawa Milki ya Uingereza na ‘kula dunia yote.’ Wakati mmoja, milki hiyo ilimiliki robo moja ya nchi kavu ya dunia na robo moja ya wakazi wa dunia.
24. Mwanahistoria mmoja alisema Milki ya Uingereza ilikuwaje tofauti?
24 Kama vile Milki ya Roma ilivyokuwa tofauti na serikali za ulimwengu zilizotangulia, mfalme aliyefananishwa na ile pembe “ndogo” pia angekuwa “mbali [“tofauti,” BHN] na hao wa kwanza.” (Danieli 7:24) Kuhusu Milki ya Uingereza, mwanahistoria H. G. Wells alitaarifu hivi: “Hakujawa na [serikali] yoyote ya aina hiyo. Jambo la kwanza na kuu katika mfumo wote huo lilikuwa ‘jamhuri yenye mfalme’ ya Muungano wa Falme za Uingereza . . . Hakuna ofisi yoyote wala akili yoyote iliyopata kamwe kufahamu Milki yote ya Uingereza. Ilikuwa muungano wa ukuzi na mamlaka zaidi tofauti kabisa na yoyote iliyopata kuitwa milki hapo awali.”
25. (a) Katika matukio ya karibuni zaidi, ile pembe ndogo ya mfano ni nini? (b) Ile pembe “ndogo” ina “macho kama macho ya mwanadamu,” na ‘kinywa kinachonena maneno makuu’ katika maana gani?
25 Ile pembe “ndogo” ilihusisha mengi zaidi ya Milki ya Uingereza. Mwaka wa 1783, Uingereza ilizipa uhuru koloni zake 13 za Amerika. Hatimaye, Marekani ikawa mshirika wa Uingereza, na kuibuka ikiwa taifa lenye nguvu zaidi duniani baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili. Bado ingali na uhusiano wenye nguvu na Uingereza. Serikali ya Uingereza na Marekani iliyotokezwa ndiyo ‘pembe yenye macho.’ Kwa kweli, serikali hiyo ya ulimwengu inaona sana, na ina akili! ‘Hunena mambo makuu,’ ikiamua sera zitakazofuatwa na sehemu kubwa ya ulimwengu na kuwa msemaji wake, au “nabii asiye wa kweli.”—Danieli 7:8, 11, 20; Ufunuo 16:13; 19:20.
ILE PEMBE NDOGO YAMPINGA MUNGU NA WATAKATIFU WAKE
26. Malaika alitabiri nini juu ya maneno na matendo ya ile pembe ya mfano kumwelekea Yehova na watumishi wake?
26 Danieli aliendelea kufafanua ono lake, akisema: “Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda.” (Danieli 7:21) Kuhusu “pembe” hiyo, au mfalme huyo, malaika wa Mungu alitabiri hivi: “Atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.” (Danieli 7:25) Sehemu hiyo ya unabii huu ilitimia jinsi gani na lini?
27. (a) “Watakatifu” wanaonyanyaswa na ile pembe “ndogo” ni nani? (b) Ile pembe ya mfano iliazimiaje “kubadili majira na sheria”?
27 “Watakatifu” walionyanyaswa na ile pembe “ndogo”—Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani—ni wafuasi watiwa-mafuta kwa roho wa Yesu walio duniani. (Waroma 1:7; 1 Petro 2:9) Kwa miaka kadhaa kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, mabaki ya watiwa-mafuta hao walionya waziwazi kwamba mwaka wa 1914 ungekuwa mwisho wa “nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa.” (Luka 21:24) Vita vilipozuka mwaka huo, ilikuwa dhahiri kwamba ile pembe “ndogo” ilikuwa imepuuza onyo hilo, kwa kuwa iliwasumbua daima watiwa-mafuta “watakatifu.” Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani hata ilipinga jitihada zao za kuendeleza matakwa (au, “sheria”) ya Yehova ya kwamba mashahidi wake wahubiri habari njema ya Ufalme ulimwenguni pote. (Mathayo 24:14) Kwa hiyo, ile pembe “ndogo” ilijaribu “kubadili majira na sheria.”
28. “Wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati” zina urefu gani?
28 Malaika wa Yehova alirejezea kipindi cha wakati cha kiunabii kuwa “wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.” Kipindi hicho kilikuwa na urefu gani? Wafafanuzi wa Biblia hukubaliana kwa ujumla kwamba usemi huo hurejezea nyakati tatu na nusu—jumla ya wakati mmoja, nyakati mbili, na nusu wakati. Kwa kuwa zile “nyakati saba” za kichaa cha Nebukadreza zilijumlika kuwa miaka saba, zile nyakati tatu na nusu ni miaka mitatu na nusu.c (Danieli 4:16, 25) Tafsiri ya An American Translation husema: “Watatiwa mikononi mwake kwa mwaka mmoja, miaka miwili, na nusu mwaka.” Tafsiri ya Biblia Habari Njema husema: “Kwa muda wa miaka mitatu na nusu.” Kipindi hichohicho chatajwa kwenye andiko la Ufunuo 11:2-7, linalotaarifu kwamba mashahidi wa Mungu wangehubiri wakiwa wamevaa nguo za gunia kwa miezi 42, au siku 1,260, kisha wauawe. Kipindi hicho kilianza na kuisha lini?
29. Ile miaka mitatu na nusu ya kiunabii ilianza lini na jinsi gani?
29 Kwa Wakristo watiwa-mafuta, wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ulikuwa wakati wa kujaribiwa. Kufikia mwisho wa mwaka wa 1914, walikuwa wakitarajia mnyanyaso. Kwa hakika, andiko la mwaka lenyewe lililochaguliwa kwa ajili ya mwaka wa 1915 lilikuwa swali la Yesu alilowauliza wanafunzi wake, “Je, mwaweza kukinywa kikombe ambacho mimi niko karibu kunywa?” Lilitegemea Mathayo 20:22. Kuanzia Desemba mwaka wa 1914, mashahidi hao wachache walihubiri “wakiwa wamevaa nguo ya gunia.”
30. Wakristo watiwa-mafuta walisumbuliwaje na Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza?
30 Vita vilipopamba moto, Wakristo watiwa-mafuta walikabili upinzani wenye kuongezeka. Baadhi yao walifungwa gerezani. Watu mmoja-mmoja, kama vile Frank Platt aliyekuwa Uingereza na Robert Clegg huko Kanada, waliteswa na wenye mamlaka wakatili. Februari 12, 1918, Kanada iliyokuwa Milki ya Uingereza ilipiga marufuku buku la saba la Studies in the Scriptures, liitwalo The Finished Mystery, lililokuwa limechapishwa karibuni, pamoja na trakti ziitwazo The Bible Students Monthly. Mwezi uliofuata, Ofisi ya Mkuu wa Sheria ya Marekani ilitangaza kugawanywa kwa buku hilo la saba kuwa kinyume cha sheria. Ikawaje? Nyumba zilisakwa, fasihi zikatwaliwa, na waabudu wa Yehova wakakamatwa!
31. “Wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati” ziliisha lini na jinsi gani?
31 Kusumbuliwa kwa watiwa-mafuta wa Mungu kulifikia upeo Juni 21, 1918, wakati ambapo msimamizi, J. F. Rutherford, na washiriki mashuhuri wa Watch Tower Bible and Tract Society walihukumiwa vifungo vya muda mrefu gerezani kwa sababu ya mashtaka yasiyo ya kweli. Ikiazimu “kubadili majira na sheria,” ile pembe “ndogo” ilikuwa imefanikiwa kuharibu utaratibu wa kazi ya kuhubiri. (Ufunuo 11:7) Kwa hiyo, kile kipindi kilichotabiriwa cha “wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati” kilimalizika Juni 1918.
32. Kwa nini ungeweza kusema kwamba “watakatifu” hawakufutiliwa mbali na ile pembe “ndogo”?
32 Lakini “watakatifu” hawakuharibiwa na ule usumbufu wa ile pembe “ndogo.” Kama ilivyotabiriwa katika kitabu cha Ufunuo, baada ya kipindi kifupi cha kutotenda, Wakristo watiwa-mafuta walipata uhai na kuwa watendaji tena. (Ufunuo 11:11-13) Machi 26, 1919, msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society na washiriki wake waliachiliwa kutoka gerezani, na baadaye wakaondolewa mashtaka yote yasiyo ya kweli waliyokuwa wameshtakiwa. Punde baadaye, mabaki watiwa-mafuta wakaanza kufanya mipango mipya kwa ajili ya utendaji zaidi. Hata hivyo, ile pembe “ndogo” ingepatwa na nini?
MZEE WA SIKU AHUKUMU
33. (a) Mzee wa Siku ni nani? (b) Ni ‘vitabu gani vilivyofunuliwa’ katika Mahakama ya kimbingu?
33 Baada ya kuwatambulisha wale wanyama wanne, Danieli aacha kumwangalia mnyama wa nne na kuona kikao mbinguni. Aona Mzee wa Siku ameketi katika kiti chake chenye utukufu akiwa Hakimu. Mzee wa Siku si mwingine ila Yehova Mungu. (Zaburi 90:2) Mahakama ya kimbingu iketipo, Danieli aona ‘vitabu vikifunuliwa.’ (Danieli 7:9, 10) Kwa kuwa Yehova ni wa tangu milele, anajua historia yote ya binadamu kana kwamba imeandikwa katika kitabu. Amewaangalia wanyama wote hao wanne naye aweza kuwahukumu kulingana na mambo ajuayo yeye mwenyewe.
34, 35. Ile pembe “ndogo” na serikali nyingine za mnyama zitapatwa na nini?
34 Danieli aendelea kusema hivi: “Nikatazama wakati huo; kwa sababu ya sauti ya yale maneno makubwa iliyoyasema ile pembe; nalitazama hata mnyama yule akauawa, mwili wake ukaharibiwa, akatolewa ateketezwe kwa moto. Na kwa habari za wale wanyama wengine, walinyang’anywa mamlaka yao; walakini maisha yao yalidumishwa kwa wakati na majira.” (Danieli 7:11, 12) Malaika amwambia Danieli hivi: “Hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuyapoteza na kuyaangamiza, hata milele.”—Danieli 7:26.
35 Kwa amri ya Hakimu Mkuu, Yehova Mungu, pembe iliyomkufuru Mungu na kuwasumbua “watakatifu” wake itapatwa na jambo lilelile lililoipata Milki ya Roma, ambayo iliwanyanyasa Wakristo wa mapema. Utawala wake hautaendelea. Hata wale “wafalme” wadogo walio kama pembe waliotokana na Milki ya Roma hawataendelea. Hata hivyo, vipi juu ya tawala zilizotokana na serikali za awali zilizofananishwa na mnyama? Kama ilivyotabiriwa, maisha yao yalidumishwa “kwa wakati na majira.” Maeneo yao yameendelea kuwa na watu hadi leo. Kwa mfano, Iraki iko kwenye eneo la Babiloni ya Kale. Uajemi (Iran) na Ugiriki zingaliko. Mabaki ya serikali hizo za ulimwengu ni sehemu ya Umoja wa Mataifa. Falme hizo pia zitaangamia serikali ya ulimwengu ya mwisho itakapoangamizwa. Serikali zote za kibinadamu zitafutiliwa mbali kwenye “vita ya siku kubwa ya Mungu Mweza-Yote.” (Ufunuo 16:14, 16) Lakini, ni nani basi atakayeutawala ulimwengu?
-